kwanza niwashukuru wadau wote mliochangia ktk uzi huu ulianzishwa na kubota kiukweli nimepata elimu kubwa sana kuhusu industry hii ya ufugaji wa kuku wa asili.
kumekuwa na imani fulani inayo aminika kuwa kuna baadhi ya mambo ili yafanikiwe yanategemea ngekewa alimaharufu kama MKONO MZURI pia katika swala la ufugaji wa kuku inaaminika ili uwe na kuku wengi inategemeana na mkono wako yaani inamaana kwamba kuna watu wana ngekewa/bahati na kuna watu kamwe hawawezi kuwa na idadi kubwa ya kuku,hii inaaminika kuwa Mungu anahusika na upendeleo wa kalama hii.Kwa mfano kuna ndugu yangu mmoja akipanda pilipilihoho hazikui lakini akimwita mtu mwingine ampandie ktk hiyo hiyo bustani yake kinachotokea hoho ustawi na kutoa matunda.JE,HII PIA INAWEZA IKAWA CHANGAMOTO NYINGINE KTK UFUGAJI WA KUKU?Asante.
Mkuu
chama2chawa: Umeleta hoja ngumu na pana sana kuweza kuielezea kwa utoshelevu ikaweza kukidhi haja. Ni hoja inayoweza kuzua malumbano yasiyoisha kiasi cha kuharibu uelekeo wa hii THREAD. Maana hoja hii imejikita kwenye imani zilizojichimbia sana kwenye jamii nyingi za kiafrika na imani hizi zinatutafuna sana tusiweke juhudi ya kung'ang'ania zaidi kuyatafuta yale tunayoamini yanaweza kutuinua kimaendeleo. Imani hizi ndiyo kwa mapana yake watu wanajikuta kwenye kutafuta ndumba zinazodhuru hadi maisha ya watu ili wapate kinachoitwa ngekewa au waondoe nuksi!
Suala hilo linawatatiza zaidi watu ambao hawajaelimika. Kadri jamii au watu wanavyoelimika zaidi ndiyo jinsi ambavyo imani kama hizo zinapungua! Mtu aliyeelimika hutamjua kwa kumiliki vyeti na madigrii bali utamjua kwa anayojiamini na kwa matendo yake, mtu aliyeelimika anatarajiwa ahusishe kufikiri juu ya ukweli wa lile analoliamini na siyo kukariri mambo kama tunavyokaririshwa bila kuhoji vitabu vya dini!
NGEKEWA au NUKSI ni maneno ambayo huyatumia watu wanaojifariji kwa kutafuta majibu rahisi kwa masuala magumu! Mtu aliefanikiwa watu humwelezea kuwa ana NGEKEWA na mtu aliyeshindwa kufanikiwa humchukulia ana NUKSI. Dunia ya leo (ya sayansi na technolojia) mtu ambaye bado anaamini hivyo atachelewa sana au ataishia kubaki nyuma! Mtu anaedhani ana mkono mbaya na akaamini hivyo huyo maendeleo hawezi kuyapata kamwe!
Hakuna binadamu anaeng'ang'ania kujifunza jambo akashindwa kulijua, tunaweza kutofautiana spidi ya kuelewa jambo tunapojifunza lakini mwisho wa siku mtu utaelewa tu, ndiyo maana tunavaa suluali, mashati na viatu kwa usahihi, kwenye vyoo vyetu vya shimo tunalenga vizuri tu, yote haya tulijifunza hatukuzaliwa tukijua yote haya na kama huamini kumbuka jinsi mtoto anavyopishanisha matundu anapoanza kufunga vifungo vya shati siku za mwanzo, au kubadili viatu mguu kulia kuvaa kushoto.
Ikitokea mtu umefanya jambo mara moja, mbili, tatu hata mara nne usifanikiwe siyo sahihi kujichukulia kwamba una nuksi au unadamu mbaya! Kama una imani juu ya jambo unalolifanya kwamba ukilimudu kulifanya linaweza kukuinua basi wewe endelea kulifanya tu maana kadri unavyoendelea kupiga mieleka ndiyo unavyozidi kulielewa vizuri zaidi mwishoni kitaeleweka tu.
Kuhusu mfano wa mpandaji wa hoho ulioutoa anaweza akawa na mkono mbaya kwa maana ya kwamba hajui kupanda hoho! Je alikuwa anapanda kwa usahihi? Ni rahisi sana kufanya utafiti ili kujua kama ni mwili wake ndiyo wenye nuksi na siyo kwamba hajui kupanda. Aende akapande sehemu tatu tofauti na watu wengine ili ionekane kama kote huko matokeo ni yale yale! Ikitokea hivyo tueleze hapa JF tumtangaze huyo Bwana maana wenzetu wa nchi zilizoendelea huyo jamaa kwao atakuwa kivutio kikubwa sana cha utalii na itabidi wampime hata damu yake waichunguze! Kwamba yeye kila akipanda hoho haziponi au hazizai au hazisitawi lol!
Kupanda miche au mbegu siyo ni kule kufukia mche kwenye udongo tu, kuna mbinu zake! Kwenye kilimo cha vitunguu na mpunga mimi mwenyewe nimewahi kukutana na baadhi ya wapandaji wangu vibarua kadhaa ambao wamewahi kunisababishia hasara kwa miche waliyopanda kufa au kutokusitawi vizuri! Hii ilitokana na wao wanapopanda wanashika miche vibaya, wanaishikia katikati ya mche na kuizamisha hivyo hivyo kwenye udongo na inajikunja kama herufi ya
U, yaani majani na mizizi inatokeza juu, shina ndiyo linazamishwa chini! Yaani mche unapandikizwa lakini ukiutazama unakuta mizizi yote imetokeza juu ya udongo! Mpandaji huyo unakuta ile strip aliyopanda yeye ama miche inakufa au inakuwa dhaifu tofauti kabisa na walikopanda wengine! Mpandaji huyu akisakamwa kuwa akipanda miche inakufa au haizai vizuri atajiona ana mkono mbaya! Kuna mifano mingi tu ya aina hii ambapo watu kwa kuwa makini wengine wanafanikiwa na kuitwa wana ngekewa au damu nzuri na wengine kwa kutokuwa makini hawafanikiwi na wanaonekana wana damu mbaya au nuksi!
Kwa hiyo Mkuu
chama2chawa kujibu hoja yako kuwepo ngekewa au kutokuwepo ngekewa kwenye eneo lolote la maisha inategemea wewe ni mtu wa mlengo gani! Watu walioelimika hilo wala siyo suala la kujadili kabisa!
Kuna jambo moja tu kwa uhakika kabisa ambalo lipo nalo linaitwa CHANCING hilo kwa hakika lipo! Kwa mfano ugonjwa wa kuku unaweza kukumba eneo fulani tu eneo lingine kuku wakasalimika; mvua inaweza kunyesha eneo fulani watu wakaokoa mazao na eneo lingine isinyeshe yakakauka; mtu anaweza kuuza hoho sokoni leo, kesho yake jirani yake akaingiza mzigo sokoni akakuta bei imeshuka au imepanda, unaweza kununua chanjo imekufa bila kujua kuku wako wakaugua na kufa jirani yako akaenda nunua kwingine chanjo nzima akatibu kuku wake wakabaki salama n.k. Lakini wataalamu wanasema kuwa kunachochangia sana kwenye mafanikio ya shughuri mbalimbali asilimia 5% ni CHANCING, na 95% inatokana na Management! Kwa hiyo iwapo kama chancing ni NGEKEWA (au NUKSI) mchango wake kwenye kufanikiwa ni asilimia 5% tu si kitu cha kutegemea wala si kitu cha kuhofia.