Umasikini ule ulitutesa sana, Isijirudie tena...

Umasikini ule ulitutesa sana, Isijirudie tena...

Nakumbuka zama zile za miaka ya 1983 hadi 1984, niko tunaishi mitaa ya Makutano Mabibo jijini Dar es salaam na Kadi yangu ya Rangi ya Kijani ikiwa na maelezo ya Kaya yetu ndani Mwake.

Mchana wa jua kali la Darisalama tukiwa tumekaa barabarani kusubiri gari la "Ugawaji" litaelekea mwelekeo upi na sisi tulifukuzie kwa nyuma. Hakuna aliyejua leo ni zamu ya duka gani kupelekewa chakula ama mahitaji mengine muhimu ili wakazi wa eneo letu waende wakanunue.

Shuleni wanafunzi wanavaa nguo zisizo na rangi maarufu kama "Maradufu" kutokana na viwanda vya kuzalisha nguo kukosa rangi za kuweka ili vitambaa hivyo viwe na rangi ya Bluu Maalum zama hizo kwa sare za shule za msingi.

Mitaani watu wanavuta sigara kwa "Puff" kwa hela ulizo nazo. Watu wanafua nguo zao kwa kutumia majani ya mpapai, sukari inakaangwa ili kutengeneza chai kwa kuwa hakuna majani ya chai na wenye majani ya chai wanaweza kutumia sukari guru badala ya sukari ya kawaida kama kiungio.

Unakwenda kwenye duka la ushirika kwa mfano kununua Sukari unalazimshwa kununua na kitu kingine kwa mfano Chujio la chai ama birika. Watu wa Darisalama tuliteseka sana na wanawake wengi walibakwa na watu waliojifanya wana bidhaa hizo "adimu" majumbani mwao..

Wakati ule Mgambo na wenyeviti wa maduka ya Ushirika walikuwa kama ni Miungu watu. Sisi kwetu kulikuwa na mgambo aliyetembea na wake za watu alivyopenda kisa yeye ana nafasi kubwa sana ya kupata vitu kwenye duka la Kaya la Mtaani kwetu.

Hayo yote yalisababishwa na Ugomvi wa Mwalimu JK Nyerere na wakubwa wa IMF na World Bank. Umaskini ule ulitutosha hatutaki hali ile ijirudie tena kwenye kizazi hiki.

CC: Mshana Jr Pascal Mayalla
Nilikuwepo! Niliona! Nina mtazamo kidogo tofauti. Ilikuwa ni kipindi cha marekebisho. Tungeanzisha viwanda wakati huo vingedumu. Nakumbuka viwanda vya sabuni na ubunifu mbali mbali wa mavazi. Hata china ilipitia hapo hapo lakini wao walienda nje kujifunza kwa wenzao baadaye wakajifungia ndani wakateseka sana baadaye wakajikwamua.
Yule mzee Rukhsa alipokuja akafungua milango ya kila kitu na mitumba kuingia ilitulemaza hadi leo. Hivi Killtex, Sungura tex, Mutex etc vilienda wapi?
 
Back
Top Bottom