Tunaishi Katika Zama Ambazo Ulinzi wa Kidigitali ni Hitaji Muhimu Sana kwa Kila Taasisi

Tunaishi Katika Zama Ambazo Ulinzi wa Kidigitali ni Hitaji Muhimu Sana kwa Kila Taasisi

The Sheriff

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2019
Posts
747
Reaction score
2,112
ULINZI WA KIDIGITALI.jpg


Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko la matumizi ya simu janja, mitandao ya kijamii na biashara ya mtandaoni. Kupitia njia hizi na nyinginezo, sote tunaweka taarifa zetu binafsi kwenye mtandao zaidi na zaidi.

Kila siku mamilioni ya watu huwasha kompyuta na vifaa vyao vya kidigitali wakiwa na lengo la kutuma, kupokea, kushiriki, kubadilishana, kutafuta au kutoa taarifa za aina yoyote. Hata hivyo, maendeleo haya ya teknolojia ya habari, pamoja na uzuri wake, yana changamoto zake na ni watumiaji wachache wanajua kuhusu mambo mabaya wanavyoweza kukumbana nayo mara tu baada ya kubofya vitufe.

Pamoja na changamoto nyingine zinazoambatana na maendeleo hayo, kuna suala la mashambulizi ya mtandaoni (cyber-attacks) na matokeo mabaya ambayo yanaweza kusababishwa nayo. Siku hizi, kwa mfano, biashara au hata nyanja yoyote ya maisha binafsi lazima inahusiana kwa njia fulani na uhifadhi wa data kidigitali. Kwa hivyo, kutunza data hizo kwa usalama wa hali ya juu si jambo la kufanya kwa maamuzi ya “liwalo na liwe” tena - ni jambo la lazima kabisa.

Leo tunategemea teknolojia kwa michakato mingi inayofanyika ndani ya mashirika na taasisi mbalimbali. Hii ni kuanzia utumaji na upokeaji wa nyaraka hadi miamala ya mamilioni ya fedha. Kwa kuwa kazi hizi zinafanywa kwa kutumia teknolojia, zinaweza kuathiriwa na mashambulizi ya mtandaoni.

Mashambulizi haya yanaweza kuvuruga utaratibu wa kila siku wa taasisi hizi, lakini matatizo makubwa zaidi ambayo hii inaweza kusababisha ni uharibifu mkubwa wa kifedha na sifa/hadhi. Kuna visa vingi vya kampuni kudukuliwa katika miaka ya hivi karibuni.

Lakini pia, si makampuni tu. Watu binafsi nao wamekuwa walengwa wa mashambulizi haya kwa kiasi kikubwa. Taarifa binafsi zinazotolewa kwenye jukwaa lolote mtandaoni, kama vile akaunti za mitandao ya kijamii au akaunti za benki mtandaoni, zinaweza kutumiwa na walaghai kuiba utambulisho au pesa.

Kwa mujibu wa Ripoti ya INTERPOL ya Tathmini ya Matishio ya Mtandaoni kwa Nchi za Afrika ya 2021, ulaghai/utapeli wa mtandaoni ni moja ya matishio makubwa zaidi ya kiusalama wa mtandaoni (27%) barani humo.

Hata hivyo, Vitisho vya mtandao vinaweza kuja kwa aina tofauti, kama vile kuwahadaa watumiaji kufichua taarifa binafsi au za kifedha, ulaghai wa kidigitali kwa kutishia kufichua picha za uchi/ ngono, au kudukua makampuni ya biashara ili kupata wafanyakazi wao na orodha za malipo ili kuwahadaa wafanyakazi kutuma kiasi kikubwa cha fedha kwa wahalifu.

Ripoti hiyo inaeleza pia kuwa katika mazingira ya uhalifu wa mtandaoni, Afrika imeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya mtandaoni, ikiwa ni pamoja na ongezeko la 238% kwenye majukwaa ya huduma za benki mtandao mnamo 2020.

Afrika ina zaidi ya watumiaji milioni 500 wa mtandao, jambo linaloweka eneo hilo mbele ya maeneo mengine kama vile Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, na Mashariki ya Kati. Kiasi hiki cha watumiaji kulingana na idadi ya watu ni sawa na karibu 38%, ambayo ina maana kwamba idadi inatarajiwa kukua katika miaka ijayo.

Huku kukiwa na ongezeko la mahitaji ya huduma za mtandaoni barani Afrika, bara hili limekuwa hatarini zaidi kwa vitisho mbalimbali vya mtandao, kwani takriban 90% ya biashara za Kiafrika zinafanya kazi bila hatua za kutosha za usalama wa mtandao.

Interpol.png

Ripoti iliyotolewa na Acronis, kampuni ya kimataifa inayoshughulika na masuala ya ulinzi wa kidigitali, inafichua vitisho vinavyoongezeka na hitaji la masuluhisho jumuishi ya ulinzi wa mtandao.

Ripoti hiyo iliyotolewa Machi, 2022 ambayo ilichunguza zaidi ya watumiaji na wasimamizi wa TEHAMA 6,200 katika taasisi mbalimbali kwenye nchi 22, imethibitisha kwamba mashirika bado yanachukulia ulinzi wa mtandao kama "kitu kizuri kuwa nacho", badala ya "kitu cha lazima kuwa nacho"

Nusu ya mashirika duniani kote hutenga chini ya 10% ya bajeti yao yote ya TEHAMA kwenye usalama wa kidigitali. Ni 23% tu ya mashirika duniani kote yanawekeza zaidi ya 15% ya bajeti yao yote ya TEHAMA katika usalama - hata licha ya hali ya usalama inayotisha.

Ukweli ni kwamba, kuna mashambulizi kwa taasisi za kibiashara. Na ni mashambulio yaliyofanikiwa pia, lakini hayapo sana katika vichwa vya habari. Washambuliaji hawabagui nani wanamshambulia na biashara huhifadhi wingi wa data nyeti binafsi kuhusu wateja na wafanyakazi, ambayo ni taarifa muhimu kwa mvamizi yeyote anayetaka kupekua na kuamua nani awe target ya baadaye.

Utafiti wa Acronis pia unasema 86% ya mashirika duniani yana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi ya mtandaoni yanayotekelezwa kisiasa – lakini wasiwasi huo hautafsiri uboreshaji wa ulinzi wao wa kidigitali.

Acronis.png

Tunaishi katika zama za kidigitali ambapo maisha yetu binafsi na ya kitaaluma yameunganishwa kwenye mtandao. Takribani kila mtu anatumia mtandao/ teknolojia, hivyo kuwapa wavamizi shabaha mpya. Kupitia mafunzo ya kutosha ya uhamasishaji wa usalama na mipango ya kulinda uhalifu mtandaoni, taasisi mbalimbali zinaweza kujifunza jinsi ya kujilinda kutokana na vitisho vinavyoibuka vya uhalifu wa mtandaoni.

Wadukuzi wanazidi kuwa werevu, wakitumia ubunifu na njia za kisasa za kupenya mitandao na mifumo ya TEHAMA. Hii inafanya kuwa muhimu kwa taasisi kutopuuza mafunzo ya usalama wa kidigitali na badala yake kuyajumuisha katika shughuli zao. Mafunzo haya kwa wafanyakazi si ya hiari tena bali ni lazima ili kushirikisha, kuwasiliana na kufanya kazi kwa tija ndani ya taasisi.

Wafanyakazi wanapokuwa na mafunzo bora ya ufahamu wa usalama, kunanakuwepo uwezekano mkubwa wa kufuatilia mara moja vitisho vinavyoweza kutokea na kuripoti matukio yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama na kuepusha usumbufu wa kiutendaji au upotevu wa fedha au hadhi ndani ya taasisi.

Hivyo, badala ya tasisi kuelekeza bajeti kubwa katika software na Artificial Intelligence pekee, ni muhimu pia kuwekeza kwa kiwango stahiki kwenye suala la usalama – ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo thabiti ya ulinzi lakini na mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyakazi.
 
Back
Top Bottom