SoC02 Ukombozi wa vijana kutoka kwenye wimbi la matumizi ya Vileo na Dawa za Kulevya Tanzania

SoC02 Ukombozi wa vijana kutoka kwenye wimbi la matumizi ya Vileo na Dawa za Kulevya Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

DMF

New Member
Joined
Jul 26, 2022
Posts
1
Reaction score
0
UKOMBOZI WA WATOTO NA VIJANA KUTOKA KWENYE WIMBI LA MATUMIZI YA VILEO NA MADAWA YA KULEVYA NCHINI TANZANIA.

Nchi yetu ya Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo vijana wake wengi kila kukicha wanajiingiza kwenye wimbi kubwa la matumizi ya vilevi kama vile pombe, ugoro, bangi na madawa mengine ya kulevya. Jambo la kusikitisha ni kuona watu wazima ndiyo wapo mstari wa mbele kuwafundisha watoto wadogo matumizi ya hivi vilezi na madawa ya kulevya kiasi kwamba matumizi yamekuwa makubwa kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu hadi mitaani. Kulingana na utafiti mdogo nilioufanya kwenye baadhi ya maeneo nchini Tanzania inaonekana matumizi makubwa ya vileo na madawa ya kulevya yapo mijini kwa kiasi kikubwa kutokana na upatikanaji wake kuwa rahisi huku kwenye maeneo ya vijijini bado hayajawa makubwa sana japo yanazidi kuongezeka kila kukicha.


SABABU ZA KUONGEZEKA KWA MATUMIZI YA VILEVI NA MATUMIZI YA MADAWA YA KULEVYA KWA WATOTO NA VIJANA NCHINI TANZANIA.
Sababu za watoto na vijana mashuleni, vyuoni pamoja na mitaani kuangukia kwenye wimbi kubwa la matumizi ya vileo na madawa ya kulevya zipo nyingi lakini sababu kubwa ni hizi zifuatazo;

Kukosekana kwa malezi ya kutosha kwa watoto
Ni wazi kabisa vijana wengi ambao wameangukia kwenye matumizi ya vileo na madawa ya kulevya ni kwasababu ya malezi kutoka kwa wazazi na walezi wao kuwa madogo japo siyo wote wamekosa malezi bali wengine wamejiingiza kwenye matumizi haya kutokana na sababu nyingine. Inaonekana vijana wengi ambao wapo mijini na wanatumia vileo na madawa ya kulevya wengi wao ni wale waliopoteza wazazi na wengine waliokosa muelekeo sahihi kutoka kwa wazazi au walezi wao na kuamua kukimbilia mijini.

Ugumu wa maisha kuanzia ngazi ya familia hadi mtu binafsi
Baadhi ya vijana na watoto wanakimbia familia zao na wengine kuruhusiwa na walezi wao kwenda sehemu mbalimbali kama mjini kutafuta riziki kutokana na hali ngumu na umasikini unaokumba familia zao. Wanapofika kwenye maeneo ya utafutaji wanakutana na changamoto nyingi kama makundi ya vijana ambayo mengine yanawashawishi kuingia kwenye matumizi ya vileo na madawa ya kulevya.

Msukumo kutoka kwa marafiki na makundi mbalimbali
Kulingana na utafiti wangu nilioufanya inaonekana vijana na watoto wengi wanaotumia vileo na madawa ya kulevya wana makundi au marafiki wa kutumia nao kwa pamoja. Hii yote ni kwasababu wengine wanashawishiwa na marafiki zao au makundi mbalimbali ya vijana. Hii changamoto ndiyo inayowaingiza wanafunzi wengi mashuleni na vyuoni kwenye matumizi ya vileo na madawa ya kulevya.

Msongo wa mawazo
Kutokana na ugumu wa maisha, changamoto mbalimbali za kijamii na mapenzi vijana wengi wanapata msongo wa mawazo huku wakifikiria njia pekee ya kupunguza mawazo ni kutumia vileo na madawa ya kulevya. Siku hizi unasikia kijana anasema “Nipe K-vant nikapunguze mawazo”

Uigaji kutoka kwa watu maarufu
Vijana na watoto wengi wanapenda kuiga watu maarufu kama wasanii ambao ni watumiaji wa vilevi na madawa ya kulevya mfano hapa Tanzania kuna msanii fulani siku za hivi karibuni ameonekana anapenda kuvuta sigara kwenye video zake huku akikohoakohoa basi baadhi ya vijana wengi huku mitaani wanasikika wakisema “Nipatie kitu cha Fulani (msanii huyo) nami nikakohoe kidogo” hii inaonesha kwamba wengine wanatumia kwa kuiga wengine.


ATHARI ZA UTUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA KWA WATOTO NA VIJANA
  • Watoto kushuka viwango vya ufaulu darasani na kuacha masomo
  • Kuongezeka kwa vitendo vya uharifu mitaani mfano wizi
  • Kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili mfano umalaya, ubakiji na kukosea heshima watu wazima.
  • kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali ya mwili kama saratani, kansa na UKIMWI.
  • Kuongezeka kwa vifo kwa vijana wadogo kutokana na utumiaji holela wa madawa.
  • Kuongezeka kwa vijana wenye matatizo ya akili mitaani kutokana na matumizi makubwa ya madawa ya kulevya.
  • Kuongezeka kwa vijana tegemezi mitaani hadi majumbani.

NJIA ZA KUPUNGUZA NA KUWANUSURU WATOTO NA VIJANA KUTOKA KWENYE WIMBI KUBWA LA MATUMIZI YA VILEO NA MADAWA YA KULEVYA
- Wazazi na walezi wahakikishe wanatoa malezi bora kwa watoto wao pia wahakikishe wanawajibika kutimiza mahitaji ya watoto wao hata ikitokea hali ni ngumu kiasi gani mzazi hapaswi kumruhusu mtoto wake kwenda kujitafutia maisha mwenyewe kabla ya kutimiza miaka 18.

- Upatikanaji wa huduma ya elimu uendelee kuimarishwa ili kupunguza wimbi kubwa la watoto wengi mitaani ambao mwisho wa siku uangukia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

- Elimu itolewe juu ya matumizi ya vilevi na madawa ya kulevya kuhusu madhara yake kwani vijana wengine waangamia kwa kukosa maarifa kwa kutokujua madhara hasi ya hivi vitu.

- Kupiga vita matumizi ya madawa ya kulevya liwe jukumu la kila mtu siyo kuwaachia walezi au wazazi na taasisi husika. Kila mtu inabidi awe mstari wa mbele kukemea ili jambo.

- Serikali izidishe juhudi katika kuzuia uingizaji wa madawa ya kulevya nchini.

- Taasisi binafsi na mashirika mbalimbali kama ya kidini yahamasishwe kuendelea kutoa elimu juu ya madhara ya madawa ya kulevya.

- Serikali ianzishe na kuendeleza utaratibu wa kuwaondoa watoto mitaani.

- Watu wazima wajiheshimu wasitumie vileo na madawa kulevya hadharani mbele ya watoto wadogo.

- Watoto waruhusiwe kutumia mitandao ya kijamii wakiwa tiyari wameshakua na kujitambua angalau kuanzia miaka 18 ili kuepusha uigaji kutoka kwa watu maarufu.

- Hayo ndiyo baadhi ya mambo yanayoweza kufanyika ili kuwanusuru watoto na vijana kutoka kwenye janga la matumizi ya vileo na madawa mengine ya kulevya.

WITO WANGU KWA WAZAZI NA JAMII NZIMA KWA UJUMLA
Malezi ya watoto siyo lazima yatoke kwa wazazi tu bali hata watu wengine wana wajibu wa kuwalea, kuwakanya na kuwarekebisha watoto na vijana katika jamii zetu hivyo basi ni wajibu wa kila mtu hata ikitokea mtu yeyote amemuadabisha mtoto wako kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya mzazi hupaswi kuchukia wala kubeza kwani unakuwa unasaidiwa kulea mtoto wako.

WITO WANGU KWA SERIKALI
Taifa haliwezi kujengwa na vijana walevi kwani athari kubwa ya madawa ya kulevya ni kupoteza nguvu kazi ya taifa hivyo basi serikali iongeze juhudi kuthibiti matumizi ya madawa ya kulevya ili kuandaa taifa la kesho lenye kuwajibika na kuchapa kazi.

“Tanzania bila matumizi ya vileo na madawa ya kulevya kwa watoto na vijana inawezekana tusimame imara kupambana kwa pamoja kutokomeza janga hili watoto na vijana ndio taifa la kesho”

Imeandaliwa na kuandikwa na DMF
Mawasiliano; 0742957229
 
Upvote 2
Back
Top Bottom