Vilio, kwikwi Tarime
na Kulwa Karedia, Tarime
HALI ya hewa ya kisiasa katika Wilaya ya Tarime imechafuka na kama ilivyotabiriwa na gazeti hili juzi, kuna kila dalili kwamba mwenendo wa mambo umeanza kuchukua sura ya hatari.
Katika hatua ambayo haikutarajiwa na ya kushangaza, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) jana jioni waliingilia kati mkusanyiko wa wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa ndani ya magari na wengine wakitembea barabarani wakirejea kutoka katika mikutano ya kampeni na kuanza kukabiliana nao kwa marungu na mabomu ya machozi.
Pengine kwa lengo la kuonyesha kwamba walikuwa wamejizatiti kukabiliana na rabsha zozote wakati huu wa kampeni, hatua hiyo ya FFU ilisababisha kuibuka kwa vurugu zilizofuatiwa na kukamatwa kwa viongozi kadhaa wa juu wa CHADEMA wakiwamo mgombea ubunge wao, Charles Mwera na yule wa udiwani, John Suguta.
Viongozi wengine wa juu wa CHADEMA waliokamatwa na polisi hao na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi, makao makuu ya wilaya ya jeshi hilo ni Mkurugenzi wa Idara ya Vijana ya chama hicho, John Mnyika.
Watu walioshuhudia tukio hilo, wakiwamo waandishi wa habari wanaeleza kwamba, lilitokea majira ya saa moja jioni wakati wana CHADEMA hao wakitokea kwenye mkutano wa hadhara wa mgombea wao wa udiwani, uliofanyika katika Kijiji cha Buhemba.
Wafuasi hao wa CHADEMA, baadhi yao wakiwa ndani ya magari makubwa na madogo, huku wengine wakikimbia kwa miguu, walikutwa na zahama hiyo wakati wakiimba nyimbo za kuwasifu viongozi wao pamoja na wagombea.
Wakiwa njiani, ghafla polisi walisimamisha msafara wa magari hayo na kuwataka waliokuwa wakikimbia kandokando mwa barabara kutawanyika haraka, huku wakiwataka waliokuwa juu ya magari, kuteremka na kutawanyika.
Katika kutekeleza amri hiyo, polisi waliamua kutumia nguvu kwa kuwapiga virungu wananchi hao na hali hiyo ilipozidi, polisi waliamua kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya.
Kwa muda wa takriban nusu saa, polisi walitembeza mkong'oto huku wakifyatua mabomu ya machozi na risasi hewani hadi katikati ya mji wa Tarime na kuwafanya wananchi wengi kukimbia huku na kule kujinusuru.
Tukio hilo la kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA limetokea siku moja tu kabla ya kuwasili katika wilaya hiyo kwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe leo.
Habari zilizozagaa wilayani hapa na zilizothibitishwa na Mbowe mwenyewe kwa simu zinaeleza kwamba, kiongozi huyo ameandaliwa mapokezi mazito wakati atakapowasili mjini hapa akitokea Mwanza.
"Ni kweli nimekamilisha mipango yote ya safari ya Tarime, nimejiandaa kikamilifu kuja kuwanadi wagombea wetu ambao naamini kwamba wanaweza kurudisha jimbo hilo ambalo tumekuwa tukilishikilia tangu mwaka 2005," alisema Mbowe kwa kujiamini alipozungumza na Tanzania Daima kwa simu.
Alisema kutokana na imani kubwa aliyonayo kwa wananchi wa Tarime, CHADEMA, inaweza kuibuka na ushindi kama mbinu chafu zinazotumiwa na vyama vingine hazitatumika katika uchaguzi huo ambao unaonekana kuwa na mvutano mkali kati ya vyama vya CCM na CHADEMA.
Katika hatua nyingine, Wilaya ya Tarime jana hiyo hiyo ilikumbwa na maafa baada ya watu watano kufariki dunia papo hapo na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali iliyotokea katika Kijiji cha Nyasoro, Wilaya ya jirani ya Rorya, mkoani Mara.
Ajali hiyo ya pili kubwa kutokea katika kipindi kisichozidi wiki moja, ikihusisha lori la Benz lenye tela, lililogonga dalalada aina ya Toyota Hiace, ilisababisha kusitishwa kwa muda kwa shughuli za kampeni za ubunge na udiwani katika Jimbo la Tarime.
Miongoni mwa waliofariki dunia katika ajali hiyo ni mume na wake zake wawili, waliokuwa wakisafiri na daladala hiyo kutoka Tarime kwenda Musoma kwa shughuli za kifamilia.
Ajali hiyo ilitokea jana, saa 3:45 asubuhi, baada ya dereva aliyekuwa akiendesha lori hilo lenye namba za usajili KAZ 821Z, kutaka kulipita daladala lenye namba za usajili T 808 AHU, lililokuwa likiendeshwa na Mwijuma Amosi, akiwa kwenye mwendo kasi.
Lori hilo lilikuwa likitoka nchi jirani ya Kenya kwenda Musoma likiwa na shehena ya mafuta aina ya petroli yanayokadiriwa kufikia lita 12,000.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Lebaratus Barlow, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kwamba jeshi hilo linamsaka dereva wa lori hilo, raia wa Kenya.
"Baada ya kutokea ajali hiyo, dereva amekimbia na hatujui ameelekea wapi, lakini napenda kuwahakikishieni kwamba tunamsaka kwa udi na uvumbi kwa kusababisha vifo vya watu watano...naamini tukishirikiana na wananchi wa eneo hili, tunaweza kufanikiwa," alisema Barlow.
Kamanda huyo alisema miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo ni mume na wake zake wawili, lakini mke mmoja amenusurika katika ajali hiyo na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Msoboro Ghati (55), Ghati Manyinyi (40) Nyanoko Ghati (60) - wote wa familia moja - huku Werma Ghati akinusurika katika jali hiyo.
Daladala hiyo ilikuwa na abiria na 17 na kati ya hao 10 walinusurika kwa kupata majereha sehemu mbalimbali za mwili.
"Gari hili lilikuwa limeegeshwa kando ya barabara ili kubeba abiria wengine, sasa yule dereva mwenye lori alijaribu kupita kwa kasi upande wa kulia na kujikuta akikutana na gari jingine ambalo kama angezidi kupita kwa mwendo kasi, basi wangegongana uso kwa uso, hivyo akaamua kurudi kushoto na kuizoa ile Hiace," alisema Kamanda Barlow.
Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kunasua miili ya marehemu watano waliokuwa wamekandamizwa chini ya magurudumu ya lori baada ya kuyapangua.
Licha ya kufanikiwa kuopoa miili hiyo, walipata wakati mgumu kutokana na kukosa vifaa vya kuopolea miili iliyokuwa imekandamizwa chini, jambo lililofanya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuwalalamikia askari kwamba wanachelewesha kazi ya uokoaji.
Lakini kazi kubwa ya uokoaji iliyoongozwa na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Operesheni Maalumu, Venance Tossi, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Issa Machibya, ilisaidia kuopolewa kwa miili hiyo baada ya kufanikiwa kufungua matairi ya kati, ambayo yalikuwa yamezibana.
Machibya alilazimika kuvaa glovu na kuanza kazi ya uokoaji huku akisisitiza kuwa hiyo ni moja ya ajali mbaya kutokea ndani ya siku tatu, baada ya Ijumaa iliyopita wanafunzi wawili kufariki dunia papo hapo baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupata ajali eneo la Msati, Tarime.
Wagombea wa vyama vyote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Kangoye, na Charles Mwera wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walikutana ana kwa ana lakini walishiriki kazi ya uokoaji bila kujali itikadi zao.
Kwa upande wake, Mwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, aliwaambia waandishi wa habari kuwa amesikitishwa na tukio hilo, hivyo kuamua kusitisha kampeni kwa siku nzima ya jana.
"Hili ni tukio kubwa lililotupata wananchi wa Tarime kwa mara ya pili ndani ya siku tatu zilizopita...nimesikitishwa na hali hii, hivyo mimi na timu yangu ya kampeni tunaahirisha kampeni zetu hadi kesho (leo)," alisema Mwera.
Ijumaa iliyopita wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari ya Rebu walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Msati, wakati wakienda katika Kijiji cha Nyamongo kushiriki michezo huku wengine 64 wakijeruhiwa.
My Take: Kwa mtindo huu wanzilishi wa vurugu ni CCM na jeshi la polisi,hiki ni kielelezo cha dalili za kung'ang'ania madaraka kwa nguvu.Sasa kama Jimbo la Tarime tu,CCM wame-misuse dola namna hii,je kuachia ikulu itakuaje? Hapana ni bora tuanze kupambana nao kwa nguvu ili hata dola itambue kwamba si taasisi au jumuiya mojawapo ya CCM.Haya masuala ni kama ya Robert Mugabe na kibaki wa Kenya.Tanzania hatuko tayari kwa hili