Wanaukumbi niliahidi kukiweka hapa ukumbini kisa cha AMNUT. Hayo yaliyopo hapo chini ni baada ya TANU kurejea kutoka Mkutano wa Tabora wa mwaka 1958 ambao uliamua TANU iingie katika Uchaguzi wa Kura Tatu. Huu ulikuwa uchaguzi wa kwanza katika Tanganyika. Someni kwa furaha:
Baada ya kurejea kutoka Tabora, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, Elias Kassenge na Bhoke Munanka walifuatana na Nyerere kwenye ziara ya Jimbo la Mashariki kuwaeleza watu umuhimu na maana halisi ya uchaguzi uliokuwa mbele yao. Nyerere aliwafafanulia watu kile ambacho Waafrika wangepoteza endapo TANU ingesusia uchaguzi. Lakini Sheikh Takadir alikuwa akishiriki katika mikutano ile kimwili tu; moyo na fikra zake havikuwa pale. Alikuwa na wasiwasi jinsi matukio yalivyokuwa yakitokea katika TANU na namna siasa ilivyokuwa ikichukua mwelekeo mpya. Sheikh Takadir alikuwa anautazama kwa hofu uongozi wa Wakristo katika TANU ambao ulikuwa ukielekea kuchukua uongozi baada kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. Kwa sababu ya yale masharti magumu ya uchaguzi, TANU ilibidi itazame nje ya uongozi wake ili kupata wagombea uchaguzi wenye sifa zilizohitajika kugombea uchaguzi dhidi ya UTP. TANU iliwachagua Julius Nyerere, Chief Abdallah Said Fundikira, John Ketto, Nesmo Eliufoo, John Mwakangale, Lawi Sijaona, Paul Bomani na George Kahama kusimama kama wagombea wa TANU. Baadhi ya hawa walikuwa watu ambao hawakuinukia katika TANU au harakati za siasa. Sheikh Takadir alihofu kuwa hawa Wakristo walioelimishwa na wamisionari na ukuzingatia kuwa walikuwa watu wapya katika harakati, mara watakaposhika madaraka watafanya juhudi kudumisha hali ile ile ya ukoloni, wakiwa hawana dhima ya kuongoza harakati kufikia lengo lake lake lililokusudiwa. Sheikh Takadir alikuwa kiongozi wa kwanza katika TANU kuwatanabaisha Waislam kuhusu hatari hii mpya iliyokuwa ikiwabili.
Sheikh Haidar Mwinyimvua, mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU na mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU katika mwaka 1958na aliyekuwa rafiki mkubwa wa Sheikh Suleiman Takadir, anakumbuka jinsi Sheikh Takadir ghafla alipotoa dukuduku lake kwa Nyerere, dukuduku ambalo lilionekana lilikuwa halina sababu:
"Ilikuwa katika ofisi ya zamani ya TANU tukisubiri kufanya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Ghafla tu Sheikh Takadir alisimama wima akishikilia fimbo yake ya kutembea akimuelekezea Nyerere huku akisema, "Huyu mtu katu hatakuja kutujali sisi atakuja kuwajali ndugu zake. Usipoziba ufa utajenga ukuta." Sheikh Takadir alirudia maneno haya mara mbili. Sisi sote katika kile chumba cha mkutano tulipigwa na butwaa kutokana na maneno yale. Nilimwona Nyerere akilia. Nyerere alitugeukia sisi na kutuuliza, "Je, Sheikh Suleiman amesema maneno yale kwa niaba yenu?" Tulijibu kwa pamoja kuwa hatukuwa na habari kuhusu shauri lile; na mkutano ukavunjika hapo hapo."
Sheikh Takadir alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kumuunga mkono Nyerere na alikuwa ameifanyia kampeni TANU kwa bidii kubwa, akihutubia mikutano jukwaa moja na Nyerere. Halikadhalika alikuwa amesaidia kufutilia mbali Ukristo wa Nyerere kwa watu wa Dar es Salaam kiasi kwamba watu mjini Dar es Salaam hawakumnasibisha Nyerere na Kanisa Katoliki ila na TANU kama chama cha wananchi. Wadhifa wa Sheikh Takadir mwenyewe kama mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU ulikuwa wa heshima kubwa. Haikuwa kwamba wale wote waliokuwemo ndani ya chumba kile hawakuelewa kile alichodokeza Sheikh Takadir. Walielewa kila neno alilotamka na maana yake halisi hasa kwa uongozi wa TANU. Kile ambacho hawakufahamu, kutambua au kusadiki kilikuwa ule ukweli kuwa Nyerere, mtoto wao mpendwa na kiongozi wao, iko siku moja atawageuka Waislam na kuwatazama kama adui zake na mahasimu kwa imani yake ya Kikristo. Lakini kwa wakati ule hili lilikuwa wazo lililokuwa mbali sana na lisilokuwa na maana yeyote kwao. TANU na chama kilichotangulia, African Association, hazikuundwa kwa ajili ya masilahi ya kikundi fulani pamoja na ukweli kuwa Waislam ndiyo waliounda vyama hivyo viwili na kuviongoza. Sheikh Takadir alikuwa ametonesha jambo nyeti sana. Njia pekee ya kuzuia mgogoro huu mpya usikue ilikuwa kwa Nyerere kuthibitisha kuwa Waislam watatendewa haki baada ya uhuru kupatikana. Kwa wakati ule, umoja wa wananachi ulikuwa muhimu kwa ajili ya harakati. Umoja wa Watanganyika ukawa ndiyo hoja kuu ya Nyerere katika hotuba zake zote kuanzia mkasa wa Takadir utokee na alishikilia hoja ya umoja katika kila hotuba yake hadi kufikia uchaguzi wa kura tatu.
Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU iliamua kuunda kamati ya haraka haraka kwenda nyumbani kwa Sheikh Takadir Mtaa wa Msimbazi kumuuliza kwa nini alimshutumu Nyerere. Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo walikuwa Idd Faiz, Mwenyekiti wa Halmashauri ya TANU, Idd Tulio na Jumbe Tambaza. Sheikh Takadir aliiambia kamati hiyo kuwa Nyerere alikuwa akitumia sharti la elimu katika uchaguzi wa kura tatu ili kuwaweka Wakristo wenzake madarakani kwa hoja kwamba wanazo zile sifa zitakiwazo kushika majukumu ya serikali. Kisha Sheikh Takadir akarudia tena maneno yale yale aliyomwelezea Nyerere, neno kwa neno, akiongeza kwamba hana majuto yoyote kwa msimamo wake huo. Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Idd Tulio walisimama na kuondoka kimya kimya. Matokeo yake ikawa Sheikh Takadir kufukuzwa kutoka TANU kwa kuanzisha suala la udini, ambalo lilidhaniwa lingewagawa wananchi. Idd Tulio akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU kushika nafasi ya Sheikh Takadir.
Kuingizwa kwa watu kama Eliofoo, Mwakangale, Sijaona, Bomani, Kahama na wengine katika Baraza la Kutunga Sheria ili kuwakilisha TANU kuliwatia wasiwasi idadi kubwa ya wanachama Waislam waliokuwepo makao makuu ya TANU. Lakini kwa hakika viongozi hawa walikuwa wazalendo wakiwakilisha sehemu muhimu nchini Tanganyika ambazo kwa mfano wale kutoka vyama vya ushirika kama Bomani kutoka Jimbo la Ziwa, walijitoa mhanga sana katika harakati. Hakuna namna ambayo Nyerere angeweza kuwakwepa kwa hofu ya kuujaza uongozi katika TANU na Baraza la Kutunga Sheria na Wakristo. Kwa upande mwingnine halikadhalika haikufikiriwa kuwa ni lazima kuwa na uwakilishi ulio sawasawa baina ya Waislam na Wakristo katika TANU au katika Baraza la Kutunga Sheria. Wakati ule tatizo la udini lilikuwa halijulikani kabisa.
Ghafla Sheikh Takadir akageuka kuwa kama mkoma. Watu wa Dar es Salaam wakampiga pande. Sheikh Takadir alikuwa dalali na alikuwa akifanya shughuli zake nyumbani kwake. Siku za nyuma mnadani kwake kulikuwa ndiyo baraza la mazungumzo la wana-TANU. Katika siku za mwanzo za TANU Sheikh Takadir alikuwa akiendesha biashara hiyo nyumba iliyokuwa Mtaa wa Nyamwezi mali ya Mwinjuma Digosi, jumbe wa serikali ya kikoloni. Mwinjuma Digosi alipotambua kuwa Nyerere alikuwa akifika pale kumfuata Sheikh Takadir, Digosi akamueleza Sheikh Takadir kuwa itabidi ahame kwa kuwa yeye ni jumbe wa serikali hawezi kuwa na mpangaji ambae anaigeuza nyumba yake mahali pa kukutana na watu wakorofi kama Nyerere.
Wanachama wa TANU walikuwa wakikutana kwa Sheikh Takadir kunywa kahawa, kupoteza wakati na kujadili siasa. Baada ya yeye kufukuzwa kutoka TANU mahali hapo palihamwa na hakuna aliyekwenda pale kama ilivyokuwa mazoea hapo siku za nyuma. Sheikh Takadir alipokwenda sokoni Kariakoo kununua mahitaji yake hakuna mfanyabiashara aliyegusa fedha zake au hata kule kumtizama tu. Alipotoa salam hakuna aliyemwitikia. Sheikh Takadir alisuswa na jamii yake na TANU. Sheikh Takadir aliuhisi hasa uzito kamili wa kupigwa pande na jamii. Biashara yake ikaanza kuanguka na vivyo hivyo afya yake ikaanza kuathirika. Akawa mpweke sana na mtu mwenye fadhaha. Enzi zile alipokuwa akisoma surat fatíha na kusoma dua kabla ya kumtambulisha Nyerere kwa watu wa Dar es Salaam katika mikutano ya awali ya TANU katika viwanja vya Mnazi Mmoja zilikuwa zimepita. Yalikuwa ya kale wakati Sheikh Takadir akijenga vyema taswira ya Nyerere akimkweza hadi kufikia kiwango cha kumnasibisha na mtume. Haukupita muda mrefu Sheikh Takadir alifariki. Lakini kabla ya kufariki Sheikh Takadir aliwaachia usia.
Kikundi cha Waislam walikuwa wamekwenda nyumbani kwake kumdhihaki, wakimtukana na kumkebehi, wakipiga makele huku wakiimba kwa sauti kubwa mwimbo, ëTakadir mtaka dini!í Kikundi hiki kilivamia nyumba yake baada ya kutoka mkutanoni ambako Nyerere alitoa hotuba ya kumshambulia Sheikh Takadir. Sheikh Takadir, inasemekana, alitoka nje ya nyumba yake kuwakabili wale Waislam na akawaambia, "Iko siku mtanikumbuka."
"Mwafrika" gazeti la kila wiki chini ya uhariri wa Heri Rashid Baghdelleh na Robert Makange, lilichapisha habari za Sheikh Suleiman Takadir katika ukurasa wa kwanza, likitangaza kufukuzwa kwake kutoka TANU kwa wino mzito, picha yake akiwa amevaa kanzu na kofia ya mkono akikodoa macho ikachapishwa gazetini. Picha ya Sheikh Takadir iliwekwa pale ili wote wauone uso wa "msaliti" anaetaka kuchelewesha uhuru kwa kutaka Waislam wapewe uthibitisho wa hali yao ya baadae kwa sababu ya mchango wao katika harakati za kudai uhuru. Mtu mmoja tu ndiyo aliyejitokeza kumuunga mkono Sheikh Takadir na huyo alikuwa Ramadhan Mashado Plantan. Akiandika katika gazeti lake la Zuhra alihoji ile harara ya Nyerere kuwatumbukiza wananchi ndani ya uchaguzi wa kura tatu ingawa ilikuwa wazi kuwa yale masharti ya kupiga kura yalikuwa ya kuchukiza na ile haraka ambayo kwayo Sheikh Takadir alifukuzwa kutoka TANU.
Wakati wa mkasa wa Sheikh Takadir, "Mwafrika" lilikuwa likifaidi mauzo makubwa kwa sababu TANU ilisusia gazeti la Baraza gazeti la kila wiki la serikali. Baghdelleh na Makange walikuwa wamechapisha makala moja ambayo serikali iliiona ni ya uchochezi. Baghdelleh na Makange walipatikana na hatia na kufungwa miezi sita gerezani. TANU ililipa kisasi kwa kuwataka wananchi wasusie gazeti la Baraza. Hakuna Mwafrika aliyenunua gazeti hilo na kwa ajili hii yake mauzo ya "Mwafrika" yalipanda sana, hivyo kuipa sakata ya Sheikh Takadir nafasi kubwa gazetini. Baraza ilikuwa katika ukingo wa kufa kabisa kama isingelikuwa juhudi na mbinu za kidiplomasia za meneja wake, Page Jones na Meneja wa Tanganyika Standard, Nihill waliokwenda makao makuu ya TANU kusuluhisha baina ya gazeti hilo la serikali na TANU. Nihill alifanya mazungumzo na makamu wa rais wa TANU, John Rupia; kaimu katibu mwenezi, Amos Kissenge; katibu wa TANU Youth League, Dr. Michael Lugazia; Dossa Aziz na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya TANU Idd Faiz. Hawa viongozi waandamizi wa TANU walitoa amri ya kusitisha ususiaji wa gazeti la Baraza. Kwa kitendo hiki TANU ilikuwa imeojieleza vyema na ilikuwa imeonyesha nguvu zake.
Katika kipindi hiki mashambulizi kwa wale Waislam walionekana wanaipinga TANU na Nyerere yalizidishwa. Sheikh Hussein Juma makamu wa rais wa UTP alikuwa na pacha mwenzake, Sheikh Hassan Juma. Sheikh Hassan Juma alikuwa akiendesha madrasa pamoja na shule ikiitwa Al Hassanein Muslim School, moja ya majaribio ingawa hafifu ya Waislam kujiendeleza katika elimu. Shule nyingi zilikuwa mikononi mwa wamisionari. Watoto wengi waliozaliwa mjini Dar es Salaam baada ya vita ya pili walisomeshwa Qurían katika Al Hassanein chini ya Sheikh Hassan Juma. Wazazi waliwatoa watoto wao katika shule hii kwa sababu waliihusisha madrasa hii na upinzani dhidi ya TANU. Watoto hawa hawakuishia katika kuacha kuhudhuria madrasa bali walitunga nyimbo za kebehi ambazo waliziimba kwa sauti kubwa walipokuwa wakipita katika shule yao ya zamani ili kuwakebehi, Sheikh Hussein Juma na nduguye pacha Sheikh Hassan. Wazee wao hawakuona haja ya kuwakataza watoto wao tabia hii isiyofaa. Kwa kawaida ilionekana kwamba yeyote aliyekuwa anaipinga au hakujinasibisha na TANU, alikuwa adui.
Huu ndiyo ukuwa mwanzo wa upinzani wa chini chini dhidi ya TANU. Mwaka 1959, Ramadhani Mashado Plantan, mhariri hodari wa gazeti la Zuhra wakati mmoja gazeti hili likiwa ndiyo sauti ya TANU na wananchi wa Tanganyika, pamoja na kikundi kidogo cha Waislam akiwemo Saleh Muhsin walijiuzulu kutoka TANU na kuunda chama chao cha upinzani, All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT). Wanachama wengine waasisi walikuwa Abdallah Mohammed ambaye alichaguliwa kuwa rais na Plantan akiwa katibu. Plantan alijitolea chumba kimoja nyumbani kwake Kirk Street, Gerezani kama ofisi ya kwanza ya AMNUT. Mara tu baada ya kuundwa kwa AMNUT, ulizuka mgogoro katika uongozi na ofisi hiyo ilibidi ihamishwe kutoka nyumbani kwa Plantan hadi Libya Street, eneo lenye Wahindi wengi katikati ya mji. Uongozi mpya ulikuja madarakani na katibu mpya Abduwahid Abdulkarim. Abduwahid Abdulkarim, kijana mwenye umri wa miaka 25 alichaguliwa kuchukua nafasi ya Plantan. Abdallah Mohamed alibakia na cheo chake kama rais. AMNUT haikuweza kumudu kodi ya nyumba katika eneo lile la matajiri wa Kihindi. AMNUT ikaihamisha ofisi yake na kwenda Kariakoo, Narungíombe Street, karibu na msikiti wa Sheikh Idris bin Saad.
Lengo kuu la AMNUT lilikuwa ni kulinda haki na maslahi ya Waislam ambayo ilikuwa ikihisi yalikuwa hatarini katika serikali iliyoshikiliwa na Wakristo. Abdulkarim alikwenda Tabora kujaribu kutafuta kuungwa mkono AMNUT lakini matokeo yalikuwa ya kukatisha tamaa. Abdulkarim alichagua Tabora kwa sababu ilikuwa mahali penye athari kubwa ya Uislamu. Hata hivyo Abdulkarim alifanikiwa kupokea mwaliko kutoka kwa Ali Muhsin Al Barwani kiongozi wa Zanzibar Nationality Party (ZNP) ahudhurie mkutano wa kamati kuu na awakilishe suala la AMNUT. Mkutano huu ulifanyika katika ofisi ya ZNP Darajani huko Zanzibar. Ali Muhsin alimwambia Abdulkarim kwamba ZNP haiwezi kujifungamanisha na tatizo la Uislam kwa sababu ZNP haikuwa inaamini kama Ukristo una uwezo wa kuhatarisha Uislam hasa ukichukulia kuwa Waislam ni wengi nchini Tanganyika. Waislam wa Tanganyika walikataa kuiunga mkono AMNUT wakihisi sera zake zilikuwa za kuwagawa watu kwa misingi ya dini. Kwa ajili hii basi AMNUT haikuwa na maslahi ya wananchi.
Lakini pigo kubwa kwa AMNUT lilikuja kutoka kwa masheikh wa Tanga. Masheikh na waalimu wa Qurían mjini Tanga walitia sahihi azimio la pamoja kuipinga AMNUT. Azimio hilo lilisema kuwa AMNUT ingezua janga. Masheikh walisisitiza kwamba wataiunga mkono TANU mpaka uhuru upatikane kwa sababu wana imani na malengo yake. AMNUT ikikabiliwa na mashambulio kama hayo kutoka tabaka ambayo ilidai inawakilisha maslahi yao, chama hicho hakikuweza kustawi. Haukupita muda mrefu AMNUT ikafa.
Mwaka 1960, Plantan sasa akiwa nje ya AMNUT na siasa, alitoa kauli moja iliyokuwa kama anatoa buriani kuteremsha pazia na kuaga jukwaa la siasa. Plantan aliwaambia Waislam kwamba hata kwa miaka mia moja hawataweza kuwafikia Wakristo. Baada ya kauli hiii hakuna kilichosikika kuhusu Ramadhani Mashado Plantan. Aliishi miaka ya mwisho ya maisha yake hapo Gerezani, akitumia wakati wake baina ya nyumba yake na msikiti wa jirani ambao alikuwa akiufagia kuuweka safi akisubiri mauti yaje akasimame mbele ya haki.
Nyerere alikubali ukweli kuwa kulikuwa na upogo baina ya Waislam na Wakristo hususan katika elimu ambayo itawazuia Waislam kushika nafasi za uongozi katika serikali ya wananchi. Nyerere aliwaomba Waislam waweke matumaini yao kwa TANU ambayo itaanzisha mabadiliko ya lazima kuwainua Waislam kwenye nafasi za usawa pamoja na Wakristo mara tu uhuru utakapopatikana. Lakini hili, Nyerere aliwakumbusha Waislam mara kwa mara kuwa linaweza kufanyika tu kwenye Tanganyika huru na siyo chini ya utawala wa Kiingereza. Waislam katika TANU, kwa upande wao, waliamini kwamba ilikuwa kinyume kwao kuanzisha chama cha kisiasa chini ya maslahi ya kikundi kimoja kama ndiyo lengo la kudai uhuru. Hili, wengi waliamini, lingesaidia kuunda vikundi vingi na kusababisha mfarakano. Kwa kweli madai yaliyokuwa yakitolewa na AMNUT hayakuwa madai ambayo yangetolewa kwa TANU katika wakati ule. Vita vya mwaka 1947 kati ya India na Pakistan vilivyosababisha kupoteza maisha ya watu wengi, vilikuwa bado vinakumbukwa na watu wengi. Chanzo cha ugomvi huo kilikuwa ushindani baina ya Waislam na Wahindu. Kabla ya mwaka 1947 India na Pakistan zilikuwa nchi moja chini ya ukoloni wa Mwingereza. Waislam na Wahindu walipigania uhuru pamoja na walifarakana mara tu ilipokuwa wazi kuwa Uingereza ingetoa uhuru kwa India. Watu wengi nchini Tanganyika walihofia kwamba kuruhusu fikra kama zile zilizotolewa na Sheikh Takadir kuota mizizi kulikuwa kukaribisha ile hali ya India na Pakistan Tanganyika. Nyerere alionya kuwa hakutaka hali kama ile ije kuisibu Tanganyika.
***
Wanaukumbi hii ndiyo historia ya wazee wangu na kama nilivyosema hapo awali mimi simsubiri Nimtz atoke Canada aje kuniandikia historia ya wazee wangu. Mimi nimeipokea hiyo kutoka katika ndimi zao wenyewe waliolipindua gurudumu la historia. Sheikh Haidar Mwinyimvua nikimfahamu hadi anafariki. Heri Baghadeleh alikuwa rafiki ya baba yangu na katika vitu vilivyokuwa vigumu kwake ni pale mwaka 1964 babu yangu alipowekwa kizuizini jela ya Uyui Tabora kwa shutuma za kutaka kuipindua serikali ya Nyerere. Bwana Jela alikuwa Mzee Munthali baba yake Kwege Muthali aliyekuwa mtangazaji wa TBC akafa katika ajali ya treni ilipogongana na gari yao ndogo pale Shaurimoyo. Baghdelleh alikuwa Regional Commissioner akienda pale jela kuwaona waliokuwa kizuizini na Mzee Munthali kama Bwana Jela alikuwa akimsindikiza. Anasema Baghdelleh akipata tabu sana kuutazama uso wa babu yangu kwa aibu. Baghdelleh alikuwa akijua kuwa hapakuwa na njama yoyote ya kumpindua Nyerere ila ni uongo mtupu. Hata hivyo akimtia moyo baba yangu kwa kumwambia, "Mzee ataachiwa hivi karibuni ondoa wasiwasi." Kadi yake ya TANU baba yangu kainunua kwa Abdulwahid Sykes tena kwa siri maana yeye alikuwa mfanyakazi wa serikali. Anaogopa akijulikana atafukuzwa kazi. Akikutana na Abdulwahid wote vinywa vinawajaa mate hawana la kusema. Nyerere amekuwa mkubwa sana hawamuwezi kamwe si yule ambae Abdulwahid alimjulisha baba yangu pale Mtaa wa Aggrey/Sikukuu nyumbani kwa Abdu mwaka 1952 siku ile usiku.
Mimi hupenda kuwakumbuka wazee wangu kwa namna hii. Kwa kuhadithia habari zao na ninamshukuru Mungu kwa kunipa historia. Wengi wetu hatukubahatika hivi. Historia hii kwangu mimi ni amana. Kitu nilichowekeshwa. Mwenyewe akijakitaka basi sina budi kumpa.