UDOM, SYDF na TISEZA Waibua Mwanga wa Uwekezaji kwa Vijana

UDOM, SYDF na TISEZA Waibua Mwanga wa Uwekezaji kwa Vijana

University of Dodoma (UDOM)

Public Institution
Joined
Feb 24, 2024
Posts
50
Reaction score
55
WhatsApp Image 2026-05-16 at 18.36.21.jpeg


Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwa kushirikiana na Shirika Lisilo la Kiserikali la Save Youth Dream Foundation (SYDF) pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), leo tarehe 15 Mei 2026, wameendesha mafunzo ya uwekezaji kwa wanafunzi yaliyofanyika katika Ukumbi wa CIVE Auditorium, kwa lengo la kuwajengea vijana uelewa na hamasa kuhusu masuala ya uwekezaji na usimamizi wa fedha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu Makamu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, amesema vijana wengi hukumbana na changamoto ya matumizi sahihi ya fedha wanazozipata, jambo linalowakwamisha kufikia malengo yao ya kifedha na maendeleo ya baadaye.

Prof. Lokina alieleza kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa vijana, kwani yatawasaidia kujifunza namna bora ya kutunza fedha, kuwekeza na kujijengea msingi imara wa kiuchumi kabla na baada ya kuhitimu masomo yao.

“Nitoe wito kwa wanafunzi kuyachukulia mafunzo haya kwa umakini mkubwa. Ningependa ifikapo mwisho wa mafunzo haya kila mwanafunzi awe ameelewa namna ya kutumia hata fedha ndogo anayoipata, iwe katika hati fungani, biashara za mtandaoni au uwekezaji mwingine wenye tija, ili fedha hiyo iweze kumzalishia manufaa na kuongeza kipato chake baadaye,” amesema Prof. Lokina.

Kwa upande wake, Meneja wa Miradi kutoka Save Youth Dream Foundation (SYDF), Bi. Winnie Kaaya, amesema programu hiyo itakuwa ikiendeshwa kila mwisho wa wiki hadi tarehe 13 Juni 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia elimu ya uwekezaji.

Naye Meneja wa Kanda ya Kati kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Bw. Venance Mashiba, amesema uwekezaji ni safari inayohitaji elimu, nidhamu na uthubutu. Amefafanua kuwa kuwapatia vijana elimu ya uwekezaji mapema huwajengea ujasiri na uwezo wa kuwa wawekezaji wakubwa na wenye mafanikio siku zijazo.

Aidha, amewahimiza vijana kutokuwa na hofu ya kuanza kuwekeza, akisisitiza kuwa uwekezaji hauna umri maalumu, bali unahitaji maamuzi sahihi na utayari wa kujifunza.

Mafunzo hayo yameelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuwaandaa wanafunzi kupanga maisha yao ya baadaye, kujenga uwezo wa kifedha na kufikia ndoto zao kupitia uwekezaji wenye tija na endelevu.
 
Back
Top Bottom