KWELI Ulaji wa mayai ya nyoka yasiyopikwa vizuri unaweza kuwa hatari kwa afya ya binadamu

KWELI Ulaji wa mayai ya nyoka yasiyopikwa vizuri unaweza kuwa hatari kwa afya ya binadamu

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Source #1
View Source #1
Mdau wa JamiiForums.com ametaka kupata uhalisia endapo mayai ya nyoka ni salama kwa bonadamu.

"Inasemekana Mayai "Egg's" yote yakiwa fresh ni salama,Sasa swali linakuja jee hata Mayai "Egg's" ya Nyoka "Snake" yakiwa fresh yanafaa kwa binadamu kula na asipate madhara yeyote?Kwa wale wataalamu wa wanyama hebu tupeni majibu Naaam"

The-Mystery-Of-Snake-Eggs6.jpg
 
Tunachokijua
Ufuatiliaji wa JamiiCheck

Inaelezwa kuwa mayai ya nyoka yanaweza kuliwa na binadamu, hata hivyo, ni lazima yapikwe na kuiva vizuri kwani kula mayai ya nyoka ambayo hayajapikwa kikamilifu, inaweza kusababisha kupata matatizo ya tumbo. Ladha yake, inaweza isipendwe na kila mtu kwani ladha yake ni tofauti na mayai ya kuku tuliyozoea.

Jambo jingine la kuzingatia ni kwamba mayai ya nyoka yanapaswa kuwa mapya kabisa. Ukuaji wa kiinitete ndani ya yai la nyoka huanza haraka sana. Hivyo basi, kama yai si jipya, linaweza kuwa na vipande vya nyama jambo ambalo haliwezi kufurahisha wala kukubalika kuliwa.
​
Baadhi ya sehemu hususani Vietinamu, Thailand, Indonesia, China, na Japan utamaduni wa mapishi wa mayai ya nyoka ni maarufu. Katika upishi wa kienyeji wa Kivietinamu, mayai ya nyoka hutolewa ndani ya mwili wa nyoka wa kike na kutumika kama viungo katika chakula maarufu cha kifungua kinywa na kuliwa pamoja na mbogamboga, wali au tambi. Mayai hayo yanachemshwa au kukaangwa kama vile mayai ya ndege.

Tovuti ya AZ Animals inabainisha kuwa mayai ya nyoka yanaweza kukusababishia maradhi endapo ukila bila kuyapika vizuri kwani unaweza kumeza vijidudu hatarishi ambapo hali hii ni sawa pia kwa mayai ya ndege wengi, na hata mayai ya kuku wasiopatiwa chanjo yanaweza kusababisha ugonjwa wa salmonella unaotokana na sumu ya chakula.

Ulaji wa mayai ya nyoka kama inavyoelezwa katika tovuti ya AltPet unaweza kuwa hatari kwani upo uwezekano wa kupata mzio au kutovumilia vyakula fulani, hatari ya bakteria au vimelea, pamoja na sumu inayoweza kuwepo kutokana na aina fulani za nyoka.

Kwa kuwa upo uwezekano wa kupata mwitikio mkali wa mzio kutokana na mayai ya nyoka, hivyo inashauriwa watu wenye historia ya mzio wa vyakula wajiepushe kuyala. Ikiwa una mzio unaojulikana, ni bora kabisa kuepuka kula mayai ya nyoka kwani yanaweza kusababisha upele, muwasho, uvimbe wa uso au koo, shida ya kupumua, kichefuchefu na kutapika.

Aidha, iwapo utapata madhara yoyote baada ya kuyala, ni muhimu kutafuta msaada wa kitabibu mara moja, kwani kwa baadhi ya watu athari zinaweza kuwa kali sana.

Kadhalika mayai ya nyoka yanaweza kuchafuliwa na bakteria kama vile 'salmonella' au vijidudu vingine hatarishi vinavyoweza kusababisha maradhi endapo yataliwa.

Vilevile ni muhimu kuwa mwangalifu sana unaposhughulika na mayai mabichi ya nyoka ili kuhakikisha hayagusani na chochote kinachoweza kuyachafua kama vile kinyesi, sehemu au vifaa visivyo safi. Kupika yai vizuri huua bakteria wengi, lakini ikiwa una shaka, ni bora kabisa kuepuka kula mayai hayo kuliko kuhatarisha afya yako.

Aina fulani za nyoka hutoa sumu ambayo huhifadhiwa ndani ya mayai yao; sumu hii inaweza kuwa hatari sana kwa binadamu wanaoyala bila kutumia mbinu sahihi za maandalizi. Hivyo basi, ni muhimu kujua ni aina gani ya nyoka aliyetoa yai kabla ya kuliandaa kwa ajili ya kuliwa. Ikiwa huna uhakika, ni busara zaidi kuepuka kuyala kuliko kuhatarisha kuugua.

Kutokana na mtazamo wa kimazingira, kwa ujumla haishauriwi kula mayai ya nyoka. Hii ni kwa sababu aina kadhaa za nyoka zipo kwenye orodha ya viumbe walio hatarini kutoweka. Matendo yako yanaweza kuathiri uwepo na uhai wao. Kwa hiyo, kula mayai ya kuku ni chaguo salama zaidi na pia yana ladha nzuri kuliko mayai ya nyoka.​
Back
Top Bottom