Unajua mambo mengine yanafanywa kwa maagizo ya serikali dhidi ya vyama vya upinzani, hususa Chadema, kwa njia ya kitoto sana. Tunajua katika suala la haki za msingi zinapotafutwa mahakamani, huwezi kumwadhibu mtu wakati kesi haijaisha.
Sasa tuje upande wa hawa wanachama wawili wa Zanzibar waliofungua kesi dhidi ya Chadema, na Mahakama kuamuru shughuli za Chadema zisimamishwe wakati kesi hii ikiendelea. Hivi kweli leo mwanachama wa CCM akifanya hiki kilichofanywa na hawa wanachama wawili, wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chadema, Mahakama itaamuru CCM wasimamishe shughuli zao?
Huu ni uonevu unaovuka mipaka haupaswi kuvumiliwa na mtu yeyote mwenye akili timamu. Ni wazi kuna mtu yuko nyuma ya uonevu huu usiovumilika, hata akidai yeye ni kiongozi mzalendo, haitakii mema nchi yetu Tanzania.
Imefikia wakati tuanze kujiuliza kama kuna mamluki wamejipenyeza na kushika uongozi wa nchi, kwa lengo la kuihujumu Tanzania. Tunakumbuka kuwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, wale walioondolewa katika mapinduzi yale waliahidi wangerudi Tanzania kwa namna moja au nyingine na kulipiza kisasi, na ndio maana hawajali utekaji, uuaji au vifo vya Watanzania. Tuna mamluki hawa katika uongozi wa taifa?