Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, amesema tume hiyo imeanza kazi ikiwa na hadidu tano za rejea zitakazoongoza uchunguzi wake na kubainisha upana pamoja na mipaka ya mamlaka yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24, 2026, Jaji Lila amesema lengo kuu la tume hiyo ni kwenda hatua zaidi ya uchunguzi wa matukio kwa kubaini watu waliohusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kutekeleza ghasia na ukiukwaji wa sheria uliojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hadidu ya kwanza, amesema, ni kuchunguza na kubainisha wahusika wa ghasia pamoja na namna kila mmoja alivyoshiriki katika kupanga, kufadhili, kuratibu au kutekeleza shughuli zilizohusiana na ghasia hizo.
Amesema eneo hilo la uchunguzi linatokana na maelezo yaliyotolewa katika ripoti ya Tume iliyotangulia, iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande, ambayo ilibainisha kuwa ghasia na fujo zilizotokea hazikuwa za bahati mbaya, bali zilidaiwa kuwa zilipangwa, kuratibiwa, kufadhiliwa na kutekelezwa kwa mpango maalum.
Hadidu ya pili ni kuchunguza matukio mahsusi yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi, ikiwemo suala la vifo visivyokuwa vya kawaida vya watoto na watu wa makundi maalum.
Ya tatu ni kuchunguza matukio ya watu kupotea katika maeneo yaliyokumbwa na ghasia na uvunjifu wa amani tangu kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Aidha, hadidu ya nne inahusu kuchunguza madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi pamoja na kubaini iwapo taratibu na miongozo iliyowekwa ilizingatiwa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Hadidu ya tano ni kuchunguza suala lolote ambalo Tume itaona ni muhimu na linalohusiana na majukumu yake.
Jaji Lila amesema hadidu hizo tano ndizo zitakazoainisha upana wa kazi na mipaka ya mamlaka ya Tume katika kutekeleza uchunguzi wake.
Amesema Tume hiyo pia itachunguza chanzo cha madhara mbalimbali yaliyotokea kutokana na ghasia na uvunjifu wa amani, ikiwemo vifo, majeruhi na watu waliopotea.
Akizungumzia ripoti ya Tume ya awali, Jaji Lila amesema Tume iliyoongozwa na Jaji Chande ilibainisha vifo vya watu 518 katika matukio hayo, huku ikieleza kuwa idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na baadhi ya waathirika kutofikiwa na utaratibu wa utambuzi.
“Tume ya Mheshimiwa Jaji Chande ilibainisha kuwa kulitokea vifo na ikataja kwa mujibu wa uchunguzi wao kwamba walibainisha vifo vya watu 518, lakini pia tume ile ilisema inawezekana idadi ni zaidi ya hapo kwa sababu si wote walipita kwenye utaratibu ambao wangeweza kutambuliwa,” amesema Jaji Lila.
Kwa mujibu wa Jaji Lila, Tume anayoiongoza ina jukumu tofauti na Tume ya Rais iliyokuwa chini ya Jaji Chande, ambayo ilijikita katika kuchunguza matukio ya ghasia yaliyotokea na kubaini aina ya vurugu, ghasia na uvunjifu wa amani uliojitokeza.
Amesema Tume ya Jaji Lila imepewa jukumu la kwenda hatua zaidi kwa kuchunguza wahusika wa kupanga, kuratibu, kufadhili na kutekeleza matukio hayo, pamoja na kuchunguza aina na kiwango cha nguvu iliyotumika katika kuyadhibiti.
“Sisi tumepewa jukumu la kwenda kuangalia wahusika ni kina nani, waliopanga, walioratibu, waliofadhili, waliotekeleza. Halafu pia tuangalie masuala ya madhara kwa maana ya watu wameumia, watu wamefariki kutokana na ghasia zile nani wahusika, na aina na kiasi cha nguvu kilichotumika kwenye kudhibiti zile ghasia. Thamani ya mtu hailinganishwi na kitu kingine chochote,” amesema Jaji Lila.
Tume hiyo, maarufu kama Tume ya Jaji Lila, iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa rasmi Agosti 7, 2026. Ina jukumu la kuchunguza wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa sheria katika matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mstaafu Shaban Ally Lila na inahusisha majaji wastaafu pamoja na majaji kutoka nje ya Tanzania. Imepewa muda wa miezi mitano kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wake.
Soma pia: Rais Samia: Tumeamua kuwashirikisha wenzetu kutoka Uganda na Namibia kupata muono mpana. Tume inakwenda kutafuta nani walichochea, waliotoa fedha