*John Cheyo naye azomewa
Waandishi Wetu, Mwanza na Dar
MBUNGE wa Same, Anne Kilango Malecela ambaye alitarajiwa kumnadi mgombe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lolencia Bukwimba katika mkutano utakaofanyika leo katika mji wa Katoro, Busanda amekwama kutua Mwanza baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kupata hitilafu na hivyo kurudi jijini Dar es Salaam.
Kilango ambaye alikuwa anatarajiwa kuwasili uwanja wa ndege wa Mwanza saa 10:30 jioni kwa ndege ya Shirika la Precision alishindwa kusafiri baada ya kupata hitilafu ikiwa angani hivyo rubani wake akaamua kuirejesha katika Uwanja wa Kimatifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Wakati Kilango akiahirisha safari hiyo, tayari viongozi waandamizi wa CCM Mkoa wa Mwanza walikuwa wameshafika katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa ajili ya kumpokea tayari kwenda Busanda ili kukiongezea nguvu chama chake katika mkutano ambao unatarajiwa kufanyika leo eneo la Katoro.
Jamani kiongozi hatofika leo kutokana na safari yake kuahirishwa kufuatia ndege aliyokuwa akisafiria kupata hitilafu muda mfupi baada ya kuruka, hivyo rubani akamua kurudi katika Uwanja wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Kilango amenieleza kuwa sasa safari yake itakuwa kesho (leo) baada ya kupata ndege, alieleza mmoja wa maofisa wa uwanja wa ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mweka Hazina wa CCM, Shanif Mansoor alithibitisha kuwa safari hiyo imeahirishwa kutokana na ndege kuwa na hitilafu.
Ni kweli safari hiyo imeahirishwa na badala yake mbunge wetu atakuja kesho(leo), kwa sababu ndege aliyokuwa akisafiria ilipata hitilafu huko Dar es Salaam, alieleza.
Wakati huo huo, Boniface Meena anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa, Mama Kilango alisema anaelekea huko kukamilisha kampeni hizo kwa kuwa tayari jimbo hilo CCM imeshashinda.
"Kuna mambo ya wanawake ambayo mimi kama mbunge ambaye nina jimbo na kama mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama ninatakiwa kumsaidia mwanamke mwenzangu," alisema Kilango.
Alisema haendi Busanda kuongeza nguvu kwa kuwa jimbo tayari ni lao ila anakwenda kumsaidia mwanamke mwenzake na kuongeza kuwa taarifa za kwamba hali si nzuri huko Busanda ni mambo ya magazeti ambayo hayamsumbui kichwa.
"Hayo ni maneno ya magazeti tu, ninachoamini ni kuwa hali ni nzuri na jimbo hilo ni mali yetu,"alisema.
Katika hatua nyingine, kampeni za uchaguzi wa ubunge Busanda zinazidi kuwa moto baada ya mkutano wa chama cha UDP kumalizika kwa watu kutawanyika huku wakimzomea Mwenyekiti wa chama hicho, John Momose Cheyo wakati akimtambulisha mgombea wao Beatrice Lubambe.
Mkutano huo ambao umefanyika katika eneo la Katoro jana ulimalizika kwa watu waliokuwa wamejaa wakimsilikiliza kusambaa huku wakipiga mayowe kumzomea alipoanza kumtambulisha mgombea wa chama chake.
Huo ni mkutano wa kwanza wa chama hicho tangu kuanza kwa kampeni hizo Aprili 29, mwaka huu.
Ilidaiwa kuwa UDP hawakuzindua kampeni zao rasmi kwa sababu ya kukabiliwa na ukata wa fedha.
Mkutano huo ambao ulianza na watu wachache, lakini baadaye waliongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukienda mbele na kusikiliza kwa makini.
Hata hivyo mambo yaliharibika baada ya Cheyo kuanza kumwaga sera zake akisema wakimchagua mgombea wa UDP atateuliwa na kuwa mbunge ambapo atasimamia maendeleo ya eneo hilo pamoja na kuhakikisha kuwa bei ya pamba inapanda hadi kuwa Sh1,000 kwa kilo moja tofauti na bei ya sasa ya Sh 400.
Nimezungumza kwa saa nzima mnanisikiliza sijatukana mtu, lakini wanasiasa wengine wanatukana hovyo hapa jukwaani, jambo hili haliwezi kufanya tulinde amani na uhuru wa kisiasa uliopo, alieleza Cheyo.
Wakati huo wananchi walikuwa wametulia na kumsikiliza kwa makini, lakini alipomsimamisha mgombea wake walishika mikono kichwani na kumzomea kwa kupiga mayowe ya uuwiiii, huku wakitawanyika.
Kutokana na hatua hiyo Cheyo na mgombea wake walilazimika kuufunga mkutano wao na kuondoka haraka wakihofia kutokea vurugu.
Hata hivyo, hali hiyo imetokea siku moja kabla ya mkutano wa CCM unaotarajiwa kufanyika leo katika mji huo wa Katoro.
Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM, Tambwe Hiza alipoulizwa kwa simu jana kuhusu hali hiyo, alisema hana wasiwasi na haoni kama ni hatari na kusisitiza kuwa wataendelea na mkutano wao kama ulivyopangwa.
Hao wanaozomea siyo wanachama wa CCM, sisi tunao wetu na mkutano wetu wa kesho (leo) utafanyika kama ulivyopangwa, wala hilo halitutishi na tunao watu ambao watahakikisha unafanyika kwa amani bila mtu kutufanyia fujo, alieleza Tambwe.