CCM: Ruksa kutumia kifo cha Wangwe kisiasa
2008-09-30 11:36:47
Na Simon Mhina
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ni `ruksa` ndugu wa Marehemu Chacha Wangwe kutumia jukwaa la kampeni za Chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Tarime kuzungumzia hisia zao juu ya mazingira ya kifo cha ndugu yao.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Pius Msekwa alisema ndugu hao wana haki kuzungumzia kifo hicho kwenye jukwaa la CCM kwani hizo ndizo haki za binadamu.
Akifafanua, mwanasiasa huyo alisema ndugu hao ukiwaondolea jukwaa la siasa, hawana sehemu nyingine ya kusema, kutoa dukuduku zao na kuonyesha hisia zao.
Msekwa ametoa kauli hiyo akijibu malalamiko ya viongozi wa Chadema kwamba baadhi ya vyama vimekigeuza kifo cha Wangwe kuwa mtaji wa kisiasa katika uchaguzi huo.
``Jamani nyie hamfahamu haki za binadamu, wale wana madukuduku yao, lakini wamekosa mahali pa kusemea, wanapopanda kwenye majukwaa yetu wanaona hiyo ni sehemu muafaka, ruksa hatuwezi kuwazuia,`` alisema.
Hata hivyo, Msekwa alisema wanaolalamikia kifo cha Wangwe sio CCM, bali ndugu zake.
Alisisitiza kwamba nchi yetu imetoa uhuru wa kujieleza kwa kila mwananchi, ili mradi asivunje sheria, hivyo wanachokifanya ndugu wa Wangwe ni sahihi.
``Kwa mfano juzi nimesikia mjane wa marehemu yeye akitumia jukwaa la vyombo vya habari kutoa hisia zake mbona hakunyimwa? Kwa hiyo na sisi hatuwezi kuwanyima fursa hiyo kama wanataka,``alisema.
Alipoulizwa kama haoni suala hilo ni sawa na uchochezi, Msekwa alisema mtu kudai kwamba haelewi mazingira ya kifo cha marehemu wake kilivyotokea sio uchochezi.
``Tutaendelea kuwakaribisha ndugu wa Wangwe kwenye mikutano yetu na hatuwezi kuwapangia cha kuzungumza,``alisema.
Alisema wameamua kufanya hivyo, kwa vile ndugu wa marehemu wamejirizisha kwamba kifo hicho kilijaa utata.
Pia alisema malalamiko kama hayo hayakuanzia kwenye jukwaa la CCM, bali kwa kaka wa Marehemu huyo Profesa Wangwe.
Kuhusu mwenendo wa kampeni, Msekwa alisema hakuna vitisho vyovyote vinavyotolewa na Polisi na hao wanaodai kuna askari `wamemwagwa` hawaelewi mambo.
Alisema vikosi vya askari vilivyomwagwa ni kwa ajili ya kuwalinda wananchi na mali zao na kuwa amini dhidi ya wezi wa ng`ombe.
``Unajua huku kuna wezi wa Ng`ombe na mapigano ya koo, hivyo lazima polisi wawe wengi,``alisema.
Alipoulizwa kama Polisi wamemtuma atoe msimamo huo, Msekwa alisema tataribu za Polisi ziko wazi, hawawezi kuletwa sehemu kwa nia ya kuvuruga, bali kulinda amani.
Alisema raia wema hawana sababu yoyote ya kuogopa Polisi.
SOURCE: Nipashe