...Nakumbukia ajali ya kusikitisha ya MV Bukoba... R.I.P waTz wenzetu zaidi ya 1000 waliopoteza maisha; hivi wahusika walosababisha uzembe ule waliishia wapi na kesi yao?
Walishinda kesi.
Hakukuwa na uzembe!
Miaka minne nakala ya hukumu kesi Mv Bukoba haijatolewa
Mwanchi
7/12/2008
Na Frederick Katulanda, Mwanza
SERIKALI imekwama kukata rufaa katika kesi ya inayowahusu watuhumiwa wa ajali ya meli ya Mv Bukoba, kwa miaka minne kutokana na Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, kushindwa kutoa nakala ya hukumu ya kesi hiyo, imefahamika.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili, unaonyesha kuwa serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kanda ya Ziwa, imekuwa ikihangaika kupata nakala hiyo bila mafanikio.
Hali hiyo imewafanya watuhumiwa wa kesi ya ajali hiyo kushindwa kujua hatima yao ya kurejeshwa kazini huku serikali ikiinyooshea kidole mahakama kutokana na kukalia kesi hiyo.
Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Novemba mwaka 2004 na Jaji Juxton Malay na watuhumiwa wake watatu kuachiwa huru, mpaka sasa nakala yake haijatolewa kwa madai kwamba, haijaandikwa na Jaji husika, hivyo mahakama kushindwa kutoa nakala yake kwa serikali na washtakiwa.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Mwanasheria wa Serikali, Kanda ya Mwanza, Edwin Kakolaki, licha ya kuwasilisha ombi la kukusudia kukata rufaa mara baada ya hukumu hiyo kusomwa, mpaka sasa bado serikali (mlalamikaji) inafuatilia nakala ya hukumu bila mafanikio.
"Hii inatusikitisha hata sisi, ofisi yangu imekuwa ikifuatilia kila mara kutaka kujua kama nakala hiyo imetoka ili tuweze kukata rufaa, lakini kila siku tumekuwa tukiambiwa bado, tunangoja, tatizo sasa limekuwa ni kwa washtakiwa ambao nao wamekuwa wakifika hapa kila mara kutaka kujua kwa vile kukosekana kwa nakala hiyo kunatunyima muda wa kukata rufaa na wao kutambua hatima yao, kama watarejeshwa kazini na kulipwa haki zao au la," alieleza Kakolaki.
Watuhumiwa wa kesi hiyo ni aliyekuwa nahodha wa meli hiyo, Jumanne Rume Mwiru, Prosper Lugumila pamoja na Alfonse Sambo.
Kakolaki alifafanua kuwa ofisi yake ilipeleka ombi la kukata rufaa Mei mwaka 2005, ikitarajia ikitoka nakala ya hukumu na mwenendo wa mashtaka itaendelea na utaratibu wa kukata rufaa, lakini mpaka leo bado hawajaipokea.
"Kutokana na hali hiyo, sina la kueleza kama msimamo wa serikali kwa vile sasa ni muda mrefu, nadhani mnaweza kuwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Elieza Fereshi, ili kusikia msimamo wa serikali kutokana na kuchelewa kwa nakala hiyo," alieleza.
Hata hivyo, habari nyingine kutoka ndani ya mahakama hiyo zinaeleza kuwa, kumekuwa na udhaifu wa kuandika nakala za hukumu za kesi mbalimbali katika mahakama hiyo.
Chanzo chetu kimoja kilieleza kuwa, kwa kawaida hukumu ya kesi huwa inasomwa mahakamani ndipo hukabidhiwa kwa mahakama ili ichapwe kwa ajili ya kumbukumbu za mahakama na walalamikaji au watuhumiwa, lakini hii ilisomwa tu na jaji bila kutolewa nakala hadi sasa.
Chanzo hicho pia kimeeleza kuwa kukwama kutolewa nakala hiyo ya hukumu kumetokana na Jaji Juxton Mlay kuwa na mzigo wa kesi nzito zipatazo 70 ambazo alizihukumu zikingoja kuandikiwa hukumu licha ya kupatiwa likizo ya mwezi mmoja maalumu kwa ajili ya kazi hiyo mwaka juzi.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Elieza Feleshi alisema, wanaendelea kusubiri nakala ya hukumu ya kesi hiyo ili waweze kuangalia mwenendo wa kesi kabla ya kukata rufaa.
Alisema katika hali ya kawaida huwezi kukata rufaa bila ya kuangalia mwenendo wa kesi ulivyokuwa; na kwamba kama wataridhika na uamuzi wa hukumu hiyo wataacha na endapo hawataridhika watakata rufaa.
Feleshi alisema wanaiomba mahakama iharakishe kutoa nakala ya hukumu ili waweze kutoa uamuzi wa ama kuendelea na kesi au la.
Kama serikali haitakata tena rufaa, hatua hiyo itafungua mlango kwa washtakiwa kulipwa haki zao na hata kurejeshwa kazini na Shirika la Reli Tanzania (TRC), au Marine Services.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, aliiambia Mwananchi Jumapili kwa simu kuwa, washtakiwa hao akiwamo aliyekuwa nahodha Rume Mwiru walikwenda ofisini kwake kumwomba awasaidie kulipwa kutokana hukumu kuchelewa kutolewa.
Alisema aliiandikia barua Kampuni ya Marine akiwaelezea kuchelewa kutoa nakala ya hukumu na kwamba huenda mpaka sasa wameshalipwa haki zao.
Kuhusu kuchelewa kutoka kwa nakala ya hukumu, Jaji Ramadhani alisema kumetokana na mkorogano wa kiutendaji fulani, lakini bado wanalishughulikia kiutawala.
Hata hivyo, bila kufafanua zaidi alisema, anashughulikia Jaji aliyehusika na hukumu hiyo.
Meli ya Mv Bukoba ilizama mwaka 1996 na kuua watu zaidi ya 1,000 wakati akiwa karibu kutia nanga katika Bandari ya Mwanza mjini.