Hii ni Kauli ya Spika Kuhusu Uteuzi
na Mwandishi Wetu
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta kwa mara nyingine tena wiki hii, amekata mzizi wa fitina kwa kuukosoa mfumo wa utawala nchini, akibainisha kuwapo kwa kasoro, hususan katika eneo la uteuzi, uwazi na uwajibikaji wa viongozi na watendaji.
Sitta, mwanasheria kitaaluma na mwanasiasa wa miaka mingi, aliyepata kushika nafasi mbalimbali za kitaaluma na kiteuzi, amesema pia kwamba, kasoro hizo ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo nchini.
Akihojiwa na kituo cha utangazaji cha Clouds FM mjini Dodoma jana asubuhi, muda mfupi kabla hajaanza kuendesha kikao cha Bunge, Sitta aliutaja ukosefu wa uwazi na uwajibikaji miongoni mwa viongozi na serikali, kuwa ni sababu nyingine kubwa zinazoikwamisha nchi kusonga mbele kwa kasi.
Akifafanua kuhusu uwazi, Sitta ambaye wiki hii alimaliza mgogoro wa chinichini kati yake na Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) kwa staili ya aina yake, alisema kuwa idara nyingi za serikali, ama kwa mfumo wa kisera, ama kwa ukiritimba wa watu binafsi, hazipo wazi kwa wananchi kwa kiasi cha kutosha.
Alisema ukosefu huo wa uwazi umekuwa ukiwanyima wananchi fursa ya kufahamu mambo muhimu, ambayo yanaendelea ndani ya serikali na hivyo kuwafanya washindwe kuchangia mawazo yao ipasavyo.
Kuhusu uteuzi, alisema wakati umefika sasa kukaanza kuwekwa vigezo vya watu wanaostahili kushika nafasi fulani badala ya jambo hilo kufanywa kama ilivyo hivi sasa.
“Pia inafaa tuanzishe utaratibu wa kupima performance (utendaji) ya mtu, si tu kukutana katika cocktail (tafrija za jioni). Watu wanatakiwa kupimwa kwa uwajibikaji wao,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, rais ndiye aliye na mamlaka ya kuwateua takriban viongozi wa ngazi mbalimbali kitaifa, kiwizara, kimikoa, kiwilaya na wale wanaoongoza asasi mbalimbali nyeti za umma.
Pamoja na Sitta kuhoji mwelekeo huo, mawazo kama hayo yamewahi kuhojiwa na wasomi mbalimbali, ambao wamekuwa wakiona rais akipewa nafasi nyingi ambazo baadhi hazistahili kufanywa naye.
Sitta kwa upande wake, alisema Tanzania yenye neema, kama ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete, inawezekana iwapo nchi itajipanga vizuri katika kutekeleza mipango ambayo nayo inapaswa kupangwa vizuri.
Ndiyo maana alisema katika kipindi cha miaka mitano atakayoliongoza Bunge, amedhamiria kufanya mabadiliko makubwa katika mhimili huo wa utawala ili kuhakikisha kuwa, unatoa mchango wake unaotakiwa katika kuleta maendeleo.
Alisema tayari mabadiliko yameshaanza kuonekana katika chombo hicho cha kutunga sheria, kwani kuna baadhi ya mambo ambayo yameanza kufanyika, ambayo yalikuwa hayafanyiki hapo kabla.
“Sasa hivi ripoti zote za kamati zinajadiliwa ndani ya Bunge. Tuna kamati 13 na jambo kama hili halijawahi kufanyika tangu tupate uhuru,” alisema Sitta na kutaja mabadiliko mengine kuwa ni kujadiliwa kwa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) jambo ambalo halijawahi kufanyika tangu enzi Edward Sokoine alipokuwa Waziri Mkuu.
“Zipo hizi ripoti za mkaguzi, zinawasilishwa na zinajadiliwa, wabunge wanaona na kuhoji jinsi mamilioni ya fedha yalivyotumika… haya ni mabadiliko makubwa,” alisema.
Katika mabadiliko mengine makubwa, kuanzia mwaka huu, Bunge litakuwa likifanya vikao vya kuishauri serikali katika upangaji wa bajeti.
Sitta alisema kuwa, vikao vya mwaka huu vitafanyika Aprili 23 na 24 kwa lengo la kuwakilisha maoni ya wananchi kuhusu upangaji wa bajeti.
“Bunge linawakilisha wananchi, maoni tutakayoyatoa ndiyo maoni ya wananchi, huu ni utaratibu ambao unafanyika sehemu nyingi duniani, na serikali inatakiwa isikilize maoni haya, si busara kukaa na kujipangia tu bajeti,” alisema.
Alibainisha kuwa, mabadiliko hayo yote yamo ndani ya nia yake ya kulifanya Bunge la Tanzania kuwa moja kati ya mabunge bora kabisa barani Afrika atakapokamilisha kipindi chake cha miaka mitano kama Spika.
“Huwa najiwekea malengo kila ninapoenda, hapa nilishasema mara nyingi kuwa nia yangu ni kulifanya Bunge la Tanzania kuwa Bunge bora kabisa barani Afrika,” alisema.
Sitta alisema kuwa ndoto ya kuifanya Tanzania kuendelea kwa kasi inawezekana iwapo tu wananchi na viongozi wataamua kujipanga vizuri.
Akitoa mfano, alisema kuwa zipo nchi ambazo miaka michache iliyopita uchumi wake ulikuwa unalingana na Tanzania, lakini leo zipo mbali kutokana na kujipanga vema na kutekeleza yale waliyojipangia.
“Unaposikia China imeendelea wakati wanafuata Ujamaa haikuwa mchezo… kwa wale Wachina, mtu wanayembaini kuwa ni mhujumu uchumi, anapigwa risasi na si masihara hata kidogo,” alisema.
Kabla hajajitosa katika siasa za waziwazi kwa mara ya pili kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, Sitta alikuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na chini ya uongozi wake, TIC ilipata kuwa moja ya vituo bora vya uwekezaji duniani.
Kabla ya kushika wadhifa huo TIC, Sitta alikuwa amewahi kuwa mbunge wa Urambo, nafasi iliyomwezesha kuteuliwa kushika uwaziri wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Ali Hassan Mwinyi.
DeleteReplyForwardSpamMove...