[Source Tanzania Daima]
DC: Zitto akamatwe
na Kulwa Karedia
KAMPENI za uchaguzi mdogo kuwania ubunge wa Jimbo la Tarime, jana zilichukua sura mpya, baada ya serikali kuingilia kati.
Serikali wilayani hapa imeagiza kukamatwa watu kumi, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani katika kampeni zinazoendelea.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Stanley Kolimba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mwenendo wa kampeni za uchaguzi zinazoendelea katika jimbo hilo.
Tangu kuanza kwa kampeni hapa Tarime kumekuwepo na malalamiko mengi yanayotolewa na vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huu... sasa serikali imelazimika kuagiza vyombo vya dola kuwakamata wanaohusishwa na tuhuma hizi, akiwemo Zitto Kabwe, alisema Kolimba.
Kolimba alibainisha kuwa, Zitto ni mmoja wa watu wanaotafutwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina, kwa madai kuwa alihusika kuwashawishi wafuasi wa CHADEMA kufanya vurugu mara baada ya mkutano uliofanyika juzi katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Nyamisangura.
Alisema katika mkutano huo, Zitto alihamasisha wafuasi wa CHADEMA kuchoma moto bendera, fulana na vitu mbalimbali vyenye nembo za Chama Cha Mapinduzi (CCM), jambo ambalo limezua malalamiko mengi kutoka kwa viongozi wa chama hicho tawala.
Alisema kwa kitendo hicho, mbunge huyo amevunja sheria na kanuni za uchaguzi, jambo ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa, kwani linaweza kusababisha hali ya uvunjifu wa amani na mshikamano uliopo.
Jumapili iliyopita, Zitto akihutubia kwenye mkutano wa hadhara, Shule ya Msingi Nyamisangura, alikuwa mmoja wa watu waliochangia mno kuchomwa kwa nguo za CCM na kusababisha hali hiyo ambayo imelalamikiwa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi huu, kikiwemo CCM, alisema Kolimba.
Tayari watu kadhaa wameshakamatwa, na Kolimba alisema kati ya watu waliokamatwa, wengi wao wanatoka Kijiji cha Goroma, ambako mmoja wao anasakwa na polisi kwa tuhuma za kumvua mtu nguo na kumwacha uchi.
Alisema matukio mengine ambayo sasa yanaonekana kusababisha uvunjifu wa amani ni pamoja na wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi kushusha bendera za vyama vingine na kupandisha za kwao.
Katika hatua nyingine, DC huyo alisema wamegundua mpango ulioandaliwa na baadhi ya vyama ambavyo hakuwa tayari kuvitaja, kuandaa vijana kutoka katika Wilaya ya Kurya nchini Kenya kuja kupiga kura Oktoba 12.
Tumeagiza vyombo vyetu vya dola kushughulikia suala hili haraka iwezekanavyo, alisema Kolimba.
Alisema kutokana na hali hiyo, wamewasiliana na viongozi wa Wilaya ya Kurya, kuona kama kweli kuna mpango huo wa kuleta vijana, jambo ambalo alisema kwa mujibu wa sheria haliruhusiwi na kwamba watakaobainika, watakamatwa mara moja.
Alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kuacha kutumia lugha za uchochezi kwa vile kufanya hivyo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Naye Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Tarime, Taitus Kagenzi, ameiomba serikali kuongeza idadi ya askari wilayani humu, ili kukabiliana na hali ya vurugu katika kampeni hizo, kwa madai kuwa askari waliopo hawatoshelezi mahitaji. Alisema askari wengi wanahitajika hasa Oktoba 12, ambayo ni siku ya kupiga kura.
Alisema idadi ya askari waliopo kwa sasa ni 423, wakiwemo maofisa mbalimbali, ambao kamwe hawawezi kusimamia shughuli ndogo ndogo, zinazotakiwa kusimamiwa na askari wa vyeo vya chini.
Msimamizi huyo alitumia nafasi hiyo kukanusha uvumi ulioenea mjini hapa kwamba anajiandaa kumtangaza mgombea wa CCM kabla ya kupata matokeo ya kura zote.
Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikisha wananchi wa Tarime kuwa, sitatangaza mgombea yeyote kwa shinikizo, kwani hakuna sheria inayoruhusu kufanya hivyo... mimi nitamtangaza yule tu aliyepata kura nyingi baada ya kura kuhesabiwa, alisema Kagenzi.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, jana alinusurika tena kupondwa jiwe, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Buhemba, mjini hapa.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mtikila kuendelea kutoa kauli za uchochezi kuhusiana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, kwamba aliuawa na si ajali kama inavyodaiwa.
Baada ya kusikia kauli hizo, kijana mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja, alikuwa na jiwe tayari kumlenga Mchungaji Mtikila, lakini mmoja wa walinzi wa mchungaji huyo, aliwahi na kumkamata kabla hajadhibitiwa na polisi.
Naye Salehe Mohamed, anaripoti kuwa Jeshi la Polisi, limeongeza posho kwa askari wake waliopo Tarime.
Hali hiyo ina lengo la kuwaondolea vishawishi vya kutumiwa vibaya na vyama vya siasa kama ilivyodaiwa juzi, ambapo inadaiwa askari mmoja alikamatwa akitaka kununua kadi za CHADEMA.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Abdallah Mssika, alisema jana kuwa wamepokea taarifa za kukamatwa askari huyo, lakini ni mapema mno kuzungumzia kabla ya kufanyika kwa uchunguzi.
Suala kuwa wananunua na kuziuza kadi za CHADEMA kwa sababu ya ukata wa fedha sikubaliani nalo, kwani tumeshaongeza posho kwa askari, naomba mnipe muda niweze kufuatilia kwa ukaribu zaidi, alisema Mssika.
Kwa upande wake CCM, nayo imetoa kauli ya kuwashutumu viongozi wa CHADEMA ikidai kuwa ni wahuni, na hawajaonyesha nia ya kuimarisha umoja wa taifa na kuendeleza amani na utulivu katika kampeni za uchaguzi mdogo, zinazoendelea mjini Tarime.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Saalam na Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, ofisi ndogo ya makao makuu, ilibainisha kuwa kauli na vitendo vya baadhi ya viongozi wa CHADEMA zinaashiria nia yao hiyo.
Taarifa hiyo ilisema kitendo cha Zitto kuwaongoza wafuasi wao kuchoma fulana zenye picha ya mgombea ubunge Tarime kwa tiketi ya CCM katika mkutano wa kampeni, kinaonyesha dhahiri uhuni na uvunjaji wa sheria.
Tunajua hizo ni mbinu za uchochezi na fujo zilizoandaliwa na CHADEMA ili kuipaka matope CCM, jambo ambalo ni la uongo, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, CCM imedai kuwa kijana Mahemba Daudi, aliyekamatwa juzi katika ofisi za CCM kwa kuuza shahada za kupigia kura, alipandikizwa na CHADEMA na CCM iligundua mtego huo na viongozi wa wilaya walitoa maelekezo yaliyosababisha kijana huyo kukamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi.
Edward Kinabo, naye anaripoti kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeshindwa kutoa msimamo wake dhidi ya vyama vinavyodaiwa kutumia kifo cha Wangwe kama mtaji wa kisiasa wa kujipatia ushindi katika uchaguzi huo, kwa kuihusisha CHADEMA na kifo hicho.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Lewis Makame, alisema jana kuwa, tume yake haina ushahidi juu ya kifo hicho kutumiwa vibaya na taarifa ya msimamizi wa uchaguzi jimboni Tarime haijaeleza kuwepo kwa hali hiyo.
Alisema yanayosemwa kuhusu kifo cha Wangwe yamekuwa yakiandikwa na vyombo vya habari na tume yake haiwezi kuzichukulia taarifa hizo kuwa ni za kweli hadi hapo zitakapothibitishwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.
Hata hivyo alisema, iwapo mtu atatumia kifo hicho kukashifu wengine, hilo litakuwa kosa, kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya uchaguzi, lakini kama mtu atakizungumzia tu kifo hicho katika kampeni, hapo hakuna kosa.
Akiunga mkono kauli hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Rajab Kiravu, alisema si kila kinachosemwa kuhusu kifo cha Wangwe, kina ubaya, kwani katika hali ya kawaida ni rahisi kwa kifo hicho kutajwa kwenye kampeni hizo, kwani ndicho kilichosababisha kuitishwa kwa uchaguzi huo.
Kwa mfano, mtu anaweza kusema kwenye kampeni kuwa uchaguzi huu unafanyika kwa sababu ya kifo cha Chacha Wangwe. Sasa mtu akisema hivyo
hiyo ni kawaida tu
si kashfa, alisema Kiravu.
Kuhusu vurugu zinazoendelea, Jaji Makame alisema NEC imesikitishwa na taarifa za kuwepo kwa matukio yanayoashiria uvunjaji wa amani katika kampeni za uchaguzi huo.
Alisema vitendo hivyo ni ukiukwaji wa sheria na endapo wanaohusika watabainika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aliviasa vyama vya siasa na wagombea wanaoshiriki katika uchaguzi huo kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi.
Aidha, aliwasihi wananchi wa Tarime kushiriki katika kampeni kwa kusikiliza kwa utulivu sera za vyama vyote na kuepuka kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuleta uvunjaji wa amani.
Tangu kuanza kwa kampeni wiki mbili zilizopita, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya vurugu na uvunjaji wa amani miongoni mwa wafuasi wa vyama vinne vya siasa; CCM, CHADEMA, NCCR MAGEUZI na DP, vilivyosimamisha wagombea wao katika uchaguzi huo.