SI KWELI Ukichangia Damu mara moja utalazimika kuchangia kila mara ili isiongezeke zaidi

SI KWELI Ukichangia Damu mara moja utalazimika kuchangia kila mara ili isiongezeke zaidi

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
1697007034621.png

Kuna imani au tuseme maneno mtaani kwamba ukitoa Damu (kuchangia Damu) mara moja basi itabidi uwe unatoa kila mara ili kudhibiti ongezeko kubwa linalotokea baada ya hapo.

Wengine wanasema usipofanya hivyo utakuwa ukipata maumivu makali ya Kichwa kila wakati.

Ukweli ni upi hapa?
 
Tunachokijua
Damu ni kimiminika muhimu kwa maisha ya binadamu. Pamoja na kazi zingine, hufanya kazi ya kusafirisha hewa ya oksijeni na virutubisho mwilini, huratibu mfumo wa kinga mwili katika kupambana na maambukizi mbalimbali ya magonjwa pamoja na kudhibiti joto kwenye kiwango cha kawaida kinachofaa kwa afya bora.

Pamoja na uwepo wa mapinduzi makubwa katika uwanda wa sayansi, teknolojia na tiba, hadi sasa hakuna mbadala wa damu inayoweza kutengenezwa kwenye maabara. Mwili wa binadamu pekee ndio unaweza kuzalisha damu inayoweza kutumika kwa binadamu mwingine.

Wagonjwa wengi hutegemea damu ili kuokoa maisha yao hasa pale wanapokuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa za kiafya kama vile upasuaji, maambukizi makali ya magonjwa (mfano Malaria), ajali na matibabu ya saratani.

Mwili wenye afya unaweza kuzalisha upya, au kutengeneza damu nyingi zaidi katika muda wa wiki 4 hadi 6 hivyo kuchangia damu ni suala jema lisilo na athari kwa afya ya mchangiaji.

Masharti ya kuchangia damu
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), yapo masharti mengi yanayopaswa kuzingatiwa kwa watu wanaotaka kuchangia damu.

Pamoja na kwamba masharti haya hutofautiana kati ya nchi na nchi, WHO inashauri kuzingatia yafuatayo;
  1. Awe na umri wa kati ya miaka 18-65.
  2. Awe na uzito unaofikia kilo 50 na kuendelea.
  3. Awe na afya bora, asiwe na mafua au maambukizi ya mfumo wa chakula.
  4. Kwa mwanaume, awe na damu inayofikia 13.0 g/dl na mwanamke 12.0 g/dl
  5. Asiwe na maambukizi ya VVU, Homa ya Ini, asiwe ametumia madawa ya kulevya pamoja na kushiriki matendo ya ngono zembe kwenye kipindi cha miezi 12.
  6. Asiwe mjamzito au ananyonyesha.
Muda wa kuchangia damu
Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, baada ya kuchangia damu, wanaume hupaswa kusubiri kwa kipindi cha walau miezi 3 kabla ya kuchangia tena huku wanawake wakishauriwa kusubiri walau miezi 4 hivyo kwa mwaka mmoja mwanamme anaweza kuchangia damu mara 4 na mwanamke anaweza kuchangia mara 3.

Ukichangia Damu mara moja utalazimika kuchangia kila mara ili isiongezeke zaidi?
Bila shaka umewahi kusikia uvumi huu, na baadhi ya watu huogopa kuchangia ili kuikwepa adha hii.

JamiiForums haikutaka kuacha uvumi huu uendelee kusambaa pasipo kupata maelezo ya kitaalamu, hivyo ilizungumza na Kizito Tamba, Health Promotion Officer wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama aliyesema kuwa uvumi huo hauna ukweli.

"Sio kweli, kuna mtu amechangia mara moja, hajarudi tena na hajapata madhara yoyote. Kuna wengine wanaoendelea kuchangia mara kwa mara pia nao hawapati madhara yoyote. Kwa sababu mwili una kiasi chake cha damu na maji, sasa kwenye hiyo damu kuna homoni inadhibiti (ina regulate), yenyewe inafanya kazi ya kuhakikisha damu yako inabaki kwenye kiwango kilicho sahihi yaani 12g/dl hadi 18g/dl (Kwa mwanamke 12-16 na wanaume 12.5-18)"

"Kwa hiyo wewe hata ukitoa saivi damu mwili utakwambia kuna kitu kimetoka, halafu utaanza kurudidha kile kiasi kilichopotea. Na chembechembe za damu huishi kwa wastani wa siku 120, uwe umetoa zitakufa uwe hujatoa zitakufa hivyo tunategemea utengenezaji unaendelea kila siku kwa sababu kuna zinazokufa na zinazoendelea kuzalishwa kila siku lakini ile homoni inaendelea kubalansi kilichopo na kile tunachotumia kila siku kwa matumizi ya kawaida."


Homoni inayoitwa Erythropoietin ambayo huzalishwa na figo ndio huusaidia mwili kutengeneza damu na uchache au wingi wake huathiri uzalishaji wa damu kwa namna hiyo hiyo.

Watu wenye matatizo ya figo wasio na uwezo wa kuzalisha homoni hii huchomwa sindano mbadala yenye homoni hizi iliyotengenezwa viwandani ili kuusaidia mwili katika kuzalisha damu.

Kupitia maelezo ya wataalamu kama ilivyofafanuliwa na Kizito Tamba pamoja na tafiti za kisayansi, JamiiForums imebaini kuwa uvumi unaodai kuwa uchagiaji wa damu husababisha mwili uzalishe damu nhyingi zaidi hauna ukweli wala uthibitisho wa kisayansi.
Kuna imani au tuseme maneno mtaani kwamba ukitoa Damu (kuchangia Damu) mara moja basi itabidi uwe unatoa kila mara ili kudhibiti ongezeko kubwa linalotokea baada ya hapo.

Wengine wanasema usipofanya hivyo utakuwa ukipata maumivu makali ya Kichwa kila wakati.

Ukweli ni upi hapa?
Uongo nimetoa damu mara moja tu hospital ya lugaro dar mwaka juzi sijatoa tena
 
Back
Top Bottom