Imekuwa ikinitoea mara kwa mara kila nikila nanasi na kisha kunywa maji nahisi uchungu mdomoni, Je hii ni kwangu tu au watu wote mnapata hali kama hii?
Kama ni wote, Kwanini baada ya kumaliza kula nanasi na ukanywa maji unasikia ladha ya uchungu mdomoni? Je kuna uhusiano gani kati ya nanasi na maji?
Kama ni wote, Kwanini baada ya kumaliza kula nanasi na ukanywa maji unasikia ladha ya uchungu mdomoni? Je kuna uhusiano gani kati ya nanasi na maji?
- Tunachokijua
- Nanasi ni moja kati ya matunda yenye vitamini, madini na virutubisho vingi vinavyoupa mwili nguvu na kuepuka kushambuliwa na maradhi, yana radhi ya utamu.
Kumekuwa na madai kuwa mtu akila nanasi kisha kunywa maji huhisi ladha ladha ya uchungu mdomoni au ladha isiyo nzuri.
Je, ni upi uhalisia wa madai haya na nini husababisha?
Jamiicheck imepitia Tafiti na Machapisho mbalimbali na kubaini kuwa ni Kweli mtu akila nanasi na kisha kula kitu au kunywa kimiminika hasa maji baadhi huhisi ladha ya tofauti au kama metali na baadhi huhisi ladha ya uchungu.
Nanasi lina kimeng'enya(Enzymes)kiitwacho bromelain ambacho kinaweza kubadilisha ladha ya vyakula na vinywaji unapokula muda mfupi baada ya kula nanasi. Unapokunywa maji baada ya kula nanasi, bromelain inaweza kuingiliana na protini kinywani mwako na kubadilisha mtazamo wako wa ladha ya maji kwa muda mfupi na kuipa ladha isiyo ya kawaida au ya metali.
Bromelain Ni moja ya vimeng'enya vinavyopatikana kwenye mananasi, hasa kwenye shina na tunda lenyewe la nanasi. Kimeng'enya hiki kina uwezo wa kuvunja protini na kulainisha nyama. Unapokula nanasi kimeng'enya hicho huathiri gamba la ulimi na kingo za kinywa, ulimi ni msuli na kuna Protini ambayo huvunjwa na kimeng'enya hicho na kuathiri ladha ya maji unayokunywa baada ya kula au kuonja mananasi kwa sababu ya athari ya bromelain kwenye ulimi.
Bromelain huvunja protini zinazopatikana kwenye ulimi na katika utando wa mdomo hali hiyo husababisha hisia tofauti za ladha baada ya bromelain kuathiri sehemu hizo. Kwa kuwa bromelain inakuwa imeshaondoa protini ambazo hulinda au kufunika ulimi, inaweza kufanya ladha kuwa kali au ya ajabu unapokunywa maji au kula vyakula vingine mara baada ya kula mananasi.
Aidha, inakuwa ni rahisi zaidi kuhisi mabadiliko ya ladha pale unapokunywa maji tofauti na kula au kunywa vitu vingine kwa kuwa maji hayana ladha yake ya asili na yakiingia kinywani husambaa sehemu kubwa na kuondoa mate kwenye ulimi mate ambayo husaidia kukinga kimeng'enya cha Bromelain kuathiri zaidi protini iliyo kwenye ulimi na kingo za kinywa.
Pia, Mananasi yana asidi, kama vile asidi ya citric, ambayo huweza kushirikiana na bromelain kuathiri hisia za ladha. Asidi inaweza kuongeza uwezekano wa Msuli au gamba la ulimi kuathiriwa kwa kuchubuliwa kutokana na uchachu kwa yale yenye uchachu, na hivyo kufanya maji yaonekane kuwa na ladha tofauti, metali au ya uchungu.
Mabadiliko ya ladha huwa ya muda mfupi kwenye kinywa kwa kuwa miundo ya protini za ulimi na seli hujirekebisha kwa muda mfupi, Na pia si watu wote hupata mabadiliko ya ladha, hii hutegemea na mwitikio wa namna mtu anapata mabadiliko kwa haraka.