Tukibaki Hai, Tutasimulia

Tukibaki Hai, Tutasimulia

TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 19


Na Steve B.S.M




Jamal akampatia Richie muhtasari wa data ile aliyompatia akaifanyie kazi.

Akamweleza ya kuwa yale yote yaliyomo katika taarifa hiyo yanamhusu binadamu na vijenzi vyake.

Data za muunganiko wa damu ya binadamu, mate ya binadamu na karibia kila kitu kuhusu kemikali zote zilizomo katika mwili hai wa binadamu.

'Chemical composition' za vyakula karibia vyote ambavyo hutumika na binadamu, na pia composition ya karibia kemikali zote ambazo ni sumu kwa matumizi ya binadamu..

'Chemical reactions' karibia zote zinazofanya mwili wa binadamu kufanya kazi kwa ufanisi wake, na athari ya kukosekana kwa kila kemikali ndani ya mwili huo.

Kemikali ambazo zipo tumboni. Kwenye mifupa. Kwenye ubongo.

Kemikali zote zinazozalishwa na ini la binadamu na kazi takribani mia tano za kikemikali zinazofanywa na 'organ' hiyo ndani ya mwili.

Alimwambia Richie,

"Kwa mujibu wa tafiti ya wanasayansi wa chuo cha California waliyoifanya katika mwili wa mwanamke mjamzito, walibaini kuna kemikali takribani mia moja na tisa katika mwili wa binadamu.

Ikiwemo kemikali hamsini na tano ambazo hazikuwahi kuripotiwa popote pale hapo nyuma.

Pia kemikali arobaini na mbili ambazo vyanzo vyake na matumizi yake katika mwili wa binadamu hayafahamiki mpaka leo hii kwa wanasayansi.

Kemikali hizo huitwa 'mystery chemicals'.

Huenda kila mmoja anazo.

Kazi yake mwilini, hakuna anayejua. Chanzo chake mwilini, hakuna anayejua pia.

Lakini ajabu ni kwamba, katika chapisho ulilonipa, zimeanishwa kemikali mia mbili ambazo ni 'mystery'.

Kemikali mpya kabisa, sijapata kuziona wala kujifunza popote pale. Haswa katika mwili wa binadamu.

Kemikali hizo sijajua kazi yake ni nini katika mwili uliotajwa. Na nilishindwa kutafuta majibu zaidi sababu ya masharti uliyonipatia."

Richie akasafisha koo lake kisha akayabandua macho yake kwenye karatasi alilokuwa anasoma.

Akamtazama Jamal usoni.

Mwanaume huyo mweusi alikuwa na macho mekundu. Ni wazi hakupata wasaa wa kutosha wa kulala usiku wa kuamkia siku hii.

Kazi hii ilikuwa kubwa mno.

Wingi wa makaratasi aliyoyashika Richie, ulithibitisha hilo.

Richie akauliza,

"Una uhakika hakuna mtu anayejua kuhusu taarifa hii?"

Jamal akaapa.

Alisema hata mwenzake anayelala naye hakupata kujua ni nini anafanya, hivyo kila kitu kipo salama.

Lakini akamwambia Richie kwamba kemikali hizo ambazo bado hawajazifahamu, huenda angepata taarifa zake kama angemshirikisha profesa wa chuoni kwao.

Alisema,

"Pengine hiko ndo' kinafanya taarifa hii kuwa siri. Huoni hilo?"

Richie akatikisa kichwa.

"Hapana, Jamal. Ni hatari. Naamini kuna taarifa nyingi zijazo, tutakapozipata kwa ukamilifu wake basi tutajua mengi. Acha kwanza nikapitie hizi."

Simu ya Jamal ikaita.

Aliichomoa mfukoni akaitazama. Jina Huncho.

Akaminya sauti kisha akaendelea na maongezi.

Alimtaka Richie ampate pesa yake aondoke kwani yuko nyuma ya muda.

Lakini akasihi chapisho lingine litakapopatikana basi apatiwe maramoja kwani kuna jambo amelihisi na nafsi yake.

Alisema,

"Yawezekana huu ukawa ni mradi wa kutengeneza watu. Sina uhakika lakini ... Sijui ... Nahisi tu."

Richie akamuuliza akiwa ameyakodoa macho yake,

"Kwanini unahisi hivyo?"

Akapandisha mabega yake na kuupinda mdomo.

Akasema,

"Kwa namna taarifa zilivyopangiliwa humo. Taarifa zenyewe zilizowasilishwa. Na usiri wake. Auhisi jambo? ... Ni hisia tu, nilishawahi kusikiasikia haya mambo ... kama nilivyosema hapo mwanzo ... Nahisi tu. Kama si hivyo basi yawezekana ni kuhusu Pharmaceuticals.

Tutapata dira baada ya kupitia kazi zijazo.

Lakini ..."

Hapa akarudi kwenye swali lake la kwanza kabisa alilouliza

"Richie, umetoa wapi hizi data?"

Richie hakuwa tayari na swali hilo. Akasema hayo ni yake na aachiwe mwenyewe.

Kama ilivyo ahadi, akatoa pesa ndani ya begi na kumpatia Jamal.

Jamal akahesabu na kuona ni timilifu. Akashukuru na kuaga.

Muda wote huo simu ya Jamal ilikuwa inaita kwa kutetemeka mfukoni.

Richie akamtazama mwanaume huyo akienda zake.

Alipotoka tu mgahawani, akatoa simu yake na kumpigia Hilda.

Akamweleza yale yote aliyopata kuambiwa na Jamal.

Alisema,

"Kama utapata muda, naomba tuonane."

Hilda akamjibu,

"Sidhani kama itawezekana leo. Kuna kazi kubwa ya boss Bryson nafanya hapa."

Richie akahamaki,

"Kazi nyingine?"

Hilda akamweleza ya kazi hiyo kuwa amepatiwa asubuhi ya siku hii pale alipokutana na Bryson mahali fulani.

Richie akapendekeza wakutane sehemu ili amsaidie kuifanya.

Pendekezo hilo likamfurahisha Hilda.

Alicheka mtu wa pembeni angesikia.

Kwa upande wa Jamal, bwana yule, kijana barobaro, aliyetoka kuongea na Richie muda si mrefu ulopita, aliingia ndani ya basi akaketi pembeni ya dirisha.

Alipoketi tu, akatoa simu yake iliyokuwa inaita mfukoni na kuipokea.

Alikunja sura akisema,

"Huncho, ukipiga mara mbili inatosha kwani nyumba inaungua moto?"

Sauti ya upande wa pili ikazozana naye. Ilikuwa ni sauti ya mwanaume ikikwaruza.

Sauti hiyo ilisema,

"Jamal, ulisema mpaka muda huu utakuwa ushantumia pesa yangu. Naona kimya, vipi?"

Jamal akamwambia yu kwenye basi. Pesa anayo mfukoni.

Punde atakaposhuka basi atamrushia kwenye simu.

Swala hilo likawa gumu kwa Huncho. Hakupenda wazo hilo.

Alitaka pesa yake cash.

Akamwelekeza Jamal mahali alipo kisha akasema anangoja hapo.

Jamal akakata simu.

Akairudisha mfukoni huku akiongea mwenyewe kwa kulalama.

Alisema,

"Madawa yatakuja kumuua huyu mjinga. Yeye anawaza unga tu, hamna kingine."

Baada ya robo saa akashuka toka kwenye basi.

Akaitoa pesa yake na kuitenganisha mfuko kisha akaendelea na safari.

Muda kidogo akawa amekutana na Huncho mahali palipojificha kiasi.

Mwanaume huyo alikuwa mrefu, mweusi, mwenye kuvalia nguo za rangi rangi nyingi.

Nywele zake amezisokota rasta zilizofika mabegani.

Usoni amevalia miwani nyeusi ya jua.

Jamal alimpatia pesa akazihesabu na kukiri zipo sawa kisha akasema,

"Tuonane tena siku nyingine."

Akaondoka zake akimwacha Jamal hapo.


***


New York Police Department, New York.

Saa sita mchana



Mpelelezi alitoka kwenye ofisi ya mkuu wake wa kazi akiwa ameshika kiuno.

Alikuwa amevalia shati jeupe na 'suspender' nyeusi. Suruali ya kitambaa na kiatu kinachong'aa.

Macho yake yalikuwa yamelegea kama mtu aliye na usingizi, kuchoka au vyote kwa pamoja.

Sauti kali iliyotoka kwenye ofisi ya mkuu wake ilifoka,

"Nakwambia unacheza na sharubu za simba. Sitakustahimili tena, afisa. Sitakustahimili tena!"

Mpelelezi akaufunga mlango na kwenda zake.

Uso wake umeparara.

Akiwa anajongea, akasikia mtu anamwita.

Aligeuka akamwona Babyface kwa mbali.

Bwana huyo alikuwa amevalia suti nyeusi nadhifu.

Nywele zake zinang'aa na kulala kama zimelambwa na paka.

Usoni mwake amevaa tabasamu pana linaloonyesha meno yake yote.

Alimpungia mpelelezi mkono, akamwonyesha ishara kuwa anakuja kisha akaenda zake mwelekeo wa ofisi ya mkuu wa upelelezi.

Mpelelezi akamtazama bwana huyo akiwa anatafakari yake kichwani.

Hakukaa hapo, akaelekea kwenye ofisi yake alipojibwaga katika kiti na kushusha pumzi ndefu puani.

Taratibu akiwa anazungusha kiti chake kwenda huku na kule, akawa anatafakari.

Alikuwa na mambo mengi kichwani.

Ni kama vile ujenzi wa ghorofa ulikuwa unaendelea katika ubongo wake.

Alitafakari mambo yanavyokwenda.

Moja baada ya jingine.

Akili yake ikampeleka mbali ...

Siku za nyuma: Majira ya saa nne asubuhi.

Kule San Fransisco, California. Majira ya saa nne asubuhi.


Aliamka kichwa kikiwa kinamuuma.

Alihisi mtu yumo ndani ya fuvu lake akibondabonda na nyundo.

Akiwa ameshika kichwa chake kuugulia maumivu, akakagua mazingira ya hapa alipo.

Palikuwa ni pageni machoni mwake.

Hayakuwa mazingira ya 'lodge' ile aloilipia.

Akaketi kitako akiwaza na kuwazua.

Palikuwa kimya sana hapa.

Hakujua amefikaje.

Aliwaza kama ni hoteli ama nyumbani mwa mtu.

Akatoka kitandani na kuufuata mlango.

Kifua chake kilikuwa wazi, akiwa amevalia suruali pekee.

Chini yuko peku, anauhisi ubaridi wa sakafu.

Kabla hajaufungua mlango, akasikia sauti ya mwanamke ikiwa inaongea huko upande wa pili.

Akatulia tuli, asikie mwanamke huyo anaongea nini.

Kwa dakika moja za kuskiliza, hakuambulia kitu.

Sauti haikusikika vema.

Ni kana kwamba mtu alikuwa anaongea akiwa ndani ya chungu.

Akaufungua mlango na kushika korido.

Alinyookea sebuleni akamkuta mwanamke akiwa ameketi kwenye kochi kubwa, mezani kuna sahani nyeupe yenye bites.

Sebule hii ilikuwa pana lakini yenye uhaba wa samani.

Makochi mawili tu yalikuwapo hapa pamoja na meza ndogo.

Ni bayana mkazi wa hapa alikuwa akipendelea zaidi nafasi kuliko mrundikano wa vitu.

Mwanamke huyo alikuwa anaongea na simu, na punde alipomwona Mpelelezi akakatisha maongezi yake ili apate kumlaki.

Alikuwa ni mwanamke yule wa Casino.

Alikuwa amevalia blauzi fupi rangi ya pink iliyoacha tumbo lake bapa kuwa wazi.

Chini amevalia kibukta kifupi rangi nyeusi chenye michirizi meupe pembeni.

Nywele zake amezibana kwa ustadi mkubwa usidhanie kabisa kama ni ndefu kiasi tunachojua.

Alitabasamu akasema,

"Karibu sana bwana. Naona umeamka."

Mpelelezi akamuuliza imekuaje akafika hapo. Alitaka kujua ni nini kilitokea jana yake usiku.

Mwanamke yule akampoza.

Akamsihi atulie kwanza, atafahamu kila kitu.

Alimuuliza,

"Unajiskiaje?"

Mpelelezi akajibu yuko sawa, lakini mwonekano wake ukiwa kinyume na anachosema.

Kila saa alikuwa anakunja uso wake kwa maumivu ya kichwa na mwenyeji wake akalibaini hilo.

Akamwambia,

"Nilikuandalia supu kwaajili ya hangover. Ni vema ukaipata sasa."

Mwanamke huyo akaenda jikoni na punde akaja na bakuli zuri lenye supu ndani yake.

Akampatia Mpelelezi akimkaribisha.

Lakini kabla Mpelelezi hajatia kitu mdomoni, akauliza,

"Nini kilitokea jana? ... Nataka kujua."

Mwanamke yule akamjibu,

"Nadhani ulikunywa kupita kiasi."

Mpelelezi akapata mashaka.

Hakuwahi kunywa kiasi cha kupoteza kabisa fahamu zake.

Hiyo jana kulitokea nini kiasi cha kushindwa kujimudu?

Ghafla akajipapasa mfukoni mwake.

Hakuhisi kitu.

Mwanamke yule akamwambia,

"Simu zako nilizihifadhi kwaajili ya usalama. Ngoja nikupatie."

Akaenda zake chumbani.

Mpelelezi akiwa hapo sebuleni peke yake, akarusha macho yake huku na kule kufanya ukaguzi wa mazingira ya hapa.

Kichwa bado kilikuwa kinamgonga.

Kuna muda alishindwa kuhimili akakishika kwanguvu.

Punde Mwanamke yule akarejea akiwa na simu mbili mkononi pamoja pia na dawa ya kutuliza maumivu.

Akampatia Mpelelezi.

Mpelelezi akanywa dawa hizo maramoja akisindikizia na maji mengi alopewa.

Akiwa anafanya hivyo, mwanamke yule akawa anamtazama kwa udadisi.

Alimwambia,

"Kunywa sasa supu yako kabla haijapoa."

Mpelelezi akafanya vivyo, lakini kiu yake ya kutaka kujua yanayoendelea hapa ikambana.

Alitaka kuuliza.

Upesi mwanamke yule akamsihi,

"Kula kwanza. Najua una maswali mengi. Nami ninayo pia."

Kisha akatabasamu.

Mpelelezi akazidi kuamini.

Mwanamke huyu alikuwa ni wa ajabu.


***
Asnt sn[emoji123]
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 20


Na Steve B.S.M



Mpelelezi hakupata kukata kiu yake.

Alipomaliza kunywa supu hii, mlango ulifunguliwa akaingia mwanaume mrefu mwenye mwili mpana.

Mwanaume huyo alikuwa amevalia shati rangi ya bluu bahari. Ameichomekea kwenye suruali nyeusi ya kitambaa.

Mikono ya shati hilo ilikunjamana mpaka karibia na viwiko, ikaacha wazi mikono minene ya bwana huyu ikionyesha wingi wa vinyweleo vyake na utajiri wa mishipa mikubwa ya damu.

Alikuwa ni bwana mwenye kaliba ya ushupavu.

Nywele ndefu za wastani, rangi nyeusi. Macho yake yameingia ndani kiasi, rangi ya kijani.

Mkono wake wa kuume ulishikilia briefcase ya kahawia, ngozi tupu.

Alimtazama Mpelelezi kwa macho ya ukali, punde mwanamke yule mwenyeji akasimama kimshangao, akamwendea akiwa anajilazimisha kutabasamu.

Alimshika mkono mwanaume huyo, akasema,

"Karibu sana, mpenzi!"

Mwanaume huyo mgeni akamtazama mwanamke huyo.

Macho yake yalikuwa makali.

Uso wake haukuwa na chembe ya urafiki. Alitazama kama mtu anayeshuku hatari mbele yake.

Mwanamke akajitabasamisha kisha akasema,

"Oh! Karibu mpenzi nikutambulishe mgeni wangu."

Aliposema hayo, akamtambulisha Mpelelezi kama rafiki wake wa siku nyingi. Hivi karibuni amekuja California hivyo amempokea na kumpa hifadhi.

Alipomaliza, akamtambulisha na mwanaume huyo kama mume wake. Wapo kwenye mahusiano ya ndoa kwa miaka miwili sasa.

Baada ya utambulisho, mwanaume huyo mgeni akampatia Mpelelezi mkono wa salamu.

Mpelelezi alipompatia wake, akaudaka na kuubana kwanguvu.

Akasema,

"Nimefurahi kukujua."

Kisha akatabasamu bila kuonyesha meno.

Sauti yake ilikuwa nzito, yenye kina kirefu. Naye Mpelelezi hakupata kujua cha kusema, akanyamaza akitabasamu.

Tabasamu la maigizo.

Bwana huyo akaenda zake chumbani. Hakugeuka mpaka anazama humo.

Naye yule mwanamke alikuwa anamtazama akiishia zake.

Alipozama chumbani, akamtazama Mpelelezi kwa tabasamu alafu akamwambia,

"Tafadhali, naomba uningoje"

Akaelekea kule alipoenda mwanaume yule.

Chumbani.

Akaufunga mlango kisha kukawa kimya kidogo.

Macho ya mpelelezi, pamoja na mazingatio yake yakawa kule chumbani.

Alitazama korido kana kwamba kuna mtu anamwona hapo.

Huku kichwani anawaza.

Anawaza ya mwanamke huyu.

Ina maana ana mume? Mbona anakesha kwenye kumbi za starehe na kamari?

Aliwezaje kumleta hapo nyumbani mpaka akalala ingali ana mwanaume anayeishi naye?

Wakati akiwa katika kumbi za starehe na kamari, mwanaume huyu anakuwa wapi?

Au ni bwana wa kusafiri mara kwa mara?

Alikuwa anajua kama mwanaume huyu anakuja leo? Mbona hakuonekana na dalili hiyo?

Ilikuwa ni surprise?

Yalikuwa ni maswali mengi. Anajiuliza na kujijibu mwenyewe ... Haelewi ... Anapanga na kupangua vitu kichwani mwake.

Katikati ya hayo, akasikia sauti.

Sauti ya mtafaruku kule chumbani.

Yule bwana na yule mwanamke walikuwa wakizozana kwa sauti.

Sauti ambayo hakuwa anaisikia vema.

Kuna muda sauti ikapanda, kuna muda sauti ikashuka.

Mwanaume alisikika akinguruma na sauti yake nzito, na mwanamke akasikika aking'aka na sauti yake nyembamba.

Majibizano hayo yakamnyima raha mpelelezi.

Akatamani kuondoka zake lakini asingeweza bila kumuaga mwenyeji.

Kuna muda alisimama, kisha akaketi.

Hapana. Alisema mwenyewe.

Siwezi.

Ikabidi angoje hapo japo hakupenda.

Baada ya muda mfupi, kheri kwake, akasikia mlango ukifunguliwa.

Alitazama akamwona mwanamke akiwa anakuja upande wake. Alikuwa amebeba uso wa mawazo.

Vidole vya mkono wake wa kuume alivizamisha ndani ya nywele zake ndefu, akijikuna.

Sasa, tofauti na hapo mwanzo, alikuwa amevalia tight ndefu nyeusi, juu blauzi yake ileile.

Alipokutana macho kwa macho na Mpelelezi, akatabasamu.

Tabasamu la uwongo.

Mpelelezi akashindwa kumrejeshea tabasamu hilo. Alihisi mwanamke huyu yu matatani na yeye ndiye sababu.

Akanyanyuka na kumlaki kwa swali.

Aliuliza,

"Kila kitu kipo sawa?"

Mwanamke akatikisa kichwa kisha akatabasamu kwa upana. Hapa uso wake ulichanua kana kwamba hamna kitu chochote kilichotokea.

Akasema,

"Bila shaka umependa supu yako, sio?"

Mpelelezi hakujibu.

Aliendelea kumtazama kwa macho ya walakini.

Mwanamke akasema,

"Ok. Naomba nikutoe."

Mpelelezi akadakia hapa akisema,

"Ndio. Ni wazo jema kabisa!"

Ni kana kwamba alikuwa anangojea kauli hii kama pumzi iliyobanwa kwa muda mrefu.

Akaendea shati lake chumbani, chumba cha wageni, akalivaa akiwa anatembea.

Alimalizia kifungo karibia na mlango wa sebule.

Wakatoka ndani na kulifuata gari nyuma ya jengo.

Lilikuwa ni gari aina ya Ford Mustang rangi ya bluu toleo jipya kabisa.

Walipanda, mwanamke akaendesha, kulifuata geti kubwa.

Geti hilo lilikuwa ni 'automatic'.

Punde gari liliposogea karibu likajifungua lenyewe.

Kabla hawajatoka, Mpelelezi akapata kutazama nyumba wanayoiacha.

Kwenye moja ya dirisha, akamwona mwanaume yule amesimama akiwatazama.

Alisimama hapo kama sanamu.

Hakuwa anatisika wala kucheza.

Mpaka wanaishia, bwana huyo alikuwa hapo amesimama.

Mpelelezi akamtafakari bwana huyo wa ajabu.

Alisema na nafsi yake kama kweli mwanaume yule alikuwa ni mume wa huyu mwanamke, ni nini kilichomvutia mwanamke huyu pale?

Alimtazama mwanamke yule aliyekua anaendesha akamwona akiwa ametulizana.

Alikuwa kimya akihangaika na usukani.

Kidogo akamtazama Mpelelezi na kutabasamu.

Tabasamu mwanana.

Akasema,

"Usijali. Najua tulikuwa na maongezi lakini hayakupata kumea. Muda utakapokuja, tutaongea vizuri. Amini."

Kidogo simu ya mwanamke huyu ikaita.

Alishusha uso akalegeza macho yake kiuchovu.

Akalalama akiupiga usukani,

"Aaaaggh!"

Aliliegesha gari pembeni akachomoa simu toka mfukoni na kupokea.

"Najua ninachofanya. Tafadhali ... Nimekuelewa ... Najua!"

Kisha akakata simu.

Mpelelezi akamuuliza,

"Kuna tatizo?"

Akajibu,

"Itabidi nikuache hapa. Si mbali na barabara kuu, utapata usafiri usijali."

Mpelelezi akashuka hapo na kusimama akilitazama gari hilo linaondoka.

Akiwa hapo ndo' akabaini koti lake la mvua halipo pamoja naye. Aliliacha kule nyumbani kwa mwanamke huyo au kule ukumbini alipopotezea fahamu?

Hakuwa anajua.

Alitoa simu mfuko wake wa kushoto, akaiona simu ya Ronelle. Mwanamke yule aliyefariki kabla hajapata kukutana naye.

Simu hiyo ikamkumbusha misheni yake ndani ya California.

Misheni ya mwanamke yule aliyejinyonga huku wasifu wake ukitumiwa na mtuhumiwa wa mauaji ya The DL.

Upesi akashika njia kuelekea kufanya kazi yake muhimu.

Angalau kichwa kilikuwa kimepoa hivyo asingepata ugumu wa kazi.

Ndani ya muda mfupi akawa amekwea basi. Amekaa siti ya dirishani.

Hapa ndo fikra zake zilizokuwa zinawandawanda zikarejea ofisini, ndani ya kituo kikuu cha Polisi New York.

Alisikia hodi mlangoni, kabla hajasema jambo akaingia bwana mmoja ndani ya suti.

Kutazama, alikuwa ni Babyface.

Akashusha pumzi kwa uchovu.

Bayana hakufurahia ujio huu.

Babyface alimtazama kwa tabasamu pana kisha akaketi pasipo kuomba. Akaegesha mguu mmoja juu ya mwingine kisha akafyonza meno yake akitazama kucha zake za mkono wa kushoto kana kwamba ametoka kuzirepea.

Kukawa kimya kidogo.

Mpelelezi alizungusha kiti chake taratibu huku na kule akiwa ameegemeza kichwa chake hapo.

Alikuwa anatazama paa kwa macho ya kichovu.

Mgeni wake alimtazama kisha akatikisa kichwa. Naye akanyamaza asiseme kitu. Ni kana kwamba kila mmoja alikuwa anangojea mwenzake aongee kwanza.

Kimya kikapita kwa dakika nzima.

Kisha,

"Unataka nini?"

Mpelelezi aliuliza.

Macho yake bado yalikuwa yanatazama paa, saa hii akitazama feni iliyokuwa imesimama.

Mikono yake aliikutanisha juu ya tumbo. Amekaa kivivu, anaendelea kujizungusha taratibu.

Babyface akamjibu,

"Unajua nini nataka, mpelelezi."

Mpelelezi akamwambia hamna anachojua, na kama kingekuwepo basi asingepoteza muda wake hapo.

Alimtazama Babyface, katika 'pozi' lake lilelile la kuegemea kiti, macho ya kivivu, akasema,

"Kama huna jipya la kuniambia, unaweza kunipisha niendelee na kazi yangu?"

Babyface akatabasamu kisha akaubidua mdomo wake.

Alitazamq pembeni kidogo kwa mafikirio kisha akamkumbusha kitu Mpelelezi,

"Unajua tuna makubaliano sisi nawe?"

Mpelelezi akaguna kwa kicheko cha ndani.

"Makubaliano?"

Akaketi vema kisha akasema akiwa ameyakaza macho ya kwamba hatambui makubaliano yoyote ambayo ameyaweka akiwa na akili zake timamu.

Na akaeleza ya kwamba, kawaida yake ni kufanya kazi peke yake. Hapa akajitambulisha kama 'Lone Wolf'.

Alisema,

"I am flying solo, man."

Kisha akarejea kwenye 'pozi' lake kana kwamba hamna kilichotokea. Saa hii alifumba macho kama mtu aliyepotelea usingizini.

Akamalizia kwa kusema,

"Ukimaliza kun'tazama, nenda zako."

Babyface akaona haya ni masikhara. Mtu huyu hakuwa 'serious'. Akajaribu kumwongelesha lakini akaongea mwenyewe. Hakuna aliyezoza naye.

Hata aliyoyasema Mpelelezi hakuyasikia zaidi ya kuona kelele zilizoingia sikio moja na kutokea jingine.

Alipuuzia yale yote alosikia.

Lakini kauli moja ikagusa hisia zake.

Alifumbua macho akamtazama mgeni wake ambaye alikuwa tayari amesimama, kichwani mwake akiwaza kama kile alichokisikia kilikuwa ni sahihi ama lah.

Ilikuwa ni kauli ya kitisho juu ya usalama wa maisha yake.

"Kama ukishindwa kufuata makubaliano tuliyoyaweka basi nitafuata makubaliano yangu binafsi ... Nahofia makubaliano hayo yanaweza yakawa si rafiki kwa uhai na maisha yako."

Babyface akamalizia,

" ... kwa maslahi mapana ya taifa "

Mpelelezi akang'aka akimuuliza kama anamtishia.

Alisimama akiyakodoa macho yake kwa ukali mithili ya mbogo aliyetengwa na kundi lake.

Babyface, kwa sura yenye utulivu, akiwa anatengenezea koti la suti yake, akamwambia,

"Kuna mstari mwembamba kati ya kitisho na uhalisia."

Kisha akaenda zake.

Mpelelezi akajaribu kumwita bila mafanikio.

Bwana huyo alienenda kana kwamba ametia pamba masikioni.

Alitoka kwenye kituo hiko kikubwa akaendea gari lake, muda kidogo gari hilo likatimka.

Likiwa linaondoka, Mpelelezi akalitazama kwa macho yaliyobanwa na ndita.

Alikuwa amesimama kwenye ngazi zinazoingia kwenye lango kuu la kituo. Hapo akiwa amefika si muda mrefu.

Akiwa analitazama gari hilo likiwa linatokomea, jambo likamjia ghafla katika fikra zake.

Hili gari ...

Alijisemea mwenyewe ...

Hili gari sio ...

Sio lile nililoliona kule San Fransisco kwenye mauaji ya Ronelle?

Gari likapotea machoni pake.

Bado aliendelea kusimama hapo akitazama upande ule gari lilipoelekea huku akiwa anatafakari.

Mwishowe akasema,

"Hapana, haiwezekani."

Alirudi ndani ya kituo akiendelea kuwaza na kuwazua kuhusu gari lile.

Yawezakana ikawa ni modeli sawa lakini si gari lile.

Alijisemea mwenyewe.

Haiwezekani likawa limetoka San Fransisco, California mpaka New York. Ni safari ndefu. Kwa ndege tu ni takribani masaa nane kasoro.

Aliendelea kubishana na mawazo yake kichwani.

Ghafla akakumbuka jambo.

Ni kuhusu maelezo aliyopewa na 'boyfriend' wake Ronelle!

Alikumbuka vema bwana huyo akisema ya kwamba alimwona mmoja wa watu waliokuwamo katika gari linaloshukiwa na mauaji ya Ronelle.

Alisema hayo baada ya Mpelelezi kumweleza picha ya gari lililobeba wahalifu.

Kwa maneno yake, bwana huyo alisema aliliona gari hilo akiwa anaingia supermarket kununua bidhaa.

Lilikuwa limepaki kando, bwana mmoja akiwa amesimama ameshikilia sigara mkononi.

Alipomuuliza sifa za bwana huyo, majibu yake yakawa tata.

Sifa hizo zilikuwa zinawiana na Babyface.

Mpelelezi akayatoa macho akiketi kama mtu aliyeishiwa na nguvu.

**
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 21


Na Steve B.S.M




"Nilimwona mwanaume mwenye nywele stadi, amevalia suti nyeusi akiwa na sigara mkono wake wa kushoto.

Sikumtilia sana maanani kwasababu nilikuwa na shughuli zangu zingine. Lakini kwa nilipomwona, kwasababu ya unadhifu na umaridadi alokuwa nao, nilimtazama kwa kiasi chake kama vile watu wengine wanapowatazama watu waliopendeza huko barabarani.

Gari la gharama kubwa alilokuwa nalo, suti kali aliyovaa na mwonekano wake wa kuvutia, vilikuwa bora sana.

Japo sikumpatia mazingatio kama mtu ninayemfahamu lakini nikimwona hata keshokutwa bado n'taweza kumtambua."

Mpelelezi aliisikia vema sauti ya boyfriend wake Ronelle katika ngoma za masikio yake, na kichwani, alikuwa anapata picha halisi ya bwana huyo akiwa anaongea.

Alikuwa anakumbuka kila kitu, kila jambo. Kila alichosema na kila alipoweka kituo.

Kwa maelezo yalivyokuwa yanataririka katika kumbukumbu yake, alizidi kuamini yanamhusu bwana mmoja ambaye yu karibu naye.

Si mwingine bali Babyface.

Lakini kwanini ashiriki kwenye mauaji ya Ronelle?

Huu ukawa mwanzo wa kuyafikiria mengi. Kuanzia namna alivyokutana na Babyface. Namna alivyoanza kufanya naye kazi kwa pamoja kwa makubaliano asiyoyakumbuka.

Mpaka kwenye namna video za watuhumiwa zilivyopotea kule Halletts Point, akielezwa na mhusika watu waliokuja kuzichukua.

Namna alivyohisi mawasiliano yake na Ronelle yamedukuliwa na mpaka kutokea kifo cha mwanamke huyo.

Zaidi namna ambavyo kesi hii imegubikwa na usiri kutoka upande wa pili. Kwanini hawako wazi juu ya matakwa yao katika jambo hili?

Kwanini watuhumiwa wa The DL?

Na kama lengo ni kuwapata kwanini wanatokomeza nyayo zinazoweza kukamilisha mchakato huo?

Akafungua droo ya meza yake.

Droo ya kwanza kabisa upande wake wa kuume.

Akatupia macho yake humo.

Miongoni mwa vitu vingi viliyvyokuwamo, kulikuwa na kijidaftari kidogo chenye jalada gumu la rangi ya pinki.

Jalada hilo likipambwa na stika mbalimbali za katunikatuni za kike: wasichana wenye nywele ndefu na macho makubwa yanayometameta.

Pembeni ya kijidaftari hiko, kulikuwa na kijikabrasha kidogo mithili ya vile vinavyowekewa pete.

Rangi yake ni nyeusi.

Mpelelezi akakitazama kijikabrasha hiko na kukinyakua.

Akakifungua.

Ndani yake kulikuwa na risasi (bullets) mbili zilizojilalia.

Akaichukua risasi moja na kuitazama kwenye kitako.

Hapo palikuwa na namba kadhaa. Namba ambazo tayari ameshazikariri kichwani.

Alizitamka namba hizo moja baada ya nyingine kisha akakunja ngumi kuificha risasi hiyo na kiganja chake.

Alijiwazia jambo.

Hapo kumbukumbu zake zikampeleka mbali mpaka siku ile kifo cha Ronelle kilipojiri.

Alikumbuka namna alivyokuwa amesimama peke yake akitafakari, mtaalamu wa sayansi ya upelelezi wa miili akamjia na kumsalimu.

Alikuwa ni mwanamke aliyevalia koti na kofia ya bluu iliyokoza zenye na maneno makubwa ya njano; POLISI.

Mwanamke huyo alimwambia ameelekezwa kuwa yeye ndo' mpelelezi anayehusika na kesi hiyo hivyo kuna mzigo alikuwa anataka kumpatia.

Alisema,
"Hizi ni risasi mbili zilizotamatisha uhai wa Ronelle. Zote zina serial numbers. Pengine zinaweza kusaidia kwenye uchunguzi."

Mpelelezi akapokea kifuko kidogo cha nylon ambacho ndani yake kama alivyoelezwa, kulikuwa na risasi mbili.

Akakiweka kifuko hiko ndani ya mfuko wa ndani wa suruali yake kwaajili ya usalama zaidi.

Alipokumbuka hayo, akakirejesha kikabrasha hiko ndani ya droo ya meza yake, kisha akakinyakua kile kidaftari chenye jalada la pinki.

Kidaftari hiko kilionekana ni cha muda kiasi, kama si hivyo basi hakikuwa kinapata matunzo sawia.

Kilijawa na vumbi, na baadhi ya kurasa zake zilikuwa zimeshikana.

Mpelelezi alikifungua akaanza kupitisha macho yake taratibu.

Kwenye kurasa yake ya kwanza palisomeka hivi;

"Hii ni diary yangu kipenzi. Mama yangu ameniletea kama zawadi baada ya kuona mimi ni mkimya sana, hivyo humu nitapata nafasi ya kuongea na kupiga kelele kadiri nitakavyo."

Kwa chini ya maneno hayo, kulikuwa na umbo la moyo. Lilichorwa na kupakwa rangi nyekundu ya kalamu.

Mbali na hayo, kulikuwa na stika kadhaa hapo, za wanyama na wasichana.

Mpelelezi akafungua ukurasa wa pili ....

Katika siku za nyuma: kule San Fransisco, California.

Mpelelezi alirusha macho yake nje ya basi akiwa anatafakari mambo.

Alimuwaza yule mwanamke aliyemkarimu nyumbani kwake baada ya kupoteza fahamu kule Casino, na pia yule mwanaume wake wa ajabu.

Aliwaza usalama wa mwanamke yule haswa baada ya kuona walihitilafiana na yule mwanaume kabla hawajatoka katika makazi yale.

Lakini pia akawaza simu ambayo mwanamke yule aliipokea na kuongea nayo kabla hajashuka kutoka kwenye gari lake akaelekea kwenye kituo cha basi.

Haya yote yakamchanganya.

Alikuwa hayaelewi kabisa.

Achilia mbali maswali yake alokuwa nayo juu ya mwanamke huyo hayakupata wasaa wa majibu.

Akaegemeza kichwa chake kwenye kioo cha dirisha. Kidogo akaja mzee fulani akaketi pembeni yake.

Alikuwa ni mwanaume aliyevalia kofia aina ya 'newsboy' rangi ya kijivu na koti kubwa jeusi. Mikononi amevalia gloves yenye 'material' ya sweta.

Usoni ana ndevu nyingi nyeupe. Pua yake nyembamba ndefu, ina masizi kwa juu.

Kwa mwonekano wake, alikuwa ni mtu wa kuombaomba asogeze siku.

Alimsalimu Mpelelezi kwa bashasha kisha akatulia.

Mpelelezi, akiwa bado ameegamia kioo cha dirisha, alijibu salamu hiyo kisha naye akaendelea na mambo yake.

Akitazama mandhari huku anafikiri.

Kidogo tu, mzee yule akaanza porojo na hadithi.

Alikuwa ni mtu mwenye maneno mengi sana, akicheka na kuteta kana kwamba kuna mtu aliyekuwa anamtilia maanani.

Kwa makelele yake, watu kadhaa walilazimika kumtazama kisha wakamjadili kama mtu asiyekuwa na akili timamu.

Lakini muda wote huo, Mpelelezi aliyekuwa amekaa kando yake hakuwa anajali.

Alikuwa yuko mbali kwa mawazo.

Mawazo ambayo yalimnyima nafasi ya kumtazama jirani yake pamoja na kelele zake hizo.

Yule mzee naye akaendelea. Akaongea na kucheka. Muda mwingine akigonga mikono yake kwa kufurahishwa na maongezi yake binafsi.

Kwa kama dakika tano hivi, mchezo ukawa vivyo hivyo.

Ikafikia kipindi Mpelelezi akashindwa kumpuuzia.

Akamwita,

"We mzee!"

Mzee yule akamtazama kwa tabasamu pana. Meno yake yalikuwa machafu sana. Macho yake pia yamejawa na matongotongo.

Mpelelezi akamtaka bwana huyo anyamaze hata kidogo kwani anachosha.

Alisema,

"Huoni hamna mtu anayekuskiza? Tunza nguvu zako kwaajili ya mambo mengine."

Mzee yule akatahamaki. Akatazama kushoto na kulia, mbele na nyuma alafu akajitetea akisema watu hao wote walikuwa wanamsikiza isipokuwa yeye tu, hivyo kama hataki basi anyamaze na kuendelea na shughuli zake.

Alisema,

"Usinisumbue!"

Kisha akaendelea kama vile hakuna kilichotokea.

Aliongea na kucheka mwenyewe. Akapiga makofi na kushangilia.

Mpelelezi alipoona maneno yake hayana msaada, akanyanyua shingo kutazama kama kuna viti vingine ndani ya basi ambavyo vina nafasi.

Akakiona kimoja mwishoni kabisa.

Akanyanyuka akiendee kutafuta amani.

Kwasababu viti vilikuwa vimejibana, akakatiza kwa tabu kwa mzee yule lakini mwishowe akafanikiwa.

Akashika korido ya basi na kwenda nyuma kabisa. Huko aliketi akatulia.

Alilalamika kumhusu bwana yule kwa usumbufu wwke lakini si muda mrefu akawa amemsahau.

Alibaini mazingira yamekuwa kimya sana. Hakuna kelele tena.

Aliporusha macho yake kutazama, akaona kiti kile kilichokuwa kimekaliwa na yule mzee kikiwa tupu!

Alitazama pembeni ya kiti hiko pia, kote kulikuwa tupu. Viti vyote viwili vilikuwa wazi, havina mtu!

Yule mzee alishashuka.

Akajikalia kwenye kiti chake na kupuuzia hayo yote. Safari ikaendelea.

Alifika huko alipokuwa anapoelekea yakiwa ni majira ya jioni. Jua lilikuwa limepoa. Taratibu kiza kinaanza kumeza uso wa dunia.

Alitazama saa yake kisha akatoka hapo kituoni mwa basi akielekea upande wa mashariki wa mji.

Kabla hajafika mbali, akahisi kitu.

Aligutuka kwelikweli.

Moyo wakw ulipasuka akiyatoa macho.

Akajipapasa mifukoni.

Hola!

Hakuwa na simu!

Akiwa ameyakodoa macho, aliendelea kujipapasa kama mtu asiyeamini anachokihisi.

Lakini haikujalisha yote alofanya, bado simu hazikuwapo.

Akatafuta mahali hapo kwenye kituo, akaketi na kutafakari.

Aliacha wapi simu?

Hakuacha mahali ... Aliacha ku ... Hapana ... Hakuacha kule ... Kumbukumbu zake zikagotea kwenye basi.

Hayaa!

Akashika kichwa chake.

Ni yule mzee! ... Nafsi yake ikasema ... Hakika ni yule mzee pale alipopishana naye kwenye kiti!

Nimekuaje mzembe kiasi hiki? Alijilaumu kwa makosa yake.

Simu yake na pia ya Ronelle ambayo ingemsaidia kwenye upelelezi sasa hazikuwapo.

Hata kama akija kuzipata, basi taarifa zake muhimu hazitakuwapo tena.

Hasara iliyoje hii?

Hakuwa na budi, akanyanyuka kuendelea zake na safari.

Lakini safari hii sasa ikiwa na ugumu kiasi kwasababu ya kupoteza mawasiliano.

Alichobakiwa nacho ni kumbukumbu ya taarifa tu kichwani mwake.

Kumbukumbu ambayo haikuelekeza vema mpaka anapoelekea, zaidi ya mji tu ambao familia ya mlengwa wake ndipo inapopatikana.

Kwa kutumia kumbukumbu hizo, ndani ya lisaa akawa amefika katika mji husika. Hapo ikabidi atumie tukio la mlengwa wake kujinyonga ili apate mwelekeo kwa urahisi.

Akaulizia familia iliyowahi kukumbwa na mkasa huo. Hapo alipoulizia watu watatu wanne, akawa amepata anachohitaji.

Alifika mbele ya makazi hayo, akasimama kuitazama nyumba hiyo kwa ukaguzi.

Ilikuwa ni nyumba ya wastani, si kubwa wala haikidhi kusema ni ndogo.

Rangi yake ilikuwa samawati iliyopauka. Madirisha yake makubwa ya vioo. Fensi ndogo ya mbao, na geti dogo la chuma.

Ndani ya fensi hiyo kulikuwa na bustani hafifu ya majani.

Hakukuwa na ua hata moja.

Kibaraza chake kidogo kilikuwa na kiti kimoja kinachoning'inia. Umbo la kiti hicho ilikuwa ni kama tufe lililokatwa.

Mwanga hafifu wa taa iliyokuwepo kibarazani ulimulika kwa uwezo wake. Shukrani bado Jua halikuwa limezama vema hivyo matumaini kwenye mwono wa macho bado yalikuwapo.

Mpelelezi alipotazama eneo hili na kujiridhisha, akasukuma geti apate kuingia ndani. Geti halikufunguka.

Alijitahidi kulisukuma lakini hakufanikiwa, zaidi geti likapiga kelele kwa ukuukuu wake.

Alitazama komeo, hakuliona. Hakuelewa geti hili limefungwaje.

Akiwa anahangaika, akasikia sauti ya kike ikisema kwa ukali,

"Wewe ni nani katika eneo la watu?"

Akarusha macho kutazama. Hakumwona mtu.

Alitazama madirishani na mlangoni, hakukuwa na alama yoyote ya mtu.

Sauti ikarudia tena,

"Unataka nini?"

Mara hii sauti ilikuwa kali zaidi.

Kwa sauti hiyo, mpelelezi akabaini anayemwongelesha ni mwanamke fulani mtu mzima, na sauti hiyo inatokea ndani ya jengo.

Akajitambulisha yeye ni polisi. Alifanya hivyo akionyeshea 'badge' yake ya kazi, basi katika namna asiyoelewa geti likafunguka na kukaa wazi.

Akazama ndani.

Alifungua mlango akajikuta sebuleni.

Humo alimkuta mwanamke mzee, makamo ya miaka hamsini hivi, akiwa amesimama anatazama kwa kukunja ndita.

Mwanamke huyo alikuwa na nywele nyeupe na nyeusi. Mwembamba aliyekongoroka. Mwili wake umefunikwa na gauni la kulalia, rangi ya fedha.

Mkononi alishikilia bunduki kubwa aina ya gobore.

Sebule hii ilikuwa kubwa lakini haba kwa samani zake.

Kochi lilikuwapo moja tu na meza ndogo ya mbao.

Mpelelezi alitamani kuketi lakini mwenyeji wake bado hakumpa ruhusa. Alimsalimu lakini hakumjibu.

Zaidi akamuuliza,

"Unataka nini?"

Mpelelezi akaeleza haja yake ya kwamba yupo hapo kwaajili ya binti wa familia hii aliyewahi kujinyonga hapo nyuma.

Alipomaliza tu kusema hayo, mwanamke huyo akaanza kushukwa na machozi.

Kwanini?

Ni nini kilimuua mwanamke huyo?

Nini mpelelezi alipata huko San Fransisco?
 
Nime kuja kutoa maoni ili kuweka alama uzi huu nikiwa na utulivu niupitie wote kwa ufasaha
 
Back
Top Bottom