Mtu mwenyewe anajichanganya, mara tumwabudu Yesu, mara Yesu ni Mungu, mara bila Yesu hatuwezi fika kwa Mungu ilimradi tafrani
Sikupenda kutoa elimu hii ya ndani sana kwa leo, lakini sina budi kufanya hivyo. Naomba nianze kueleza kwa kina kwanini tunasema Yesu ni Mungu. Vitabu vitakatifu vimeeleza wazi kwamba Yesu ni Mungu. Na hizi ndio sababu kuu zinazothibitisha kwamba Yesu ni Mungu.
1. YESU ALIKUWEPO KABLA YA KUZALIWA
Ufuatao ni ushahidi wa kibiblia kwamba YESU KRISTO ni Mungu.
Yohana 8:58
Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye IBRAHIMU ASIJAKUWAKO, MIMI NIKO.
NIKO ni jina la Mungu peke yake. Tunakutana na jina hilo pale Musa alipoongea na Mungu na kutumwa kuwakomboa wana wa Israeli kutoka Misri. Imeandikwa:
Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n’nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO (Kutoka 3:13-14).
Mwanadamu yuko kwa sababu Mungu alisababisha awepo. Gari liko kwa sababu injinia au mbunifu alisababisha liwepo. Nyumba ipo kwa sababu fundi alisababisha iwepo. Lakini Mungu YEYE YUKO TU!! Hayupo kwa kusababishwa na yeyote! Ndiyo maana akasema MIMI NIKO AMBAYE NIKO! Yesu ni NIKO. Kwa hiyo, Yeye ni Mungu.
2. YESU NA BABA NI WAMOJA
Yohana 10:30
Mimi na Baba tu umoja.
Waislamu wana msemo wao kwamba eti, Yesu na Mungu ni wamoja katika malengo, si katika asili yao. Basi huwa nawauliza swali kuhusu aya ifuatayo ya Isaya, nao wanazimika na kukosa jibu:
Isaya 9:6
Maana kwa ajili yetu MTOTO amezaliwa, Tumepewa MTOTO MWANAMUME; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, MUNGU MWENYE NGUVU, BABA WA MILELE, Mfalme wa amani.
Aya hii iko wazi kabisa. anayetajwa ni Yesu kwamba Yeye ni Mungu mwenye nguvu.
Yohana 14:9
Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? ALIYENIONA MIMI AMEMWONA BABA; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
Maneno haya Yesu aliyasema baada ya kuulizwa swali lililo wazi kabisa, ambalo lilikuwa na lengo la kumjua MUNGU BABA! Imeandikwa: Filipo akamwambia, Bwana, UTUONYESHE BABA, yatutosha. Ndipo Yesu akajibu waziwazi: ALIYENIONA MIMI AMEMWONA BABA. Maana yake ni kuwa, “Mimi ndio Baba mwenyewe.”
3. YESU NI MWANZO NA MWISHO
Ufunuo 1:17 na Ufunuo 22:13
Mimi ni wa kwanza na wa mwisho
Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.
Ni Mungu TU ndiye mwenye uwezo wa kuwa wa kwanza na wa mwisho; Yesu ni Alfa na Omega. Kwa hiyo Yeye ni Mungu.
4. YESU NI NENO
Yohana 1:1
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye NENO ALIKUWA MUNGU.
Andiko hili Waislamu hawalipendi kabisa. ni kwa sababu liko wazi mno. Yesu ni Neno; na Neno ni Mungu; hivyo, Yesu ni Mungu!
5. THOMASO AKIRI KUWA YESU NI MUNGU, NA YESU HAKUKATAA KUITWA MUNGU
Yohana 20:28
Tomaso akajibu, akamwambia, BWANA WANGU NA MUNGU WANGU!
Tomaso aliposema hivi, Bwana Yesu hakukanusha na kusema, “Mimi sio Mungu.” Badala yake: Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. (Yoh 20:29).
Kama Thomaso alikuwa muongo, kwanini Yesu hakukataa kuitwa Mungu. Imani zote zinakiri kuwa Yesu hakufanya dhambi na hakuwa na dhambi.
6. DAMU YA YESU INAMAMLAKA
Matendo 20:28
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, ALILOLINUNUA KWA DAMU YAKE MWENYEWE.
Ni Mungu gani mwenye damu huyu? Jibu liko wazi. Huyu ni Yesu Kristo. Huyu ndiye aliyetoa uhai wake na kumwaga damu yake msalabani; na hapo ndipo alipoanzisha Kanisa.
7. KATIKA YESU, KILA KITU KILIUMBWA
Wakolosai 1:16
Kwa kuwa KATIKA YEYE VITU VYOTE VILIUMBWA, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.
Katika Yeye Yesu vitu vyote viliumbwa. Ina maana kuwa vitu vyote vilitokana na Yesu; maana Yesu ni Neno la Mungu. Na tunajua kuwa Muumba wa vitu vyote ni Mungu; hivyo, Yesu ni Muumba – Yeye ni Mungu!!
8. KATIKA YESU, UNAKAA UTIMILIFU WA MUNGU
Wakolosai 2:9
Maana KATIKA YEYE UNAKAA UTIMILIFU WOTE WA MUNGU, kwa jinsi ya kimwili.
Sisi sote ni watu wasio wakamilifu. Tunaanguka tena na tena kwenye dhambi. Kwa hiyo, hakuna mwanadamu wa kawaida ambaye anaweza kujigamba kwamba yeye ametimia kama alivyo Mungu. Lakini katika Yesu “utimilifu WOTE wa Mungu unakaa.” Kwa nini? Kwa sababu Yeye ndiye Mungu huyohuyo.
9. YESU NI MUNGU PAMOJA NASI “EMMANUEL”
1Timotheo 3:16
Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. MUNGU ALIDHIHIRISHWA KATIKA MWILI, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.
Ni Mungu gani aliyedhihirishwa katika mwili? Jibu liko wazi. Ni Yesu Kristo peke yake.
10. YESU NI MUNGU MKUU NA MWOKOZI WETU
Tito 2:13
….tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU MKUU NA MWOKOZI WETU
Yesu Kristo ni Mungu Mkuu!!