Informer
JF-Expert Member
- Jul 29, 2006
- 1,606
- 6,672
Toka: Geneva, Uswisi.
Waheshimiwa Wabunge salaam.
Poleni sana kwa mapambano na hongereni kwa kazi nzuri mnayoifanya. Naendelea kuifuatilia kazi yenu kwa ukaribu sana.
Bila shaka mlisikia kwamba nilipeleka malalamiko juu ya mambo niliyotendewa na Tanzania ya Magufuli kwenye Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) miezi michache iliyopita.
Bunge letu ni mwanachama wa IPU na hivyo linawajibika kuheshimu na kuzingatia haki za Wabunge wake kwa mujibu wa sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu na za Wabunge.
Wiki mbili zilizopita niliitwa kwenye kikao cha Kamati ya Haki za Binadamu ya IPU, Geneva, Uswisi, ili kutoa maelezo ya ziada kuhusu malalamiko yangu. Leo Kamati ya Haki za Binadamu ya IPU imetoa taarifa yake ya uchunguzi wa malalamiko hayo.
Kama mtakavyoona kwenye taarifa yenyewe, Kamati imetoa uamuzi muhimu sana kuhusu suala hili na kuhusu masuala ya haki za Wabunge kwa ujumla. Kamati ya Haki za Binadamu ya IPU imesema yafuatayo kuhusu malalamiko yangu:
1. Kamati imekubali kwamba malalamiko yangu yanakubalika chini ya Kanuni za Uchunguzi na Uamuzi wa Malalamiko za IPU na Kamati ina mamlaka ya kuyachunguza.
2. Kamati imesikitishwa sana na jaribio la mauaji dhidi yangu na tuhuma za kuhusika kwa mamlaka za kiserikali katika jaribio hilo. Mahsusi kabisa, Kamati imehoji vitisho vilivyokuwa vinatolewa dhidi yangu kabla ya shambulio; kuondolewa kwa walinzi wa eneo la makazi yangu muda mfupi kabla ya shambulio hilo; na kuondolewa na kupotezwa kwa kamera za CCTV kutoka kwenye jengo la makazi yangu. Kamati imeomba kupatiwa maelezo rasmi na ya kina kuhusu masuala haya, na taarifa rasmi kuhusu waliohusika na shambulio hilo na wale waliowatuma.
3. Kamati imesisitiza kwamba vitisho dhidi ya maisha na usalama wa Wabunge, vikiachwa bila kuadhibiwa, sio tu vinakiuka haki ya kuishi, ya kuwa salama na ya uhuru wa mawazo ya Wabunge, bali pia inaathiri uwezo wa Bunge kama taasisi kutekeleza wajibu wake.
4. Kamati imesikitishwa na kitendo cha mimi kuvuliwa Ubunge wakati sababu za kutokuwepo kwangu zikiwa zinajulikana wazi kwa mamlaka ya Bunge na umma kwa ujumla. IPU imeomba maelezo kutoka Bunge la Tanzania kuhusu sababu na hoja za uamuzi huo.
5. Kamati imesikitishwa kufahamu kwamba nilikamatwa na polisi mara kadhaa, na kwamba bado ninakabiliwa na mashtaka kadhaa ya jinai yanayoenda kinyume na haki zake za msingi za binadamu, na inapenda kupata maelezo rasmi kuhusu misingi ya kiushahidi na ya kisheria ya kila mojawapo ya mashtaka hayo.
6. Kamati inatambua kwamba ninataka kurudi Tanzania haraka iwezekanavyo, na inapendekeza kuwa ujumbe wa Kamati unisindikize wakati nitakaporudi, kwa imani kwamba kutembelea Tanzania kutatoa fursa ya kukutana na mamlaka za kiserikali, kibunge na kimahakama, pamoja na wadau wengine, ili kuiwezesha Kamati kuelewa suala hili vizuri zaidi.
7. Kamati inamuomba Katibu Mkuu wa IPU kuwasilisha uamuzi huu kwa mamlaka ya kibunge ya Tanzania na kuomba ruhusa ya kutembelea Tanzania kama ilivyopendekezwa.
8. Kamati itaendelea na uchunguzi wa malalamiko haya katika kikao chake kijacho.
Kama mtakavyoona kwenye taarifa ya Kamati, IPU imekuwa ikipokea malalamiko ya manyanyaso ya Wabunge, hasa wa vyama vya upinzani, kutoka sehemu mbali mbali duniani na kuyachunguza.
Kitu cha kufurahisha ni kwamba IPU imechunguza maamuzi ya kuwafukuza au kuwasimamisha Wabunge kuhudhuria vikao vya Bunge, vitendo ambavyo vimekithiri sana katika Bunge letu.
Ushauri wangu ni kwamba Wabunge wetu wote ambao wameathiriwa na vitendo hivi wawasilishe malalamiko yao kwa IPU ili yachunguzwe. Mtaona kwenye taarifa hii jinsi ambavyo malalamiko kutoka sehemu mbali mbali duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yameshughulikiwa.
Kufanya hivyo kutaongeza shinikizo kwa utawala huu wa mabavu, pamoja na uongozi wa Bunge. Angalau wananchi wetu, na Serikali ya Magufuli na Bunge la Spika Ndugai, watajua kwamba vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na za Wabunge wa upinzani zinamulikiwa taa na dunia.
Kama hili linakubalika, niko tayari kuwasaidia kuandaa hoja za kupeleka IPU au, bora zaidi, kuwaomba mawakili wangu wa London, yaani Amsterdam & Partners, kufanya hivyo kwa niaba yetu wote.
Wasalaam.
Tundu Lissu
Makamu Mwenyekiti Tanganyika.
Kwa taarifa zaidi, soma kiambatanisho hiki