Wananchi wa Uingereza leo wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wa kuchagua Waziri Mkuu na Wabunge.
Wagombea wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda ni Waziri Mkuu wa sasa Rishi Sunak kutoka Chama cha Conservative na Keir Starmer kutoka Chama cha Labour.
Vyombo vya habari vingi vimetabiri kuwa Chama Cha Labour na mgombea wake Keir Starmer kitashinda uchaguazi huo kwa kura nyingi.
Watu milioni 46 wanastahili kupiga kura kwenye uchaguzi huu.
Vituo vya kupiga kura vitafunguliwa saa moja asubuhi mpaka saa nne usiku.
Uchaguzi mkuu wa mwisho ulifanyika mwaka 2019 ambapo mgombea wa Chama cha Conservative, Boris Johnson alishinda uchaguzi huo.
=========
Utabiri baada ya kura kupigwa nchini Uingereza unaonesha kuwa chama cha Labour kimeibuka na ushindi wa kishindo, huku kiongozi wake, Keir Starmer akielekea kuchukuwa nafasi ya Rishi Sunak kama waziri mkuu mpya.
Matokeo yaliyopitiwa na mashirika mbalimbali ya habari yanaashiria kuwa chama cha Labour kinachofuata siasa za mrengo wa kati kushoto kimepata viti 410 kati ya 650 bungeni, huku wahafidhina wa mrengo wa kulia, Conservative, wakimudu kukusanya viti 131 tu, kiwango cha chini kabisa kwa chama hicho kwa zaidi ya miaka 100 sasa.
"Kwa kila aliyeipigia kampeni Labour kwenye uchaguzi huu, kwa kila aliyetupigia kura na kukiamini chama chetu cha Labour kilichobadilika, ahsanteni." AliandikaStarmerkwenye mitandao ya kijamii.
Naibu wake, Angela Rayner, aliliambia shirika la utangazaji la BBC kwamba wametiwa moyo sana na matokeo, lakini asingeweza kusema zaidi mpaka pale matokeo yote yawe yamekusanywa na kutangazwa rasmi.