JESHI la Polisi limesema askari aliyekamatwa wilayani Tarime akijaribu kununua kadi 20 za uanachama wa Chadema, alikuwa kazini.
Kiongozi wa Kikosi cha Operesheni Maalum ya jeshi hilo jimboni Tarime, Venance Tossi aliliambia gazeti hili jana kuwa askari huyo ni wa kikosi chake ambaye alikuwa katika "kazi maalum" ya kikachero.
"Huyu ni askari wetu wa kikundi maalum cha intelijensia yaani ukachero aliyekuwa kazini. Sasa huwezi kuwatambua polisi wote na ndio maana alikamatwa," alisema Kamanda Tossi bila kusema aina ya kazi aliyokuwa akifanya askari huyo.
Alisema mawazo yaliyojengeka kwamba askari huyo alilenga kufanya hujuma katika uchaguzi huo sio sahihi kwani alikuwa kazini na kukamatwa kwake ni ajali ya uwajibikaji.
"Ni vema nikwambie ukweli ili msiandike uongo. Huku tuna vikosi vingi sana ambavyo vinafanya kazi tofauti wengine wako kwenye uniform (sare) na wengine wanavaa kiraia. Huyo ni askari wetu, alikuwa kazini," alisema.
Kabla ya taarifa ya kamanda Tossi, kaimu mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini, DCI, Kamishina Peter Kivuyo alisema polisi itatumia kanuni na taratibu zake kumwadhibu askari huyo ikithibitika kuwa alifanya hivyo kinyume na maelekezo ya kazi.
Alisema ni mapema mno kuzungumzia suala hilo sasa kwani ofisi yake haijapata taarifa za kiutendaji kutoka Tarime, lakini alisisitiza kuwa ikithibitika alifanya hivyo nje ya maelekezo ya kazi, askari huyo tashughulikiwa kwa taratibu za kijeshi.
"Ni mapema mno kuzungumzia suala hilo sasa kwa kuwa bado hatuna hakika na tukio lenyewe, lakini ikithibitika kwamba alifanya hivyo nje ya maelekezo ya kazi, polisi itamchukulia hatua kwa mujibu wa taratibu na kanuni za kazi zilizopitishwa kisheria," alisema Kivuyo.
Ufafanuzi alioutoa Kamanda Tossi, ambaye juzi aligoma kuzungumzia suala hilo, umethibitisha madai ya Chadema kuwa kijana huyo ni muajiriwa wa Jeshi la Polisi.
Kijana huyo, ambaye anadaiwa kutokea Arusha, alikamatwa baada ya kubanwa na walinzi wa Chadema wakati alipoenda kujaribu kununua kadi 20 za uanachama.
Kijana huyo, Emmanuel Zacharia, ni mmoja wa polisi 400 waliomwagwa wilayani Tarime kwa ajili ya oparesheni maalum ya kidemokrasia na kuzuia mapigano baina ya koo.
Mara baada ya kufika ofisi za Chadema, watu waliokuwepo eneo hilo "hawakuwa na amani" naye na katika mahojiano walimuona akibabaika na ndipo walipomuweka chini ya ulinzi na kumpekua. Katika upekuzi huo walimkuta na barua ya polisi inayomtambulisha benki kuwa apewe huduma anayotaka.
Kukamatwa kwake kulitokea siku moja baada ya mwanafunzi wa kidato cha tatu kukamatwa kwenye ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) akisaka mteja wa kununua shahada za kupigia kura.