Uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa Serikali ya Tanzania

Uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa Serikali ya Tanzania

Manyanza

Platinum Member
Joined
Nov 4, 2010
Posts
22,269
Reaction score
58,563
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyopo jijini Arusha imetoa uamuzi muhimu unaoitaka Tanzania kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Katiba vinavyohusiana na masuala ya uchaguzi na haki za kidemokrasia.

Uamuzi huo umetolewa Machi 6, 2026 katika kikao cha 80 cha mahakama hiyo baada ya kusikiliza kesi kadhaa zilizofunguliwa dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zikiwemo zilizowasilishwa na Abdul Omary Nondo, Deusdedit Valentine Rweyemamu na Paul Revocatus Kaunda, pamoja na Ado Shaibu na wenzake.

Katika maamuzi yake, mahakama hiyo imebainisha kuwa baadhi ya vifungu vya Katiba ya Tanzania na Katiba ya Zanzibar vinakiuka Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu kwa kuzuia mahakama kuchunguza au kuhoji maamuzi yanayofanywa na Tume za Uchaguzi.

Mahakama hiyo imeeleza kuwa kifungu cha 74(12) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kifungu cha 119(3) cha Katiba ya Zanzibar vinaweka zuio kwa mahakama yoyote kushughulikia masuala yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Tume za Uchaguzi, jambo ambalo limeonekana kukiuka haki ya wananchi kupata haki mahakamani.

Kutokana na uamuzi huo, Mahakama ya Afrika imeiamuru Tanzania kufanya marekebisho ya Katiba ili kuondoa vifungu hivyo vinavyoweka vikwazo kwa mahakama kuchunguza masuala ya uchaguzi.

Aidha, mahakama hiyo pia imeamua kuwa kifungu cha 41(7) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachozuia mahakama kusikiliza pingamizi dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Rais kinakiuka haki za msingi za binadamu, hivyo kuagiza kifungu hicho kirekebishwe ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Mahakama pia imeielekeza Tanzania kuchapisha hukumu hiyo kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwenye tovuti za Mahakama ya Tanzania pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria ndani ya miezi kadhaa, ili umma uweze kuipata na kuisoma.

Vilevile, serikali imeagizwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa maamuzi hayo kwa Mahakama ya Afrika ndani ya muda uliopangwa na kuendelea kutoa taarifa za maendeleo ya utekelezaji hadi mahakama itakaporidhika.

Katika kesi nyingine iliyowasilishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mahakama hiyo pia ilijadili suala la haki ya wafungwa na Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki katika uchaguzi. Hata hivyo, mahakama imehifadhi uamuzi wa mwisho wa hoja hiyo na kuendelea kushughulikia shauri hilo katika hatua zinazofuata.
 
Hivi SSH alijua kilichompeleka AfCHPR? Au ndo elimu mbali mbali hazimfanyi mtu kujitambua?
 
Back
Top Bottom