Bwana Nyerere,
Wazee wangu hawakuwa waasi kwa serikali kwani hiyo
serikali waliiweka madarakani wao wenyewe kwa mikono yao.
Nakuwekea hapa kwa ufupi kipi kilimpeleka babu yangu jela.
Nawaachia wanaukumbi waseme kama babu yangu alikuwa msaliti
au mzalendo.
Soma ukiwa akili yako umeifungua.
Kilichofuata baada ya kupatikana uhuru ilikuwa ni kukamatwa,
kuwekwa kizuizini na kuhamishwa kwa masheikh na Waislam
wengine waliodhaniwa kuwa wanapinga utawala wa Wakristo
serikalini. Mashuhuri miongoni mwao walikuwa:
Sheikh Hassan bin Amir, Abdillah Schneider Plantan, Sheikh
Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi
Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sharff Hussein
Badawiy, Shariff Mwinyibaba, Shariff Adnan, Bilali Rehani Waikela,
Sheikh Jumanne Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh
Hashim Haji Abdallah, Sheikh Nurdin Hussein, Salum Abdallah,
Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al Amin Maftah, Rajab Kiguu cha
Mbuzi na wengine wengi.
Lakini ukweli ulikuwa kwamba si wote katika wale waliokamatwa
na kuwekwa kizuizini walijihusisha na siasa.
Baadhi yao walikamatwa kwa sababu tu walikuwa wakishirikiana
na wale waliodhaniwa ni wapinzani wa Nyerere.
Maalim Matar na Shariff Adnan walifungwa jela kwa sababu tu
walihusika na msikiti wa Badawiy mjini Dar es Salaam ambako
Sheikh Hassan bin Amir, wakati huo akichukuliwa kuwa ndiyo
roho ya waumini wa Tanganyika, alikuwa ikiendesha madrasa
yake kila magharibi pale msikitini.
Shariff Hussein na nduguye Mwinyibaba walihamishiwa Kenya,
walikotoka si kwa sababu walikuwa wamejishughulisha katika
harakati za kuipinga serikali, ila lakini kwa sababu walikuwa
waangalizi wa msikiti wa Badawiy.
Sheikh Mzee Ali Comorian alitiwa kizuizini kwa sababu kila mara
alikuwa akifuatana na Sheikh Hassan bin Amir kama vile alikuwa
kivuli cha sheikh.
Hakuna katika orodha hii ya masheikh hata mmoja aliyefikishwa
mahakamani kwa kesi ya uhaini.
Jina lenye mstari Salum Abdallah ni babu yangu.
Salum Abdallah aliongoza mgomo (General Strike) wa 1947.
Salum Abdallah alikuwa mfadhili wa AA hadi TAA Tabora.
Salum Abdallah alikuwa katika kamati ya siri ya kuibuka na TANU
1954akihudhuria mikutano yote ya ''uchochezi'' dhidi ya Waingereza.
Salum Abdallah alitoa fedha nyingi kupita wote kumpa Germano Pacha
kuja Dar es Salaam kuwakilisha Western Province katika kuasisi TANU.
Salum Abdallah ni mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU
Salum Abdallah 1955 alikuwa rais muaisisi wa Tanganyika Railway
African Union (TRAU) chama hiki kilipigana bega kwa bega na TANU
katika kupigania uhuru.
Katibu wake akiwa Chrisant Kassanga Tumbo.
Salum Abdallah aliongoza mgomo wa Railway wa 1960 uliodumui siku
82 mgomo kama huu wa miezi 3 haujapata kutokea.
Viongozi wa TRAU walipokea msaada kutoka chama cha wafanyakazi wa
Reli Uingereza na chama cha wafanyakazi kutoka Ujerumani ya Mashariki.
Hiki ndicho kilichoiwezesha TRAU kudumu katika mgomo kwa miezi 3.
Wafanyakazi wakipata posho kuzikimu familia zao.
Salum Abdallah katika mkutano wa Moshi 1962 alimpinga Nyerere
katika suala la kuweka vyama vya wafanyakazi chini ya TANU.
Hii ndiyo sababu ya yeye kuwekwa kuzuizini.
Babu yangu hakuwa haini.
Babu yangu alikuwa mzalendo mpigania uhuru kwa vitendo toka
enzi za African Association akiwa akiwa Dar es Salaam.
Nyerere alipata hofu ya wazalendo kama hawa waliokuwa na uwezo
wa kuwakusanya wananchi pamoja kudai haki zao.
Mgomo ule wa 1960 ndiyo uliomfanya Nyerere apate hofu na Salum
Abdallah.
Akiwa jela ya Uyui taarifa zikamfika Salum Abdallah kuwa TRAU
na vyama vyote vya wafanyakazi vimevunjwa na Nyerere na chama
kimoja cha vibaraka NUTA kimeundwa kuwawakilisha wafanyakazi wa
nchi nzima.
Salum Abdallah hadi anaingia kaburini alikuwa na orodha ya watu wake
akiwaita waongo, vibaraka, wasaliti na wengi katika hao walikuwa katika
NUTA, TANU, na serikalini...
Julius Nyerere...
Michael Kamaliza...
Rashid Kawawa...
Wanaukumbi tafuteni majina ya watu hawa ambao babu yangu
aliwaorodhesha kama waongo, vibaraka na wasaliti.
Si tabu kuwajua.
Alipokufa 1974 TANU walifika mazikoni na walisoma taazia ya kumsifia
babu yangu na kumwita mzalendo aliyejitolea kwa hali na mali yake
kuipigania nchi yake.
Huyu alikuwa Mmnanyema kizazi cha kwanza kuzaliwa Tanganyika baba
yake Samitungo Mwekapopo aliingia nchini kama askari katika jeshi la
Wajerumani.
Bwana Nyerere huyu ndiye babu Salum Abdallah yangu ambae kaanza
harakati za kupigania uhuru wa nchin hii wala hamjui Nyerere.