Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Hapo ndipo nabaki kustaajabu ya filauni tu,
Mohamed Said anahisi watanzania wote ni wajinga,
Mwalimu atambulishwe 1952 akiwa ni mgeni kabisa katika siasa za TAA na akiwa nimchanga kabisa wa siasa, kisha mwaka mmoja tu baadae yani 1953 amshinde Abdul Sykes kwa kishindo aliyekuwa rais wa chama hicho, mtu maarufu na mkongwe na zaidi mwasisi wa chama hicho? Mwenye ushawishi mkubwa kwa wazee wa kariakoo?
Haiingii akilini hata kidogo na hii Mohamed Said amewadhara na kuwatusi wale anaodai ni wazee wake!
Nahisi washamlaani kwa aina ya maandiko yake!
Ni nukuu ndefu kidogo lakini isome ni muhimu:
Kisa Cha Julius Kambarage Nyerere, 1952
Mwaka wa1952 Julius Kambarage alikuja Dar es Salaam kama mwalimu katika St. Francisí College, Pugu. Nyerere alikuwa na Mwapachu huko Makerere na wakawa pomoja Tabora mwaka wa1945 na baadaye nchini Uingereza kwa masomo ya juu. Mwapachu na Nyerere walikaa bweni moja walipokuwa wanafunzi Makerere wakati ambapo Kasella Bantu na Nyerere walifundisha pamoja hapo Tabora.
Kasella Bantu alikuwa na msimamo usiotetereka katika kupinga ukoloni. Alijiuzulu kufundisha na kwenda Dar es Salaam kujiunga na Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC). Inawezekana Nyerere kwa kufuatia harakati za TAA, alisikia habari za Abdulwahid kupitia kwa Mwapachu alipokuwa bado yuko Uingereza. Katika hotuba ya kuwaaga wazee wa Dar es Salaam, (wazee wa Kiislam waliomuunga mkono wakati wa kudai uhuru) aliyoitoa tarehe 5 Novemba, 1985 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Nyerere aliwaambia waliohudhuria kuwa Kasella Bantu ndiye aliyempeleka nyumbani kwa Abdulwahid na kumtambulisha.
Hii ilikuwa mara ya kwanza Nyerere kuzungumza hadharani kuhusu kufika kwake Dar es Salaam na ilikuwa mara yake ya kwanza kuihusisha hadharani historia yake, ya TANU na jina la Abdulwahid .[1]
Nyerere alikuwa mgeni kabisa mjini Dar es Salaam na kama ilivyokuwa mazoea, Kasella Bantu alimpeleka Nyerere kwa Abdulwahid kumtambulisha na vilevile akutane na watu wengine maarufu wa pale mjini. Mbali na Dossa Aziz aliyekutana na Nyerere kwa muda mfupi katika mkutano mkuu wa TAA Aprili 1946, Kasella Bantu mwenyewe na Denis Phombeah, hakuna mtu mwingine mbali ya hao hapo makao makuu ya TAA aliyewahi kusikia habari za Nyerere.
Abdulwahid, Nyerere, Ally, Dossa Aziz, Mhando, Rupia, Dunstan Omar na wengine walikuwa wakikutana kila Jumapili nyumbani kwa Dossa Aziz Congo Street au nyumbani kwa Abdulwahid, Stanley Street. Hizi ndizo zilikuwa baraza mbili ambazo wazalendo walikuwa wakikutana kujadili mustakabali wa Tanganyika.
Majadiliano ya siasa miongoni mwa vijana hawa sasa yalivuka kutoka manungíuniko ya ndani ya nchi na kuingia kujadili masuala ya kimataifa ya mlengo wa kushoto na hasa kuhusu kuwa na utawala wa Waafrika Tanganyika. Nyerere alimwona Abdulwahid kama mtu mwenye akili sana, asiye na choyo na mtu wa kupendeka. Abdulwahid alimuona Nyerere, kama mtu aliyeelimika sana na mwenye ustadi katika majadiliano.
Nyerere alipata nafasi ya kuifahamu dunia vizuri na kupata msimamo wa siasa kutokana na uhusiano wake na Fabian Society, wakati alipokuwa mwanafunzi Uingereza. Mijadala mizito sana ilijitokeza katika vile vikao vya kila Jumapili wakati akili na ujuzi wa siasa wa Abdulwahid vilipopambana na uhodari wa majadiliano wa Nyerere. Wakati ule Nyerere hakuwa na wa ujuzi wowote katika siasa ukimlinganisha na Abdulwahid. Wakati African Association Tabora kiliposhiriki katika mgomo wa mwaka 1947 Nyerere hakujihusisha na harakati zile za wafanyakazi ingawa yeye ndiye alikuwa katibu wa chama.
Kutokana na urafiki huu pakawa na kuheshimiana na mapenzi makubwa baina ya Abdulwahid na Nyerere. Kila Jumapili Nyerere alikuwa akisafiri kutoka Pugu hadi Dar es Salaam kuhudhuria baraza lile lililokuwa likijadili siasa za Tanganyika. Baada ya kikao, Dossa Aziz au Dunstan Omar alimrudisha Nyerere kwa gari hadi Pugu. Hivi ndivyo Nyerere alivyokuja kuingia ndani ya TAA makao makuu na hatimaye akaja kupendekezwa kugombea cheo cha juu kabisa cha uongozi wa chama mnamo Aprili, 1953.
Uongozi wa TAA ulimpendekeza Julius Nyerere ili kukiimarisha chama kwa kuwa na Waafrika wenye elimu ya juu ndani yake. Ilibakia kwa Nyerere kukubali au kukataa. Kujadili siasa haikuwa sawa na kuongoza chama kilichokusudia kunyakua madaraka kutoka kwa serikali ya kikoloni. Hivi vilikuwa ni vita dhidi ya ukoloni na ilibidi mtu ajitayarishe kwa lolote ambalo lingetokea.
Nyerere alikuwa mwalimu wa Kikatoliki aliyekuzwa katika makuzi ya kunyenyekea kanisa na serikali. Vilevile Nyerere alikuwa chini ya ulezi wa Father Richard Walsh, aliyempatia nafasi ya masomo Scotland. Inasemekana Father Walsh alikuwa na ëushawishi wa kutosha juu ya maisha na fikraí za Nyerere.[1]Alimlea Nyerere na akamsaidia kupata nafasi ya kusoma nje ya nchi.
Katika hali kama hii haikutarajiwa kwa Nyerere asimame kuipinga serikali. Kanisa lilimtarajia afanye kazi ya ualimu katika moja ya shule zake nchini Tanganyika. Nyerere alikuwa ndiyo kwanza amerudi kutoka masomoni Uingereza mwaka uliopita na alikuwa anataka kutulia aanze maisha. Vijana wenzake wa mjini aliowakuta katika siasa pale Dar es Salaam kama Abdulwahid na mdogo wake Ally, na Dossa Aziz walikuwa watu wenye uwezo wao na wakiishi ndani ya mji wao ukilinganisha na yeye mgeni, tena amekulia kijijini.
Nyerere alijua yeye akiwa Mkristo, kamwe hangeweza kujijengea nguvu ya siasa katika mazingira yale ya Dar es Salaam ya miaka ya 1950 ambako siasa zilitawaliwa na Waislam. Kwa sababu hii, Nyerere alisita kukubali shauri la kuongoza TAA.
Uongozi wa TAA ulitambua thamani ya elimu ya Nyerere na uwezo wake wa uongozi kwa chama na nchi yenyewe hapo baadaye. Abdulwahid pamoja na viongozi wenzake wa TAA waliamini kwamba kuwa na Mwafrika aliye na elimu ya juu kama rais wa chama kungeimarisha uongozi wa TAA na kutoa sura nzuri machoni mwa serikali ya kikoloni na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukitembela Tanganyika. Nyerere amenukuliwa kusema kuwa ilikuwa dhamira yake kufundisha kwa muda kisha aingie kwenye siasa.[1]Hatimaye Nyerere alishawishiwa kukubali kuchukua jukumu la kuongoza TAA.
Miaka mingi baada ya Tanganyika kupata uhuru, Abdulwahid aliulizwa kwa nini hakuliondoa jina lake kwenye ule uchaguzi wa mwaka 1953 ili kumpalilia njia Nyerere achukue uongozi bila kupingwa. Abdulwahid alijibu:
''Kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya Nyerere wakati huo na baadhi ya wanachama ndani ya kamati yangu mwenyewe ya utendaji walikuwa wakinishinikiza nisikubali kushindwa hivi hivi. Nilikuwa mgombea niliyependwa na kuondoa jina langu kungevuruga uchaguzi. TAA kilikuwa chama cha kisiasa chenye nguvu kilichokuwa kikiamini katika uchaguzi wa kidemokrasia. Uongozi wa chama ulikuwa upatikane kwa ushindani wa uwezo na sifa njema za uongozi. Tulimchagua Nyerere kugombea kwa sababu tulikuwa na imani naye nami nilikuwa mmoja katika wale walioamua hivyo.''[1]