Hotuba ya Bajeti ya Miundombinu 2007 - na Andrew Chenge
32. Mheshimiwa Spika, kuhusu usafiri jijini Dar es Salaam,
Shirika la UDA limeendelea kutoa huduma ingawa kwa kiwango
kidogo. Katika kipindi cha 2006/2007, Shirika lilikuwa na wastani wa
mabasi 22 yaliyokuwa barabarani kwa siku. Shirika pia lilinunua
mabasi mapya 3 na kufufua mabasi 10 yaliyokuwa yamesimama.
Jumla ya abiria 1,698,263 walisafirishwa katika mwaka 2006/07,
ikilinganishwa na Mwaka 2005/06, ambapo jumla ya abiria 994,924
walisafirishwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 80. Hata hivyo, kiwango
kikubwa (zaidi ya asilimia 70) ya huduma za usafiri jijini Dar es
Salaam ziliendelea kutolewa na watoa huduma binafsi maarufu kwa
jina la Dala dala. Katika mwaka 2007/08 Wizara itaendelea na
taratibu za kurekebisha utendaji wa Shirika ili liweze kutoa huduma
kwa ufanisi zaidi.
Mradi wa CRDB wa mabasi ya Wanafunzi wafunguliwa 07/06/2010
1 Comment
Jumatatu ya leo, majira ya asubuhi ya Juni 7 katika viwanja vya Karimjee, benki ya CRDB imezindua rasmi mradi wa mabasi ya Wanafunzi kwa Mkoa wa jiji la Dar Es Salaam kwa lengo la kuwaondolea wanafunzi kero na adha mbalimbali wanazokumbana nazo mara kwa mara waendapo na kurejea shuleni na majumbani.
Jumla ya mabasi matano yenye uwezo wa kubeba wanafunzi mia moja yametengwa rasmi kwa shughuli hiyo ya kupakia Wanafunzi tu katika sehemu mbalimbali za Jiji la Dar Es Salaam.
muonekano wa mojawapo ya mabasi ya mradi wa CRDB wa Wanafunzi
Mabasi hayo yenye thamani ya sh. milioni 500 pamoja na ushuru yalikabidhiwa kwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA). Mabasi hayo yataanza kutoa huduma wiki ijayo kati ya
Kariakoo - Chanika, Kariakoo –Tegeta na Kariakoo –Mbezi Louis, maeneo ambayo yana kero kubwa ya usafiri kwa wanafunzi.
Akizindua mradi wa mabasi hayo katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilitaka shirika la UDA kuwa macho ili usije ukafia mikononi mwao.
Pinda alisema itakuwa aibu na fedheha kwa wanafunzi walioshuhudia uzinduzi huo, kuona mradi unayeyuka. Waziri Mkuu Pinda akizindua mradi huo kwa Niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema Dar es Salaam ina zaidi ya wanafunzi 500,000 wanaohitaji usafiri kila siku. Alisema ili kutosheleza mahitaji ya usafiri kwa wanafunzi hao, kila asubuhi na jioni, yanahitajika mabasi 10,000. Kutokana na hilo, aliwahimiza wadau wengine kuchangia, akisema serikali iko tayari kuondoa ushuru kwa watakaokuwa tayari kununua mabasi kwa ajili ya mradi huo. Waziri Mkuu alisema ni ruksa kwa kila taasisi itakayotoa msaada kuweka nembo yake kujitangaza katika mabasi hayo.
Kwa upande wake, Meneja wa UDA,
Martin Milanzi, alisema nauli kwa wanafunzi itakuwa sh. 100.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk.
Charles Kimei, alisema wameamua kutoa msaada huo kwa kutambua kero wanazopata wanafunzi katika usafiri. Dk. Kimei alitoa wito kwa wadau wengine kusaidia katika kuondoa kero ya usafiri kwa wanafunzi mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
William Lukuvi, alilitaka UDA kuhakikisha linaweka utaratibu mzuri wa kusimamia mabasi hayo. Lukuvi alikumbushia mradi kama huo aliowahi kuuasisi, lakini ulikufa baada ya yeye kupanda cheo na kuhamishwa kutoka mkoa wa Dar es Salaam.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Jumanne Maghembe; Waziri wa Miundombinu, Dk.
Shukuru Kawambwa; Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
Adam Kimbisa; Mkurugenzi Mtendaji wa SUMATRA,
Israel Sekirasa; Mwenyekiti wa Bodi ya UDA,
Idd Simba na
wanafunzi wa shule kadhaa za Dar es Salaam.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Boko ya Jijini Dar es salaam wakipanda kwenye moja ya mabasi matano yaliyotolewa kwa mradi na Benki ya ya CRDB ampapo yameanza kutoa huduma hiyo jana. Wanafunzi hao walikutwa katika eneo la Boko Kilometa 30 toka katikati ya jiji.
Mabasi matano ya wanafunzi yaliyotolewa na benki ya CRDB, sasa yameanza kazi rasmi ya kusafirisha wanafunzi katika sehemu mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) linalosimamia mabasi hayo, Victor Milanzi, alisema mabasi hayo yanafanya kazi vizuri na yamekuwa yakipata abiria wengi.
"Yameanza leo (jana) kwa kuwa wanafunzi walikuwa wamefunga na sisi tukaona ni vyema yakasubiri hadi wafungue, Sasa wamefungua na yameingia barabarani kufanya kazi," alisema Milanzi.
Alisema mabasi hayo yameanza kutoa huduma zake katika njia za Mbagala Kariakoo, Chanika Kariakoo, Kariakoo-Kimara-Mbezi na Kariakoo Tegeta.
Milanzi aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa kutakuwa na wakaguzi watakaokuwa wakifuatilia utendaji wa kila siku wa mabasi hayo na kwamba pamoja na mambo mengine watakuwa wakikagua tiketi na mapato ya mabasi hayo.
Milanzi alisema baada ya muda wanatarajia kuanza kutoa tiketi za msimu ambapo wanafunzi watakuwa wakikata tiketi za mwezi mzima.
"Kwa sasa tiketi ni za kawaida na nauli ni Sh 100 ila kama mabadiliko yanaweza kufanyika baadae ikionekana kuna haja ya kufanya hivyo," alisema Milanzi.
Alisema kutakuwa na wakaguzi watakaokuwa wakifuatilia utendaji wa kila siku wa mabasi hayo.