Tarime sasa angani (Mwananchi)
*Aliyekataa kumpikia chai Nchimbi, atua Chadema
Na Waandishi Wetu, Tarime, Dar
NI TUKIO baada ya tukio katika kampeni za uchaguzi wa diwani na mbunge wilayani Tarime baada ya Chama Cha Mpinduzi (CCM) kuamua kujiimarisha kwa kuagiza helikopta mbili, siku moja baada ya Chadema kunogesha zaidi harakati zake kwa kuanza kampeni za angani.
Uamuzi huo wa CCM uliotangazwa jana, unafanya kampeni za vyama hivyo viwili vinavyopambana vikali jimboni Tarime kuwa "anga kwa anga".
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye katika kampeni za urais mwaka 2005 alizunguka sehemu kubwa ya nchi kwa kutumia helikopta ya kukodi, alitangaza juzi kuwa angeanza kutumia helikopta na baada ya vikwazo kadhaa vya kibali, alianza kutumia usafiri huo wa anga jana jioni.
Helikopta ya kukodi ya Chadema yenye namba Sy-Hsn ilitua mjini hapa jana saa 9:45 alasiri ikiwa na mkurugenzi wa sheria na katiba wa chama hicho, Tundu Lissu. Ilitua kwenye uwanja wa michezo Tarime.
Mara baada ya kutua uwanjani hapo Lissu alipokewa na umati wa wakazi wa Tarime, lakini chama hicho kikakataliwa kibali cha kufanya mkutano Sirani. Hadi jana jioni walikuwa wakihangaikia kibali.
Wakati Chadema wakijiweka sawa, CCM nao walitangaza kuanza kampeni za angani kama walivyofanya wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteto, ambako vyama vyote viwili vilitumia helikopta.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere alisema jana kuwa maandalizi yote ya kukodiwa helikopta hizo mbili yamekamilika na wakati wowote zitatua mjini Tarime.
"Ni kweli tuna helikopta mbili zipo tayari... tunamsubiri Mbowe aanze kampeni za helikopta, nasi tutamfuata huko huko angani," alisema Nyerere na kusisitiza kuwa nia yao ni kudhihirisha kuwa CCM ndio chama tawala.
Kama CCM ikianza kutumia helikopta hizo leo, itakuwa ni mara ya pili kutumia baada ya kupambana na Chadema angani kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteto, ambapo CCM ilishinda.
Huku mapambano ya angani yakitarajiwa kuanza leo, Chadema ililamba dume wakati katibu aliyetangaza kukataa kuhamishiwa ofisi za makao makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM, kwenda "kumpikia chai (mwenyekiti wa umoja huo, Emmanuel) Nchimbi" kutangaza kujiunga na Chadema.
Mwita Mwikwabe Waitara, ambaye alikuwa katibu wa Jumuiya ya Vijana ya CCM mkoani Tanga, alikabidhi kadi yake ya CCM kwa viongozi wa Chadema jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Sirari.
"Nimeamua kujiunga na Chadema sababu ya sera zake ni nzuri na zinapingana na vitendo vyote vya uonevu na ufisadi," alisema Waitara, ambaye alidai kuwa kuondolewa kwake Tanga kulitokana na kusema bayana kuwa anaunga mkono kauli ya mgombea uenyekiti wa UV-CCM, Nape Nnauye na vita dhidi ya mafisadi.
"Waliniadhibu kwa kusema ukweli na kukabiliana na mafisadi, hivyo nina imani kuwa nikiwa Chadema, naweza kuwatetea wananchi vizuri kuliko CCM."
Katika kampeni zilizofanyika kwenye viwanja tofauti, kila chama kilikuwa na majigambo yake.
Kada wa CCM, Feruzi Banno alisema ushindi wa CCM hautegemei vijana wa mjini Tarime ambao alisema wengi hawajajiandikisha kupiga kura.
"Sisi tupo makini tunawajua wapiga kura na ndio tunawafuata kuwaomba kura katika vijiji vyote vya wilaya ya Tarime na ndio sababu tuna uhakika wa ushindi," alisema Bano, ambaye amewahi kuwa kiongozi katika jumuiya ya vijana makao makuu kabla ya kuwa katibu wa CCM katika wilaya mbalimbali
Naye katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alitarajia kuanza kampeni nzito za kata kwa kata katika Jimbo la Tarime.
"Maandalizi yote yapo tayari na hii ni hatua ya mwisho ya kuimaliza Chadema," alisema kada mmoja wa CCM ambaye yupo kwenye timu ya kampeni .
Katika hatua nyingine, wananchi wa Tarime, ambao wana vitambulisho vya kupiga kura lakini wana matatizo katika orodha ya wapiga kura, wameambiwa kuwa wanaweza kupata taarifa rasmi kuhusu mustakabali wao kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu.
Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasiass Kagenzi alisema matatizo yote yamefanyiwa kazi na mkanganyiko uliotokana na orodha zilizobandikwa, hasa kwa watu waliofanyiwa marekebisho mwezi Agosti mwaka huu.
"Tumefanyia kazi tatizo hilo na sasa limekwisha kwa hiyo kila mtu aliye na kitambulisho cha kupiga kura, anaweza kutuma ujumbe kwenye namba 0753123179 ili kujua sehemu anayotakiwa kupigia kura," alisema Kagenzi.
Kagenzi alisema, ujumbe huo utakaokuwa wa bure kwa wapiga kura wote wanatakiwa kuandika namba tatu(3) mkato, namba ya kitambulisho cha kupigia kura na kutuma ujumbe kwenye namba hiyo.
Alisema hiyo ni mara ya kwanza kutumia utaratibu huo wa kisayansi ili kuwezesha watu wote kupata nafasi ya kupiga kura.
Alisema watu ambao hawakuandikishwa mwaka 2005 na waliofanyiwa marekebisho katika daftari hawataorodheshwa na hawatapiga kura.
Alisema hiyo ni kwa ajili ya kudhibiti wageni na watu ambao hawana sifa ya kupiga kura.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema orodha mpya imeshatolewa na kubandikwa katika vituo ikiwa na majina yote sahihi.
Kagenzi pia aliwataka wanasiasa wanaotangaza kuwa mgombea wao asipopita kutakuwa na umwagaji damu hawaitakii mema Tarime kwani wengi ni wageni na siyo wakazi wa jimbo hilo.
"Wengi wanaosema hayo ni watu waliokuja kushawishi watu mambo ya vita, lakini baada ya uchaguzi watapanda ndege na kuondoka na baadaye kutuacha Wana Tarime tukiwa na matatizo," alisema Kagenzi.
Aliwataka wananchi wengi kujitokeza ili kutumia haki yao ya kuchagua kiongozi wanayemtaka na ofisi yake iko wazi kwa mtu yeyote mwenye tatizo ili aweze kusaidiwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame alisema polisi walioko Tarime siyo wengi kama inavyoelezwa licha ya askari 450 kuwasili kwa ajili ya kusimamia vituo 406 wakati wa uchaguzi.
Makame, ambaye aliwasili tarime jana na kupokea taarifa ya msimamizi wa uchaguzi, alisema hakuna haja ya wananchi wa Tarime kuwa na hofu kwani polisi wako kwa ajili ya kuweka ulinzi na usalama.
"Kutakuwa na vituo 406 na polisi waliopo ni mmoja kila kituo na wengine watakuwa wakiangalia zoezi la usalama wakati wa uchaguzi," alisema Makame.
Alisema kutokana na uchaguzi wa Tarime kuwa na msisimuko na ushindani polisi wamejitahidi kuimarisha ulinzi ili kusitokee matatizo.
Makame alisema, mpaka sasa mambo yanakwenda sawa na atakutana na viongozi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Alisema mawakala wa vyama watakuwa katika kila kituo ili wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kufuata taratibbu za kukaa mita 200 toka kituo cha kupiga kura ili kuondoa malalamiko na vurugu.
Naye msajili wa vyama vya siasa, John Tendwa alisema polisi hawana budi kujiimarisha ili kukabiliana na uwezekano wa kutokea kwa vurugu, huku akiwataka viongozi wa vyama kuacha kampeni za majungu na badala yake waheshimu kanuni na sheria za kampeni.
Alisema kiongozi aliyeshambuliwa alishindwa kufuata taratibu na kanuni za kampeni, na kuanza kutumia jukwaa vibaya kwa kusema mambo ambayo hayaendani na kampeni zao.
Alisema kushinda katika uchaguzi hakutokani na kurushiana majungu wala kutukanana bali kutumia jukwaa la siasa kwa kujinadi na kutoa sera ambazo zitawafanya wakubalike kwa wapiga kura wao.
Tendwa, pia alisema katika kampeni hizo, hakuna chama hata kimoja -kati ya CCM, NCCR-Mageuzi, Chadema na DP vilivyosimamisha wagombea- kinachofuata kanuni na sheria za uchaguzi za Tanzania, kitu ambacho alisema si sahihi.
Wakati huo huo, makada mbali mbali wa CCM wametoweka katika kampeni za ubunge na diwani mjini hapa akiwepo makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa ambaye amerejea jijini Dar es Salaam kimya kimya.
Wengine ambao walikuwa kwenye kampeni na kuondoka ni pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Stevin Wassira ambaye pia ni Waziri wa Kilimo na Chakula, Gaudensia Kabaka Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na mjumbe wa NEC Nimrod
Mkono.
Kiongozi mwingine wa CCM ambaye ametoweka, ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, James Wanyacha lakini hata hivyo wakati viongozi hao wakiondoka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana, Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka ambaye amekuwa akitoa mchango mkubwa kwenye kampeni za CCM wamebaki.
Uchaguzi mdogo Jimbo la Tarime unatarajiwa kufanyika Jumapili Oktoba 12 mwaka huu ambapo mchuano mkali ni kati ya CCM na Chadema katika nafasi zote za ubunge na
udiwani wa Kata ya Tarime mjini.
Imeandaliwa na Mussa Juma, Fita Lutonja na Mpoki Bukuku