Lissu amewakemea wamasai wa Ngorongoro kudanganya.
Asema waache kutumika vibaya. Abainisha ukweli kuhusu manufaa ya kuhama Ngorongoro.
Asema waache kutumika vibaya. Abainisha ukweli kuhusu manufaa ya kuhama Ngorongoro.
- Tunachokijua
- Kumeibuka taarifa yenye picha na nukuu inayoonekana kuwa ni ya Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA ikiwa na ujumbe unaodaiwa ni wa kiongozi huyo ukiwakemea Wamasai wa Ngorongoro kudanganya, ikifafanua huduma ambazo wanapewa baada ya kuhamishwa kwenye maeneo yao.
"Wanaohama kutoka hifadhi ya ngorongoro kisheria na kwa hiari hujengewa nyumba, wanapewa ardhi ekari mbili na nusu za kilimo na ekari tano eneo la malisho pamoja na shilingi milioni 10 hadi 15 na kusogezewa huduma zote za kijamii, waache kutumika" imesema nukuu hiyo iliyohifadhiwa hapa.
Ukweli upoje?
Katika kufuatilia uhalisia wa taarifa hiyo, JamiiCheck imewasiliana na Lissu ambaye amekana kuhusika na Nukuu hiyo na kueleza msimamo wake kuhusu yanayoendelea Ngorongoro.
Lissu amesema, "Hii sio ya kwangu. Mimi naunga mkono mapambano ya Wamaasai wanaopinga kuondolewa kwenye ardhi yao ya asili. Walioandika ujinga huu ni wale wanaotaka kuwaondoa."
Pia, ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck umebaini Agosti 18, 2024, Lissu alichapisha ujumbe unaokinzana na madai yaliyopo kwenye nukuu ya sasa.
"Wamaasai wa Ngorongoro wanapinga kuondolewa kwa nguvu kutoka Ngorongoro. Serikali ya Samia imewanyang'anya elimu, afya, maji & chakula. Imewafuta kwa maelfu kwenye Daftari la Wapiga Kura. Licha ya ukatili huu, wananchi hawa wamekataa kuondoka kwenye eneo lao. Mimi nawaunga mkono" aliandika Lissu kwenye ujumbe uliohifadhiwa hapa.
Tundu Lissu amekuwa mkosoaji mkubwa wa mpango wa kuhamisha wamasai kutoka eneo la Ngorongoro na Aprili 30, 2024 aliwahi kunukuliwa akisema Tanzania ina Rais asiye Mtanganyika anayeweza kwenda Ngorongoro akatoa amri kwa wanajeshi hawa, akasema fukuza wamasai wote ngorongoro wapeleke Msomera Handeni, 547Km kutoka ngorongoro.
Kauli ya Lissu ilipingwa mara kadhaa na viongozi na wanachama wa CCM wakiwemo Amos Makalla na Nape Nnauye ambao waliita kuwa kauli ya kibaguzi isiyopaswa kutoka kwenye kinywa cha kiongozi kama Lissu hivyo kuwataka watanzania waipuuze.