Kuna kitu kimoja ambacho wanaolia "dhulma" wanadhani Watanzania hawakijui sana. Wakati wa Nyerere kama kuna kitu kilikuwa kinapigwa vita sana ni kile alichokiita "undugunization" yaani kwa neno la kimombo "nepotism". Tafsiri moja ya nepotism inasema ni "
patronage bestowed or favoritism shown on the basis of family relationship, as in business and politics".
Sasa undugunization ulianza kwa kasi baada ya kuanza kuwa na kada ya watumishi wa umma wasomi ambao wameanza kushika nafasi. Kwa kiasi wale waliopata nafasi kidogo walianza kuwaingiza wana familia wao kwenye hizo ajira. Kama Baba alikuwa meneja wa Benki basi mtoto wake akigraduate naye anatafutiwa kazi benki; hii ilikuwa kweli kwenye polisi, na ilikuwa kweli kwenye ajira nyingi sana. Na kwa kadiri watu walivyozidi kupata nafasi za juu ndivyo nao walivyozidi kuwaingiza ndugu zao kwenye ajira na hawakufungwa na ofisi zao kwani waliweza kuwaunganisha na marafiki zao kwenye kada nyingine. Hivyo, mtu anaweza kuwa yuko Ikulu lakini mtoto au jamaa yake akaunganishwa kupata kazi Benki Kuu, au taasisi nyingine.
Lakini hili halikuishia tena kwenye undugu wa damu likawa limeingia hata kwenye undugu wa "kijiji kimoja"; ambapo hapa utakuta watu ambao wanatoka kijiji kimoja (hata kabila moja) wanadai undugu na kuombeana msaada. Hivyo, mtoto atatoka Tarime na kwenda kwa 'mjomba' Arusha ambaye ni afisa wa JWTZ ambaye atamtafuta kazi kujiunga na jeshi. Matokeo yake utakuta watu wa kabila moja nao wakiwa wamejazana sehemu fulani.
Huu undugunization ndio kwa kiasi kikubwa sana umekithiri na sijui kama kuna Mtanzania ambaye hana ndugu au jamaa aliyenufaika na kumfahamu mtu fulani. Lakini katika maana yake pana zaidi huu 'undugunization' ulifika hadi kwa marafiki. Watu waliosoma pamoja wanasaidiana na marafiki wanapeana nafasi na hata kwa watoto wao. Kwa mfano, mtu ambaye ni Mkristu mwenye tafiki Muislamu anaweza kuombwa na rafiki yake kumtafutia "binti" yake ajira na akafanya hivyo. Yule binti ataingia kwenye ajira na hakuna mtu ataweza kuona upendeleo kwa sababu aliyeingia ni Muislamu na kaingizwa na Mkristu (au kinyume chake).
Hili unaliona hata kwenye teuzi mbalimbali. Mtu Muislamu anaweza akamteua mtu Mkristu ambaye anaweza asiwe na uwezo sana lakini watu wasione "upendeleo" kwa sababu wamefungwa na kuangalia dini tu. Ukiniuliza mimi kitu kinachowanyima watu nafasi kuendelea katika ajira siyo "dini" hasa bali 'undugu" ambapo pamoja na nepotism sasa kuna 'cronyism' yaani '
thepracticeoffavoringone'sclosefriends,especiallyinpoliticalappointments.'
Mfano mzuri sana wa haya mawili ni nafasi za ajira kule BoT ambao tuliona majina ya watoto wa vigogo yakijazana na kupeana nafasi mbalimbali. Sidhani kama kuna mtu anaweza akasema wale walipewa upendeleo kwa sababu ya dini zao. Na hivi karibuni tumeona pia kwenye viwanja vilivyouzwa kule Kigamboni ambapo wanasiasa na watumishi wakubwa serikalini wamepewa viwanja hivyo kwa kufahamiana na wahusika.