SAUTI YA ASKOFU KWA WATETEZI WA HAKI KATIKA JAMII!
Haki haiwezi kufa! Mtu anaweza kuwaua watetezi wa haki, lakini hawezi kufanikiwa kuiua haki! Haki haiwezi kununuliwa! Mtu anaweza kuwanunua wapigania haki, lakini hawezi kuinunua haki yenyewe! Haki haitishwi! Mtu anaweza kuwatisha watetezi wa haki, lakini hawezi kuitisha haki yenyewe! Haki hainyamazishwi! Mtu anaweza kuwanyamazisha watetezi wa haki, lakini haki itaendelea kupiga kelele! Haki hazeeki na hachoki. Watetezi wa haki wanaweza kuchoka na kuzeeka, lakini haki hachoki na wala hazeeki, na badala yake huwainua wengine walio na ujasiri kuliko wa mwanzo!
Mtu anaweza kudhoofisha na kubomoa majengo, taasisi, vyombo, na vifaa vinavyotumika katika kupaza sauti ya Haki, lakini hawezi kufanikiwa kuidhoofisha na kuibomoa haki! Haki ni ushahidi wa uwepo wa Mungu aliye hai katika jamii! Ukisikia kelele, sauti, vilio na miito ya haki usipambane nayo! Ujue kuwa hizo ni kelele za Mungu mwenyewe! Hizo ni sauti kutoka kwa Mungu aliye Haki! Haki ndiye Hekima mwenyewe anayetajwa katika Biblia Takatifu kitabu cha Mithali 8:1-36.
Ewe mtu unayetetea na kupigania haki mahali popote, katika taasisi ye yote na katika mazingira ye yote! Usikatishwe tamaa unapoona sauti ulizozitegemea zikinyamaza; na wala usiogope kuona uovu ukijiimarisha zaidi katika jamii. Haki hahitaji umati wa watu katika kushinda mapambano na wala hahitaji jeshi ili kuwanyamazisha madui zake! Yeye Haki ni Wakati! Wakati wake ukifika, Haki hupita katikati ya matusi, kejeli, dharau, watesi, majeshi na umma wa watu na kisha kuanza kuhesabu mateka na kuitweka bendera ya ushindi! Wakati wa Haki ukifika, hata wale waliomtweza, waliopambana katika kumtusi, waliowaua na kuwanyamazisha watetezi wa Haki; wote kwa pamoja watapaza sauti zao kumshangilia Haki! Haki hana dini ingawa anawatumia watu wa dini na wasio wa dini katika kutangaza uwepo wake!
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki