Huu utafiti umefanywa na Thomas Ngawaiya
Na Godfrey Lutego
Uchaguzi mdogo wa mbunge na Diwani wa jimbo la Tarime mkoani Mara unafanyika kesho huku ushindani mkubwa ukiwa kati ya mgombea wa chama tawala, CCM, Bw. Christopher Kangoye nawa chama cha upinzani, CHADEMA, Bw. Charles Mwera.
Vyama vingine vinavyoshiriki katika uchaguzi huo unaofanyika kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe aliyefariki kwa ajali ya gari ni NCCR Mageuzi na DP cha Mchungaji Christohper Mtikila. TLP wanawaunga mkono NCCR Mageuzi huku CUF wakikaririwa kutokuwa na upande wowote katika uchaguzi huo.
Wagombea hao wa ubunge na udiwani na viongozi wakuu wa vyama vyao, wapambe wao na wanachama na wafuasi wa vyama vyao kwa zaidi ya wiki mbili wamekuwa katika kampeni za kunadi sera zao ili kuomba kura wachaguliwe kuwakilisha wananchi wao katika kipindi kilichobaki kufikia mwaka 2010 uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na Taasisi ya Utawala bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), CCM ina nafasi kubwa ya kutwaa jimbo hilo kwa ushindi wa asilimia 65 ikifuatiwa na CHADEMA iliyokuwa inalishikilia inayopewa nafasi ya kupata asilimia 35 na vyama vinavyobaki vinatarajiwa kupata asilimia 5.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa CEGODETA, Bw. thomas Ngawaiya anasema tathmini iliyofanywa na taasisi yake inaonesha CCM watalipoka jimbo hilo kwa CHADEMA.
Hata hivyo, tathmini hiyo inatofautiana kidogo na tathmini iliyotolewa na gazeti moja likikariri wanaodaiwa kuwa wananchi wa Tarime kuwa CHADEMA itaendelea kutetea jimbo hilo kwa ushindi wa asilimia 50 huku CCM ikipata asilimia 45 na vyama vingine vilivyobaki asilimia 5.
Kwa kurejea tathmini hiyo, kinachojitokeza hapa ni kuwa, zote mbili zinakubaliana na ukweli kuwa, vyama vilivyobaki, NCCR Mageuzi na DP havina nguvu na vinasindikiza tu wenzao katika uchaguzi huo ndio maana vina nafasi ya kupata asilimia tano kwa tathmini zote.
Lakini kwa kurejea malumbano ya kisiasa yanayoendelea katika uchaguzi huo kuhusu DP na NCCR Mageuzi na viongozi wake kutuhumiwa kuipinga CHADEMA na kuisaidia CCM ishinde, CCM ndiyo inapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda kwa faida ya utengano wa wapinzani. Waswahili husema, vita ya panzi furaha ya kunguru.
Ni wazi basi kuwa kuvunjika kwa umoja wa vyama vya upinzani vya CHADEMA, NCCR Mageuzi, TLP na CUF na kitendo cha TLP kutomuunga mkono mgombea wa CHADEMA ingawa pia haisemi inamuunga mkono nani wakati CUF pia ikisema haiungi mkono mtu yeyote kunaipa CCM ahueni ya kukataliwa na wapiga kura Tarime.
CCM inapata ahueni hiyo kwa sababu tayari wapinzani wamegeukana na hivyo kufanya wanachama wa vyama vya upinzani ambavyo vina nguvu huko Tarime, NCCR Mageuzi ambacho kinatamba kuwa na wanachama kwenye vitongoji vingi na vijiji vingi kuliko CHADEMA na TLP na CUF wasimpigie kura mgombea wa CHADEMA, Mwera.
Hatua ya Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Bw. James Mbatia na Katibu Mkuu wake, Dkt. Sengondo Mvungi ya kuipinga CHADEMA hadharani na kuikana kutokana na kampeni zake za kibabe na vurugu ilikuwa ni hitimisho na ushahidi tosha wa jinsi gani CHADEMA na mgombea wao hawana lao tena kwa wanachama wa NCCR Mageuzi.
Mbaya zaidi ni hatua ya Mwanasheria na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Bw. Tundu Lissu kuthibitisha kuwa ndoa ya vyama vya upinzani vya TLP, CHADEMA, NCCR Mageuzi na CUF haipo tena kwa sababu ya matamshi na vitendo vya viongozi na wanachama wa vyama hivyo akirejea waliyosema Tarime kwenye kampeni na pia kabla ya kampeni wakiihusisha CHADEMA na kifo cha Wangwe.
Bw. Lissu alikaririwa akisema kwa Wenyeviti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wa TLP, Bw. Agustine Mrema kudai CHADEMA ina mkono katika kifo cha Wangwe huku TLP ikidai Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alishangilia kifo hicho alipokuwa Afrika Kusini kulitosha kuonesha kuwa wao si wamoja tena, ndoa yao imekufa na ilimalizwa kwa Bw. Mbatia kuituhumu kwa rafu Tarime kiasi cha kutaka chama hicho kifutwe.
Ni wazi basi CHADEMA inapambana kubakiza jimbo hilo mikononi mwake ikiwa chama mkiwa, kisiye na msaidizi, mtetezi wala jirani wa kugombolezea hali inayofanya kiwe na wakati mgumu zaidi licha ya kuongeza nguvu za Bw. Mbowe kuungana na timu yake kampeni huku akitumia helikopta kumnadi mgombea wake na pia kujiunga kwa aliyekuwa Katibu wa UVCCM mkoa wa Tanga, Bw. Mwita Waitara.
Kimahesabu ya yamkini, kama vyama vyenye asilimia tano vitaisaidia CCM kwa sababu wapinzani wamefarakana, basi katika tathmini ya kwanza, CCM itajipatia kura asilimia 70 na hata ya pili asilimia 55 na hivyo ina maana itaishinda CHADEMA ambayo itaendelea kubaki na 50
ya awalina 45 ya pili hasa ukizingatia kuwa, mwaka 2005 ilipata kura za huruma za wana CCM waliosalitiana na pia uchaguzi ulikuwa nchi nzima wakati sasa ni jimbo moja hivyo CCM imejipanga kwa nguvu zote kulitwaa jimbo hilo.
CHADEMA kupewa asilimia 50 na wananchi wenyewe wakati ndio kilikuwa chama tawala katika jimbo hilo ni ushahidi tosha kuwa, haikubaliki tena kwani baada ya kiliyofanya kwa miaka miwili, ilitarajiwa iwe imeongezeka umaarufu na kujijengea uhalali zaidi wa kuchaguliwa pale.
CHADEMA ina hali ngumu zaidi kwa sababu hata Polisi ambao ndio walipaswa kuwa watetezi wao wakuu, kimbilio lao wamekerwa na ubabe na vurugu zao walizowafanyia Polisi waliokuwa wakiwalinda kwenye mikutano yao ikiwa ni pamoja na kuwatukana kuwa wametumwa na CCM na kuwaponda mawe, kukaidi amri zao kiasi cha kuwafanya wasambaratishe maandamano yao yasiyo halali waliyofanya wakidai wanawasindikiza wagombea baada ya kampeni.
Ni wazi uhusiano wao na Polisi si mzuri, umekuwa wa paka na panya ndio maana ilifikia wanachama na wafuasi wa CHADEMA kumkamata mtu waliyedai ni Polisi akinunua kadi za CHADEMA kwenye ofisi za chama hicho jambo ambalo Kamishna wa Polisi anayesimamia Operesheni maalum, Bw. Vicent Tossi kukanusha hakuwa Polisi wao.
Vitendo vyao vya vurugu vikiwemo vya wanachama na wafuasi wake kudaiwa kumpiga Mchungaji Mtikila mawe kwenye mkutano wake wa kampeni kwa madai kuwa katumwa na CCM, hatua ya Naibu katibu Mkuu, Bw. Zitto Kabwe kuwaongoza wafuasi na wanachama wao kuchoma moto bendera ya CCM na wanachama na wafuasi wengine kumvisha mbwa, t-shirt yenye picha ya mgombea wa CCM ni ushahidi tosha wa madai ya Polisi dhidi ya CHADEMA kuwa chenye vurugu lakini hodari wa kulalamika kuonewa.
Ni jukumu la wananchi wa Tarime kuchagua kusuka au kunyoa kwani kama ni sera wamezisikia na kwa muda huu wanajua nani mwenye sera za amani na maendeleo ambayo imekuwa sera kuu ya CCM na hivyo watakuwa na nafasi ya kuchagua kati ya pumba za wanaoeneza chuki, uhasama, vurugu na fitina, kukatana mapanga au CCM ambayo imejikita kutumikia wananchi ili hatimaye waneemeke.
Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bw. Pius Msekwa ambao wamekuwa Tarime kwa muda mrefu wakiongoza timu ya kampeni ya CCM wameinadi vyema CCM kama chama makini, chenye mwelekeo, kilicho na dola, chenye mgombea safi, msomi na aliye tayari kuendelea kuwatumikia wananchi wa Tarime kwani tayari alishawanunulia vitanda vya sh. milioni 600 katika hospitali yao na hivyo ni jukumu la wananchi wa Tarime kuonesha kwa vitendo kuwa waliwaelewa vyema viongozi hao kwa kuichagua CCM na wagombea wake wapate maisha bora.
Wananchi wa Tarime wanapaswa kupima maisha bora yaliyotokana na zaidi ya sh. bilioni 10 ambazo Halmashauri ya wilaya ya Tarime imekuwa ikipata kutokana na ruzuku ya Serikali Kuu na pia makusanyo ya Halmashauri ambayo ilikuwa inaundwa na CHADEMA ambayo wameyaona kwa miaka hii miwili na nusu kama yanalingana na fedha hizo.
Madai ya marehemu Wangwe kuhusu ufisadi wa fedha ndani ya CHADEMA yanapaswa kuwa taa ya kuwamulikia waone ukweli wa ahadi za CHADEMA kwa watu wake hasa wa eneo kama Tarime lenye makusanyo makubwa ya mapato kutokana na biashara kutokana na kuwa eneo la mpakani na Kenya kama yanalingana na walichofanyiwa.
Walichofanya CHADEMA kulipia ada wanafunzi ndicho CCM imekuwa ikifanya na inaendelea kufanya kwa kuhakikisha wanafunzi wanasoma bure au kwa kuchangia kidogo kupitia mikopo kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu na hivyo hakuna jipya bali utekelezaji wa sera makini za CCM hivyo ni vyema wakapewa wenye nazo wazitekeleze badala ya kuwaachia wanaojaribu kuziiga.
Kuhusu madai makuu ya wana Tarime yanayofanya wawe mbogo kuwa ni maskini wakati wanazungukwa na madini, tayari Serikali kupitia Tume ya Jaji Mark Bomani ambayo Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. Kabwe alikuwa Mjumbe wake imerejea sheria za madini kwa lengo la kunufaisha wazawa hivyo hawana haja ya kuendelea kuifanya kama ajenda ya kuinyima kura CCM kuiiadhibu.
Mbali ya sheria kupitiwa upya, tayari wenye migodi Tarime kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali wameonesha nia ya kutatua matatizo ya maeneo ya migodi Tarime wakianza na kuanzisha mahusiano mazuri na wakazi wa huko hivyo hilo halipaswi kuwa ajenda ya kuinyima kura CCM kwani ndiyo yenye Serikali inayosimamia sheria wanazozililia.
Ukiacha hoja hiyo, CCM huenda ikanufaika pia na umoja uliojionyesha katika uchaguzi huu wa makundi ambayo awali yalikuwa yanapingana ya Bw. Chambiri na wenzake kwa hatimaye kupata mgombea aliyekuwa anakubalika na wengi tangu mwaka 2005 na hivyo kufanya kura za CCM zisigawanyike kama ilivyotokea uchaguzi wa 2005 ambapo waasi walimpigia Wangwe kuwakomoa waliompitisha Chambiri. Kwa wana CCM wenye mawazo ya uasi bado, huu ni muda wa kutafakari faida ya walichofanya 2005.
Kimsingi hakuna faida bali hasara ambayo imefanya sasa CCM itumie nguvu ya ziada kiasi cha Bw. Makamba na timu yake kubwa kwenda huko wakitumia helikopta mbili kulikomboa jimbo ambalo awali lilikuwa lao wakasalitiana.
Kwao usaliti unapaswa kuwa fundisho kuwa uhalifu haulipi.
Je, Waitara ataisaidia CHADEMA? Jibu ni hapana. Pamoja na kujitoa kwa mbwembwe za kukataa kuwa mpika chai wa Mwenyekiti wa UVCCM, Bw. Nchimbi, bado Waitara hakuwa tishio katika UVCCM na CCM yenyewe ndio maana akaishia kushika nafasi ya tatu katika kuwania ubunge wa Tarime kwa tiketi ya CCM.
Kimsingi wana Tarime wamempa jibu ambalo hata UVCCM walimpa kwa kumrejesha makao makuu kuwa Karani wakimaanisha kuwa, alikuwa hajaiva kiuongozi. Hatua ya wana CCM Tarime kumpa nafasi ya tatu ilikuwa ni sawa na kumwambia pia hajaiva, ajaribu tena bahati.
Lakini pengine Waitara amejipambanua tu ni kiongozi wa aina gani. Ni mwenye kupenda madaraka ndio maana alisema hawezi kuwa karani wakati elimu yake ni ya Chuo Kikuu na anawazidi makatibu wengine wa UVCCM. Viongozi kama hawa ni hatari, hawaifai UVCCM wala CCM. Pengine wanafaa CHADEMA ndio maana ameenda huko na kukaribishwa kwa mbwembwe zote kama shujaa.
Na kama hivyo ndivyo, ni hatari kuchagua chama cha watu wanaopenda madaraka na wako tayari kumwaga damu kwani Waitara amekaririwa akisema, watalinda kura hata kwa kumwaga damu ili mradi tu lazima washinde. Huyo ndiye aliyekuwa kiongozi wa CCM kimakosa kwani kuna madai awali akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kabwe, walijiunga na CHADEMA alipoona hakupata kitu, akarudi CCM na sasa karejea kulikomfaa tangu awali.
Ni vipi basi wananchi wa Tarime wamsikilize mtu asiye na msimamo, mwenye kutangatanga na mkabila kwani katika malalamiko yake, alilalamikia CCM kukumbatia wageni wa Dar es Salaam kunadi mgombea wa CCM Tarime na kuacha wazawa wa huko bila kujali kuwa, kama suala ni hilo, hata watu wa Tanga wangemlalamikia yeye kuwa Katibu wa UVCCM Tanga wakati ni mtu wa Tarime.
Wakati wanapochagua mbunge, wananchi wa Tarime ambao ni mchanganyiko wa makabila ambao bado wanauguza majeraha ya vita vya koo, Walenchoka na Wanyanchori na hivyo wanajua ubaya wake, wanapaswa kuachana na propaganda za kina Waitara wasijute baadaye.
Alipotangaza kutaka mafisadi washughulikiwe CCM huku viongozi wake wa juu, NEC na CC wakisema chama kama chama hakina mafisadi hadi itakapothibitishwa hivyo na mahakama, Waitara alikuwa anaonesha asivyo na maadili kwa wakubwa wake na wenye akili zao walijua ajenda yake ni umaarufu akidhani umaarufu binafsi unasaidia. Pengine kwa CHADEMA, kwa CCM maarufu ni chama, si mtu.
CCM inabaki kuwa chama chenye taratibu zake, chenye kuheshimu demokrasia ndio maana hata Serikali yake inaheshimu utawala wa sheria lakini kama familia, haikosi watoto watukutu watakaonyea kambi lakini kama mlezi, siku zote haitachoka kuwasamehe wanapokosea na kuwasaidia kuwaonyesha njia ili wajirudi na kutubu. Chama cha aina hiyo ndiyo cha kuchagua siyo vinavyomwaga damu.