Ugiriki, siku ya Alhamisi imekuwa nchi ya kwanza ya kikristo wa ki-Orthodox kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja - wakati mgumu kwa jumuiya ya LGBTQ ya nchi hiyo, jumuiya ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipigania kuonekana na haki katika kivuli cha kanisa la Ugiriki lenye ushawishi mkubwa.
Mswada huo pia unaruhusu wapenzi wa jinsia moja kuasili watoto na kutoa haki kamili za mzazi kwa wenzi waliooana, ingawa mswada umekataa kuruhusu wapenzi wa jinsia moja kuwa wazazi kwa njia ya kupandikiza mbegu kwa wanawake wengine wawazalie (surrogacy) , kizuizi ambacho kimesababisha ukosoaji kutoka kwa vikundi vya kutetea haki za binadamu.
Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba Ugiriki "inajivunia kuwa Nchi ya 16 katika Jumuiya ya umoja wa ulaya kutunga sheria ya usawa wa ndoa.β Aliita hatua hiyo "hatua muhimu kwa haki za binadamu, ikionyesha Ugiriki ya leo - nchi inayoendelea, na ya kidemokrasia, iliyojitolea kwa maadili ya Ulaya."
Kura ya Alhamisi ilivuka mipaka ya vyama, huku wabunge 176 kati ya 300 katika Bunge la Hellenic wakipiga kura kuunga mkono hatua hiyo. Sabini na sita walikataa mswada huo, wawili hawakupiga kura na 46 hawakuwepo.
Mabadiliko hayo yanakuja licha ya upinzani mkali kutoka kwa kanisa la Ugiriki linalozingatia masuala ya kijamii, ambalo mwaka jana lilitoa taarifa ikisema kwamba ndoa za watu wa jinsia moja hazifuati mfumo wa kitamaduni wa familia na kwamba watoto si mifugo kwa mtu yeyote anayetaka kujisikia kama mlezi, na kuamua kuwalea. Lilitoa kauli hiyo kuashiria wapenzi wa jinsia moja wanaochukua watoto na kuamua kuwalea kwa kujisikia tu eti kwa sababu wapenzi hao hawawezi kuzaa. Kwamba wanapekea watoto wanaolelea na walezi wa aina hiyo nao kuangukia katika hali hiyo ya kimaisha.
Ugiriki ni nchi ambayo inaongozwa kwa sheria za kisekulari, maana yake ni kwamba serikali yake inafanya kazi kando na dini. Ingawa Ugiriki ina historia ndefu ya utamaduni wa Kikristo, serikali yake inazingatia uhuru wa dini na ina misingi ya kidemokrasia.
Ukristo wa Ki-Orthodox una nguvu kubwa nchini Ugiriki. Kanisa la Ki-Orthodox la Ugiriki ni sehemu muhimu ya utamaduni, historia, na jamii ya Ugiriki. Ingawa nchi hiyo inazingatia uhuru wa dini, Kanisa la Ki-Orthodox linabaki kuwa moja ya taasisi muhimu zaidi na inaathiri sana maisha ya watu na siasa za nchi hiyo.