Tukizungumzia ujenzi wa reli wa kampuni za China barani Afrika, hatuwezi kusahau Reli maarufu ya TAZARA. Reli hiyo iliyojengwa miaka ya 1970 ina urefu wa kilomita 1,860.5, na inapita katika mikoa 4 ya Tanzania na mikoa 2 nchini Zambia, na ni njia kuu inayounganisha nchi hizo mbili. Wakati nchi zote za Magharibi zilipokataa kuzisaidia nchi hizo mbili kujenga reli hii, China ambayo wakati huo bado ilikuwa nyuma kimaendeleo, ilitoa mikopo, teknolojia, na wahandisi na mafundi zaidi ya 56,000, ili kujenga reli hiyo. Reli hiyo baadaye ilisifiwa kama ukumbusho wa "undugu" kati ya China na Afrika. Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye ni rais wa kwanza wa Tanzania, alisema, “Katika historia, wageni walijenga reli barani Afrika ili kupora utajiri wa Afrika. Kinyume chake, Wachina wametusaidia kukuza uchumi wa kitaifa."
Miaka 50 imepita haraka. Kutokana na uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika na maendeleo ya pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja", katika miaka ya hivi karibuni, China imeshiriki katika juhudi za kuboresha miundombinu barani Afrika kwa hatua madhubuti, na ujenzi wa reli umepamba moto katika ushirikiano wa pande hizo mbili.
Reli ya SGR inayounganisha mji mkuu wa Kenya Nairobi na mji wa bandari wa nchi hiyo Mombasa, ilijengwa na kampuni ya China, na ni moja ya miradi muhimu ya utekelezaji wa pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja" barani Afrika. Tangu izinduliwe tarehe 31 Mei mwaka 2017, reli hiyo imerahisisha kwa kiasi kikubwa usafiri wa watu na mizigo, ambao awali ulikuwa mgumu na kuchukua muda mrefu njiani. Licha ya hayo, reli hiyo pia imetoa nafasi za ajira karibu elfu 50 kwa Wakenya. Takwimu zinaonesha kuwa, reli hiyo imeongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Kenya kwa asilimia 1.5, na kuwa injini mpya kwa maendeleo ya uchumi.
Mbali na Kenya, reli ya SGR pia imenufaisha nchi nyingine za Afrika Mashariki, zikiwemo Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Uganda. Usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizo zisizo na bandari na nchi za nje kwa njia ya bahari unategemea kwa kiasi kikubwa bandari ya Mombasa ya Kenya. Reli hiyo imezisaidia kuongeza kasi ya usafirishaji na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa. Katibu Mkuu wa Chama tawala nchini Kenya cha Jubilee, Raphael Tuju amelipongeza pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kwa kuungana vizuri na malengo ya maendeleo endelevu barani Afrika.
Mbali na Reli ya SGR ya Kenya, katika miaka ya hivi karibuni, China pia imesaidia nchi nyingine nyingi za Afrika kujenga reli, zikiwemo reli inayounganisha mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa na Djibouti, reli inayounganisha mji wa Abuja na Kaduna nchini Nigeria, na reli Benguela nchini Angola. Reli hizo zilizojengwa kufuatia vigezo, teknolojia na mitaji ya China ni kama “mishipa ya chuma” ya maendeleo ya uchumi na jamii barani Afrika, na pia ni alama ya ushirikiano wa kirafikia kati ya China na Afrika.