FM: Uchochezi si moja ya sifa zangu. Nakuwekea kiapnde hiki uone ukoloni ulivyokuwa ukitazamwa na Waislam na uone vipi dini hizi mbili zilivyoathiriwa na utawala wa Waingereza. Huu ni muhtasari tu:
Mwaka 1951 mgogoro wa ardhi ya Wameru ulipoanza tawi la TAA mjini Tabora lilikabili changamoto hiyo kupitia juhudi binafsi za Saadan Abdu Kandoro. Kandoro aliitisha mkutano wa matawi ya TAA ya Mwanza, Kigoma na Tabora kujadili suala hilo. Uongozi wa TAA Tabora, kwa kujihusisha katika mgogoro kama huu, ilikuja kuwa ngome ya upinzani dhidi ya ukoloni. Germano Pacha, katibu wa TAA katika Jimbo la Magharibi, alikuwa miongoni mwa wale wajumbe ambao tarehe 29 Oktoba, 1953 walikwenda Government House kuonana na Gavana Edward Twining ili kujadili ule waraka wa serikali, yaani Government Circular No. 5 uliopiga marufuku wafanyakazi serikalini kujishughulisha na siasa. Mwaka uliofuata TAA ilibadilishwa kuwa TANU na Pacha alikuwa miongoni mwa wanachama waasisi. Pacha alianza kuifanyia kampeni TANU mara tu aliporudi kutoka mkutano wa TAA ulioasisi TANU. Akiwa mhitimu wa Seminari ya Kipalapala ilikuwa rahisi sana kwake kupata kumbi za kanisani, Tabora vijijijni ambamo alifanya baadhi ya mikutano yake ya mwanzoni ya kampeni za TANU. Jambo hili lilizusha ugomvi dhidi ya Pacha. Jambo lile liliwaudhi viongozi Waislam katika TANU mjini Tabora. Wamishonari walijulikana kuwa makachero wa wakoloni na wapinzani wa Uislamu. Kwa hiyo uongozi wa Waislam mjini Tabora ukamsusa Pacha na kwa muda kwa ajili ya kufanya baadhi ya mikutano ya TANU katika kumbi za makanisa. Ususiaji huu ukaifanya TANU katika Jimbo la Magharibi kuzorota. TANU haikuweza kupamba moto Tabora kama ilivyotarajiwa. Moto wa siasa uliokuwa Tabora tangu mwaka 1945 ulionekana kufifia kwa kuzuka chama kipya cha siasa.
Juhudi za kuihuisha TANU zilikuja mwaka 1955 mwaka mmoja baadae kupitia Young New Strong Football Club -kilabu ya kandanda iliyoanzishwa miaka mingi nyuma ambayo ilikuwa maarufu pale mjini. Wanachama wa kilabu hiyo baadhi yao ndiyo walikuwa waasisi wa African Association, mashuhuri miongoni mwao walikuwa Fundi Mhindi na Maulidi Kivuruga. Mwenyekiti wa kilabu hiyo alikuwa Juma Mrisho, mcheza kandanda mashuhuri kwa siku zile. Shaaban Mohamed Silabu na Bilali Rehani Waikela walikuwa katibu na naibu katibu. Uongozi huu wa klabu hiyo ya kandanda ulikutana katika nyumba ya Abeid Kazimoto aliyekuwa akifanya kazi Medical Department, kujadili jinsi ya kuifufua TANU. Sasa ilikuwa wazi kuwa Pacha, kama Mkristo na kabila yake Mlulwa kutoka Mpanda, hawezi kukubalika na Wamanyema wa Tabora. Wamanyema walikuwa wanajulikana kwa tabia yao ya ukaidi. Wakati huo TANU ilibidi ikubaliwe na Waislam wakazi wa mijini kabla ya kusambaa kwenye sehemu nyinginezo. Wamanyema kama Waislam wa mijini walikuwa nguvu thabiti ya kisiasa ambayo haikuwa raihisi kupuuzwa. Alichokuwa akikabiliana nacho Pacha kilikuwa sawasa na kile Nyerere kilimkabili baada ya kumshinda Abdulwahid Sykes katika ule uchaguzi wa TAA wa mwaka 1953. Waislam waliacha kuiunga mkono TANU kwa sababu zile zile zilizomsibu Nyerere. Uongozi wa kilabu uliamua kumualika Julius Nyerere na Bibi Titi Mohammed kuja Tabora ili kujadili tatizo hilo na kulitafutia jawabu.
Mwaka 1955 Bibi Titi Mohamed na Julius Nyerere waliitika mwaliko na kuja Tabora. Mkutano ulifanyika katika ile kilabu ya kandanda. Waliohudhuria mkutano ule walikuwa Germano Pacha, Juma Mrisho, Shaaban Mohamed Silabu, Bilali Rehani Waikela, Mohamed Mataka wakati ule akiwa muadhin wa Masjid Nur - msikiti wa Wamanyema pale Tabora, Hassan Mohamed Ikunji, Ramadhani Mussa Wajaku, Swedi Mambosasa, Said Ali Kiruwi na Hamis Khalfan. Uongozi wa kilabu ulimwambia Nyerere na Bibi Titi kuwa kilabu hiyo ya kandanda ilikuwa ikitaka udugu na TANU ili ifanye kampeni ya kuipatia TANU wanachama wengi. Uongozi huo wa TANU kutoka makao makuu Dar es Salaam uliambiwa kuwa maadam kilabu hiyo ilikuwa ikipendwa na kuungwa mkono na watu wa Tabora na ilikuwa maarufu sana, sifa hizo zingeweza kutumiwa kwa manufaa ya TANU. Vilevile Nyerere alifahamishwa kuwa kilabu hiyo ingependa kuvijumuisha vyama vitatu vya lelemama na vikundi vya taarabu, Nujum ul Azhar, Waridatil Hubb na Egyptian Club. Nyerere na Titi waliyakubali mapendekezo haya na usiku ule akifuatana na uongozi wa kilabu Nyerere alizungumza na kikundi cha watu waliyokusanyika nje ya nyumba ya kilabu juu ya hali ya Tanganyika katika siku zijazo. Nyerere alikuwa amerudi Tabora ambapo alianza siasa kiasi cha miaka minane nyuma. Jambo muhimu katika kipindi hiki pale Tabora ni kuwa wasomi wa Makerere waliokuwa St. Maryís School hawakuwapo katika harakati hizi na katika mikakati iliyokuwa ikipangwa.
Bibi mmoja wa Kiganda, Nyange bint Chande, mwanachama wa moja ya vikundi vya lelemama mjini Tabora alijitolea nyumba yake kama ofisi ya kwanza ya TANU katika Jimbo la Magharibi. Uchaguzi ulifanyika na Shaabani Marijani alichaguliwa Mwenyekiti wa Wilaya na Idd Said Ludete Katibu wa TANU. Bilali Waikela akawa mjumbe wa kamati. Kadi za kwanza za uanachama wa TANU ziliuzwa ndani ya soko la Tabora na Amani Idd na Pacha, Katibu wa Jimbo wa TANU. Pacha alikuwa na lingo la kuni pale sokoni kama biashara yake. Baadae Amani Idd alisaidiwa kazi hiyo ya kuuza kadi za TANU na Dharura bint Abdulrahman.