Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Mashkuura yaa jamiiya. Nimefurahi sana huu usanifu wa lugha.
Dr Hamza. (Barubaru)
Mwalimu, duh nimefurahi kutambua kwamba upo. Natumaini na familia nzima wote wazima. Tunakukaribisha tena na tena. Usipotee hivyo ndugu yangu.
Ha ha ha.............!!!!!!mmnipa raha mtimani! shukrani
Umenikumbusha makange na week end ndo inaanza...Lol
Belinda amejaribu, wa kisamvu amebaini
Nyama choma na chachandu, mchanganyiko makini
Ugali kweli mtamu, jaribu wa rozigadeni (Rose Garden! Lol)
Ugali ule kwa makange, mpishi utamsifu
Haufanani na makande, ingawa nayo nadhifu
Ugali yake makange, kila siku utausifu
Ugali pia mtamu, hata kwa dagaa chaza
Ukitaka dagaa watamu, ni wa Kigoma au wa Mwanza
Ugali dagaa mtamu, hakika huwezi saza
Tuko pamoja Mkuu. Asante.Maamuma shukrani..... narudi hivi punde
Wote nimewashangaa, mlosifia ugali,
Mmefanya ukangaa, kwa sifa zisizo kweli,
Wengine mwagaagaa, kushangilia ugali,
Utamu ni wa ugali, au chake kitoweo?
Kila palipo ugali, hapakosi kitoweo,
Kumeza tonge muhali, bila chake kimezeo,
Na huo ndio ukweli, mawio hadi machweo,
Utamu ni wa ugali, au chake kitoweo?
Mnasifia ugali, pembeni mwataja mboga,
Hebu semeni ukweli, mboga ndio inanoga,
Acheni kututapeli, kutugeuza mizoga,
Utamu ni wa ugali, au chake kitoweo?
Mzee Mwanakijiji, ndugu yangu wa daima,
Ugali si kama uji, bila mboga utatema,
Bora wali wa Ujiji, usiokuwa na nyama,
Utamu ni wa ugali, au chake kitoweo?
Yametajwa matembele, mlenda pia kisamvu,
Pweza, dagaa mchele, kachumbari na mnavu,
Nyama nayo vilevile, ya mchuzi ama kavu,
Utamu ni wa ugali, au chake kitoweo?
Ugali huli mkavu, kama ubwabwa wa Kyela,
Yatakuvimba mashavu, tonge huwezi kulila,
Yataka uwe shupavu, vinginevyo ni madhila,
Utamu si wa ugali, bali chake kitoweo!
Msinione mbishi, bali ni yangu maoni,
Wala msinishawishi, niyakubali ya nani,
Maswali siyajalishi, kuweni uhuru moyoni,
Utamu si wa ugali, bali chake kitoweo!
Ugali kweli mtamu,
Kwa huo ninayo hamu,
Kwa mboga yenye saumu!
Ugali tangu shuleni
Jamani hadi jeshini
Nikaula na chuoni
Ugali iwe mchana
Kwenye upepo mwanana
Mwenzenu ninajichana
Ugali hata jioni,
Mezani au jikoni
Nikishatoka kazini
Ugali iwe kwa mboga
Sima kwa kweli yanoga
Kwa tembele na maboga!
Ugali kwa kurumagia
Vidole kujilambia
Na nyama inanukia!
Ugali ule kwa mchuzi
Wa samaki hata mbuzi,
Mwanawane kama kazi!
Ugali msosi wa nguvu
Haupikwi kwa wavivu,
Au walio wachovu
Ugali uwe kiporo
Alfajiri na mmajoro
Kwa mapanki ya Nyamanoro!
Ugali nimesifia
Wali ninautungia
Beti nitaupangia,
Ugali nafakamia
Matonge navingiria
Nakula nafikiria
UGALI KWELI MTAMU!!
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Wali ukitiwa nazi,
Kama uchi wenye vuzi,
Hata kama mwanafunzi,
Utadinda kama tozi.
Ugali kweli mtamu,
Kwa huo ninayo hamu,
Kwa mboga yenye saumu!
........UGALI KWELI MTAMU!!
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)