TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.
Na Steve B.S.M
Sehemu ya Nane.
Brooklyn, New York.
Saa saba ya mchana
Richie alimtazama Hilda akajikuta anatabasamu mwenyewe. Moyo wake ulikuwa unahisi baridi kumwona mwanamke huyu, lakini zaidi kumwona hapa nyumbani kwake. Ilikuwa ni jambo maalum kabisa.
Alikuwa jikoni anakaanga mayai lakini kila saa akichungulia mlango kumtazama Hilda aliyekuwa ameketi kwenye kochi kwa ustaarabu.
Mwanamke huyo alikuwa amevalia blauzi ya pinki yenye maneno yanayometameta kifuani. Chini alivalia 'tight' nyeusi iliyoishia juu kidogo ya enka zake.
Macho yake ndani ya miwani yalikuwa yako bize na runinga. Mchezo mzuri wa basketball ulikuwa unarushwa hapo. Aliutazama kila hatua muda mwingine akitupa mikono yake kiushabiki. Wazi timu yake pendwa ilikuwa inacheza muda huu.
Richie, aliyekuwa amevalia apron nyeusi yenye pichapicha za matunda mbalimbali, hakuishiwa hamu ya kumtazama mwanamke huyo. Kwake alikuwa mpya. Kitendo cha kumwona akiwa mbali na nguo anazoshindia kazini kilimvutia macho yake.
Kuna muda alikutana na Hilda uso kwa uso akatabasamu, lakini mara nyingi, alipokuwa akitazama, alimkuta mwanamke huyo amekunjia shingo runingani.
Yai lilipoiva, aliliweka kwenye sahani pana aliyoitoa kwenye kabati dogo la vyombo.
Alitoa juisi kwenye jokofu lake la mlango wa mmoja, akaimiminia kwenye glasi kubwa aliyoambatanisha pamoja na sahani ile yenye yai.
Alitembea kuelekea sebuleni akiwa anatabasamu, naye Hilda alimpokea kwa tabasamu pana akitazama sahani anayoletewa. Ilikuwa imesheheni mayai. Ukitazama kwa harakaharaka yalikaangwa kama mayai kumi hivi.
Hilda alijawa na mate mdomoni. Alitazama juisi pia, akajikuta mdomo wake unakuwa mkavu ghafla. Tumbo lilimnguruma.
"Utaniwia radhi, hiki ndo kitu nachoweza kupika," Richie alisema akiweka sahani na glasi juu ya kistuli kidogo. Hilda alimpongeza kwa kuwa mpishi mzuri japokuwa bado hakuonja. Aliamini kwa macho tu, chakula kile kilikuwa kitamu. Hakujua aliyasema hayo tokea kichwani au tumboni.
Aliponawa, alifakamia chakula hicho kwa upesi kana kwamba mtu aliyebanwa na njaa kali. Alisahau kabisa ule mchezo kwenye runinga. Alihangaika kuhudumia tumbo lake kwanza kabla ya yote.
Ukimtazama namna anavyokula, huwezi uliza kwanini mwili wake ni kipipa.
Richie alikuwa amelenga kula, mikono yake ilikuwa inachuruza maji aliyotoka kunawa, lakini alivyomuona Hilda namna alavyo, aliamua kusitisha.
Alikaa pembeni akimtazama mwamke huyo namna anavyofurahia chakula cha mikono yake, akajikuta anatabasamu mara kwa mara. Japo hakula lakini aliridhika.
"Wuuuuuuu!" Hilda alipiga kelele. Alinyanyua glasi yake akaimalizia juisi alafu akabeua. "Nimeshiba!" Aliutupia mwili wake mzito kwenye kochi akashusha pumzi ndefu.
"Ahsante, Richie. Nimependa chakula chako na nimeshiba."
Richiw alitabasamu kushukuru. Alitoa vyombo akavipeleka jikoni. Alivua nguo yake ya upishi kisha akaketi kwenye kochi moja na Hilda.
Hakujua kwanini ila moyo wake ulikuwa unamdunda sana. Mara kadhaa aliyakuta macho yake kwenye mapaja ya Hilda asijue yamefikaje.
"Richie," Hilda aliita. Bado mwili wake ulikuwa umeegamia kochi. Yuko hoi kwa shibe. "Uliniitia wito gani hapa kwako? maana si kwa vile ulivyonisisitiza." aliuliza akimtazama Richie kwa mbali ndani ya vioo vyake vya macho.
Richie alitazama kando kidogo akifikiria. Alitaka awe makini na mdomo wake. Alitazama ni namna gani anaweza akaunganisha ubongo wake na ulimi.
"Hilda, hamna jambo kubwa kama unavyotarajia. Leo ni weekend. Mara nyingi nakuwa mpweke hapa nyumbani. Nilifikiria tu huenda ungenipa kampani."
Hilda alibinua mdomo wake. Hakuona kama kuna tatizo kuwepo hapo. Kwakuwa Richie alinyamaza, basi yeye aliendelea kutazama runinga, wakati huo bwana huyo akiendelea kumtazama.
Kuna jambo lilikuwa limemjaa kifuani. Macho yake yalisema wazi.
Baada ya muda kidogo, vijisekunde vichache, alimuuliza Hilda kuhusu usiku ule. Usiku ambao alimwacha kazini mpaka muda mbaya akisema kuna kazi anafanya.
Hilda alimtazama mwanaume kidogo kisha akaendelea na mambo yake. Hakuona jambo kubwa. Alimjibu Richie kwamba alikaa hapo kazini mpaka majira ya saa nne usiku kisha akaondoka zake.
"Saa nne?"
"Ndio."
Kwanini unanidanganya Hilda? Richie aliuliza kifuani mwake akimtazama Hilda. Ni lini utaona sahihi kuniambia ukweli? Aliumia na nafsi yake.
Alitaka kuongea zaidi lakini mdomo wake ulisita. Aliamini ni stara akiendelea kunyamaza huku akingoja muda sahihi utakapowadia.
Kwa sasa alikata shauri, hakutaka shari. Alidhamiria kuutumia muda huu kufurahi na mwanamke huyo kadiri atakavyoweza, kwa kile kidogo alichokidhamiria na kukipanga.
Alitabasamu mwenyewe kwa yale aliyoyaona kichwani mwake.
"Hilda." aliita kwa sauti tulivu. Hilda aligeuza shingo akamtazama .
"Kuna kitu kizuri nimekuandalia, natumai utafurahi."
Hilda alitabasamu kabla hajajua kitu hicho. Alikaa vizuri akamtazama Richie kwa macho ya hamu. Macho hayo yalitatiza nafsi ya Richie.
"Ni nini hiko?"
Richie hakusema kitu. Akiwa anamtazama Hilda machoni, aliingiza mkono yake mfuko wa kulia wa suruali, akatoa karatasi mbili ndogo zenye rangi nyekundu.
Zilikuwa ni tiketi za sinema. Tena kwa filamu ya moto iliyotoka hivi karibuni. Hilda alipobaini hilo aliachama kwa furaha, akamkumbatia Richie kwanguvu.
"Umejuaje nilikuwa nataka nikatazame filamu hii?"
Richie akiwa amejawa na furaha, ameizungusha mikono yake katika kiuno kinene cha Hilda, alimwambia kwa kujivunia kuwa alimwona akiwa anatazama 'trailer' ya filamu hiyo mara kwa mara akiwa ofisini, hapo akajua anaipenda.
Hilda alifurahi kusikia hilo. Alimshika akambusu Richie shavuni. Macho yawe yalijawa na raha. Alitazama tiketi yake kana kwamba mtu asiyeamini anachoona. Alirusha kiganja chake kama mtu aliyeungua na moto.
Furaha hii haikudumu muda mrefu, ni punde, simu ya Hilda iliyokuwepo mezani, ilitetemeka ikiita. Wa kwanza kuitazama alikuwa ni Richie. Kwenye kioo lilitokea jina la 'Boss Bryson'.
Hilda alipokea simu hiyo upesi. Aliongea maneno machache kisha akasema sawa, nipo njiani.
Aliweka simu yake kwenye kijibegi chake cheusi kisha akamuaga Richie. Anaondoka amepata dharura.
"Vipi kuhusu sinema?"
"Haitawezekana leo, Richie. Inabidi niende. Ni muhimu!"
Ni muhimu? Richie alisema na nafsi yake akimtazama Hilda namna anavyoweweseka kuvaa viatu ajiondoe eneo hili.
"Lakini leo ni weekend, Hilda!" Alilalama. Shingo yake aliiweka upande, mkononi ameshikilia tiketi.
"Kwahiyo nikatae wito wa boss? ... Natumai unamjua vizuri, sina haja ya kujieleza."
Richie aling'ata meno akishuhudia mwanamke huyo anaondoka. Moyo ulisinyaa. Mambo yalibadilika ghafla mbele ya macho yake katika namna ambayo hakuamini!
Aliketi kwenye kochi akatazama tiketi aliyoshikilia mkononi. Chozi lilimlenga. Alichanachana tiketi hiyo kwa hasira kisha akajilaza hapo akitazama dari.
Kwanini lakini, Bryson? ... Kwanini leo?
Alisikia kitu kinateremka toka jicho lake la kulia.
***
Queens, New York.
Saa tatu ya usiku.
Bwana aliyekuwa amevalia kofia ya kahawia aina ya panama yenye riboni nyeusi, alikuwa ndani ya gari dogo lililogeshwa pembezoni mwa barabara akiwa anatazama jambo.
Bwana huyo alivalia sweta kola ya V, rangi ya kijivu iliyokolea. Ndani ya sweta hilo alivalia shati drafti, rangi nyeusi na nyeupe. Mkononi mwake ameshikilia kamera.
Uso wake haukuonekana vema sababu ya kofia aloivaa. Kofia hiyo aliishusha chini, na kwasababu ya udumavu wa mwanga kwenye gari hili, kivuli cheusi kilimeza sura yake isionekane inavyotakiwa.
Uso wa bwana huyu ulikuwa umegeukia kutazama jengo kubwa lililopo mkabala na hapa alipoegeshea gari.
Jengo hilo lilikuwa ni maarufu sana kwa michezo mbalimbali ya kamari katika jiji hili la New York, kwa jina; Resorts World Casino.
Katika mwisho huu wa wiki, watu maelfu na mamia walikuwepo hapo wakitumia pesa zao kwa kadiri waonavyo ni sawa. Palikuwa na magari pomoni, lakini miongoni mwa yote hayo bado halikufika lile ambalo bwana huyu ndani ya gari alikuwa analingoja.
Aliendelea kutazama. Muda fulani ulipita lakini hakuchoka. Kidogo, gari liliingia katika eneo hilo, akalisindikiza kwa kichwa chake. Alinyanyua mkono wake wenye kamera akalinasa gari hilo kwa picha kadhaa mpaka pale lilipojiegesha sehemu maalumu ya kumbi ile ya starehe.
Alitulia kidogo akitazama. Aliposhuka mtu ndani ya gari, akaendelea na zoezi lake la upigaji picha kwa mfululizo mpaka mtu huyo aliyekuwa amevalia kwa unadhifu alipozama ndani ya jengo la Resorts Casino.
Alipiga simu akasema, "ameshafika."
Alitoa maelezo ya namna bwana yule aliyemchukua picha alivyokuwa amevaa kisha akakata simu na kuiweka mfukoni.
Alilaza kiti cha gari, akajilaza humo kizani.
Ndani ya muda mfupi, kule kwenye maegesho ya magari, alishuka mwanaume mmoja alyevalia suti nyeusi. Alikuwa mnadhifu sana kuanzia nywele mpaka miguuni, na gari lake lilikuwa Chevrolet ya gharama, rangi nyeusi.
Aliingia ndani ya jengo hilo, akikaribishwa vema na wahudumu wa kike waliovalia matabasamu yao bora, sare zilizobana na sauti mwanana.
Ndani palikuwa pakubwa. Pamejaa mashine mamia za michezo. Meza za kutosha kwa ajili ya yeyote kujichagulia mchezo autakao lakini mbali na ukubwa huo bado watu walifurika wakafanya eneo hilo kuwa finyu. Miongoni mwa watu hao alikuwa ni Mpelelezi.
Alivalia shati jeupe lenye kola fupi. Suruali nyeusi ya kitambaa aliyoichomekea juu kidogo ya kiuno.
Alikuwa ameketi mahali sahihi kwake. Meza kubwa iliyowapa fursa ya watu nane waliokuwa wanacheza kamari kujinafasi. Miongoni mwao watatu walikuwa ni wanawake ambao si wachezaji bali wapo sambamba na wachezaji ili kuwapa kampani.
Walikuwa warembo waliojipamba haswa. Nyuso zao zilikandikwa 'make up' zikavutia mithili ya waridi lililostawi. Nywele maridadi, midomo mekundu, ngozi zao nyororo na nguo zao holela. Walikuwa wanavutia kuwatazama kila saa.
Mpelelezi alicheza mizunguko kadhaa akionyesha umaridadi wake mchezoni. Alishinda michezo miwili ya mwanzoni lakini akapoteza mitatu iliyofuatia ambayo wenzake waligawana ngwe hizo.
Kwa ustadi mkubwa, alizirusha kete zake akashinda mchezo uliofuatia. Na tena unaofuatia. Katika wale wanaume watano, wawili wakaacha kucheza. Walishatumia vya kutosha. Kwenye uwanja wakabakia Mpelelezi na mwanaume mmoja mnene aliyekuwa anapewa kampani na mwanamke pembeni.
Bwana huyo alikuwa na asili ya kiashia. Macho madogo. Nywele zake fupi. Shingoni ana mikufu kadhaa ya dhahabu. Mikononi ana bangili na pete za gharama.
Aliweka dau kubwa mezani akamsihi Mpelelezi waende kikubwa. Atakayeshinda, abebe pesa ya maana. Mpelelezi, pasipo na kufikiri sana, aliridhia ombi hilo akitabasamu lakini walikubaliana kuwa wataenda mikupuo mitatu. Atakayeshinda mikupuo miwili basi atabeba kila kilichopo mezani.
Mchezo ukaanza. Ilikuwa ni mwendo mchezo na pombe. Wahudumu waliokuwa wanapita kila saa walihakikisha watu hawapungukiwi na cha kukatia kitu zao. Glasi kwa glasi
Mkupuo wa kwanza ulienda kwa upesi, bwana yule mnene akashinda. Alitabasamu kwa dharau huku akikandwakandwa mabega na mwanamke aliyepembezoni yake.
Walicheza tena mkupuo wa pili, huu nao bwana huyo akashinda. Alitanua mikono yake akivuta pesa iliyowekwa mezani. Alifanya hivyo akiwa anacheka kicheko kisichofungua mdomo.
Alimtazama mshindani wake akamuuliza kama angetaka kuendelea.
"Una ulichobakiza?"
Mpelelezi alitafakari kwanza. Yote aliyokuwa ameyavuna kwenye mchezo uliopita, vilishayoyoma. Alibakiwa na pesa ya ziada tu katika pochi yake.
Alitafakari akitazama pesa zile zilivyonyingi upande wa yule bwana. Akakata shauri. Alitaka kucheza tena.
"Sina pesa nyingi, lakini kuna nilichokibakiza. Unaonaje sasa kila mmoja akachezesha chote alichonacho. All or Nothing."
Bwana yule mnene alitabasamu kiupande akikuna kidevu chake cheupe. Alimuuliza Mpelelezi kama ana uhakika na anachotaka kukifanya, alipopata uthibitisho, basi akaridhia.
Alisukumizia pesa katikati ya meza kisha akampatia Mpelelezi nafasi ya kwanza ya kucheza.
"Hapana. Wewe ndiye mshindi. Anza, tafadhali," Mpelelezi alisihi. Bwana yule akaanza.
Alitupa mkupuo wake wa dhahabu, akapata alama za juu! Alicheka kwa furaha akimtazama mrembo wake ambaye naye alicheka pasipo kuelewa kitu. Ushindi ulikuwa unanukia.
Mpelelezi alishika kete zake akiwa ana mkazo kiasi. Uso wake aliukunja akijaribu kuomba mungu wa bahati awe upande wake. Kwa namna mwenziwe alivyopata basi naye apate zaidi japo nafasi ilikuwa finyu.
Mshindani wake alikuwa ameacha pointi moja tu, tano kati ya sita. Hivyo ili ashinde hakupaswa kupata yoyote isipokuwa sita ya sita!
Alishusha pumzi ndogo akiwa ameshika kete yake mkononi. Akili yake yote ilikuwa hapo. Alirusha kete hizo kwa namna zote anavyojua, zilipotua, amini usiamini, akawa amepata alama zote!
Alifurahi mno. Alitoa kicheko kikubwa cha ushindi akitikisa ngumi za mikono yake. Upande wa pili, yule bwana hakuwa anaelewa nini kilichotokea. Hakuamini macho yake. Alimtazama mwanamke aliyekuwa naye kwa macho ya hasira, mwanamke yule akahofia. Upesi alitoa mikono yake mabegani mwa mwanaume huyo.
Mpelelezi alizikusanya pesa zake akiwa na tabasamu pana. Zilikuwa ni mlima wa noti kadha wa kadha. Alizikunja vema pesa hizo akiwa anapiga mluzi taratibu. Alikuwa na furaha sana.
Akiwa anafanya zoezi hili, mwanaume yule mnene alikuwa anamtazama kwa macho ya ghadhabu. Aliona amedhulumiwa. Aliomba mchezo uendelee lakini mpelelezi hakuwa tayari.
"Inatosha kwa leo. Labda siku nyingine tukibahatika kuonana."
Hakutaka kungoja. Vishawishi ni vingi. Alitunza pesa zake akaaga. Alitoka kwenye ukumbi huo wa kuchezea kamari, kabla hajaenda nje, alipitia chooni apate kujisaidia kwani pombe alizokunywa zilikuwa zinasumbua kibofu.
Alipotoka chooni, kwenye korido nyembamba, alikutana na bwana yule mnene akiwa na wenzake wanne. Wanaume hawa, jumla watano kwa idadi, walikuwa ndo' walewale waliokuwa na mpelelezi huyu katika meza ya kamari.
Kumbe wote walikuwa wamoja.
Bwana yule mnene alimwambia Mpelelezi arejeshe fedha zake zote na riba juu kama alitaka kutoka na uhai wake katika hilo jengo.
Wanaume wengine waliokuwa wanakuja na kutoka chooni waliwapita kana kwamba hawaoni kitu. Kila mmoja alikuwa ameshika zake. Wengine ndo' kwanza walitembea kwa kasi kujiepushia mabalaa.
"Tulicheza kwa kuridhia, sivyo? Hiyo pesa unayoongelea imetokea wapi?"
Bwana yule mnene hakuongeza tena neno. Kwa ishara ya kichwa aliamuru mpelelezi avamiwe mara moja. Kufumba na kufumbua watu wanne wakamfuata kwa shari!
Alijitahidi kuwamudu kimapigano. Alitumia mikono, miguu na kichwa chake kujitetea kadiri alivyoweza lakini watu wale walikuwa wengi kwa idadi. Japo aliwamudu lakini hakudumu kwa muda mrefu akaanza kuzidiwa.
Aliporusha ngumi moja, alipigwa tatu. Mmoja alimkandika teke la tumbo akaanguka chini mithili ya kiroba. Alihisi maumivu makali sana.
Alishika tumbo lake akikunja uso.
Hakupewa muda wa kupumzika, mabwana wakamfuata tena. Kabla hawajamgusa, sauti kali ilifoka nyuma yao;
"Heeey!"
Walitazama wakamwona bwana alliyevalia suti nyeusi iliyomkaa vema mwilini. Bwana huyo alikuwa amesimama kiukakamavu akiwatazama hawa mabwanyenye kwa macho makali.
Sura yake ilikuwa mithili ya mtoto, laini isiyokuwa na ndevu. Mdomo wake ulikuwa mdogo kidevu chake kikichongoka. Masikio yake mapana, nywele zake nyeusi zimeficha paji lake la uso.
"Unataka kufa?" Aliuliza bonge akimsogelea. "Ukishindwa kufuata mambo yako, basi utalifuata kaburi."
Bwana yule ndani ya suti alimtazama Mpelelezi akapaza sauti kumuuliza kama yuko salama. Mpelelezi alimwonyeshea dole gumba akijitahidi kusimama.
Ghafla wale mabwana walimvamia yule mgeni lakini wote walilambishwa sakafu ndani ya sekunde chache. Kila mmoja alilala akiugulia maumivu. Hawajiwezi.
Bwana yule alimpa pole Mpelelezi alafu akamuaga.
"Ngoja kwanza, ndugu yangu," Mpelelezi alimsihi. Alimshukuru kwa kumsaidia lakini alitaka kumfahamu bwana huyo ni nani haswa. Aliamini hakuwa raia wa kawaida. Namna alivyowamaliza watesi wake kulimpa maswali.
"Mimi ni mtu wa sanaa za mapigano," bwana huyo alisema na kuongezea, "natumai upo salama."
Walibadilishana namba kila mtu akashika njia yake.
Mpelelezi alifuata usafiri wake alipoupaki, akiwa anaugulia maumivu, alijiweka humo akakagua kwanza pesa yake. Zote zilikuwa salama salmini.
Alitabasamu.
Kabla hajawasha gari aondoke, alihisi kichwa kuwa kizito. Macho yalijenga ukungu na mwili ulipoteza nguvu.
Alijitahidi kuwasha gari lakini hakuweza kuweka gia aondoke. Alipoteza fahamu.
***