Kaka wa Chacha Wangwe aihama CCM
Makubo Haruni, Tarime
Daily News; Tuesday,August 12, 2008 @00:02
Anajiandaa kuwania ubunge kupitia NCCR-Mageuzi
KAKA wa aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, Peter Wangwe, amekihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na anajiandaa kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi ili kugombea ubunge katika jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na ndugu yake kwa takribani miaka miwili.
NCCR- Mageuzi mkoani Mara ilitangaza kumpata mgombea wake huyo, Peter mwenye umri wa miaka 55, ambaye kwa miaka 11 alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Mara, Steven Sebeki alisema jana kuwa chama hicho kitamsimamisha Peter kuwania ubunge baada ya kukubali kung'oka kutoka katika chama tawala, CCM.
Sebeki alisema licha ya Chama cha Wananchi (CUF) kumnyemelea Peter aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa miaka 11 kabla ya kustaafu udiwani mwaka 2005, amekubali kujiunga na NCCR- Mageuzi na juhudi zinafanywa za kuanza kumnadi muda wa kampeni utakapowadia.
Peter maarufu kwa jina la Keba, alikiri kusaka nafasi hiyo kupitia upinzani, ingawa alisema hajachukua kadi ya chama chochote kati ya CUF na NCCR-Mageuzi, kwa maelezo kuwa bado yuko katika mazungumzo ya kifamilia kumtafuta atakayetunza familia ya marehemu Chacha.
Peter, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema ameamua kuondoka CCM ambako alikuwa Meneja Kampeni kwa miaka 20, kwa madai ya kufungwa mdomo na mwanachama wa chama hicho anaposema ukweli kuhusu masuala mbalimbali ya serikali, kuliko ilivyo kwa upinzani ambako kama alivyokuwa mdogowe, alisema wazi bila kukoromewa na ye yote kuhusu hujuma na ufisadi akitetea wapigakura wake.
''Ni kweli viongozi wa vyama hivyo wamenifuata na kunitaka kugombea kwa tiketi ya vyama vyao, lakini NCCR- Mageuzi kilinitaka zaidi, alisema Peter na kuongeza: Mimi kwa sasa sina hata raha na wala sijisikii kuwa ndani ya CCM, walionifanyia hila wakati wa kura za maoni mwaka 2005, nilipogombea ubunge na kunifanya nishike nafasi ya nne, na kutokana na kurudisha jina ambalo lilikuwa halikubaliki, upinzani uliibuka mshindi kwa kura nyingi, alidai mwanasiasa huyo.
Alipoulizwa kuhusu taratibu za vyama vya upinzani kuungana na kumpata mgombea mmoja kushindana na CCM, Kamishna Sebeki alisema kila chama kipo katika mbio za kushika dola, hivyo kwa kipindi cha uchaguzi mdogo, itakuwa ni zamu ya NCCR-Mageuzi kusimamisha mgombea na kuungwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), CUF na Tanzania Labour (TLP), vyenye ushirikiano.
Wakati NCCR-Mageuzi ikiwa na uhakika wa kupata mgombea, vyama vingine havijatoa tamko licha ya wananchi nao kutoa maoni mbalimbali kuhusu watu wanaofaa kushika mikoba ya Chacha aliyekufa kwa ajali ya gari katika eneo la Pandambili Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Julai 28, mwaka huu, akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Tayari wapo wanaotajwa kupewa nafasi ya kuwania kiti hicho, wakiwamo mwanasiasa wa siku nyingi, Enock Haruni (Macho), mtunzi wa vitabu vya kujifunzia katika masomo ya sekondari, Nyambari Nyang'wine, Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ryoba Kangoye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Charles Mwera na John Heche. Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, uchaguzi mdogo utafanyika siku 90 tangu kifo cha mbunge, hivyo kwa utaratibu huo, nafasi ya Wangwe itajazwa mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.