Weka antena yako vizuri mkuu uturushie vyema yatakayo jiri.
Mgombea ubunge wa CCM awapigia magoti wananchi wa Busanda
Na Frederick Katulanda, Busanda
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza vibaya uzinduzi wa kampeni zake za uchaguzi mdogo Jimbo la Busanda katika Kata ya Kaseme, Busanda baada ya kupata watu wachache tofauti na mikutano ya Chadema na CUF ambavyo vilizindua rasmi mikutano yao Jumamosi iliyopita katika maeneo tofauti.
Wakati ikiwa hivyo katika ufunguzi huo, mgombea wao Lolencia Masele Bukwimba alijinadi kwa kuwapigia magoti wapiga kura huku akiomba wampigie kura kwa kuwa ni mwenyeji wa eneo hilo.
Bukwimba alisema ameamua kugombea ili awatumikie baada ya kuwatumikia wananchi nje ya jimbo hilo kwa muda mrefu akiwa katika mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.
Alisema ameamua kurejea Busanda kugombea ubunge ili kuwasaidia katika harakati za maendeleo na kwamba, atakaa huko kinyume na madai ya wanaosema atawatelekeza na kwenda kuishi Dar es Salaam.
Nimekuja kugombea kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, ingawa kuna watu wanadai kuwa mkinichagua nitakuwa nakaa Dar, siyo kweli kwetu ni katika kijiji cha Nyabulolo na mume wangu ni huyu hapa ameniruhusu kugombea, naye atakaa hapa Nyabulolo hivyo nawaombeni kura zenu, alieleza Bukwimba huku akipiga magoti na kurejea kwa lugha ya Kisukuma.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa katika uzinduzi huo, Katibu wa chama hicho, Yusuf Makamba aliionya Chadema kuwa isitarajie kuibuka na ushindi katika jimbo hilo kwa vile jimbo hilo ni lao kutokana na kumilikiwa na marehemu, Faustine Kabuzi Rwiromba sawa na ilivyokuwa kampeni za uchaguzi mdogo wa Tarime ambapo Chadema walishinda.
Makamba alisema CCM wana hakika ya kushinda kama ilivyokuwa kwa Chadema Tarime, kutokana na umiliki wa awali wa jimbo hilo kuwa mikononi mwao na kufananisha uchaguzi huo ni kiraka katika suruali iliyotatuka ambayo unapotaka kuiziba ni lazima utumie rangi na aina ya kitambaa cha suruali halisi.
Hiki ni kiraka. Sasa suruali ikitoboka na ukitaka kuziba kwa kiraka, utatumia kitambaa cha rangi gani kama si ilele ya suruali. Kwa hiyo Chadema na wenzako mnapaswa kujua kuwa jimbo hili ni mali ya CCM kama ilivyokuwa kwao katika jimbo la Tarime na wakalirejesha, alisisitiza Makamba.
Akijibu hoja za upinzani ambazo zimekuwa zikitolewa katika mikutano ya kampeni kuwa CCM imejaa mafisadi, alisema ufisadi ni wa mtu mmoja na wala siyo chama, hivyo CCM isilaumiwe kwa hilo badala yake alaumiwe anayehusika na ufisadi.
Alisema chama kinao watu safi hivyo kukiita ni chama cha ufisadi kama wapinzani wanavyodai ni makosa na upotoshaji mkubwa, hivyo kuwataka wananchi kupuuza madai hayo.
Hawa wakija hapa wanasema CCM ni mafisadi, hebu niambieni wao Chadema walipewa fedha kwa ajili ya kugawa pikipiki na baiskeli nchi nzima na wafadhili lakini hawakugawa, badala yake walipeleka stakabadi bandia kwa mfadhili huyo, hapa nani ni fisadi kama sio wao, alihoji Makamba.
Akizindua kampeni hizo jana, Msekwa alisema wanao uhakika wa kushinda kutokana na nguzo kuu tano ambazo ni umoja, mshikamano, wingi wa wanachama, sera safi pamoja na mfumo bora wa uteuaji wagombea.
Alisema CCM ina uhakika wa kushinda katika uchaguzi huo kutokana na historia ya mageuzi na kwamba, kutokana na kuwa na wanachama wengi wamekuwa wakishinda katika chaguzi mbalimbali.
Mwaka 2005 katika uchaguzi wa wabunge UDP na TLP vilipata kiti kimoja wakati CUF ilipata viti 19 kwa upande wa visiwani, Chadema viti vitano na CCM kuibuka kidedea kwa kupata viti 206 kikiwemo cha Busanda, hivyo nasisitiza kwamba tutashinda, alieleza.
Hata hivyo mkutano huo ulihudhuriwa na watu wachache huku sehemu ya wahudhuriaji hao ikijazwa na wanafunzi wa sekondari ya Kaseme, jambo ambalo lilifanya baadhi ya viongozi wa chama hicho kukosoa kuwa mkutano huo wa ufunguzi ungefanyika alikozaliwa mgombea huyo au Katoro.
Licha ya John Malecela kukwama kufika katika kampeni hizo kutokana na kuchelewa kufika Busanda, CCM ilikuwa ikilitumia kundi la uhamasishaji la TOT, huku timu ya wabunge wa Kanda ya Ziwa akina, Samwel Chitalilo, Anthony Diallo, Lawrence Masha, Dalali Shibiliti na Festusi Limbu wakishuhudia.
Leo kampeni za chama hicho zitaendelea katika kata ya Nyarugusu na kuhutubiwa na Malecela.
Sasa mzee makamba anakataaa nini??? Waliokuwa wanashutumiana hivi karibuni kuwa fulani na fulani ni mafisadi papa nao wakasema fulani ni nyangumi; HAWA WOTE NI WANANCHAMA WA CHAMA GANI??? CHADEMA, CUF, NCCR AU CCM??? Nahisi ktk huo mkutano hakukuwa na kuuliza maswali au hao watoto wa shule ni wa bweni maana hata magazeti, tv hakuna huko
Sasa km CCM hawana jipya hao watu watatokea wapi???