Asante mkuu. Jibu langu litakua refu kidogo. Ni matumaini yangu sitawapoteza watu.
Kwa anaetaka kujua kwa kitaalam zaidi kuhusu
Neutrinos anaweza kupata taarifa hizi kwenye internet (search for it). Hapa nitajaribu kuelezea kwa lugha rahisi haya yafuatayo:
- Neutrino ni nini?
- Neutrino zinatengenezwaje?
- Neutrino zina faida gani kwetu?
- Je neutrino zina madhara kwetu?
Neutrino ni nini?
Tulijifunza kwenye sayansi ya sekondari kuwa
atom ina viambata vitatu navyo ni:
- Protons (+ve charged na zina uzito),
- Neutrons (haina chaji na zina uzito), na
- Electrons (-ve charged na karibuni hazina uzito - lakini zinao kidogo).
Ukweli ni kuwa kuna chembe chembe (sub-atomic particles) nyingi zaidi kuliko hizo tatu tulizojufunza.
Neutrino (ziko za aina 3) ni moja ya hizo chembe (sub-atomic particles) ambazo hazina chaji kabisa na uzito wake ni mdogo sana kuliko hata wa electrons (uzito wa neutrino milioni moja ni sawa na uzito wa electron moja).
Neutrino zinatengenezwaje?
Kukiwa tu na mlipuko wa ki-nyuklia (kama vile kwenye jua letu, nyota, super nova, mabomu au mitambo ya nyuklia) basi neutrino zinatengenezwa. Popote pale atom zinapopasuliwa (fission, kama mabomu ya nyuklia) au atom zinapounganishwa (fusion, kama kwenye jua au nyota) basi neutrinos zinatengenezwa. Jua letu linatumwagia neutrino billion 65 kwa sekunde katika kila eneo la sentimita moja ya mraba hapa duniani.
Tofauti na mwanga wa kawaida au hata ultra-violet na X-rays, neutrinos hazizuiwi na chochote kile. Zikitua hapa aridhini basi hupita moja kwa moja mpaka upande wa pili wa dunia kwa kasi ya mwanga na kuendelea. Kwa hiyo hata wewe hivi tunavyosema unalabuliwa na neutrino 65 billion kwa sekunde katika kila eneo la sentimita moja ya mraba ya mwili wako (na hiyo ni kutoka kwenye jua tu - na kuna za ziada kutoka sehemu nyingine).
Usifikirie kuwa usiku utakuwa salama, la hasha. Jua likiwa upande mwengine wa dunia hizo neutrino zake zitapenyeza mpaka upande wa pili ambako ni usiku na kukuzaba tu. We kaa mkao wa kula tu mkuu.
Neutrino zina faida gani kwetu?
Kwa kuwa neutrino hazina chaji basi haziathiriwi na nguvu za smaku (electromagnetic fields). Wakati hatuwezi kutumia mwanga wa kawaida kuchunguza kilichopo ndani ya jua letu au nyota na galaxies nyingine, tunaweza kutumia hizi neutrinos kama kurunzi (tochi) ya kuchungulia pasipoweza kuchungulika kwa sasa. Bado utafiti unaendelea wa kutengenezea hizi kurunzi za neutrinos.
Pia kama hizi kurunzi zitapatikana inawezekana tukaachana na upigwaji picha hatarishi wa matibabu kama vile X-rays, MRI (wanasema sio hatarishi lakini sijui), n.k. na tutumie
neutrino-scans badala yake?
Unaona utamu huo mkuu.
Je neutrino zina madhara kwetu?
Hili sina uhakika nalo bado lakini nawaza tu. Kama neutrino nyingi kama hizi zinapita kwenye miili yetu, ya wanyama, miti, na viumbe hai vyote, je inawezekana kutubadilishia (mutations) maumbile ya DNA zetu? Kama ni kweli je tunaweza kutengeneza ngao au mwemvuli (neutrino shields) wa kujikinga nazo?
Sijui, lakini hapa ndio tunapofikia utamu wa sayansi.