View attachment 3579043
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya nchini, kimeratibu kikao maalum cha kitaifa kilichowakutanisha wataalamu wa radiolojia na tiba ya mionzi kwa lengo la kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
View attachment 3579039
Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Havard, uliopo ndani ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), na kililenga kuunda Kikundi Kazi (Technical Working Group) pamoja na kuandaa hadidu za rejea zitakazoongoza utekelezaji wa mradi wa huduma za uchunguzi wa papo kwa papo (Point of Care Ultrasound, POCUS) kwa kutumia akili unde (AI).
Wadau walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na wawakilishi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za Kanda Maalum, Hospitali za Wilaya, pamoja na Taasisi muhimu zikiwemo Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
View attachment 3579040
Akichangia mada wakati wa kikao hicho, mwakilishi kutoka UDOM, Dkt. Sophia Gibore, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SoNPH), alisema kuwa hatua hiyo imechochewa na utekelezaji wa Mradi wa SAFARI, unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa mapema, hususan kwa wanawake katika vituo vya afya vya ngazi ya msingi.
View attachment 3579041
Alieleza kuwa matumizi ya teknolojia ya akili unde katika uchunguzi wa ultrasound yataongeza uwezo wa kugundua changamoto za kiafya kwa wakati, kuboresha ubora wa matibabu, na kuchangia kupunguza vifo vya mama na mtoto, ikiwa ni miongoni mwa vipaumbele vya afya vya Taifa.
Kwa upande wake, Dkt. Gerald Mrema, mtaalamu wa radiografia kutoka Wizara ya Afya na mratibu wa huduma za uchunguzi na tiba kwa kutumia mionzi, aliipongeza UDOM kwa ubunifu huo pamoja na juhudi zake katika kuendeleza tafiti zenye tija. Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu, Serikali na Taasisi za Afya ili kukuza Utafiti, kujenga uwezo wa wataalamu, na kuimarisha mfumo wa afya unaojibu mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Kwa kauli moja, wadau walieleza kuridhishwa na hatua hiyo, wakitambua mchango wa Mradi wa SAFARI katika kuleta jukwaa muhimu la majadiliano ya kitaifa. Walibainisha kuwa teknolojia ya POCUS ina uwezo mkubwa wa kuboresha utoaji wa huduma za afya, hususan katika maeneo yenye upungufu wa wataalamu bingwa.
View attachment 3579042
Kikao hiki ni sehemu ya muendelezo wa juhudi zilizoanza katika kikao cha awali kilichofanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 30 Machi hadi 2 Aprili 2026, ambapo wadau walipata mwongozo wa awali wa kuanzisha na kutekeleza mradi huo. Hatua hii inaashiria dira ya pamoja kuelekea mfumo wa afya ulioimarishwa unaotegemea maarifa, teknolojia na ushirikiano katika kufikia maendeleo endelevu.
View attachment 3579044