Alicia Lissu, mke wa Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania,Tundu Lissu, amefunguka kuhusu mzigo mzito wa kiuchumi na kisaikolojia unaoikabili familia yake, akieleza kuwa anakabiliwa na wakati mgumu wa kulea watoto peke yake tangu mumewe alipokamatwa na kuwekwa kizuizini.
Tundu Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alikamatwa mwezi Aprili 2025 wakati wa kampeni za "Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi," na kwa sasa anakabiliwa na shtaka la uhaini ambalo halina dhamana na linaweza kupelekea adhabu ya kifo. Alicia, anayefuatilia mwenendo huo akiwa uhamishoni nchini Ubelgiji, ameiambia BBC Africa Eye kuwa hajazungumza wala kumwona mumewe kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa kutokana na vizuizi vya mawasiliano vilivyopo gerezani.
Katika mahojiano hayo ya kiutu (human interest), Alicia amekiri kuwa hali hiyo imemlazimu kubeba majukumu yote ya familia ghafla, jambo ambalo hakuwa amejizatiti nalo. "Kwa mara ya kwanza kabisa, nilijikuta kuwa sina msaada wowote kutoka kwa Lissu. Hakuwepo na pia hakuna msaada wa kifedha. Ninalazimika kujitunza pamoja na kuwalea watoto wetu," amesema Alicia, akieleza namna anavyopambana kuwatuliza wanawe waliopo masomoni nchini Marekani ambao wamejawa na hofu kubwa.
Hata hivyo, Alicia amesisitiza kuwa changamoto hizo na kumbukumbu za mapambano ya muda mrefu ikiwemo shambulio la risasi 16 la mwaka 2017 hazijafifisha fahari yake kwa mumewe, akimtaja kama kiongozi mwenye ujasiri wa kipekee asiyeweza kurudishwa nyuma na hofu.
Kwa upande wake, Serikali ya Tanzania imetetea mazingira ya nchi ikieleza kuwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya kiraia vimepanuliwa kwa kiwango kikubwa kuliko mataifa yote ya Afrika Mashariki. Mamlaka zimebainisha kuwa hatua dhidi ya kiongozi huyo zifuata sheria zote za nchi na kwamba kesi yake haiwezi kuingiliwa kisiasa kwa kuwa tayari iko mikononi mwa mhimili huru wa mahakama.
#TunduLissu #AliciaLissu #CHADEMA #S SiasaTanzania #Uhaini BBCSwahili SasaLive