TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa inatolewa kwa Umma kwamba Kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA imefanya kikao chake Januari 26, 2008 chini ya Mwenyekiti Freeman Mbowe.
Kikao hicho maalumu cha Kamati kuu kilifanyika katika Hoteli ya Markham jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na ajenda nyingine kilijadili na kumpitisha Victor Parkimaro Kimesera kuwa mgombea ubunge jimbo la Kiteto kupitia CHADEMA. Kimesera ndiye aliyekuwa mgombea pekee aliyependekezwa na Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Wilaya ya Kiteto kilichoketi Kibaya Januari 20, mwaka 2008.
Kimesera amewahi kuwa mgombea katika jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kupata asilimia 42 ya kura zote wakati huo. Kimesera mwenye shahada ya falsafa amewahi kuwa mtendaji mkuu wa taasisi na makampuni mbalimbali ndani na nje ya Tanzania. Kimesera amewahi pia kuwa Katibu Mtendaji na Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA katika nyakati mbalimbali. Kwa sasa Kimesera ni Mkurugenzi wa Baraza la Wazee wa CHADEMA Taifa. Kadhalika Kamati kuu imepitisha Mkakati/Mpango wa Kampeni ya uchaguzi katika Jimbo la Kiteto.
Aidha Kamati Kuu imepitisha pia Mwongozo kuhusu utekelezaji wa maadili, itifaki na kanuni za chama juu ya uendeshaji wa kampeni za uchaguzi ndani ya chama; kutokana na kanuni za chama vifungu vya 10.1, 10.2 na 10.3. Lengo la mwongozo huo ni kufafanua mambo yanayoruhusiwa na mambo yasiyoruhusiwa kufanywa na wagombea na viongozi wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani ya chama ili kuhakikisha chaguzi za ndani ya chama zinakuwa huru, zenye uwazi na haki.
Wakati huo huo, Kurugenzi ya Habari na Uenezi inapenda kuchukua fursa hii kuutaarifu umma wa watanzania kwamba tayari CHADEMA imekwishaanza kujipanga kushinda uchaguzi katika jimbo la Kiteto.
Timu ya Awali ya Kampeni inaondoka hivi karibuni kwenda kukamilisha maandalizi ya awali ikijumuisha Dr Ben Kapwani -Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa; Joseph Fuime-Mwenyekiti wa Mkoa wa Ruvuma; Afisa Mwandamizi wa Sera na Utafiti- Danda Juju Martin, Mheshimiwa Halima Mdee- Mbunge wa Viti maalum na Wakili wa kujitegemea; Jafari Kasisiko- Mwenyekiti wa Mkoa wa Kigoma na Chiku Abwao- Mjumbe wa Kamati Kuu.
Aidha Kampeni za CHADEMA zitazinduliwa rasmi Februari Mosi na Dr Wilbroad Slaa(Mb)- Katibu Mkuu. Kadhalika viongozi wengine watakaoshiriki kampeni hizo ni pamoja na Chacha Wangwe(Mb)-Makamu Mwenyekiti na Zitto Kabwe(Mb)- Naibu Katibu Mkuu; wakurugenzi, madiwani na viongozi mbalimbali wa chama wilayani Kiteto. Pamoja na viongozi wa CHADEMA, Kampeni hizo pia zitahusisha viongozi wa vyama vilivyoko kwenye ushirikiano vya CUF, TLP na NCCR Mageuzi ambavyo kwa pamoja vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja. Viongozi wengine wa kitaifa watakaoshiriki kampeni hizo watatangazwa katika hatua za baadaye.
Kurugenzi ya Habari na Uenezi inapenda kusisitiza kuwa CHADEMA imejizatiti kushinda jimbo la Kiteto kutokana kuwa na timu mahiri na mgombea anayekubalika katika jimbo hilo. Aidha CHADEMA imedhamiria kukuabiliana na vitendo vya hujuma wakati wa uchaguzi huo na itahadharisha kwamba mbinu yoyote ya kupenyeza fedha za ufisadi kwa lengo la kuwaghilibu wapiga kura katika jimbo hilo zitazimwa kwa nguvu ya umma. Kurugenzi ya Habari na Uenezi inapenda kukumbusha kuwa kwa mwelekeo Wabunge waliowengi wa CCM na hali ya ufisadi uliopo nchini, wananchi hawapaswi kwa sababu yoyote ile kuwaongezea mbunge CCM. Hii ni fursa pekee kwa wananchi kuongeza mbunge mwingine wa upinzani bungeni kwa lengo la kutoa fikra mbadala zenye kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa kwa demokrasia na maendeleo ya nchi yetu.
Aidha Kurugenzi ya Habari na Uenezi ingependa kutumia fursa hii pia kutangaza kwamba uchaguzi wa ndani ya chama unaanza Februari Mosi, 2008 kama ilivyotangazwa kwa kuanzia na Uchaguzi katika ngazi ya Msingi ambao utafanyika kwa miezi miwili mpaka tarehe 31 Mwezi Machi 2008. Kwa lengo la kufanikisha uchaguzi huu, Kurugenzi inasambaza rasmi Maelekezo ya Taratibu za Uendeshaji wa Uchaguzi Ndani ya Chama Ngazi ya Msingi na Tawi( Nakala za Nyaraka hii inasambazwa pia kwa waandishi wa habari kama sehemu ya taarifa hii). Kurugenzi ya Habari na Uenezi inahimiza umma wa watanzania hususani wanaCHADEMA na wapenzi wa CHADEMA kushiriki kwenye mchakato huu kwa lengo la kujenga oganizesheni ya chama mbadala kuanzia ngazi ya chini kabisa. Pamoja na uchaguzi wa Viongozi wengine wa chama katika ngazi hizo, mabalozi wa CHADEMA ambao ni wawakilishi wa chama katika nyumba kumi watachaguliwa. Mchakato huu utahusisha pia uundaji wa Mabaraza ya chama katika ngazi hizo. Mabaraza hayo ni Baraza la Wazee, Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) na Baraza la Wanawake wa CHADEMA(BAWACHA).
Imetolewa 28 Januari 2008 na;
Erasto K. Tumbo
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
0713 47 47 07