TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 15
Na Steve B.S.M
Mahali pasipojulikana. Saa tano na robo usiku.
Jennifer aliingia akiwa amebebelea kisosi chenye kikombw kidogo cha kahawa. Mwanamama huyo alikuwa ndani ya 'sare' zake kama kawaida. Miguu yake imezama ndani ya viatu vyeupe vya manyoya. Anatembea kwa stara asiangushe alichobeba.
Aliweka kisosi chake kwenye meza ndogo ya kioo, akamkaribisha mlengwa wake.
Alisema kwa ishara,
"Karibu. Nimekutengenezea kama vile ulivyoniagiza."
Aliposema hivyo akatabasamu.
Mitchelle, aliyekuwa ameketi mkabala naye, akatabasamu pia. Mwanamke huyo aliyekuwa amevalia nguo zake za jioni, nguo nyepesi za kuingiza hewa, alikuwa anaingoja kahawa hii kwa hamu zote.
Mdomo wake ulijawa mate alipoona kikombe kinachofuka moshi na kutoa harufu maridhawa. Koo lake lilimeza mate yaliyokuwa yanamwagika kinywani.
Kabla hajaongea kitu, akanyanyua kikombe hiki na kukiweka mdomoni. Akaria mafundo matatu. Akajiskia vema. Moyo wake mweupe. Alilegeza macho yake akinywa, na alipokirejesha kikombe mezani akatabasamu kwa upana zaidi.
Akamwambia Jennifer,
"Katika sababu kumi zinazonifanya niwe na wewe, Jennifer, nane zote ni kahawa yako. Mbili ndo' hizo zingine."
Jennifer akatabasamu. Akamuuliza Mitchelle kama anaweza kwenda zake kuweka kahawa yake ndani ya chupa maana itapoa, Mitchelle akamruhusu aendeze.
Alimwambia,
"Nishapata hiki kikombe, sasa hiyo nyingine unaweza kuiweka kwenye chupa kwaajili ya baadae."
Jennifer akaenda zake. Mitchelle akaendelea kunywa kahawa yake taratibu akifurahia fundo baada ya fundo.
Mazingira ya hapa alipokuwa yalikuwa ni tofauti kabisa na yale ambayo tumeyazoea kule Halletts Point. Sebule hii ilikuwa ndogo kiasi lakini yenye kujitosheleza.
Zulia la zambarau na sofa mbili 'confortable'. Runinga ya nchi zote ukutani huku 'showcase' yake ikivutia kwa rangi nyeusi na nyeupe.
Ukutani kuna 'wallpapers' rangi ya fedha yenye michirizi ya maua mekundu na kwenye dari kuna taa mbili kubwa ila zenye mwanga usioumiza macho. Taa hizo zilikuwa na maumbo ya kisasa ambayo kwa macho yalikuwa yanavutia mno kutazama.
Chini, tofauti na nyumba zingine ama tuseme nyumba zilizonyingi, kulikuwa na mbao badala ya 'tiles'. Mbao hizo zilikuwa zimepolishiwa vema, zinang'aa na mwanga huu wa taa za sebuleni.
Hapa alipokaa Mitchelle, ungeweza kuona sehemu maalumu ya kulia chakula upande wake wa magharibi. Huko kulikuwa na viti vinne na meza nyeusi ya 'marble' yenye michirizi meupe.
Akiwa anaelekea kumaliza kahawa yake tamu, simu yake iliyokuwa kando ikaita.
Akaitazama simu hiyo kisha akaipokea.
Akasema,
"Taiwan, ulikuwa wapi siku zote hizo?"
Mwanaume aliyekuwa anaongea upande wa pili, akaomba kwanza radhi kisha akasema,
"Nililazimika kuwa kimya kwa siku kadhaa kwasababu za usalama. Mambo hayakuwa mazuri huku, polisi walikuwa wakirandaranda maeneo haya baada ya kupata taarifa kuhusu mali lukuki zilizofukiwa."
Taarifa hizo zikamshtua Mitchelle.
Aliuliza,
"Polisi wamejuaje kuna mali huko?"
Taiwan akamweleza mawazo yake kwamba huenda kuna mtu aliyevujisha siri, lakini akamtoa hofu Mitchelle kwa kumweleza kuwa kila kitu kipo sawa.
Alijua namna ya kumaliza sakata hilo.
Alisema,
"Ilibidi nitumie hongo kunyamazisha kikosi kazi. Nimetumia takribani dola alfu tano."
Mitchelle akapuuzia taarifa hiyo.
Aliuliza,
"Vipi hali ya Kiellin na Truce?"
Taiwan akasita kidogo.
Alinyamaza, Mitchelle akamkurupusha kwa kulirudia swali lake kwa ukali.
Alisema,
"Kuna chochote kimetokea, Taiwan?"
Sauti yake ya ukali ilimfanya Jennifer aliyekuwepo jikoni akiosha vyombo ashituke na nafsi yake.
Akatulia tuli asikie kwa umakini ni nini kinachomsibu boss wake. Aliacha kila kitu akiacha masikio yafanye kazi yake kwa weledi.
Taiwan, upande wa pili wa simu, baada ya ukimya wake mdogo, akasema:
"Ni hali ya Kiellin. Imekuwa mbaya zaidi. Moyo wake unafeli. Anahema kwa shida sana. Daktari amesema tujiandae kwa lolote lile linaloweza kutokea."
Mitchelle akashusha pumzi kwanza kisha akanyamaza kimya.
Akili yake ilienda mbali. Ndani ya muda mfupi, macho yake yalibadilika yakaanza kulowana na kuwa mekundu.
Ukimya wake ulimfanya Taiwan aulize kama wako pamoja katika mawasiliano lakini hakujibiwa kitu na mwanamke huyo. Bado alikaa kimya.
Ni kwasababu tu Taiwan hakuweza kukata simu hii ndo' maana aliendelea kuwapo hewani.
Alingoja Mitchelle aongee.
Mitchelle alitafakari kwa muda wake kisha akasema aliyoyaona sawa.
Bado hakukata tamaa.
Alimwambia Taiwan,
"Fanya kadiri unavyojua ... Namna yoyote ile iliyokuwa chini ya jua kuhakikisha wanakuwa hai. Haijalishi pesa kiasi gani, narudia hili kwa mara nyingine. Mimi si kitu bila wao. Unajua hilo, Taiwan."
Taiwan akasema,
"Najua hilo, mkuu. Naendelea kufanya kadiri vile ninavyoweza. Nitatafuta wataalamu zaidi na zaidi watusaidie kwenye hili."
Simu ilipokata, Mitchelle akajilaza kwenye kochi.
Jicho lake la kushoto likachuruza chozi.
Alitazama dari akiwa mbali kwa mawazo.
Jennifer alifika hapo, akatazama kikombe cha kahawa na kukiona kinaishilia.
Akamuuliza boss wake kama angetaka nyongeza lakini hakupata majibu. Boss hakuwa hapo achilia mbali na kwamba hakuwa hata anamtazama.
Alikuwa yupo kwenye maumivu dimbwini mwa mawazo.
Lakini upande wa pili wa shilingi, upande ule alokuwa anawasiliana nao hapo awali kwa njia ya simu, hali ilikuwa ni tofauti kabisa.
Ni huko jiji la Taipei ndani ya dola ya Taiwan, kisiwa kinachopatikana mashariki ya mbali ya dunia na mashariki ya karibu na Uchina.
Bwana Taiwan, kitendo cha kumaliza tu kuongea na simu, alirusha ngumi yake hewani kwa furaha.
Alirusha ngumi hiyo mara mbili akisema, "yes-yes-yes!"
Alikuwa ni mwanaume mwenye nywele ndefu nyeusi alizozibana vema kisogoni.
Uso wake bapa ulikuwa na macho madogo ya 'kichina' na sharubu saizi ya kati.
Meno yake matatu yalikuwa ya dhahabu. Shingoni mwake amevalia cheni moja ya dhahabu na masikio yake yote yalikuwa na hereni yenye vito vya almasi.
Vito vinavyometameta.
Alichonga nyusi yake ya kushoto akiikata vijimistari viwili.
Mkononi alikuwa na simu toleo jipya kabisa.
Alikuwa ni mfupi, mnene kiasi. Amevalia koti jeusi la ngozi na tisheti nyeusi iliyoandikwa kwa herufi kubwa rangi nyeupe.
GO F*CK YOURSELF.
Chini alikuwa na 'raba' safi nyeupe, chapa ya 'nike'.
Mbele ya hapa aliposimama palikuwa ni mahali maarufu ndani ya Taipei kwa starehe zake za usiku, almaarufu kwa jina la OMNI Nightclub.
Humo kulikuwa na kufuru za kila aina. Muziki, pombe na wanawake.
Pesa yako tu.
Taiwan aliweka mikono yake mfukoni, kisha kwa madaha, akarejea ndani ya jengo hili la 'maraha'.
Ndani yake taa za rangi ya kijani na bluu zilikuwa zinaruka huku na kule kuangaza kwa mwanga wake hafifu.
Muziki ulikuwa mkubwa mno kiasi cha kutoskizana. Watu walikuwa wengi wakiruka, kunywa na kucheza.
Wahudumu, ambao walikuwa wanawake waliovalia bikini rangi ya pinki, walikatiza huku na kule, wapo 'bize' kwelikweli kuhudumia watu.
Sahani na vijindoo walivyobeba vilikuwa na chupa kadha wa kadha zenye kujawa na pombe za aina mbalimbali.
Palichangamka kweli.
Taiwan, aliyerudi humu ndani hakuchukua muda mrefu kujikuta katika sehemu yake maalum, VIP section, ambayo alikuwa na wenzake watatu pamoja na wanawake takribani sita.
Wote hao walikuwa ni watu wenye asili ya Ashia haswa uchina.
Wanawake walikuwa vifua wazi wakiwashikashika na kuwakandakanda 'maboss' wao ambao ndo' hawa wanaume.
Taiwan, kwa upekee wake kabisa, alikuwa anahudumiwa na wanawake watatu.
Wanawake hawa walikuwa wanatabasamu kila walipotazamwa na Taiwan usoni. Hata akiwatazama kwa kwa uso 'serious' wao ni kukenua tu.
Haki pesa mbaya nyie.
Taiwan, akitumia mkono wake kuupunga kwa wahudumu, akaagiza vinywaji zaidi viporomoshwe kwenye meza yao. Marafiki zake wakafurahi mno kusikia jambo hilo.
Wakapiga kelele wakimwita boss boss boss. Naye Taiwan akawasihi wanywe mpaka wachoke kwani pesa zipo.
Tena nyingi sana.
Alisema,
"Hapa nimetoka kuongea na simu ya pesa. Nimeseti mitambo na mambo yameshaitika. Tunywe tufurahi! Leo ni siku nzuri."
Mmoja kati ya wale wanaopewa ofa alikuwa ni bwana anayeitwa Yu. Yeye uso wake ulikuwa mwembamba ingali masikio yake ni mapana
Nywele zake alizoweka rangi nyeupe amezisuka twende kilioni. Mdomo wake una lips nyembamba na shingoni ana cheni mbili rangi ya fedha.
Bwana huyo kwa kumtazama tu ungebaini ni mtumiaji ama mteja wa madawa ya kulevya achilia mbali mkono wake kuume kuwa na alama lukuki za sindano.
Alimwita Taiwan akamuuliza,
"Ni yule dada wa Marekani?"
Taiwan akatikisa kichwa kuridhia. Basi bwana Yu akacheka kicheko cha kinafki kisha akauliza
"Ulishamwambia kuwa Kiellin amefariki?"
Taiwan akatikisa kichwa.
Akasema,
"Nitamwambia nikishapata pesa za kutosha. Kwa sasa acha n'tumie pesa hizi za daktari na matibabu kwanza ... Unajua nini? ... Nikimwambia anaweza kuja huku alafu mwisho wa siku mrija wangu wa raha ukakatwa. Nitakuja kumwambia baadae sana."
Yu akauliza tena,
"Huoni unajiingiza kwenye matati-"
Taiwan akamkatiza.
Alimuuliza akiwa amemtolea macho,
"Umechoka kunywa?"
Yu akatikisa kichwa kwa woga. Taiwan akaamuru wale wanawake wote waje upande wake, nao wakatii. Sasa wakawa wanamkanda kwa kumgombania maana mikono ilikuwa mingi huku mwili ni mmoja.
Akasema kwa kujigamba,
"Hapa ni mimi, na pesa ni mimi. Kama umechoka kula na kunywa ni kheri ukanyamaza kuliko kunipigia kelele. Vinginevyo, ondoka hapa."
Tangu hapo bwana Yu hakuongea kamwe.
***
San Fransisco, California. Saa sita usiku kasoro dakika chache tu.
Mvua bado ilikuwa inanyesha japo kwa sasa kasi yake ilikuwa imepungua.
Gari lillilokuwa kwenye mwendo wa kasi lilisimama ghafla likatoa kilio kikali cha matairi yaliyoumana na lami.
Upesi akashuka Mpelelezi.
Alikuwa amevalia koti kubwa jeusi la mvua. Kichwa chake kimefunikwa na kijikofia cha koti hilo.
Macho yake yalitazama vema nyumba iliyokuwa imesimama mkabala naye.
Nyumba hiyo ilikuwa kubwa kwa wastani. Nyeupe kwa rangi. Imejengwa kwa mbao na dezaini ya kupendeza.
Kabla hajasogea zaidi, Mpelelezi akamwambia dereva,
"Usiondoke. Nakuja hapa muda si mrefu."
Lakini dereva alikuwa na hofu usoni. Kichwa chake kilikuwa kinachuruza jasho jingi, ameyatoa macho na anahema kwanguvu.
Bila shaka mwendo aliokuja nao ulikaribia kumtoa roho.
Alitikisa kichwa kukubali alichoambiwa kisha akatulia kumshuhudia Mpelelezi anayeenda ndani ya nyumba ile.
Alipoona Mpelelezi amesogea vyakutosha, akawasha gari na kutimka.
Alisema,
"Hapana. Hata hiyo pesa baki nayo. Mtu wa namna gani wewe usiyejali uhai wa mwenzio!"
Mpelelezi akatazama gari hilo likiyoyoma asielewe ni nini kimemkuta dereva.
Alinyoosha mikono yake kupunga lakini dereva hakujali wala kutazama. Alikazia mwendo wake kama mwendawazimu.
Mpelelezi akiwa bado hapo anabung'aa, mara akasikia sauti ya gari linalotimka kwa kasi!
Kugeuka, akaliona gari likiwa linatokea nyuma ya nyumba hii.
Gari hilo lilikuwa ni SUV nyeusi ileile ambayo alifanikiwa kuiona akiwa kule kwenye hoteli anayopumzikia.
Gari hilo lilitimka kwa kasi mno. Mpelelezi alijaribu kulikimbiza lakini hamna alichoambulia zaidi ya moshi tu.
Alisimama akihema.
Hakutaka kuamini alichokuwa anakiwaza kichwani. Kilikuwa ni kitu kibaya asichotaka kamwe kitokee.
Upesi akakimbilia kuifuata nyumba, akakuta mlango wa sebuleni ukiwa umevunjwa, umesimama hoi pembeni.
Aliporusha macho yake ndani, akaona mwili wa mwanamke ukiwa umelala chini, unavuja damu kichwani.
Mwili huo haukuwa hata na lepe la uhai ndani yake.
***