KWELI Ulaji wa maboga unaweza kusaidia kuimarisha afya ya macho

KWELI Ulaji wa maboga unaweza kusaidia kuimarisha afya ya macho

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Wakuu wa JamiiCheck naomba msaada wa hili, kuna rafiki angu mmoja ameniambia kula maboga kunasaidia kuimarisha afya ya macho. Je, ni kweli?
1754380976464.png

​
 
Tunachokijua
Kwa jamii ya kitanzania Maboga yamekuwa yakitumiwa kama chakula cha asili ambacho kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakipatikana zaidi maeneo ya vijijini. Inawezekana wewe unayesoma andiko hili ni miongoni wa walaji wazuri wa maboga au kushuhudia yakiliwa na wengine, lakini umewahi kujiuliza ni upi umuhimu wa ulaji wa maboga kwa afya ya binadamu hasa macho?

Mdau wa JamiiForums alihitaji kupata msaada wa kujua uhalisia kupitia JamiiCheck kuhusu hoja inayohusisha ulaji wa maboga na umuhimu wake kwenye afya ya macho ambapo zimepitiwa tafiti pamoja na machapisho ya kisayansi yanayofafanua kwa kina kuhusu hoja hii.

Kwa mujibu wa tovuti ya Milan eye Center Maboga ni chanzo bora cha zinki, vitamini C, vitamini A, lutein, na zeaxanthin, na hivyo kuyafanya kuwa lishe nzuri kwa afya ya macho na mwili kwa ujumla.
Virutubisho hivyo ni muhimu kwa afya ya macho ambapo Vitamini A hulinda kornea (cornea) na husaidia macho kuona vizuri katika mwanga hafifu.

Vitamini C hupunguza hatari ya kuharibika kwa sehemu ya kati ya retina (macular degeneration,) ambayo ni moja ya sababu kuu za upofu kwa watu wazima.

Virutubisho vya Lutenin na zeaxanthin husaidia kupunguza hatari ya magonjwa sugu ya macho kama lenzi ya jicho kuwa na ukungu au mawingu (cataracts ) na kuharibiwa kwa sehemu ya kati ya retina (macular degeneration) inayohusiana na uzee. Pia husaidia kuchuja mwanga mkali usiokuwa salama kwa macho.

Zinki hupatikana kwa kiwango kikubwa kwenye jicho, hasa katika retina, na ina jukumu muhimu katika kusaidia vitamini A kufika kwenye retina ili kuzalisha melanini, ambayo hulinda macho dhidi ya mwanga mkali.

Tovuti ya Dr Agarwals Eye Hospital inabainisha kuwa Mbegu za maboga ni chanzo bora cha zinki, madini muhimu yanayosaidia kusafirisha vitamini A hadi kwenye retina ya jicho. Zinki pia huchangia afya ya kornea, kwa kuilinda dhidi ya madhara yanayosababishwa na sumu mwilini (free radicals). Utafiti umeonyesha kuwa kuwa na kiwango cha kutosha cha zinki kunaweza kusaidia kuzuia upofu wa usiku na kupunguza hatari ya macular degeneration kwa watu wazima wanaozeeka.

Mbegu za maboga zina virutubishi vingi vinavyosaidia kudhibiti sumu mwilini, pia zina mafuta yenye afya, jambo linalosababisha lishe kamili kwa kulinda macho kwa ujumla.

Tovuti ya American Macular Degeneration Foundation inashauri unapotumia maboga kwa kupika ili kupata virutubisho kuimarisha afya ya macho, ni muhimu kuzingatia uchaguzi wa maboga, mathalani maboga mabichi (fresh) badala ya yale yaliyokaushwa au kuwekwa kwenye makopo (canned). Maboga mabichi yana 'lutein na zeaxanthin' kwa wingi virutubisho muhimu kwa macho ambavyo hupotea kwa kiasi kikubwa wakati wa usindikaji wa kuwekwa kwenye makopo.​
Back
Top Bottom