Ndugu zangu watanzania, nawasalimu!
Najitokeza hapa kutoa mawazo, maoni uelewa na uchambuzi wangu wa kisheria na kiuhalisia juu ya Tamko la ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar. Natumai watanzania wengi wameshaona au kusikia kauli hiyo ya ZEC iliyotolewa na Mwenyekiti wake Mh. Jecha. Nitakwenda taratibu ili ukianza mjadala uwe umenyooka na wenye mashiko.
Kwanza kabisa nikiri kutokuona kifungu chochote cha Sheria kinachompa mamlaka Mwenyekiti wa ZEC kutoa tamko/taarifa aliyoitoa kuhusu kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar. Ingawa ni kwa haraka, nimepitia the Zanzibar Electoral Commission Act, 1992 (inayoanzisha na kuipa kazi ZEC) na the Election Act No. 11 of 1984 (inayoratibu chaguzi za Zanzibar) lakini sikuiona mamlaka ya Mwenyekiti wa ZEC ya kufuta uchaguzi mzima.
Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (the Zanzibar Electoral Commission Act, 1992),chini ya kifungu cha 5, inaipa ZEC kazi ya kuratibu na kusimamia chaguzi za Urais,Uwakilishi na chaguzi za Serikali za Mitaa,pamoja na mambo mengine. Ndiyo kusema, ZEC husimamia chaguzi za ndani ya Zanzibar za ngazi tajwa. Ndiyo NEC ya kule Zanzibar. Naamini kwamba hata kwa Urais wa Muungano, ZEC husimamia uchaguzi huo kwa niaba ya NEC.
Nasisitiza kuwa ZEC, kwakuwa sikuona, haina mamlaka ya kufuta uchaguzi. Ingeweza kuahirisha upigaji kura na kadhalika kama kungekuwa na hali ya sintofahamu kama inavyotakiwa na kifungu cha 74 cha Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 (the Election Act No. 11 of 1984). Sasa ZEC imeshafuta uchaguzi mzima wa Zanzibar. Nini madhara yake kwa uchaguzi huu wa Tanzania hasa kwa ngazi ya Urais na Ubunge?
Inafahamika kuwa Wazanzibari walishiriki pamoja nasi kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kiuhalisia, kila mpigakura Mzanzibari,siku ya kupiga kura, alipiga kura za aina nne: Rais wa JMT, Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Wabunge.
Ni kura ile ile ya mpiga kura yule yule iliyohesabiwa sehemu zote nne. Kura hii ikiwa halali sehemu moja, itakuwa halali sehemu zote na kinyume chake kitakuwa sahihi, yaani, ikiwa batili sehemu moja ni batili sehemu zote. Hii ni kwakuwa idadi ya wapiga kura wa nafasi zote nne ni ile ile;vituo ni vile vile na hata wasimamizi ni wale wale.
Kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar, katika uhalisia na sheria, ni kufuta kura zote zilizopigwa huko Zanzibar. Hata zilizotumwa kwa NEC kwa ajili ya Urais na Ubunge wa JMT zimekuwa batili.
Kwahiyo, kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hazitatimia kwakuwa zile za Zanzibar zinapaswa kuondolewa kwakuwa zimetamkwa kuwa si kura halali. Hata Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halitaanza na kutimia bila Wabunge wa Zanzibar kwakuwa kura za Wabunge wa kutoka Zanzibar zinapaswa kurudiwa.
Ndiyo maana nasema kuwa ZEC, kwa tamko/taarifa ao ya leo, wanakwamisha hata uchaguzi wa Urais na Ubunge wa Tanzania nzima kwakuwa bila ya kura na Wabunge wa Zanzibar, hakutaundika hata Serikali wala kupatikana Rais wa Muungano. Niko tayari kufahamishwa vinginevyo.