Laki tano ni pesa ndogo sana linapotokea suala la msiba. Pamoja na hayo, sidhani kuwa serikali imeshindwa kuwajengea mnara na kaukuta mpaka iamue kupora michango ya rambirambi.
Kwa kuwa dalili za awali zinaonyesha kuwa kuna uzembe wa watendaji wa serikali, inabidi hao watu waandae mashtaka rasmi ya madai dhidi ya hasara na maafa waliyopata walipwe "PROPER INSURANCE BENEFITS" kama binadamu wengine wanavyolipwa bima wanapopata madhara mbalimbali. Hii ndiyo haki wanayostahili.
Tunashuhudia watu wanaogongwa na vyombo vingine kama magari wanalipwa mamilioni na bima zinazosimamia vyombo husika. Inakuwaje kwenye hiki kivuko? ARE WE SERIOUS?
Haya mambo ya laki tano ambayo hata kusafirisha maiti tu ni shida, achilia mbali gharama nyinginezo kwa kweli hayapaswi kukubalika na watu wenye akili timamu. Ikumbukwe kuwa kuna madhara na naumivu mengi yameachwa nyuma ya huu msiba ambayo kama jamii lazima tuelimishane na tuelewe. Mfano kuna mateso yanaachwa kwa wategemezi wa wale waliofia kwenye kivuko. Wapo watoto wameachwa yatima (Mfano waliopoteza wazazi wote), wapo watoto wachanga waliokuwa wanasubiri mama zao warudi kutoka sokoni wawanyonyeshe, wapo waliokuwa wanasubiri mama au baba warudi ndio waweze kupata mlo wa siku hiyo. Kwa kweli wapo wahanga wengi sana ambao serikali hii imeamua kuwafumbia macho na kujifanya haioni.
Kwa kweli kama haya mambo yataachwa hivi hivi kama yanavyosemwa na hawa waliojipa majina ya malaika na watua mizigo ya wenye dhambi, na watetezi wa wanyonge, basi watanzania tutakubaliane kuwa sisi ni kizazi cha vichaa na washenzi. Tufumbe macho na tubariki maovu haya yanayotendwa na wanaojiita watetezi wa wanyonge. Tuendelee kuwaabudu, maisha yasonge.
USHAURI WANGU
Wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wajitokeze wawafanyie uhakiki kila familia iliyoathirika kwa namna moja ama nyingine wakadai fidia (INSURANCE) stahiki mahakamani.