Masha akwaa kisiki
NEC yatupa pingamiza lake
na Waandishi wetu
JITIHADA za Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi na mbunge anayemaliza muda wake katika Jimbo la Nyamagana, Lawrence Masha, za kupita bila kupingwa katika kinyanganyiro cha ubunge katika jimbo hilo zimegonga mwamba baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutengua uamuzi wa awali wa msimamizi wa uchaguzi kumzuia mgombea wa CHADEMA.
Taarifa ambazo Tanzania Daima, imezipata, zinadai kuwa NEC imeamua kumrejesha mgombea wa CHADEMA, Ezekiah Wenje, baada ya kuridhishwa na vielelezo vya uraia wake.
Chanzo kimoja kimeidokeza Tanzania Daima kuwa kurejeshwa kwa Wenje katika kinyanganyiro hicho kitazidisha chachu ya uchaguzi wa ubunge, ambayo tayari ilionekana kutokuwa na msisimko baada ya Masha kuwa mgombea pekee.
Kimeendelea kudokeza kuwa wakati wowote kuanzia leo NEC itatangaza uamuzi huo ambao umepokewa kwa hisia mbalimbali na baadhi ya wakazi wa Jimbo la Nyamagana na wafuatiliaji wa masuala ya siasa.
Waziri Masha aliwasilisha pingamizi dhidi ya Wenje kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Wilson Kabwe, ambaye aliridhika na nyaraka zilizowasilishwa na waziri huyo, hivyo kuamua kumuengua mgombea huyo.
Baada ya uamuzi huo, Wenje aliamua kukata rufaa NEC kwa kuambatanisha vielelezo vyake kuthibitisha kuwa ni raia wa Tanzania na si raia wa Kenya kama Waziri Masha alivyodai. Mmoja wa viongozi wa juu wa CHADEMA alithibitisha kuona barua ya NEC, ikiwaarifu kulitupa pingamizi lililowekwa na Waziri Masha, hivyo kumruhusu Wenje kuanza pilikapilika za kampeni.
kiongozi huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazeti kwa misingi kuwa si msemaji wa chama hicho, alisema tayari wameshaanza maandalizi ya kampeni na wana uhakika wa kumbwaga tena Waziri Masha katika kinyanganyiro hicho.
Ni kweli NEC imemrejesha mgombea wetu baada ya kuona vielelezo vilivyotolewa na mgombea wa CCM vina upungufu na vya mgombea wetu kuwa ni sahihi
tunaamini kwamba haki imetendeka na kinachofuata ni mapambano sasa, alisema kiongozi huyo.
Tanzania Daima ilizungumza na Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu, alisema yeye hawezi kutangaza taarifa hizo kwa vyombo vya habari bali anapeleka kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo husika, mlalamikaji na mlalamikiwa.
Aliongeza kuwa jana alikuwa yupo nje ya ofisi hivyo hayupo katika nafasi nzuri ya kulizungumza na kulielekeza gazeti hili limtafute msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Nyamagana na Ilemela, Wilson Kabwe.
Tanzania Daima ilizungumza na Kabwe kwa njia ya simu ambaye alisema hadi jana jioni alikuwa hajapata maelekezo hayo lakini kama akiyapata atayafikisha kwa wahusika ili wajiandae na pilikapilika za kampeni.
Naye, Waziri Masha aliiambia Tanzania Daima kuwa haoni tatizo la pingamizi lake kutupwa na yuko tayari kwa mchuano wa kutetea kiti chake.
Alisema tetesi za kurejeshwa kwa Wenje, amesizisikia kutoka kwa baadhi ya watu lakini amejiandaa kukabiliana naye kwenye kinyanganyiro hicho ambacho anaamini atashinda.
Sioni tatizo na kurejeshwa kwa mpinzani wangu
sina maoni yoyote, ninachomwambia akaribie sana, naamini tutakutana katika kinyanganyiro, alisema Waziri Masha.
Aliongeza kuwa amejiandaa vema katika uchaguzi huo, hakuna mgombea yeyote ndani ya jimbo hilo anayeweza kupambana naye na anajua ataibuka na ushindi wa kishindo. Wakati huo huo, taarifa zilizopatikana kutoka jijini Mwanza zinasema kuwa wanachama wa CHADEMA wamepokea kwa furaha kubwa kurejeshwa kwa mgombea huyo na kuahidi kwamba CCM itakiona cha moto.Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi, alithibitisha kurejeshwa kwa mgombea huyo na kuongeza kuwa hivi sasa wanajiandaa na upangaji wa ratiba ya mikutano ya kampeni.
Tumepokea kwa furaha taarifa za NEC za kumrejesha Wenje katika kinyanganyiro
ninakuthibitishieni kwamba ni mgombea halali sasa, kazi imeanza kwetu ili tuchukue jimbo, alisema Mushumbusi.
Alisema kutokana na uamuzi huo, CHADEMA mkoa imeandaa mapokezi makubwa yatakayolitikisa jiji kwa ajili ya kumpokea mgombea huyo akitokea Dar es Salaam.
Hali katika Jimbo la Nyamagana jana ilionekana kubadilika baada ya mamia ya wananchi kujitokeza mitaani kushangilia uamuzi huo. Wakizungumza na Tanzania Daima, wanachama wa chama hicho, wananchi na wana CCM wakiwamo baadhi ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, mkoa na kata, walieleza kufurahishwa na NEC kumrudisha Wenje kugombea jimboni humo.
Nimesikia Wenje amerudishwa kupambana na huyo Masha
kimsingi ndiye mbunge aliyetaka kuporwa kisiasa ushindi wake, alisema John Samson. Sababu nyingine zilizotolewa na Masha ni kudai Wenje ni mkazi wa Burola A, wakati si kweli kwani hana makazi katika mtaa huo na kwamba mgombea huyo pia alisema uongo juu ya cheo chake katika Kampuni ya Nation Media Group ni meneja wakati ni ofisa masoko. Masha ni Waziri wa Mambo ya Ndani na hatua yake ya kudai kuwa Wenje si raia na kufuatiwa na malalamiko ya Wenje kuwa Masha alimtishia maisha pamoja na kutuma maofisa Uhamiaji kwenda wilayani Rorya ambako Wenje amezaliwa kuchunguza uraia wake, kitendo kilichotafsriwa kuwa alitumia madaraka yake vibaya.
NB:The highlighted parts are interesting.Kama alikuwa aogopi, pingamizi aliweka la nini, oh, sizitaki mbichi hizi.