Kwa niaba ya Alyh Bab, gombesugu, basi chukuwa huu mpini walaahai...kutoka kwa Harith Ghassany.
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia
HATA kama hupendi kusoma vitabu; hiki si cha kukosa. Kwanza kimeandikwa kwa Kiswahili fasaha; lugha yetu mama inayoanza kufifishwa na kuchujwa na kizazi kisichosoma vitabu siku hizi. Pili, kimepikwa na mtaalamu halisi. Dk Harith Ghassany alizaliwa Zanzibar akapata shahada ya udaktari wa Falsafa Chuo Kikuu cha Harvard, Massachussets, Marekani. Harvard ni chuo cha kale sana; kilianzishwa mwaka 1636 na kwa muda mrefu kimeorodheshwa na magazeti, watalaamu na chama cha vyuo vikuu duniani kuwa cha kwanza duniani.
Fani yake kuu ni utafiti. Dk Ghassany ambaye anasema alitafiti kitabu hiki muhimu kuanzia 2004 hadi 2009 alikuwa awali Profesa Msaidizi Chuo cha Udaktari na Sayansi za Afya , Chuo Kikuu cha Sultani Qaboos, kilichoko Muscat, Oman, Uarabuni. Nilipomhoji kutokea Marekani anakoishi, Dk Ghassany alifafanua lengo la kuandika kigongo hiki chenye kurasa 500: Nia yangu ni kuziondoa fitina za upotoshaji wa historia ili uhusiano mkongwe baina ya Wazanzibari, baina ya Wazanzibari na Watanganyika (Watanzania) na baina ya Waafrika na Waarabu, upate kuendelea kutiririka na kuimarika kwa maslahi ya kujenga amani na neema kwa faida ya walio wengi na vizazi vya baadaye vya pande zote. Sijawahi kusoma kitabu kinachomhusu kila Mtanzania kama hiki.
Licha ya kuhadithia, kinatafakari maswali mengi. Je, neno Afrika asilia yake nini? Vipi tukaitwa Tanzania? Vipi Wazanzibari wengine hawautaki Muungano? Mapinduzi ya Unguja yalianzia wapi? Nani hasa alihusika? Je, viongozi waliopindua ndiyo waliotawala? Ndani ya sura ya pili, inayohusu Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi, ukurasa 23, mwandishi anatueleza bila kupepesa macho: Msomaji anatakiwa awe makini kabisa na hata kabla hajaendelea kusoma inampasa afahamu kuwa viongozi wakubwa wa Chama cha Afro Shirazi kama marehemu, Mzee Abeid Amani Karume, marehemu Mzee Thabiti Kombo Jecha au Sheikh Aboud Jumbe hawakushiriki katika mipango halisi ya mapinduzi ya Zanzibar. Si kitabu cha kisasi chenye azma ya kusakama wakuu wa nchi na mashujaa wetu wa zamani kibwege; au kuwachafua. Dk Ghassany anakiri hana kabisa mshawasha wa kutaka kuja kuwa mwanasiasa au mgombea kiti cha urais. Zamani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipenda kutuambia wasomi tusisahau tulikotoka. Kambarage alimlinganisha msomi na kijana aliyetumwa na kijiji chenye njaa kukitafutia ahueni kisha arudi kuwasaidia wanavijiji wenzake.
Dk Ghassany ni msomi wa kabila hilo. Katimiza wajibu wake. Anasema kitabu kilikuwa kigumu kukiandika na pia kigumu kukisoma. Moja ya msingi mahsusi wa kazi za historia ni kutukumbusha watu tuliowasahau na mafunzo yake.
Tunamkumbuka John Okello? Je, Oscar Kambona, mpinzani mkuu wa hayati Nyerere na ujamaa aliyeishia uhamishoni hapa London, alihusikaje katika mapinduzi ya visiwani? Je, nini kilitokea wakati wa maasi ya wanajeshi wa Tanganyika mwaka huo huo wa 1964? Je, silaha za mapinduzi ya Zanzibar zilitoka wapi? Je, vyama vingine kama Umma Party cha hayati Abdulrahaman Babu vilifanya nini? Kassim Hanga ni nani? Je, kwanini Kassim Hanga akanyongwa miaka michache baada ya mapinduzi ya Unguja, 1964? Je, aliyekuwa zamani kiongozi wa Algeria, Ahmed Ben Bella (ambaye yu hai) alihusikaje? Je, wanamapinduzi maarufu wa Cuba Fidel Castro na Che Guevara walihusika? Kwanini shirika la Upelelezi la Marekani, CIA lilikuwa likiogopa sana Unguja? Je, vipi maelfu ya Wazanzibari wamezagaa ulimwenguni wakiishi Ulaya, Marekani na Uarabuni, baada ya kuikimbia nchi yao? Je, mwanajeshi maarufu Kanali Ali Mahfoudh alifanya nini? Maswali mengi yamejibiwa si tu kwa utafiti maridadi alioufanya mtaalamu huyu bali pia kupitia midomo ya waliohusika.
Kitabu kimejazana hati za siri, za kiserikali na pia mahojiano na wazee hai walioshika mapanga enzi hizo. Wengine wao kama Victor Mkello (aliyekuwa zamani mmoja wa viongozi wakubwa wa Chama cha Wafanyakazi na TANU wanahadithia kinauga ubaga ama walivyotiwa ndani, walivyosakamwa na nani alifanya nini katika ngazi za juu. Hiki si kitabu cha mchezo. Kuna pia mchango wa mzalendo na mwanahistoria mwingine Mohamed Said (aliyeandika vitabu viwili vinavyohusika na historia ya TANU, kimojawapo Uchaguzi wa mwaka 1958 katika kutafiti habari kibao.
Alivyokuwa mkweli, mbali ya utafiti na picha lukuki; Dk Ghassany aliwaonyesha viongozi wa sasa Unguja na bara muswaada wa kitabu kabla ya kuutoa. Anasema : Mustakbali utakuwa mzuri iwapo utajiri wake mkubwa wa kihistoria wa kijiografia wa Zanzibar na Tanzania utatumika kuuimarisha Muungano wake na Tanganyika baada ya Baraza adhimu la wawakilishi kuipitia na kuifanyia marekebisho katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuyalinda maslahi ya Zanzibar na kuonyesha njia mpya ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania. Unguja na Pwani kijumla ndiko lilipo chimbuko la lugha ya Kiswahili. Kama kazi ya fasihi ya lugha hii tukufu, kitabu kitakusaidia msomaji (hata uwe si mpenzi wa mambo mazito ya kihistoria na kisiasa) kuboresha ujuzi wako wa Kiswahili fasaha, hasa vijana. Kwa watu wa makamo na wazee, wataalamu na wapenda nchi yetu watapata changamoto na jopo la kufanya majadiliano, kupitia mambo ambayo tuliyasikia tu mitaani miaka 40 iliyopita.
Huu mpini mwingine kutoka kwa Ahmed Rajabu.
Siku John Okelo alipotimuliwa Zanzibar
Ahmed Rajab
YAFUATAYO ni masimulizi mafupi ya kipindi kifupi cha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 1964 yaliyoipindua serikali ya ubia ya chama cha Zanzibar Nationalist (maarufu Hizbu) na kile cha Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP). Tunaangazia nini hasa kilitokea usiku wa Jumamosi Januari 11, yaliyojiri siku ya pili yake na mwezi mzima wa Januari, mwaka 1964 .
Tumeyakusanya masimulizi haya baada ya kuzungumza na walioshiriki katika Mapinduzi hayo ambao baadaye walisaidia kudhibiti madaraka na kuunda taasisi zilizoziba pengo la Serikali iliyopinduliwa ya Waziri Mkuu, Muhammed Shamte Hamadi.
Usiku wa manane wa Januari 11, makada wapatao 200 wa Umoja wa Vijana wa Afro-Shirazi (Afro-Shirazi Youth League) walielekea kwenye kambi ya polisi ya Ziwani, nje kidogo ya mji huko Unguja.
Wakiongozwa na Yusuf Himid wapinduzi hao hawakukabiliwa na upinzani walipofika Ziwani ila waliikuta ghala ya silaha iko wazi na wakazinyakua silaha na kukimbia nazo hadi kwenye uwanja ulio nje ya jengo la Raha Leo.
Hapo ndipo palipokuwa makao makuu ya Mapinduzi kwa siku chache na ndipo wapinduzi walikokuwa wakipewa silaha. Studio za redio ya Serikali pia zilikuwa hapo.
Moja ya sababu zilizoyafanya Mapinduzi yafanikiwe haraka ni uamuzi wa viongozi wa Serikali iliyopinduliwa Sheikh Muhammed Shamte na Sheikh Ali Muhsin Barwani kuwataka wafuasi wao wasitumie nguvu kuyapinga.
Hivyo, mbali na mapigano yaliyozuka saa za asubuhi ya Jumapili Januari 12, mbele ya Steshini ya Polisi Malindi, hapajazuka mapigano Unguja kati ya waliopindua na waliopinduliwa. Pemba nako pia hakukuwa na upinzani ijapokuwa kisiwa hicho kilikuwa ngome ya vyama vya ZNP na ZPPP.
Wengi wa wapiganaji waliokuwa kwenye Stesheni ya Polisi ya Malindi walikuwa wakuu wa polisi Wakiingereza. Wakipigana na makada wa Umma Party ambao ndio pia waliouteka uwanja wa ndege, bandari pamoja na kituo cha mawasiliano ya nje cha Cable & Wireless, kilichokuwa kwenye jengo ambalo sasa ni Hoteli ya Serena Mji Mkongwe.
Kwa hakika, kinyume cha baadhi ya watu walivyoandika hapakutokea mauaji ya kimbari. Aliyeanzisha uvumi huo alikuwa John Okello aliyeandika kwenye kitabu chake kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar kwamba watu zaidi ya elfu kumi waliuliwa. Okello aliongeza kwamba aliamrishwa na Yesu Kristo kuwakomboa Waafrika wa Zanzibar kutoka kwa wageni.
Tutamrejelea Okello na wengine waliokuwa Raha Leo baadaye. Kwanza tukumbushe kwamba mkesha wa Januari 12, mwaka 1964, Zanzibar haikuwa na jeshi. Kulikuwa polisi waliokuwa wakiongozwa na Waingereza. Wengi wa askari polisi walikuwa raia wa Tanganyika. Serikali iliyopinduliwa ilikataa kuandikiana mkataba wa kijeshi na Uingereza kwa sababu ikihisi mkataba kama huo utaonekana kuwa wa kikoloni.
Hatuwezi kusema ni nani hasa aliyepiga risasi ya mwanzo au ya mwisho katika Mapinduzi. Naitoshe tusemapo kwamba kwa vile hakukuwa na upinzani, Serikali iliyokuwa madarakani iliporomoka kama nyumba ya karata.
Tuwarejelee sasa waliokuwa Raha Leo, makao makuu ya Mapinduzi kwa siku chache. Kwanza tumuangalie Okello ambaye sauti yake ndiyo iliyokuwa ikivuma kwenye Redio Zanzibar.
Hatuna uhakika nani alimpeleka Okello Raha Leo. Wengine wanasema ni Yusuf Himidi. Wengine wanasema ni Seif Bakari aliyetoa rai atumiwe kutoa matangazo kwenye redio kwa vile sauti yake ilikuwa na lafudhi ngeni ya kutisha.
Uhakika tulio nao ni kwamba Okello alipotokea Raha Leo na mabastola yake, Aboud Jumbe alishtuka na akauliza: Nani huyu? Katokea wapi?
Kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 27 hakujulikana kabla ya Mapinduzi. Alikuwa mtu asiyejua kuandika wala kusoma na akili zake zikimtosha mwenyewe. Hakuwa na sifa za uongozi na wala hakushiriki katika vuguvugu lolote la kisiasa.
Akijibandika cheo cha kijeshi cha
Field Marshall ni yeye aliyetangaza kwamba serikali ya ZNP/ZPPP imepinduliwa.
Kwa hakika, kazi hiyo ya kutangaza kufanikiwa kwa Mapinduzi kwanza alipewa Ramadhan Haji, mmoja wa wapinduzi. Lakini alikataa. Jina la Okello lisingelisikika lau Ramadhan Haji angekubali kutangaza kwamba Serikali imepinduliwa na kwamba wapinduzi waliidhibiti nchi.
Waliokuwa wakiongoza mambo Raha Leo tangu Mapinduzi yaanze, hadi Jumatatu Januari 13, walikuwa Aboud Jumbe, mmoja wa viongozi wa chama cha Afro-Shirazi (ASP), Thabit Kombo (Katibu Mkuu wa ASP) na Badawi Qullatein wa Umma Party. Muda wote huo, Sheikh Abeid Amani Karume (kiongozi wa ASP), Abdulrahman Babu (mwenyekiti wa Umma Party) na Abdalla Kassim Hanga (ASP) walikuwa Dar es Salaam.
Mnamo siku hizo hizo liliundwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri lililokuwa na mamlaka kamili ya kuiendesha Zanzibar. Mabaraza hayo mawili yalikuwa taasisi kuu za Serikali ya kimapinduzi ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Na sio ile iitwayo Kamati ya Watu Kumi na Nne ambayo baadhi ya watu wanasema kuwa ndiyo iliyoandaa Mapinduzi.
Okello akipenda kujigamba kwamba ndiye aliyeyapanga na kuyaongoza Mapinduzi. Alikuwa akitoa matamshi ya kushtusha na ya ajabu-ajabu kwenye Redio Zanzibar. Kwa mfano, siku moja alidai kwamba alipwe mshahara mkubwa zaidi ya aliokuwa akilipwa Rais Karume. Siku nyingine akasema kwamba kasri zote alizokuwa akitumia sultani kupumzikia apewe yeye.
Kuna siku aliyotoa hukumu kwamba mzee mmoja wa zaidi ya miaka 60 afungwe kwa miaka 99. Alisema kama huyo bwana atakufa gerezani basi mwanawe afungwe ili kuendeleza kifungo na mwanawe akifa basi mjukuu wake afungwe mpaka itimie miaka 99.
Nyakati nyingine aliwaonya watu wazitie moto familia zao na wao wenyewe mpaka wafe kabla ya majeshi yangu kuja. Alikuwa akitoa vitisho visivyowahi kamwe kusikika Zanzibar.
Kuna siku alitangaza kwamba wakazi wa eneo moja ambako alikuwa apite, wajipange foleni barabarani wakiwa wamevaa chupi tu.
Okello alikuwa ni adha, kitisho, kichekesho na fedheha kwa Zanzibar. Viongozi wapya wa nchi walichoka naye na wakaamua kumchukulia hatua. Salim Rashid, mmoja wa viongozi wa Umma Party aliyekuwa katibu wa Baraza la Mapinduzi anasema kwamba, kwanza alilizungumza suala la Okello na Sheikh Karume. Halafu akalizungumza na Brigadia Yusuf Himid na mwisho yeye, Yusuf Himid na Kanali Ali Mahfoudh wakalitafutia dawa.
Ilisadifu kuwa siku moja Okello alisafiri kwenda Dar es Salaam akifuatana na Jaha Ubwa, aliyekuwa katibu wake. Walipokuwa wanatarajiwa kurudi Zanzibar, Karume, Yusuf Himid, Salim Rashid na Ali Mahfoudh walikwenda uwanja wa ndege kumsubiri.
Siku hiyo anaikumbuka vizuri Luteni Hashil Seif aliyekuwa ofisa wa zamu kwenye kambi ya jeshi huko Migombani karibu na uwanja wa ndege. Alipigiwa simu akitakiwa aende kwa haraka uwanja wa ndege. Hakuambiwa anaitiwa nini.
Alipofika ndipo alipoambiwa kwamba kuna ndege ya Shirika la Ndege la Afrika ya Mashariki iliyokuwa inakuja kutoka Dar es Salaam ndani yake wakiwemo pia Okello na Jaha Ubwa. Akaelezwa kwamba awaruhusu abiria wote pamoja na Ubwa washuke, lakini amzuie Okello asishuke. Halafu amwambie rubani ampeleke Okello Kenya.
Hashil naye akampigia simu komredi mwenzake Luteni Amour Dugheshina kumwita aende uwanja wa ndege amsaidie. Maluteni wote wawili walikuwa na bunduki za aina ya machine gun.
Ndege ilipotua walipanda ndani ya ndege, wakampokonya silaha Okello na kutekeleza amri waliopewa. Rubani wa ndege alikasirika sana. Uso wake ulighadhibika, utafikiri mnyama aliyekosewa risasi, alieleza Hashil.
Lakini rubani hakuwa na la kufanya ila kuiwasha ndege na kuelekea Kenya.
Huku nyuma Salim Rashid akampigia simu Oginga Odinga, Makamu wa Rais wa Kenya, kumuarifu kwamba wamemfukuza Okello na wanamrejesha Kenya. Alifanya hivyo kwa makosa kwa sababu kutokana na jina lake akifikiri kuwa Okello ni Mjaluo kutoka Kenya.
Kumbe alikuwa mtu wa kabila la Acholi aliyezaliwa Uganda na alikwenda Unguja kabla ya kuhamia Pemba ambako alikuwa mwashi, mtiaji rangi nyumba na mpasuaji mawe.
Swali la kujiuliza hapa ni; je, iwapo kweli Okello alikuwa kiongozi mpendwa wa Mapinduzi ilikuwaje wafuasi wake na wanamapinduzi wenzake wasimtetee alipoadhiriwa uwanja wa ndege na kufukuzwa nchini? Ilikuwaje akafukuzwa kwa urahisi hivyo?
Kuna uzushi mwingi kuhusu kipindi hiki kifupi cha historia ya Zanzibar. Kwa mfano, kuna filamu ya kubuni ya Wataliana inayoonyesha maiti chungu nzima za watu waliopigwa risasi. Filamu hiyo ilikuwa na lengo moja tu; kuonyesha ukatili na unyama wa Waafrika.
Hakuna ithibati yoyote kwamba watu waliouawa katika siku za mwanzo za Mapinduzi walifika elfu kumi. Ukweli ni kwamba jumla ya watu waliouawa siku hizo haipindukii 200, katika sehemu za mjini hawazidi 25.
Uzushi mwingine ni kwamba walipelekwa Watanganyika, Zanzibar wakiwa na silaha kwenda kupindua. Na si kweli kwamba Mapinduzi yalikuwa na msisitizo wa kikabila. Katika kipindi cha mwanzo cha Mapinduzi msisitizo ulikuwa wa kitabaka. Nyimbo zilizokuwa zikiimbwa kwenye Redio Zanzibar zikiwazungumzia wakwezi na wakulima na wafanyakazi kwa jumla na si makabila.
Mapinduzi ya Zanzibar yalianzisha taasisi mpya za utawala zikiwa pamoja na Baraza la Mapinduzi, Baraza la Mawaziri na ofisi ya Rais. Taasisi hizo zilikuwa zifanye kazi kwa muda wa mwaka mmoja tu kwa vile ilikwishaamuliwa kwamba Januari 1965 pafanywe uchaguzi wa kulichagua Bunge la Katiba, lililokuwa litunge Katiba ya kudumu ya Zanzibar.
Baraza la Mapinduzi la Zanzibar pamoja na Serikali mpya zilianza kwa ubia baina ya chama cha ASP na Umma Party. Ingawa wanachama wa ASP ndio waliofanya Mapinduzi waliutambua mchango wa wafuasi wa Umma Party na hasa mchango wa makada wao waliopata mafunzo ya kijeshi nchini Cuba.
Vijana hao wa Umma walizitia wasiwasi serikali za Marekani na Uingereza na kuzifanya ziamini kuwa utawala mpya wa Zanzibar ulikuwa wa kikomunisti. Dhana hiyo ndiyo iliyosababisha kuchukuliwa hatua ya kuyachimba na kuyagandamiza Mapinduzi ya Zanzibar yaliyodumu kutoka Januari 12, hadi 26 Aprili, mwaka 1964.
Cc..
Wickama,
Mag3,
gombesugu,
Barubaru,
Nguruvi3,
Kadogoo,
JokaKuu,
WildCard,
THE BIG SHOW,
Jasusi,
zomba,
Spike Lee,
Pasco,
Mzee Mwanakijiji,