Ubepari ulivyoandaa misingi ya utandawazi na matokeo ya nchi zinazoendelea

Ubepari ulivyoandaa misingi ya utandawazi na matokeo ya nchi zinazoendelea

Elius W Ndabila

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2019
Posts
339
Reaction score
678
UBEBARI NAMNA ULIVYOJIKITA KUJENGA NGUZO YA UTANDAWAZI.

Na Elius Ndabila
0768239284

Historia inatufunza kuwa ubepari kama mfumo wa mahusiano ya kijamii hushamiri na kuendeshwa kwa kutegemea "udhaifu" wa upande mmoja katika mahusiano hayo. Ni wazi kuwa mfumo huu unaishi katika kuupalilia udhaifu wa watu kisha kutengeneza mnyororo usiokwisha wa kuwanyonya na kuwalaghai kupitia udhaifu wao walionao.

Imepita miaka mingi sana tangu Waafrika tuingizwe katika hatua za awali tu za ukuaji wa ubepari ulioasisiwa na ukoloni. Na kwa muda wote huo (kwa ujumla wetu) tumejikuta tukiwa upande dhaifu wa "mahusiano" hayo.

Watoto wadogo wanapozaliwa hawaingii moja kwa moja katika dhana ya utegemezi wa kiuchumi, fikra za kidhalimu n.k ila huingizwa na watangulizi wao kupitia mifumo ya kufikiri, taasisi za kijamii na utamaduni kwa ujumla. Vitu hivi vina mchango mkubwa katika kuitengeneza jamii ili jamii iweze kuchora mstari unaotenga "baya na jema","kizuri na kibaya","mambo yanayostahili kufanywa na yasiyostahili kufanywa",na namna "bora" ya kuyafanya mambo hayo, hivyo kuhalalisha matokeo.

Tunaishi chini ya mfumo wa kiuchumi(wa kibepari) ambao kidunia umetawaliwa na mataifa ya magharibi(Kwa sasa yakiongozwa na Marekani. Mfumo huu ni mfumo wa kidhalimu na kinyama sana, zaidi kwa sababu ulianzishwa, kukua na kustawi katika mazingira ya kidhalimu na kinyama. Kihistoria, huwezi kuzungumzia uwepo wa mfumo huu bila kutaja matukio kama biashara ya utumwa ambapo mamilioni ya Waafrika walipelekwa utumwani kufanya kazi mashambani katika kuzimu iitwayo Amerika. Huwezi kuacha kuzungumzia mauaji ya kimbari/ya kinyama (Ya mamilioni "wahindi wekundu" wa Marekani, mauaji ya Waaborijini wa Australia nk) .Zaidi sana ukoloni/kutawaliwa kwa bara la Afrika na sehemu mbalimbali duniani.

Wanazuoni wa Ulaya na iliyokuja kuitwa Marekani kama Charles Darwin na wengineo walitoa dhana mbalimbali ili kuhalalisha mfumo huu na makandokando yake.Mfano wa dhana hizo ni "survival of the fittest" au kilichokuja kuitwa "Social Darwinism" pamoja na dhana ya tofauti za rangi(racism). Dhana hizi zilihalalisha unyonyaji na ukandamizaji wa watu walioonekana/kusemekana kuwa ni "dhaifu".

Ubepari ni zaidi ya mfumo wa "kuzalisha, kusambaza na kula bidhaa na huduma" bali ni njia ya "kufikiri, kutazamia(kuazimia) kupata mali na kuhalalisha unyonyaji".Na ukiwa kama mfumo wa kiuchumi ndani yake si tu bidhaa na huduma zinazobadilishwa au watu fulani kuhusishwa katika mchakato huo, bali ni mpangilio wa watu kiakili kuwaandaa kuwa wazalishaji na watumiaji wa bidhaa na huduma hizo. Biashara ni mahusiano baina ya watu.Mahusiano haya yalikuwepo kabla hata pesa haijagunduliwa. Hivyo, biashara kama mahusiano ni zao la utamaduni(nyenzo ya watu kuhusiana) na utamaduni ni zao la fikra au Dr. Marimba Ani anavyoiita "utamaroho" yaani kile kiini cha ndani kabisa cha fikra kinachozaa utamaduni.

Hivyo basi, kwa mfumo huu kustawi na matokeo yake kuhalalishwa bila pingamizi unahitaji kwanza "ubeberu wa kiutamaduni"(cultural imperialism) uchukue njia. Na ndio maana kabla ya ukoloni kuanzishwa kwanza walianza "wamishionari,wapelelezi na wafanyabiashara" kuandaa mazingira na kubadilisha kiini cha fikra za "watawaliwa watarajiwa".Ambapo inahusisha kubadilishwa kwa namna jamii inavyofikiri na kuhusiana.

Hivi sasa nafasi za vitangulizi hivi zimechukua sura za elimu, dini, matangazo ya biashara(advertisement),ushauri uelekezi,vyombo vya habari, NGOs nk. Madhara yake yanaweza kuonekana kuanzia katika ngazi ya serikali hadi kwa mtu mmoja mmoja. Si ajabu kusikia vijana wakinunua mavazi ya Gucci au viatu vya Jordan kwa mamia elfu ya shilingi, si ajabu kukuta kinadada wakinunua madawa ya kujichubua na nywele za bandia kwa maelfu ya shilingi.Haya yote si mambo ya kawaida, lakini ubeberu wa kifikra "umeandaa mazingira" ya haya yote kutokea.

Katika kitabu cha Makuadi wa soko huria(Mhusika Alhaji Said) anasema "Dunia imebadilika sana, hakuna mambo ya ubeberu na ubepari tena enzi hizi. Sasa tunaishi dunia ya utandawazi na masoko huria yasiyoepukika" . Huyu anawakilisha madhara ya ubeberu wa kifikra ambapo tunaona "utandawazi" ndio mustakabali wetu. Ubeberu wa kifikra na kiutamaduni(cultural imperialism) ndani ya utandawazi umehalalisha mahusiano ya kinyonyaji na kufanya zile dhana zilizounyoshea kidole udhalimu huu kuanza kufutika. "Kutokuepukika" kwa masoko hayo anakosema bwana Said ni zao la kiini cha ubeberu wa kiutamaduni(cultural imperialism) unaotawala mifumo ya kufikiri, mahitaji ya watu na mahusiano ya kijamii. Je tumejifunza nini kwa miaka mingi ya kuhusishwa kwetu kwenye mfumo huu? Tunasubiri tupoteze mangapi? Je tuache ubepari na gari lake la "utandawazi" viamue mustakabali wetu?

Kabla ya kulijibu swali la tatu, lazima tujiulize katika mfumo huu wa utandawazi, ni nani anaye "mtandawaza" mwenzake? Historia inatujibu kuwa waafrika tumekuwa "watandawazwa" kwa miaka yote hii, tena kwa mijeredi na bunduki.Watandawazwa ni wale waendao na "fashion" kwa kuwaangalia na kwenda na upepo wa watandawaza, na kugeuka kuwa soko la bidhaa. Watandazwa ni wale wanaoiga kama kasuku majina, dini, tamaduni, na lugha za watandawaza.

Mwisho nimshukuru sana Ndugu Melk_Kabala ambaye kwa kiasi kikubwa maandiko yake nimeyatumia kuboresha andiko langu.
 
Ubepari ndio mfumo sahihi ambao hata Mungu ameuruhusu. Soma kisa cha talanta kwenye biblia, asiyefanya kazi na asile
 
Ubepari ndiyo mfumo pekee ambao umeondoa umasikini katika dunia ya leo. Ukiangalia nchi zote ambazo zimepiga vita umasikini zimefuata mfumo wa ubepari. Angalia nchi za Asia kama Singapore, South Korea, Indonesia, Hong Kong, Taiwan na zingine wanazoziita "tiger economies" zote zimefuata mfumo wa Ubepari. Hata nchi za kikomunisti kama China na Vietnam waliruhusu mfumo wa Ubepari na ndiyo uchumi wao umekua. India umasikini wa wengi umefutwa na Ubepari.

Ujamaa/socialism ni mfumo wa kusambaza umasikini siyo wa kuinua maisha ya jamii na nchi. Maana yake wote tuwe masikini na ndiyo maana kwenye historia umeshindwa na watu wanaukataa. Mwenye hela anaonekana ni adui bila kujua kuwa mwenye hela ndiyo anayeleta ajira. Masikini mwenzako hawezi kukupa ajira.Mwenye hela ananyang'anywa kipato chake, mali zake, alizopata kwa jasho lake halafu wanapewa wengine. Sasa nani atafanya kazi kwa bidii na ubunifu kama akijua akipata mafanikio ataporwa? Mwishowe wote mnakuwa masikini.
 
Back
Top Bottom