Tukibaki Hai, Tutasimulia

Tukibaki Hai, Tutasimulia

[emoji1786] BONUS PART [emoji1786]

New York Police Department.

Saa Mbili Asubuhi


Afisa mmoja wa polisi alifika katika ofisi ya mpelelezi akiwa ameshikilia bahasha kubwa ya kaki.

Afisa huyo, mwembamba mrefu, mwendo wake wa kikakamavu, alikuwa na macho ya kizungu mithili ya paka. Sura yake ilikuwa ya kazi, na kofia yake aliyoishusha mpaka kwenye nyusi ilizidi kumfanya atishe.

Alimkabidhi mpelelezi bahasha kisha akamwambia kuwa hicho ndicho walikipata kwa kupitia kitengo maalum za 'CCTV Surveillance'. Baada ya hapo alienda zake asingoje hata maneno ya ziada. Alikuwa ni mjumbe tu.

Mpelelezi alikagua bahasha ile aliyoletwa akakuta maelezo kadhaa na picha vilevile. Miongoni mwa picha hizo alikuwapo Ferdinand na gari walilolikodisha siku ambayo tukio la mauaji lilitokea The DL.

Maelezo yalieleza ya kwamba bwana huyo, pamoja na mwenzake ambaye alikuwa mwanamke, waliutumia usafiri huu wa uber kufika kwenye makazi yao ambayo bado hayajajulikana.

Mpelelezi alijikuta anatabasamu. Sasa aliona kazi yake imeelekea ukingoni mwa ushindi.

Mara moja, kwa kupitia maelezo aliyoyapata, haswa ya gari, alinyookea kwenye ofisi za kampuni ya Uber inayopatikana katika jiji hili kubwa.

Huko aliingia makaoni akataka taarifa, katika mfumo mzima wa Uber, za mtu aliye-request uber yenye 'plate number' zilizopo pichani, saa fulani kutoka kweye bar ya The DL. Alikuwa anataka kujua kila kitu, ikiwemo na ramani ilionyesha gari hilo lilipeleka wateja wapi.

Kuwasababu ya ithibati ya polisi, kampuni haikuwa na namna zaidi ya kuingia kwenye data kusaka kinachodaiwa. Ndani ya muda mfupi, mpelelezi akawa amepata karibia ya kila anachohitaji.

Kabla ya 'move' yoyote ya kusogelea walengsa wake, alimtafuta dereva aliyehusika na kuwasafirisha watu hao, yeye akamhoji maswali kadhaa haswa juu ya haiba ya wateja hao ambao alimkumbushia kwa kutumia picha.

Alipomaliza hapo, alirejea kwenye ofisi yake, akaketi akiyapanga mambo kichwani kwa ustadi wake alobarikiwa na ujuzi wake aliosomea.

Alihoji kila taarifa aliyopata. Kwanza, kwanini watu hawa walifanya mauaji? Kwanini mwaname yule aliingia hapo bar akiwa amejificha na kofia ina maana alidhamiria kuja kufanya tukio? Kwanini walitumia usafiri wa uber, si usafiri binafsi au daladala?

Kwanini taarifa anazozitumia mtu aliye-request uber, si sahihi kwa maana ya kwamba namba yake ya taifa na taarifa zingine alizozianisha hazikuwepo kabisa kwenye mfumo wa serikali?

Na kwanini watu hao walishukia njiani, si mbele, karibu au ndani ya jengo la makazi ambalo ni rahisi kubainika?

Maswali haya alijiuliza akiitazama picha ya mwanamke ambayo alipewa na mfumo maalum wa utambuzi wa serikali. Punde alipoweka namba ambazo mteja yule alikuwa amejisajili nazo, zilimletea hiyo picha.

Ilikuwa ni picha ya mwanamke mdogo, makamo ya miaka ishirini na moja mpaka ishirini na tano hivi. Amebana nywele zake anatabasamu.

Mpelelezi alinyanyua simu yake ya mezani akaagiza mtu fulani kufika ofisini kwake upesi. Punde kidogo, alifika afisa mmoja mnene aliyekuwa amening'iniza 'badge' yake shingoni, amevalia miwani na 'form six' nyekundu.

Mpelelezi alimkabidhi bwana huyo picha ile aliyokuwa anaitazama akamwambia atafute taarifa zote kuihusu alafu amletee mara moja.

Bwana huyo alipotoka, akaingia tena yule afisa aliyekuja mwanzoni. Saa hii alikuwa na bahasha nyingine. Alimkabidhi mpelelezi akamwambia kuwa hiyo ni taarifa kuhusu kesi ya mauaji ya Afisa Parker, nayo taarifa ilikuwa imetoka kwenye kitengo cha 'CCTV Surveillance'.

Kitengo hicho kilikuwa kimepewa jukumu la kutafuta chochote kile kinachohusiana na kesi ya mauaji ya Afisa Parker. Taarifa ambayo mpelelezi alikuwa anataka kuiwianisha na ile aliyoipata toka kwa majirani kuhusu wageni wanaotuhumiwa kufanya mauaji ya afisa huyo nyumbani kwake.

Zilikuwa ni picha kadhaa za gari lililohusika, picha ambazo kwake hazikuwa ngeni, alishazipitia nyingizo, lakini miongoni mwa picha hizo, kuna moja ilimvutia zaidi.

Ilikuwa ndiyo picha pekee ya karibu kushinda zote. Aliitazama picha hii kwa umakini akaona kivuli cha uso wa dereva wa gari lile lililohusika na mauaji.

Sura haikuwa wazi lakini alipata kitu zaidi. Umbo la kichwa na mabega ya aliyekuwa anaendesha yalionyesha jinsia ya kiume na pia mtindo wake wa nywele ulionekana.

Aliichukua picha hiyo akaigundisha kwenye ubao wake mdogo kwa kutumia pini, kisha akampigia simu mtaalamu wa michoro ndani ya kitengo hicho cha polisi.

Alimwambia mtaalamu huyo afike haraka katika ofisi yake. Ndani ya sekunde chache, bwana akafika. Alikuwa ni mtu mwenye makamo ya miaka arobaini. Mwanaume mwenye nywele nyeusi na nyeupe zilizojiviringita.

Alimsihi aitazame ile picha ubaoni na kisha askilize maelezo ya majirani kuhusu mtu waliyemuona kisha amtengenezee picha yenye walau ukaribu wa utambulisho wake.

Wataalamu hawa huwa wanatumika pale ambapo hamna namna yoyote ya kupata picha muhimu za mnato kumuhusu mhusika ila maelezo yao yapo kwa kupitia kauli za washuhudiaji.

Picha hizo zinazotengenezwa angalau hutoa nafasi ama mahali pa kuanzia endapo zikiwa na ukaribu wa angalau asilimia sabini na mhusika mwenyewe.

Basi wakati mtaalamu akiwa anachukua taarifa muhimu, Mpelelezi alijiveka koti lake akatoka ndani ya ofisi.

Alijiweka kwenye gari lake kisha akatimka kuelekea magharibi mwa eneo walilopo. Alikuwa amedhamiria kufika eneo lile ambalo wahusika wake wa mauaji ya The DL walishukia wakitoka kwenye usafiri wa uber.

Alipofika hapo, majira haya palikuwa na shughuli nyingi, watu wakikatiza huku na kule kila mtu na mambo yake.

Alipakagua kwa macho yake ya stadi, akasogelea moja ya fremu kubwa ya duka inayopatikana eneo hili.

Ndani alikutana na mwanaume na mwanamke mzee ambao ndo' wamiliki na wauzaji. Walimkaribisha na kumuuliza namna gani ya kumsaidia, bwana huyo akasema anahitaji rekodi ya kamera yao ya nje, kuna tukio muhimu anadhani huenda likawa limenaswa na macho hayo ya teknolojia.

Bila hiyana walimpatia.

Alifanya hivyo kwenye maduka kama matano ambayo aliyabahatisha kuwa na kamera za uangalizi.

Kwa mwenendo wa kamera hizo, akiunganisha matukio na hatua ya walengwa wake, alijikuta anamini kabisa kuwa wahusika walielekea kwenye jengo kubwa la kifahari la Halletts Point!

Hayo ndo' yalikuwa makazi ya watuhumiwa wa mauaji yaliyotokea The DL.

Kwa msaada wa data za kamera za barabarani, na hizi alizopata toka kwa watu binafsi, hatimaye kiu yake ya taarifa ilikata.

Alitabasamu akilitazama jengo hilo kubwa la kuvutia.

Akiwa anafanya yote haya, kuna mtu alikuwa anahakikisha anapata picha ya kila kitu kinachoendelea. Kila hatua aliyokuwa anaipiga bwana huyo na kila aliyekuwa anaongea naye.

Mtu huyo, mpiga picha, alikuwa ndiye yuleyule aliyefanya kazi hii kulekule kwenye makazi ya Afisa Parker wakati mpelelezi akifanya kazi yake ya uchunguzi.

Alizitazama picha zake na alipoona kila kitu ni chema, alipotea
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.


Na Steve B.S.M


Sehemu ya Nane.



Brooklyn, New York.


Saa saba ya mchana



Richie alimtazama Hilda akajikuta anatabasamu mwenyewe. Moyo wake ulikuwa unahisi baridi kumwona mwanamke huyu, lakini zaidi kumwona hapa nyumbani kwake. Ilikuwa ni jambo maalum kabisa.

Alikuwa jikoni anakaanga mayai lakini kila saa akichungulia mlango kumtazama Hilda aliyekuwa ameketi kwenye kochi kwa ustaarabu.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia blauzi ya pinki yenye maneno yanayometameta kifuani. Chini alivalia 'tight' nyeusi iliyoishia juu kidogo ya enka zake.

Macho yake ndani ya miwani yalikuwa yako bize na runinga. Mchezo mzuri wa basketball ulikuwa unarushwa hapo. Aliutazama kila hatua muda mwingine akitupa mikono yake kiushabiki. Wazi timu yake pendwa ilikuwa inacheza muda huu.

Richie, aliyekuwa amevalia apron nyeusi yenye pichapicha za matunda mbalimbali, hakuishiwa hamu ya kumtazama mwanamke huyo. Kwake alikuwa mpya. Kitendo cha kumwona akiwa mbali na nguo anazoshindia kazini kilimvutia macho yake.

Kuna muda alikutana na Hilda uso kwa uso akatabasamu, lakini mara nyingi, alipokuwa akitazama, alimkuta mwanamke huyo amekunjia shingo runingani.

Yai lilipoiva, aliliweka kwenye sahani pana aliyoitoa kwenye kabati dogo la vyombo.

Alitoa juisi kwenye jokofu lake la mlango wa mmoja, akaimiminia kwenye glasi kubwa aliyoambatanisha pamoja na sahani ile yenye yai.

Alitembea kuelekea sebuleni akiwa anatabasamu, naye Hilda alimpokea kwa tabasamu pana akitazama sahani anayoletewa. Ilikuwa imesheheni mayai. Ukitazama kwa harakaharaka yalikaangwa kama mayai kumi hivi.

Hilda alijawa na mate mdomoni. Alitazama juisi pia, akajikuta mdomo wake unakuwa mkavu ghafla. Tumbo lilimnguruma.

"Utaniwia radhi, hiki ndo kitu nachoweza kupika," Richie alisema akiweka sahani na glasi juu ya kistuli kidogo. Hilda alimpongeza kwa kuwa mpishi mzuri japokuwa bado hakuonja. Aliamini kwa macho tu, chakula kile kilikuwa kitamu. Hakujua aliyasema hayo tokea kichwani au tumboni.

Aliponawa, alifakamia chakula hicho kwa upesi kana kwamba mtu aliyebanwa na njaa kali. Alisahau kabisa ule mchezo kwenye runinga. Alihangaika kuhudumia tumbo lake kwanza kabla ya yote.

Ukimtazama namna anavyokula, huwezi uliza kwanini mwili wake ni kipipa.

Richie alikuwa amelenga kula, mikono yake ilikuwa inachuruza maji aliyotoka kunawa, lakini alivyomuona Hilda namna alavyo, aliamua kusitisha.

Alikaa pembeni akimtazama mwamke huyo namna anavyofurahia chakula cha mikono yake, akajikuta anatabasamu mara kwa mara. Japo hakula lakini aliridhika.

"Wuuuuuuu!" Hilda alipiga kelele. Alinyanyua glasi yake akaimalizia juisi alafu akabeua. "Nimeshiba!" Aliutupia mwili wake mzito kwenye kochi akashusha pumzi ndefu.

"Ahsante, Richie. Nimependa chakula chako na nimeshiba."

Richiw alitabasamu kushukuru. Alitoa vyombo akavipeleka jikoni. Alivua nguo yake ya upishi kisha akaketi kwenye kochi moja na Hilda.

Hakujua kwanini ila moyo wake ulikuwa unamdunda sana. Mara kadhaa aliyakuta macho yake kwenye mapaja ya Hilda asijue yamefikaje.

"Richie," Hilda aliita. Bado mwili wake ulikuwa umeegamia kochi. Yuko hoi kwa shibe. "Uliniitia wito gani hapa kwako? maana si kwa vile ulivyonisisitiza." aliuliza akimtazama Richie kwa mbali ndani ya vioo vyake vya macho.

Richie alitazama kando kidogo akifikiria. Alitaka awe makini na mdomo wake. Alitazama ni namna gani anaweza akaunganisha ubongo wake na ulimi.

"Hilda, hamna jambo kubwa kama unavyotarajia. Leo ni weekend. Mara nyingi nakuwa mpweke hapa nyumbani. Nilifikiria tu huenda ungenipa kampani."

Hilda alibinua mdomo wake. Hakuona kama kuna tatizo kuwepo hapo. Kwakuwa Richie alinyamaza, basi yeye aliendelea kutazama runinga, wakati huo bwana huyo akiendelea kumtazama.

Kuna jambo lilikuwa limemjaa kifuani. Macho yake yalisema wazi.

Baada ya muda kidogo, vijisekunde vichache, alimuuliza Hilda kuhusu usiku ule. Usiku ambao alimwacha kazini mpaka muda mbaya akisema kuna kazi anafanya.

Hilda alimtazama mwanaume kidogo kisha akaendelea na mambo yake. Hakuona jambo kubwa. Alimjibu Richie kwamba alikaa hapo kazini mpaka majira ya saa nne usiku kisha akaondoka zake.

"Saa nne?"

"Ndio."

Kwanini unanidanganya Hilda? Richie aliuliza kifuani mwake akimtazama Hilda. Ni lini utaona sahihi kuniambia ukweli? Aliumia na nafsi yake.

Alitaka kuongea zaidi lakini mdomo wake ulisita. Aliamini ni stara akiendelea kunyamaza huku akingoja muda sahihi utakapowadia.

Kwa sasa alikata shauri, hakutaka shari. Alidhamiria kuutumia muda huu kufurahi na mwanamke huyo kadiri atakavyoweza, kwa kile kidogo alichokidhamiria na kukipanga.

Alitabasamu mwenyewe kwa yale aliyoyaona kichwani mwake.

"Hilda." aliita kwa sauti tulivu. Hilda aligeuza shingo akamtazama .

"Kuna kitu kizuri nimekuandalia, natumai utafurahi."

Hilda alitabasamu kabla hajajua kitu hicho. Alikaa vizuri akamtazama Richie kwa macho ya hamu. Macho hayo yalitatiza nafsi ya Richie.

"Ni nini hiko?"

Richie hakusema kitu. Akiwa anamtazama Hilda machoni, aliingiza mkono yake mfuko wa kulia wa suruali, akatoa karatasi mbili ndogo zenye rangi nyekundu.

Zilikuwa ni tiketi za sinema. Tena kwa filamu ya moto iliyotoka hivi karibuni. Hilda alipobaini hilo aliachama kwa furaha, akamkumbatia Richie kwanguvu.

"Umejuaje nilikuwa nataka nikatazame filamu hii?"

Richie akiwa amejawa na furaha, ameizungusha mikono yake katika kiuno kinene cha Hilda, alimwambia kwa kujivunia kuwa alimwona akiwa anatazama 'trailer' ya filamu hiyo mara kwa mara akiwa ofisini, hapo akajua anaipenda.

Hilda alifurahi kusikia hilo. Alimshika akambusu Richie shavuni. Macho yawe yalijawa na raha. Alitazama tiketi yake kana kwamba mtu asiyeamini anachoona. Alirusha kiganja chake kama mtu aliyeungua na moto.

Furaha hii haikudumu muda mrefu, ni punde, simu ya Hilda iliyokuwepo mezani, ilitetemeka ikiita. Wa kwanza kuitazama alikuwa ni Richie. Kwenye kioo lilitokea jina la 'Boss Bryson'.

Hilda alipokea simu hiyo upesi. Aliongea maneno machache kisha akasema sawa, nipo njiani.

Aliweka simu yake kwenye kijibegi chake cheusi kisha akamuaga Richie. Anaondoka amepata dharura.

"Vipi kuhusu sinema?"

"Haitawezekana leo, Richie. Inabidi niende. Ni muhimu!"

Ni muhimu? Richie alisema na nafsi yake akimtazama Hilda namna anavyoweweseka kuvaa viatu ajiondoe eneo hili.

"Lakini leo ni weekend, Hilda!" Alilalama. Shingo yake aliiweka upande, mkononi ameshikilia tiketi.

"Kwahiyo nikatae wito wa boss? ... Natumai unamjua vizuri, sina haja ya kujieleza."

Richie aling'ata meno akishuhudia mwanamke huyo anaondoka. Moyo ulisinyaa. Mambo yalibadilika ghafla mbele ya macho yake katika namna ambayo hakuamini!

Aliketi kwenye kochi akatazama tiketi aliyoshikilia mkononi. Chozi lilimlenga. Alichanachana tiketi hiyo kwa hasira kisha akajilaza hapo akitazama dari.

Kwanini lakini, Bryson? ... Kwanini leo?

Alisikia kitu kinateremka toka jicho lake la kulia.



***


Queens, New York.


Saa tatu ya usiku.



Bwana aliyekuwa amevalia kofia ya kahawia aina ya panama yenye riboni nyeusi, alikuwa ndani ya gari dogo lililogeshwa pembezoni mwa barabara akiwa anatazama jambo.

Bwana huyo alivalia sweta kola ya V, rangi ya kijivu iliyokolea. Ndani ya sweta hilo alivalia shati drafti, rangi nyeusi na nyeupe. Mkononi mwake ameshikilia kamera.

Uso wake haukuonekana vema sababu ya kofia aloivaa. Kofia hiyo aliishusha chini, na kwasababu ya udumavu wa mwanga kwenye gari hili, kivuli cheusi kilimeza sura yake isionekane inavyotakiwa.

Uso wa bwana huyu ulikuwa umegeukia kutazama jengo kubwa lililopo mkabala na hapa alipoegeshea gari.

Jengo hilo lilikuwa ni maarufu sana kwa michezo mbalimbali ya kamari katika jiji hili la New York, kwa jina; Resorts World Casino.

Katika mwisho huu wa wiki, watu maelfu na mamia walikuwepo hapo wakitumia pesa zao kwa kadiri waonavyo ni sawa. Palikuwa na magari pomoni, lakini miongoni mwa yote hayo bado halikufika lile ambalo bwana huyu ndani ya gari alikuwa analingoja.

Aliendelea kutazama. Muda fulani ulipita lakini hakuchoka. Kidogo, gari liliingia katika eneo hilo, akalisindikiza kwa kichwa chake. Alinyanyua mkono wake wenye kamera akalinasa gari hilo kwa picha kadhaa mpaka pale lilipojiegesha sehemu maalumu ya kumbi ile ya starehe.

Alitulia kidogo akitazama. Aliposhuka mtu ndani ya gari, akaendelea na zoezi lake la upigaji picha kwa mfululizo mpaka mtu huyo aliyekuwa amevalia kwa unadhifu alipozama ndani ya jengo la Resorts Casino.

Alipiga simu akasema, "ameshafika."

Alitoa maelezo ya namna bwana yule aliyemchukua picha alivyokuwa amevaa kisha akakata simu na kuiweka mfukoni.

Alilaza kiti cha gari, akajilaza humo kizani.

Ndani ya muda mfupi, kule kwenye maegesho ya magari, alishuka mwanaume mmoja alyevalia suti nyeusi. Alikuwa mnadhifu sana kuanzia nywele mpaka miguuni, na gari lake lilikuwa Chevrolet ya gharama, rangi nyeusi.

Aliingia ndani ya jengo hilo, akikaribishwa vema na wahudumu wa kike waliovalia matabasamu yao bora, sare zilizobana na sauti mwanana.

Ndani palikuwa pakubwa. Pamejaa mashine mamia za michezo. Meza za kutosha kwa ajili ya yeyote kujichagulia mchezo autakao lakini mbali na ukubwa huo bado watu walifurika wakafanya eneo hilo kuwa finyu. Miongoni mwa watu hao alikuwa ni Mpelelezi.

Alivalia shati jeupe lenye kola fupi. Suruali nyeusi ya kitambaa aliyoichomekea juu kidogo ya kiuno.

Alikuwa ameketi mahali sahihi kwake. Meza kubwa iliyowapa fursa ya watu nane waliokuwa wanacheza kamari kujinafasi. Miongoni mwao watatu walikuwa ni wanawake ambao si wachezaji bali wapo sambamba na wachezaji ili kuwapa kampani.

Walikuwa warembo waliojipamba haswa. Nyuso zao zilikandikwa 'make up' zikavutia mithili ya waridi lililostawi. Nywele maridadi, midomo mekundu, ngozi zao nyororo na nguo zao holela. Walikuwa wanavutia kuwatazama kila saa.

Mpelelezi alicheza mizunguko kadhaa akionyesha umaridadi wake mchezoni. Alishinda michezo miwili ya mwanzoni lakini akapoteza mitatu iliyofuatia ambayo wenzake waligawana ngwe hizo.

Kwa ustadi mkubwa, alizirusha kete zake akashinda mchezo uliofuatia. Na tena unaofuatia. Katika wale wanaume watano, wawili wakaacha kucheza. Walishatumia vya kutosha. Kwenye uwanja wakabakia Mpelelezi na mwanaume mmoja mnene aliyekuwa anapewa kampani na mwanamke pembeni.

Bwana huyo alikuwa na asili ya kiashia. Macho madogo. Nywele zake fupi. Shingoni ana mikufu kadhaa ya dhahabu. Mikononi ana bangili na pete za gharama.

Aliweka dau kubwa mezani akamsihi Mpelelezi waende kikubwa. Atakayeshinda, abebe pesa ya maana. Mpelelezi, pasipo na kufikiri sana, aliridhia ombi hilo akitabasamu lakini walikubaliana kuwa wataenda mikupuo mitatu. Atakayeshinda mikupuo miwili basi atabeba kila kilichopo mezani.

Mchezo ukaanza. Ilikuwa ni mwendo mchezo na pombe. Wahudumu waliokuwa wanapita kila saa walihakikisha watu hawapungukiwi na cha kukatia kitu zao. Glasi kwa glasi

Mkupuo wa kwanza ulienda kwa upesi, bwana yule mnene akashinda. Alitabasamu kwa dharau huku akikandwakandwa mabega na mwanamke aliyepembezoni yake.

Walicheza tena mkupuo wa pili, huu nao bwana huyo akashinda. Alitanua mikono yake akivuta pesa iliyowekwa mezani. Alifanya hivyo akiwa anacheka kicheko kisichofungua mdomo.

Alimtazama mshindani wake akamuuliza kama angetaka kuendelea.

"Una ulichobakiza?"

Mpelelezi alitafakari kwanza. Yote aliyokuwa ameyavuna kwenye mchezo uliopita, vilishayoyoma. Alibakiwa na pesa ya ziada tu katika pochi yake.

Alitafakari akitazama pesa zile zilivyonyingi upande wa yule bwana. Akakata shauri. Alitaka kucheza tena.

"Sina pesa nyingi, lakini kuna nilichokibakiza. Unaonaje sasa kila mmoja akachezesha chote alichonacho. All or Nothing."

Bwana yule mnene alitabasamu kiupande akikuna kidevu chake cheupe. Alimuuliza Mpelelezi kama ana uhakika na anachotaka kukifanya, alipopata uthibitisho, basi akaridhia.

Alisukumizia pesa katikati ya meza kisha akampatia Mpelelezi nafasi ya kwanza ya kucheza.

"Hapana. Wewe ndiye mshindi. Anza, tafadhali," Mpelelezi alisihi. Bwana yule akaanza.

Alitupa mkupuo wake wa dhahabu, akapata alama za juu! Alicheka kwa furaha akimtazama mrembo wake ambaye naye alicheka pasipo kuelewa kitu. Ushindi ulikuwa unanukia.

Mpelelezi alishika kete zake akiwa ana mkazo kiasi. Uso wake aliukunja akijaribu kuomba mungu wa bahati awe upande wake. Kwa namna mwenziwe alivyopata basi naye apate zaidi japo nafasi ilikuwa finyu.

Mshindani wake alikuwa ameacha pointi moja tu, tano kati ya sita. Hivyo ili ashinde hakupaswa kupata yoyote isipokuwa sita ya sita!

Alishusha pumzi ndogo akiwa ameshika kete yake mkononi. Akili yake yote ilikuwa hapo. Alirusha kete hizo kwa namna zote anavyojua, zilipotua, amini usiamini, akawa amepata alama zote!

Alifurahi mno. Alitoa kicheko kikubwa cha ushindi akitikisa ngumi za mikono yake. Upande wa pili, yule bwana hakuwa anaelewa nini kilichotokea. Hakuamini macho yake. Alimtazama mwanamke aliyekuwa naye kwa macho ya hasira, mwanamke yule akahofia. Upesi alitoa mikono yake mabegani mwa mwanaume huyo.

Mpelelezi alizikusanya pesa zake akiwa na tabasamu pana. Zilikuwa ni mlima wa noti kadha wa kadha. Alizikunja vema pesa hizo akiwa anapiga mluzi taratibu. Alikuwa na furaha sana.

Akiwa anafanya zoezi hili, mwanaume yule mnene alikuwa anamtazama kwa macho ya ghadhabu. Aliona amedhulumiwa. Aliomba mchezo uendelee lakini mpelelezi hakuwa tayari.

"Inatosha kwa leo. Labda siku nyingine tukibahatika kuonana."

Hakutaka kungoja. Vishawishi ni vingi. Alitunza pesa zake akaaga. Alitoka kwenye ukumbi huo wa kuchezea kamari, kabla hajaenda nje, alipitia chooni apate kujisaidia kwani pombe alizokunywa zilikuwa zinasumbua kibofu.

Alipotoka chooni, kwenye korido nyembamba, alikutana na bwana yule mnene akiwa na wenzake wanne. Wanaume hawa, jumla watano kwa idadi, walikuwa ndo' walewale waliokuwa na mpelelezi huyu katika meza ya kamari.

Kumbe wote walikuwa wamoja.

Bwana yule mnene alimwambia Mpelelezi arejeshe fedha zake zote na riba juu kama alitaka kutoka na uhai wake katika hilo jengo.

Wanaume wengine waliokuwa wanakuja na kutoka chooni waliwapita kana kwamba hawaoni kitu. Kila mmoja alikuwa ameshika zake. Wengine ndo' kwanza walitembea kwa kasi kujiepushia mabalaa.

"Tulicheza kwa kuridhia, sivyo? Hiyo pesa unayoongelea imetokea wapi?"

Bwana yule mnene hakuongeza tena neno. Kwa ishara ya kichwa aliamuru mpelelezi avamiwe mara moja. Kufumba na kufumbua watu wanne wakamfuata kwa shari!

Alijitahidi kuwamudu kimapigano. Alitumia mikono, miguu na kichwa chake kujitetea kadiri alivyoweza lakini watu wale walikuwa wengi kwa idadi. Japo aliwamudu lakini hakudumu kwa muda mrefu akaanza kuzidiwa.

Aliporusha ngumi moja, alipigwa tatu. Mmoja alimkandika teke la tumbo akaanguka chini mithili ya kiroba. Alihisi maumivu makali sana.

Alishika tumbo lake akikunja uso.

Hakupewa muda wa kupumzika, mabwana wakamfuata tena. Kabla hawajamgusa, sauti kali ilifoka nyuma yao;

"Heeey!"

Walitazama wakamwona bwana alliyevalia suti nyeusi iliyomkaa vema mwilini. Bwana huyo alikuwa amesimama kiukakamavu akiwatazama hawa mabwanyenye kwa macho makali.

Sura yake ilikuwa mithili ya mtoto, laini isiyokuwa na ndevu. Mdomo wake ulikuwa mdogo kidevu chake kikichongoka. Masikio yake mapana, nywele zake nyeusi zimeficha paji lake la uso.

"Unataka kufa?" Aliuliza bonge akimsogelea. "Ukishindwa kufuata mambo yako, basi utalifuata kaburi."

Bwana yule ndani ya suti alimtazama Mpelelezi akapaza sauti kumuuliza kama yuko salama. Mpelelezi alimwonyeshea dole gumba akijitahidi kusimama.

Ghafla wale mabwana walimvamia yule mgeni lakini wote walilambishwa sakafu ndani ya sekunde chache. Kila mmoja alilala akiugulia maumivu. Hawajiwezi.

Bwana yule alimpa pole Mpelelezi alafu akamuaga.

"Ngoja kwanza, ndugu yangu," Mpelelezi alimsihi. Alimshukuru kwa kumsaidia lakini alitaka kumfahamu bwana huyo ni nani haswa. Aliamini hakuwa raia wa kawaida. Namna alivyowamaliza watesi wake kulimpa maswali.

"Mimi ni mtu wa sanaa za mapigano," bwana huyo alisema na kuongezea, "natumai upo salama."

Walibadilishana namba kila mtu akashika njia yake.

Mpelelezi alifuata usafiri wake alipoupaki, akiwa anaugulia maumivu, alijiweka humo akakagua kwanza pesa yake. Zote zilikuwa salama salmini.

Alitabasamu.

Kabla hajawasha gari aondoke, alihisi kichwa kuwa kizito. Macho yalijenga ukungu na mwili ulipoteza nguvu.

Alijitahidi kuwasha gari lakini hakuweza kuweka gia aondoke. Alipoteza fahamu.



***
 
[emoji91] BONUS PART [emoji91]

Halletts Point, New York.

Saa moja ya asubuhi


"Kwahiyo tunafanyaje?" Ferdinand aliuliza akimtazama Mitchelle kwa macho ya udadisi. Mitchelle alikuwa ameketi akiuegeshea mguu mmoja juu ya mwingine. Macho yake yalikuwa yanatazama meza lakini akiwa mbali kifikra.

Mwili wake ulikuwa ndani ya gauni jeupe mithili ya taulo. Nywele zake zimefungwa na kitambaa cha sufi kilichotengeneza mlima kichwani.

Bwana Ferdinand yeye alikuwa amevalia tisheti ya Hawaii na bukta ya kimichezo iliyoacha wazi miguu yake yenye vinyweleo lukuki.

Waliketi hapa wakipata kifungua kinywa. Mitchelle alikuwa anakunywa kahawa bora aliyoandaliwa na Jennifer. Ferdinand alikuwa anakunywa sharubati ya malimao. Aliamini ina afya zaidi ukiipata asubuhi kabla ya mengine.

Mitchelle alikunywa kahawa yake mafundo mawili ya mkupuo. Alimtazama Ferdinand kwa macho ya ndani akamuuliza kuhusu ile kazi aliyompatia. Kazi ya kusanifu wanausalama waliokuwa wanahusika na kesi ya The DL.

Japo Feridinand alishawahi kumgusia awali lakini leo alitaka kusikia tena jambo hili.

"Natumai nilikamilisha kila jambo," Ferdinand alisema kwa kujiamini. "Kama nilivyokupatia taarifa, mpelelezi hakufanikiwa kupata chochote cha maana. Kielelezo pekee alichokuwa nacho ni sura yangu tu lakini hakuna taarifa yotote anayoweza kuipata, unajua hilo."

Mitchelle alitaka kujua zaidi lakini Ferdinand alimwambia hakuna kingine cha ziada. Mshirika wa mpelelezi katika kesi yao, Afisa Parker, alishafariki. Mpelelezi anaweza akashikilia jambo hili kwa muda fulani lakini mwisho wa siku atafunga mjadala kwa kutopata ushahidi.

"Naamini tukiwa low, hii kesi baada ya muda itakwisha," alimalizia Ferdinand kisha akanywa kinywaji chake.

Alipotazama alikutana uso kwa uso na Mitchelle. Mwanamke huyo alikuwa anamtazama kwa macho ya mashaka.

"Ferdinand, huoni hii kesi ndo' kwanza inaanza?"

"Enh?"

"Kitendo cha sura yako kuonekana kwenye runinga, ulikuwa ndo' mwisho wa usalama wetu. Unafahamu kuwa tumeishi kwa usalama kwa muda mrefu sababu ya kutokufahamika kama tuko hai. Sasa hiyo kinga hatunayo tena. Zoezi hili halitakoma mpaka pale tutakapotokomezwa kwenye uso wa dunia."

Ferdinand alitulia kimya akitafakari. Mitchelle alitazama kando, uso wake ukidhihirisha namna gani alivyomezwa na tafakuri. Aliporejea kwenye kikombe chake cha kahawa, alishapata cha kunena.

"Mchezo umeshaanza Ferdy. Huoni? Hata kama hatukutaka kuucheza, sasa hatuna namna tena."

Mitchelle alipohakikisha kikombe chake cha kahawa kimeisha, alishusha pumzi akisikiliza akili yake namna inavyopanga mambo. Alitulia kwa kama sekunde kumi na tano hivi, hapa pakawa kimya. Aliacha ubongo wake uzungumze wakati mdomo wake ukiwa umefunga.

"Wameshatutangulia hatua mbele," Mitchelle alimwambia mwenziwe pasipo kumtazama. "Tukiruhusu waongeze hatua moja tu ya ziada, tumekwisha."

Ferdinand bado alikuwa gizani. Hakupata maana halisi ya Mitchelle. Aljaribu kutuliza kichwa chake akingoja kauli toka kwenye kinywa cha mwanamke huyu. Kauli ambayo ilikuwa inakuja kila baada ya ukimya fulani.

Mitchelle, kwa kile alichoamini kichwani mwake, mauaji ya Afisa Parker yalikuwa ni ya kimkakati. Kitendo cha afisa huyo mwenye mahusiano na kesi ya The DL kuuawa kisha kutelekezwa mbele ya hadhira halikuwa jambo la bahati mbaya.

Kwa namna nyepesi tu, jambo hilo litarudi kwenye kesi aliyokuwa anaishughulikia muda mfupi kabla ya kupoteza uhai wake, hivyo watuhumiwa wa kesi ya The DL watakuwa kipaumbele.

"Lakini Mitchelle," Ferdinand alitia neno. "Hamna ushahidi wowote wa kutuhusisha sisi na tukio hilo."

"Ferdy, hatujui adui yetu amebeba zana gani kwenye mkoba wake. Hamna mtu atakeyefaidika na kifo cha Afisa Parker zaidi ya mtu anayetuhitaji. Kwa kifo hiki, na namna ambavyo kilivyofanyika, kila mtu atakiri kuwa wahusika ni wakufunzi hatari wanaotakiwa kuchukuliwa hatua mara moja!"

"Na hapo ndipo The System itakapoingia," Ferdinand alimalizia, Mitchelle akatikisa kichwa.

"Lakini vipi kuhusu mpelelezi? Hawatamuua pia?"

"Hawana haja hiyo. Ni mtu wa karibu zaidi na kesi hii kuliko yeyote yule. Mauaji ya Afisa Parker ni kwaajili yake huyu. Huu ndo' mlango. Wakifanikiwa kushika hiki kitasa basi kila kitu kitaisha kwa urahisi bila kutengeneza 'attention' kubwa kwa watu.

Kwa kupitia mdomo wa Mpelelezi huyu kuhusu mwenendo wa kesi ya The DL kwenye vyombo vya habari, tutageuka kuwa adui kwa watu na kwa serikali. Hakutakuwa na wakili upande wetu. Hapo uwanja utabakia baina yetu, tukiwa peke yetu, na wao wakiwa na kila kitu nyuma yao."

Mitchelle alimalizia kwa kusema;

"Kamari ipo kwa Mpelelezi huyu "

Ferdinad akalirudia swali lake, "Kwahiyo tunafanyaje?"

"Ni swala muda tu kabla hawajaanika taarifa zangu," Mitchelle alimwambia wakitazamana. "Wanajua ni mimi nipo na wewe lakini lazima watafutie pa kuanzia. Lazima wapate sababu ya kufanya oparesheni yao kwa amani na kisheria, na mimi ndo' lengo lao kuu."

"Unamaanisha nini?"

"Ferdinand, kama kuuawa ungeshakuwa umekufa hivi sasa. Unadhani hawafahamu kuwa mwili wako unahimili risasi?"

"Lakini yule bwana alisema ametumwa kuniua."

"Lakini matendo yake hayakuonyesha hilo, Ferdinand. Kupigwa kwako risasi yaweza kuwa ujumbe au chochote kile lakini sio kwa kukumaliza. Hili linamaanisha uhai wako una faida kwao kuliko kifo chako. Hatujajua ni faida gani hiyo, pengine ni kunikamata mimi!"

"Sawa, Mitchelle. Sasa tunafanyaje?"

"Sasa inabidi ufe."

"Nini?"

"Inabidi ufe, Ferdinand. Kifo chako kitatibua mipango waliyonayo mezani."


***
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 09


Na Steve B.S.M



New York Police Department, New York.


Saa tano ya asubuhi.


Mpelelezi alikuwa anahisi maumivu ya kichwa. Alifungua kikopo kidogo chenye vidonge vingi vyeupe ndani yake, akajiwekea vidonge vitatu kwenye kiganja chake na kuvibugia bila maji.

Tangu asubuhi ya mapema mpaka sasa, alishakunywa vidonge vinne vya kukata maumivu. Kichwa kilikuwa kinapoa na kurudi tena kwenye makali yake.

Akiwa amekaa, nguo alizovalia ni zilezile alizokuwa nazo kwenye kumbi ya kamari jana yake, alishika paji lake la uso akilijaribu kulikandakanda na vidole viwili, gumba na kinachofuatia.

Alijaribu kukumbuka nini kilitokea lakini hakupata picha kamili. Kitu pekee alichokumbuka ipasavyo ni yale yote yaliyoishia pale alipopanda gari lake tu. Baada ya hapo alikuja kukurupuka asubuhi baada ya kugongewa kioo na mtu anayehusika na 'parking'.

Kichwa chake, alichokuwa anahisi ni kizito, hakikumpa majibu aliyokuwa anataka. Baada ya kufikiri sana aliona ni bure. Aliamini mapigano yale, baina yake na wacheza kamari, ndiyo yalimuathiri kiasi cha kujikuta anapoteza fahamu.

Alijinyoosha mwili akiugulia maumivu ya viungo. Alishika simu yake akitazama jambo, punde mtu akaingia. Alikuwa ni yule bwana, mtaalamu wa michoro. Mkononi mwake ameshikilia bahasha.

Walipeana salamu kisha bwana huyo akampatia Mpelelezi bahasha ile alokuja nayo akimwambia ni ile kazi alompatia.

"Nadhani itasaidia kwenye upelelezi," bwana huyo alisema kisha akajiendea zake.

Ndani ya bahasha kulikuwa na karatasi tatu. Karatasi moja ilikuwa na mchoro halisi, uliochorwa kwa penseli ya mkaa, wakati zingine mbili zikiwa ni nakala vivuli.

Mpelelezi alitazama michoro hiyo kwa umakini, kwa kama dakika mbili hivi, kisha akavuta droo ya meza yake alimotoa bahasha moja yenye picha mbili.

Picha za Ferdinand.

Aliwianisha picha hizo kwa macho yake ya kazi.

Aliona kuna uwiano ndani yake.

Mabega ya mhusika, mtindo wake wa nywele na hata umbo la fuvu la sura yake vilikuwa vinafanana. Kwa sura ilikuwa ni wastani, ila umbo hili la mwili lilikuwa ni sawa sawia.

Aliziweka picha hizo mezani akiwaza jambo la kufanya.

Kichwa kilimuuma. Kila alipojifikirisha aliona anayatibua maumivu. Alitazama saa yake ya mkononi. Alikata shauri kwenda kujipumzisha.

Aliweka vitu vyake vizuri ndani ya droo alilolifunga na funguo baada ya kuvipiga picha na simu yake kisha akanyanyuka kiuzito toka kitini.

Hajapiga hatua, simu yake iliita. Alikuwa mtu wa kitengo cha taarifa na uchambuzi. Alimwambia ana taarifa kuhusu ile picha ya mwanamke alompatia.

"Njoo ofisini," Mpelelezi alisema akirejea kitini. Muda kidogo, mgeni wake alifika hapo. Alikuwa ni yuleyule aliyepewa kazi hiyo, afisa mnene anayevaliwa miwani.

Alimweleza mpelelezi kuwa picha ile ilikuwa ni ya binti wa huko California. Mwanafunzi wa chuo ambaye aliwahi kujimaliza uhai kwa kujinyonga miaka miwili iliyopita.

"Alijinyonga?" Mpelelezi alirudia kwa kuuliza.

"Ndio," alijibu bwana huyo kwa uhakika. "Kwa mujibu wa taarifa, alikuwa anasumbuliwa na sonona."

"Sonona?"

"Hakuwa mtu wa marafiki. Alikuwa anaishi peke yake. Muda mwingi alikuwa mpweke hata kwenye mazingira ya watu wengi darasani."

Mpelelezi aliitazama ile picha kwa kuirudia. Alimsihi afisa huyo aendelee kutafuta taarifa zaidi kumhusu huyo mtu. Endapo akipata familia au watu wake wa karibu itapendeza zaidi.

"Sawa, nitajitahidi," alisema bwana huyo akaaga. Kidogo mpelelezi akawa amesahau dhamira yake ya kuondoka. Alipata cha kuwaza. Alijiuliza nini mahusiano yaliyopo baina ya mwanamke yule anayemtafuta na huyu aliyejinyonga.

Kichwa tu kilimuuma.

Aliona ni kheri anakili taarifa hizi kwenye tarakilishi yake iliyokuwepo mezani, muda akili yake itakapotulia basi afanye jambo kwa umakini.

Akiwa ananakili, pia ameona atoe na zile taarifa kwenye droo apige picha na kutunza, simu yake iliita. Alikuwa ni mkuu wake wa kazi katika kitengo hichi cha upelelezi.

Alipokea akapewa taarifa kuwa anahitajika ofisini mwa mkuu maramoja. Aliacha kazi yake akaelekea huko.

Alifungua mlango wa kioo uliopachikwa cheo cha aliyekuwemo ndani: 'Chief of Detectives'. Macho yake yalitua kwa wageni wawili waliokuwa wamevalia suti nyeusi maridadi. Mmoja alikaa upande wa kushoto, mwingine akiwa amekaa upande wa kuume wa mkuu.

Kati ya watu hawa, mmoja hakuwa mgeni machoni mwake. Akili yake ilimwambia anamfahamu mtu huyo japo hakukumbuka alimwonea wapi.

Alisalimu kisha akaketi. Macho yalimtazama tena yule mwanaume ambaye si mgeni kisha yakahamia kwa mkuu wake, mwanaume wa makamo ya miaka hamsini, kichwa chake kina uwaraza mpana, nywele zikibakia juu ya masikio tu. Macho yake ya kahawia, uso wenye taya pana na sharubu nyeupe.

Mkuu alimtambulisha mpelelezi kuwa wale watu wawili walikuwa hapo ni wageni wake. Wapo hapo kwaajili ya kesi ya mauaji ya The DL.

Hakujua ni nini ila hapa ndo' Mpelelezi alijikuta anamkumbuka bwana yule aliyekuwa anamshuku anamfahamu muda wote huo.

Huyo bwana alikuwa ndiye yule aliyemsaidia kwenye mapigano kule kwenye ukumbi wa kamari.

Alimtazama tena.



SIKU YA NYUMA:


Gari 'tinted', aina ya Chevrolet Suburban nyeusi, iliyokuwa imeegeshwa katikati ya jiji la New York majira haya ya asubuhi, ilikuwa imebebelea watu watatu waliokuwa wamevalia suti nyeusi; mmoja alikuwa dereva, amekaa peke yake kiti cha mbele, wawili walikaa nyuma.

Kati ya hao wawili waliokuwa nyuma, mmoja wao hakuwa mgeni machoni petu. Kuna mahali tulipata kumwona.

Mwanaume huyo, kwa macho kamili, alimuarifu mwenziwe wa pembeni kwamba wamepata vielelezo vya kuanzia na amepanga ndani ya siku hiyo kuonana na mhusika uso kwa uso, ikiwezekana kufanya maandalizi ya makutano yao ya baadae.

Bwana yule mwingine wa pembeni, ambaye alikuwa mtulivu sana, mwanaume wa makamo ya miaka arobaini aliyevalia miwani isiyokuwa na fremu za kuonekana, macho yake ya kulegea yalikuwa yanatazama picha alizokabidhiwa.

Picha za Mpelelezi, akiwa katika mazingira tofautitofauti, zilikuwa pomoni, lakini pia picha kadhaa za Ferdinand.

Picha moja ilimwonyesha Ferdinand akiwa katika tukio lile la Afisa Parker kukutwa akiwa amekufa ndani ya gari mjini. Picha ya pili ilimwonyesha bwana huyo akiwa karibu na makazi ya Afisa Parker. Picha ya tatu ilimwonyesha akiwa karibu na moja ya kumbi za kamari.

Yule bwana, ambaye si mgeni, alieleza ya kwamba wakati wanamfuatilia Mpelelezi walibaini Ferdinand naye alikuwa kazini. Bila shaka alikuwa katika misheni inayohusu kesi yao ya The DL kwani wahusika alokuwa anawafuatilia ndo' wale wanaoshikilia kesi.

Lakini kwa tukio hilo, ilikuwa rahisi kumfuatilia bwana huyo, mara mbili, japo mara zote hizo hawakufanikiwa kubaini makazi yake halisi. Hawakufahamu namna alivyowapotea. Mara ya tatu, ndipo walitekeleza agizo la kumfyatulia risasi kama ilivyoamrishwa.

"Kulikuwa na haja gani ya kufanya vile?" Aliuliza bwana huyu aliyekuwa anatoa taarifa. Mwenziwe alimtazama kisha akaurudisha uso wake kwenye picha.

"Ni mbinu ya kumwondolea utimamu kwenye mipango yake," alijibu, akaongezea; "Shambulizi huathiri umakini wa mtu. Hatujui wamepanga nini. Kwa kupitia tukio hilo watajua wamefahamika hivyo watalazimika kuchukua hatua upesi. Upesi na uholela ni ndugu wa karibu. Tunategemea itakuwa kamari nzuri kuwapata wengine."

"Haudhani tukio hilo linaweza kuwafanya wakaongeza umakini kwenye kujificha?"

"Kati ya haya mawili, moja likifeli, lingine litazaa matunda ama yote kuzaa kwa wakati mmoja. Endapo wakiongeza umakini wakajificha zaidi, basi kazi ya mpelelezi itatupa nyavu. Kwa harakati zake, naamini kuna ambayo hatuyafahamu. Hicho ndo' tunakihitaji ... kwa picha hizi, ni rahisi kuaminika kuwa Ferdinand alihusika na mauaji ya Parker na pia kuthibitisha yu mbioni kumuua Mpelelezi."

Bwana huyo alimalizia kwa kutoa amri ya kazi, mwenziwe akashuka kwenda zake kisha yeye akaendelea kufanya pembuzi wa vile vyote alivyokuwa navyo mkononi.

Alishika 'microchip' na 'tube' yenye kimiminika cha kijani, akavitazama.

Vitu hivyo ndo' vile alivyopokonywa Ferdinand baada ya kupigwa risasi siku ile.

Alichomoa simu mfukoni mwake akapiga. Aliongea na simu hiyo gari likienda.


MUDA WA SASA:


Mpelelezi alitazama bahasha aliyokabidhiwa na mkuu wake wa kazi. Ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na picha za bwana Ferdinand, picha akiwa kwenye yale maeneo yanayoshukiwa kwa mauaji.

Akiwa anazitazama, mkuu wake alimweleza ya kwamba bwana huyo ndiye mhusika wa mauaji ya Afisa Parker na wageni hawa wamekuwa wakimfuatilia kwa muda sasa.

Aliamriwa kuwapatia mabwana hao yale yote aliyofanikiwa kujifunza kwenye kesi hiyo. Hilo ni agizo toka ngazi za juu za usalama.

Yaliongelewa mengi lakini Mpelelezi huyu alikuwa na maanani madogo sana. Mengine hakuyasikia. Mengine hakuyaelewa. Kichwa hakikuwa sawa. Kuna muda alihisi kelele tu masikioni. Alitamani muda uishe ajiendee zake.

"Mpelelezi, uko sawa?" aliuliza yule bwana mwenye uso mchanga. Mpelelezi alifunga macho yake kwanguvu akasema kichwa kinamsumbua kwa maumivu makali.

Katika hali hiyo, wale mabwana walisihi aweke sahihi kwenye makubaliano ya kazi ambayo walikuja nayo ili wapishe ratiba zingine kuendelea.

Kwa kutaka kupumzika, Mpelelezi aliridhia aliyoambiwa. Alipomaliza, alitoka akajiendea zake ofisini kwake alipokaa kwa muda mfupi kabla hajatoka kufuata gari lake.

Nje alikutana na yule bwana aliyempa mkono wa msaada jana yake usiku. Alikuwa amesimama kando ya gari yake akimngoja.

"Nimefurahi tumekutana tena," alisema bwana huyo kisha akatabasamu kwa mbali. "Natumai tutasaidiana na kwenye hili, sivyo?"

Mpelezi alimtazama bwana huyo kwa macho malegevu yenye uchovu. Alikuwa anajivuta akiufuata mlango wa gari lake

"Nilikuuliza wewe ni nani ukaniambia ni mwanasanaa wa mapigano."

"Unadhani pale palikuwa sehemu salama kueleza kazi yangu? Hata wewe usingeniambia kama ni mpelelezi!"

Mpelelezi alifungua mlango wa gari, bwana huyo akamzuia. Alimwambia hayupo katika hali nzuri ya kiafya, angeomba amsaidie kumwendesha kwenda nyumbani.

Mpelelezi alisita lakini kwa namna alivyokuwa anajisikia, na bwana yule akimsihi jambo aliloliona ni la kweli, alikata shauri la kuketi sehemu ya abiria akimpatia mgeni usukani.

Wakiwa njiani walizungumza mengi.

Mengi ambayo kama Mpelelezi angekuja kuulizwa hapo baadae, si ajabu asingekumbuka hata.


***


Brookhaven, New York.


Kitongoji cha Upton. Maabara ya Taifa.


Saa kumi jioni.


Dr. Lambert alijitahidi kutembea kwa upesi akitazama nyuma yake mithili ya mtu anayehisi kukimbizwa. Mkono wake wa kuume alikuwa ameukunja ngumi, akiutupa huku na kule kulifuata gari lake kati ya mengi yaliyoegeshwa hapa.

Alikuwa amevalia suruali ya kitambaa, rangi kahawia, na shati la sufi la mikono mifupi.

Alipojiweka kwenye gari, alihema kwa mikupuo kwanza kuikamata pumzi yake kisha akatulia akitafakari. Alihakikisha ame-lock milango na kufunga vioo vya madirisha. Alitulia humo kwa kama dakika nne hivi, tuli kama maji ya mtungini.

Kuna kitu kilikuwa kinamtatiza.

Alitazama kwenye vioo vya gari lake kama kuna mtu anakuja ama yu karibu naye. Hakukuwa na mtu. Alikuna kichwa chake chenye mvi akatulia.

Kidogo aliandika namba kadhaa kwenye simu yake akapiga. Simu ilipokelewa baada ya muda mdogo. Alikuwa ni mwanamke upande wa pili.

"Kwanini hamkuniambia?" alifoka. "Haya yote mlikuwa mnayajua lakini mkakaa kimya. Mnataka kuniweka kwenye hali gani?"

Mzee huyo aling'aka kwa namna gani usalama wa maisha yake ulivyokuwa hatiani.

Alieleza namna alivyohojiwa kwa masaa mawili na maafisa usalama, siku hiyo baada ya kazi, kwasababu ya kukamatwa kwa kemikali nyeti ambayo inaaminika imetoka kwenye maabara yao.

Alijipambanua kuwa hali si shwari. Kwaajili ya usalama wake, inabidi mawasiliano baina yao yasitishwe kwa muda ama itafutwe njia mbadala kwani baada ya tukio hilo watakuwa chini ya uangalizi mkali.

"Kila mmoja amehojiwa kwa nafasi yake," alipaza sauti. "Sifahamu wenzangu wamesema nini. Ofisi zetu zimekaguliwa na marejeleo ya kamera yamefanyika siku nzima. Kwa lolote likalonitokea basi mfahamu kuwa mkono wenu umehusika."

Alikata simu kisha akatoa 'line' aliyoitupa baada ya kuitafuna mara nne.

Alitazama tena usalama, alipoona ni shwari akaendesha gari kuelekea getini. Huko alikuta walinzi wawili wakiwa wamesimama, mmoja anaongea na 'radiocall' wakati mwingine akiwa anafanya ukaguzi.

Huyu anayefanya ukaguzi alisogelea gari akatazama dereva. Alipohakikisha ni mtu anayefahamika, alimpa ruhusa aende zake.

Kabla hajasogea mbali, yule mlinzi aliyekuwa anaongea na 'radiocall' alisimama njiani akawonyesha ishara ya kumtaka asimame!

Moyo ulimpasuka kisha ukaanza kwenda mbio.

Alimtazama mlinzi huyo akiwa anamjongea, bado anaongea na radio call yake.

"Ndio, afande ... sawa, over."

Mlinzi huyo alimtazama mwenzake akamtikisia kichwa kwa ishara kisha akamtazama Dr. Lambert kwa macho ya udadisi. Dokta alimuuliza kama kuna shida lakini hakusema neno. Uso wake ulikuwa umefinyana kwa ndita.

Alitupa macho yake huku na kule ndani ya gari la dokta huyo.

Alitazama kwa umakini sana.

Alipoona haijatosha, alimwamuru mzee huyo ashuke na kusimama kando.

"Ni vema mkaniambia shida ni nini, vijana. Pengine naweza nikawasaidia."

Bwana yule mwenye radio call hakutaka maneno. Alichofanya ni kurejea amri yake kwa mkazo kisha akasimama kwa lolote litakalojiri.

Dr. Lambert alitetemeka. Alikabwa na hofu kali. Alishuka kwenye gari, kama alivyoamriwa, akasimama kando akishuhudia. Aliweza kukaza mikono lakini ungetazama miguu yake ungeona namna gani inavyogongana.

Alihisi huu ni mwisho.

Walinzi waligawana majukumu kila mmoja akishika upande wake. Gari lilikaguliwa chini, kwenye viti na kwenye madroo yake. Hakukuwa na kitu.

Mlinzi yule mwenye radiocall alipata wazo fulani. Alifungua kile kidude kinachokaa juu ya kichwa cha dereva kikishushwa kusaidia kukabiliana na mwanga mkali wa jua unapomulika machoni.

Humo alikuta karatasi nyeupe zilizochoka, tano kwa idadi. Alizichomoa akasimama kuzikagua kwa macho makali.

Alizitazama karatasi hizo huku akiibia kumtazama Dokta. Alipomaliza, alisonga kando kidogo akawasiliana kwa kutumia radiocall yake. Dokta alimuacha na mlinzi mwingine.

Alipoongea kidogo, Dokta asisikie nini kinachozungumzwa, alirejea akasema,

"Tafadhali, dokta naomba tuongozane."

Dokta alihisi miguu yake inapoteza nguvu.


***
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 10


Na Steve B.S.M



Dr. Lambert aliingizwa ndani ya jengo, akiwa ameongozana na walinzi wawili, mpaka kwenye ofisi ya mkemia mkuu.

Aliingizwa ndani ya ofisi wakati karatasi ile aloyokamatwa nayo akikabidhiwa mkemia mkuu kwa ajili ya utambuzi.

Alikaa hapo, chini ya ulinzi, kwa muda mchache kabla ya mkemia mkuu hajaungana naye kwaajili ya maongezi machache.

Mkemia huyo, mwanaume aliyechongoka mabega na uso, nywele nyeusi zilizokuwa shaghalabaghala na miwani kubwa ya macho, makamo ya umri wake ni arobaini na tano, alimtazama Dr. Lambert kwa macho yake mapole.

Alifikichafikicha mkono wake wa kushoto kama mtu anayenawa mikono. Alitengenezea miwani yake usoni alafu akashusha pumzi ndefu. Ni kama vile alikuwa anatafuta mahali pa kuanzia.

Walinzi walikuwa wamesimama wakiwatazama. Sio wale wa getini tena, ni wengine waliovalia suti nyeusi. Mmoja ana miwani meusi na kifaa cha mawasiliano sikioni.

Mkemia alimuuliza Dr. Lambert kuhusu taarifa zile kwenye makaratasi ambayo yametolewa katika gari lake.

Alimuuliza Dokta huyo ni vipi taarifa hizo zilikuwamo katika usafiri wake holela na nini zilikuwa lengo lake.

Dr. Lambert, akiwa anajitahidi mno kupambana na hofu yake, alieleza ya kwamba taarifa hizo ni za kitambo sana, hilo linaweza kuthibitishwa na ubora wa karatasi zenyewe, lakini pia hazihusiki na lolote lile kati ya yale yanayotuhumiwa na maabara na usalama.

Aliziweka karatasi hizo muda akiwa anapitia rejeleo fulani la kisayansi kisha akasahau kuziondoa hapo.

"Ni makosa tu ya kibinaadam. Hamna cha ziada."

Maelezo yake yote yalinakiliwa, pia yalikuwa yanasikilizwa na watu wengine wa usalama kwa upande wa pili.

Mkemia alirudia maswali yake kama kuna litakalobadilika lakini hakukuwa na jipya. Bado Dr. Lambert alishikilia hoja yake ileille.

Mkemia alipiga simu yake ya mezani, punde akafika mtaalamu mmoja wa maabara aliyempatia makaratasi ya Dr. Lambert na kumwambatanishia kazi ya kufanya.

Baada ya robo saa, bwana huyo alipiga simu. Alishamaliza kazi. Mkuu wake alisikiliza ripoti yake alafu akapiga simu kwa mkuu wa usalama.

"Hamna jambo."

"Kivipi?"

"Taarifa haziwiani ... hakuna ushahidi wa yeye kuhusika moja kwa moja na ile kemikali. Formula zilizopo kwenye karatasi ni tofauti kabisa na zilizotumika kutengenzea ile dawa."

"Kwahiyo nani anahusika?"

"Bado tunafanyia kazi, mkuu. Tukipata majibu tutakurejea."

"Sina huo muda! Unasikia? Huo muda wa kupoteza sina kabisa. Nataka kila kitu kumhusu huyo bwana mliyemkamata. Hata kama gharama yake ikiwa kubwa namna gani. Sijali!"

Maramoja lilitolewa agizo la kuambatana na Dr. Lambert mpaka nyumbani kwake kwaajili ya uchunguzi zaidi.

Wanausalama watatu wakiwa ndani ya 'SUV' nyeusi walishika barabara upesi na ndani ya muda mchache wakawa wametinga kwenye makazi ya mhusika wao.

Watu waliokuwa eneo hilo walitahamaki kumwona Dr. Lambert akiwa anasindikizwa na wanaume wasiokuwa na uso wa furaha, ndani ya suti nyeusi.

Walitazama, kwa macho ya udadisi, mpaka mwanaume huyo alipotokomea katika uso wao chini ya ulinzi mkali.

Dr. Lambert alifungua mlango wa makazi yake, na punde ulipokuwa wazi alibakia hapo akiwa na mwanaume mmoja huku wawili waliozama ndani wakifanya ukaguzi mkali! ... Macho yake ya kizee yalikuwa yanachungulia wanachofanya mabwana hao.

Walitupa vitu huku na kule. Walifungua hiki na kile. Waligusa hivi na vile. Hakuna kitu kilichoachwa salama. Hadi ukuta ulipondwapondwa kubaini kama kuna mlango wa siri.

Walipomaliza kila ncha ya eneo hapo sebuleni, wakafungua na chumbani pia kukagua. Zoezi lilikuwa ni lilelile. Hakuna walichokiacha salama. Ukaguzi ulikuwa mkali. Kama ungekuwa mtu anayekaa hapa, ungeumia kwa namna vitu vikitupwa na kuachwa shaghalabaghala.

Hawakujali!

Walimaliza zoezi hapo wasione jambo. Sasa ikabakia sehemu moja tu katika eneo hili, nalo ni chumba kilichokuwa kimejitenga.

Chumba kilichokuwa kina mlango rangi ya samawati.

Walitaka kuuvunja mlango lakini Dr. Lambert aliwasihi kutumia diplomasia. Uharibifu waliokuwa wameufanya hapo ulikuwa unatosha. Haikuwa na haja ya kufanya zaidi.

Aliwapatia ufunguo mabwana hao wakaingia ndani kwa fujo.

Ama! Walikuta maabara ndogo iliyosheheni vifaa lukuki vya kisasa. Walistaajabu kwa namna vifaa hivyo vilivyopangwa. Kila kitu kilikuwa katika stadi yake.

Walikagua eneo hilo kwa macho wakisogea huku na kule. Waliona pazia lililokuwa limefungwa, wakaliendea wapate kutazama yaliyomo humo, wakati huo mmoja akitoa taarifa makao makuu juu ya kile kilichokuwa kinaendelea.

Walifungua pazia wakarusha macho. Hakukuwa na kitu zaidi ya kitanda kidogo chembamba.

Walirejea upande waliotokea, wakaendelea kutazama na kukagua. Hapa hawakuharibu kitu hata kimoja, walihofia huenda ikawa ushahidi. Waliendelea kutazama huku wakingoja usaidizi wa kisayansi tokea makaoni.

Dakika zilisonga.

Joto liliongezeka.

Walitiririka jasho ndani ya suti zao.

Mmoja alikohoa, kidogo naye mwenzake akafuatia. Walikohoa kwa pamoja tena na kisha kila mmoja akakohoa kivyake.

Walikohoa zaid ya hapo. Zaidi na zaidi. Mwenzao aliyekuwa nje, pamoja na dokta, alihisi hali hiyo si ya kawaida upesi akaenda kuwajulia hali wenzake.

Aliwakuta wakiwa chini, wameshikilia shingo zao wanakohoa. Mishipa ya shingo imewasimama. Macho yao mekundu mithili ya nyanya mbovu!

Alijawa na hofu na butwaa. Alimshika huyu kisha yule akiuliza nini kimejiri. Alipaza sauti kumwamrisha dokta aje humo ndani kutoa msaada lakini hamna aliemuitikia. Alikuwa mwenyewe.

Alinyanyuka kwa hasira amfuate daktari. Kabla hajapiga hatua ya pili, akakohoa. Huo ndo' ukawa mwanzo wa balaa.

Alikohoa pasipo kukoma. Alikohoa mfululizo kama mwehu. Kila alipotaka kuongea ama kusogea, kikohozi kilimtamatisha upesi. Aliinama akikohoa koh-koh-koh! ... koh-koh-koh!

Kwa vikohozi hivi vya mfululizo, alishindwa kuhema vizuri. Taratibu alianza kuhisi kichwa kinamuelemea. Macho yanapoteza nguvu. Miguu inashindwa kubeba mwili.

Aliangukia magoti yake. Alitamani kuita dokta lakini kikohozi hakikumpa nafasi kamwe. Alitoa macho kama balbu ya solar, mdomo kama kapu.

Mwisho wake ulikuwa ni kudondoka chini, akatulia. Tuli.

Alitulia kama wenzake wawili waliomtangulia.

Kitambo kidogo, dokta aliingia akiwa amevalia mask nyeupe iliyofunika mdomo na pua yake. Aliwatazama watu wale watatu. Hawakuwa na fahamu ndani yao. Aliwaburuza, kwa nguvu zake za uzee, akawaweka pamoja.

Baada ya hapo aliendea sebuleni akabofya kitufe fulani kilichokuwapo ukutani.

Alitazama saa yake ya mkononi, akajisemea mwenyewe ya kwamba ana dakika chache tu za kuweka kila kitu sawa kabla eneo hilo halijafurika wanausalama na wanasayansi kutoka maabara ya taifa.

Alirejea kwenye maabara yake ndogo, akajifungia humo.


Baada ya Masaa Matatu:


"Kwahiyo hamjafanikiwa kupata kitu?" Bwana aliuliza kwa macho makali ndani ya miwani yake. Sauti yake ilikuwa kali na kavu mithili ya mtu anayekunywa vinywaji vikali.

Bwana huyu alikuwa ndiye yule aliyekabidhiwa picha za Ferdinand, Mpelelezi na kemikali ndani ya gari. Simu yake alikuwa ameikamata kwa hasira akis'kiza anayoambiwa na mtu wa ng'ambo.

Amesimama wima nje ya jengo refu la kahawia la McGowan. Mbali naye kidogo, kuna gari moja la wagonjwa linalowaka taa za bluu na nyekundu. Mbali na hilo kuna magari mawili 'SUV' meusi.

Jua lilikuwa lishazama. Taa zinawaka huku na kule. Giza linaelekea kukomaa.

"Tumefanya 'sampling' na uchambuzi wa kemikali zote, hakuna inayowiana na ile uliyotuletea, na mpaka sasa hatujapata kuona sababu haswa ya bwana Ferdinand kumiliki kemikali hiyo. Tunafanya tafi--"

Bwana huyo alikata simu akang'ata meno. Alisimama hapo akitafakari. Hakuelewa mambo haya yanayotukia. Aliweka simu yake mfukoni akalijongea lile gari la wagonjwa.

Nyuma ya gari hilo, walikuwa wameketi wale mabwana watatu, walinzi walioongozana na Dr. Lambert kwenye makazi yake. Mabwana hao walikuwa wametoka kupata tiba lakini bado hawajatengemaa. Miili ilikuwa dhaifu. Vichwa vizito vinawagonga. Mmoja wao alikuwa amevaa 'mask' ya kujipatia hewa safi toka kwenye mtungi uliokuwemo ndani ya gari hilo.

Walimwona mkuu wao wa kazi anakuja upande wao, upesi wakakaa sawa. Walijitahidi kwa ukakamavu mchache uliobakia mwilini mwao kuonyesha heshima yao.

Mkuu wa kazi alisimama kuwatazama maafisa hao kwa macho ya hasira. Alitamani kuwameza. Nao hawa maafisa walitazama kwa uoga, nyuso zao zikijawa na haya.
Kwa yale yaliyotokea, ilikuwa ni aibu kujitambulisha kuwa ni wanausalama.

"Hatukufahamu mkuu," mmoja alijitetea. Aliongea pasipo kumtazama mkuu wake wa kazi. Macho yake yalitazama chini lakini kwa tahadhari. "Hatukujua kama mule ndani kutakuwa na kemikali hatari. Tumekosea."

Mkuu hakusema jambo. Aliona ni bure. Alijiondokea akafuata gari lake. Aliketi kwenye kiti cha nyuma akiwaza mambo haya. Hakika yalikuwa yanamvuruga. Japo hamna kitu kilichopatikana lakini swala la maafisa wake kupoteza fahamu katika maabara ile ndogo ya Dr. Lambert kilimfikirisha.

Kwa kutumia simu yake, alitoa amri ya kuachiwa kwa Dr. Lambert kutoka kifungoni kisha akaagiza bwana huyo afuatiliwe nyendo zake kwa ukaribu. Endapo lolote likibainika basi apewe taarifa haraka iwezekanavyo.

Baada ya simu hiyo, alimwamuru dereva kuondoka eneo hilo.


***


Kesho yake, asubuhi ya mapema, jiji la New York liliamshwa na habari ya kutisha kwenye maredio, runinga, mitandaoni na magazetini!

Kila mmoja aliyepata nafasi yake alisoma habari hiyo akistaajabu juu ya nini kilichotokea. Lilikuwa ni jambo jipya katika jiji hili lakini zaidi lilikuwa ni la kuogofya.

Habari ziliripoti kuwa katika kitongoji cha Brooklyn, yalitokea mauaji ya kikatili yaliyotokana na na mlipuko mkubwa uliotokea majira ya usiku unaokaribia na alfajiri ndani ya moja ya jengo moja maarufu kwa wauzaji na wanunuaji wa madawa ya kulevya kukutania kwa ajili ya kufanyia biashara zao haramu.

Katika sakata hilo, ilisadikika watu zaidi ya kumi walifariki papohapo. Miili yao ilisambaratishwa na bomu pasiwepo hata vya kuokota vikazikwe kwa heshima ya utu.

Majirani, pamoja na manusura wachache wa tukio hilo, walieleza yale waliyoyashuhudia, na kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, taarifa zao zilirushwa hapa na pale, huku na kule. Sio tu ndani ya New York bali Marekani nzima!

Wachache waliobahatika kurekodi tukio hilo adhimu, waligeuka kuwa mali kwa video zao kusambaa kama moto wa nyika mitandaoni, na hata baadhi ya vyombo vya habari vyenye uweledi walizitumia video hizo kama nyenzo pekee ya kuonyesha kilichojiri.

Basi ikawa hapa na pale watu wakizungumza na kupiga soga. Pia huko mitandaoni, watu wakimwaga maoni yao juu ya tukio hilo. Mlengo mkubwa wa watu wakikemea udhaifu wa jeshi la polisi kwenye kudhibiti mitandao ya madawa ya kulevya pasipo kujali maafa wanayoyasababisha.

Kwa kupitia video hizo ambazo ziligeuka kuwa maarufu ndani ya muda mchache mno, polisi waliweza kubaini sura kadhaa za wahanga. Takribani watu sita waligundulika maramoja huku wengine, kwasababu mbalimbali aidha za mwanga ama mwelekeo wa kamera, haikuwezekana kutambulika kwa upesi. Ulikuwa unangojwa upelelezi zaidi kwaajili ya kutambua wadhfa wao.

Picha za wale waliotambulika zilisambaa kwenye vyombo vya habari, kila chombo kikitaka kuwa cha kwanza kwenye kuripoti taarifa motomoto kwa wateja wake. Picha hizo kutoka kwenye video, ziliboreshwa zikaonekana vema. Macho na pua. Midomo na nywele, pia maumbo ya mwili.

Miongoni mwa picha hizo, ilikuwa ni ya Ferdinand.

Muda kidogo, mkuu wa kitengo cha polisi cha New York alitoa tamko kwenye vyombo vya habari kuhusu hayo yaliyojiri. Alielezea muda wa tukio hilo na pia jitihada za polisi kwenye kulishughulikia haraka iwezekanavyo.

Aliwasihi wananchi kuwa watulivu huku jeshi la polisi likifanya kazi yake, lakini pia alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wa dhati juu ya janga hilo ili kuwawajibisha wale wote waliohusika nalo kwa njia moja ama nyingine.

Wakati huo akiwa anatoa hotuba, mkuu wa kitengo cha upelelezi alikuwa yuko pembeni kidogo, yu 'bize' anahangaika na simu yake.

Bwana huyo alikuwa amevalia shati jeupe na kizibao cheusi kilichoendana na suruali yake. Upara wake ulifunikwa kwa kofia aina ya panama, rangi nyeusi yenye riboni nyeupe.

Alikuwa ameukunja uso akitazama simu hiyo kana kwamba kuna kitu kimeenda kombo. Aliibonyeza kwanguvu akiiweka sikioni, kisha aliitazama akaibonyeza tena na kuiweka sikioni.

Zoezi lilikuwa linajirudiarudia pasipo matunda. Alisimama akashika kiuno chake, akarudia tena zoezi hilo kabla ya kurejea kuungana na wenzie.

Lisaa limoja baada ya hotuba hii ya mkuu wa polisi, taarifa rasmi ilitolewa juu ya kutambua mabaki ya watu wengine waliokuwemo katika tukio la mlipuko. Watu wawili wa ziada, kwa kutumia mabaki yao madogo ya mwili yaliyofanyiwa uchunguzi, walibainika sura na wadhfa wao, upesi wakasambaa mtandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Baada ya lisaa lingine, walibainika wahanga wengine waliobakia. Kwa kuwianisha vinasaba vyao na taarifa zilizotunzwa kwenye 'database' ya usalama na serikali, nyuso zao ziliwekwa bayana mmoja baada ya mwingine.

Shida ilikuja pale ambapo mmoja kati ya wale walioonekana katika ile video ya wahanga wa bomu iliyosambaa mitandaoni, hakutambulika!

Japo kila kielelezo kilikusanywa toka eneo husika na vikasanifiwa na wataalamu wa hali ya juu, hakukuwa na majibu yoyote yaliyokuja.

Bwana huyo si mwingine bali Ferdinand. Mwanaume ambaye alikuwa anasakwa na polisi kuhusu kesi ya mauaji ya The DL!

Jambo hilo lilileta utata na mkanganyiko kwa polisi. Mkuu wa kitengo cha upelelezi, katika muda wake mchache, alikutana na afisa wa usalama aliyekuwa kwenye makubaliano ya kushirikiana na Mpelelezi wake juu ya kesi ya bwana huyu anayesadikika kufia motoni.

Afisa huyo wa usalama, rahisi kumrejelea kama 'babyface', aliomba apatiwe mabaki yote ya mwili yaliyofanyiwa uchunguzi kubaini utambulisho wa wahanga wa ajali ile kwa ajili ya wao kwenda kufanyia tafiti zaidi, lakini katika hilo aliomba kuwe na usiri mkubwa.

Haikutakiwa taarifa hii kuwa bayana kwa umma.

"Ondoa shaka," mkuu wa upelelezi alimsihi. "Nitalifanyia kazi ndani ya muda mfupi."

Baada ya masaa mawili, afisa huyo wa usalama akawa ameshapata kila kitu alichokihitaji. Wakati huo wote mwenza wake, yaani Mpelelezi, akiwa hana ufahamu na lolote lile linaloendelea.

Simu yake ilikuwa inaita pasipo majibu. Mkuu wake ameshapiga mpaka amechoka sasa. Ana shaka hata habari hizi za mauaji ya bomu kama kweli zitakuwa zimemfikia.

Uchunguzi uliporejelewa kwenye maabara za usalama, ilikuja kubainika kuwa ni kweli Ferdinand alikuwamo katika eneo la tukio! Mabaki kadhaa ya mwili yalithibisha hilo pale yalipowianishwa na wasifu wa bwana huyo katika 'database' za ofisi ya usalama. Wasifu ambao, hamna chombo kingine chochote cha usalama walikuwa nao, isipokuwa wao tu.

Ingawa ilikuwa ngumu kuamini, lakini vielelezo vilionyesha kuwa Ferdinand amekufa.


***
 
Back
Top Bottom